Tafuta

Kwaresima ni kipindi maalum cha maandalizi ya Fumbo la Pasaka, kiini cha imani ya Kanisa! Kwaresima ni kipindi maalum cha maandalizi ya Fumbo la Pasaka, kiini cha imani ya Kanisa! 

Kwaresima ni maandalizi ya Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, kiini cha imani ya Kanisa!

Baba Mtakatifu Francisko anatualika tuipokee Kwaresima ya mwaka huu kama kipindi mahsusi cha wongofu; kipindi cha kumrudia Mungu. Kwaresima kwa makusudi yake ni kipindi cha kujiandaa kwa maadhimisho ya Pasaka. Lakini hapo hapo Papa anaonesha kuwa Pasaka hiyo inayoandaliwa na Kwaresima ndiyo chemichemi yenyewe ya wongofu: Muhimu: Sala, Kufunga na Matendo!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu.  Katika mzunguko wa mwaka wa Kanisa, tumeingia sasa katika kipindi cha Kwaresima, kipindi ambacho hata mwaka huu Mwenyezi Mungu ametujalia ili kiwe kwetu wakati muafaka wa kujiandaa kuiadhimisha Pasaka kwa moyo uliomgeukia Mungu kwa sala, toba, wongofu na matendo ya huruma. Leo tutayafafanua masomo ya dominika ya kwanza ya Kwaresima na kuingia kiufupi katika tafakari yake.

Somo la kwanza (Mwa. 2:7-9, 3:1-7) ni kutoka kitabu cha Mwanzo. Somo hili linaelezea asili ya mwanadamu na asili ya anguko lake kuu katika dhambi. Kuhusu asili ya mwanadamu, somo linatupa ukweli wa ufunuo wa Mungu kuwa mwanadamu aliumbwa. Asili yake ni Mungu ambaye alimuumba. Alimuumba kutoka udongo na akampulizia pumzi ya uhai naye akawa nafsi hai. Somo linaonesha pia hali ya neema aliyokuwa nayo mwanadamu baada ya kuumbwa kwake. Mungu aliweka mbele yake kila kitu alichohitaji ili mwanadamu huyu aendelee kuwa katika furaha ya mahusiano na Muumba wake. Ghafla anatokea nyoka. Anamshawishi mwanadamu kuuangalia upya mpango wa mahusiano yake na Muumba wake; ni kama anamualika kuukosoa na kuurekebisha ili uwe mzuri zaidi. Na hapo ndipo dhambi inaingia ulimwenguni.

Kiini cha dhambi hii, ambayo tunaiita pia dhambi ya asili, ni mwanadamu kutokutii agizo ambalo Mungu alimpa, agizo ambalo kwalo angeheshimu mpango wa mahusiano kati yake na Muumba wake. Kwa hali hii, mwanadamu aliuasi uuambaji. Alikataa kujiona kuwa kiumbe mbele ya Mungu muumbaji akataka uhusiano huu kati ya kiumbe na Muumbaji uwe kama ni uhusiano kati ya nguvu mbili zinazolingana katika maamuzi. Dhambi hii si ndogo kwa sababu ilikwenda kukata palepale kwenye mzizi au mzingi wa mahusiano kati ya mtu na Mungu. Na matokeo yake mahusiano yaliyokuwa ndiyo chanzo cha furaha kwa mwanadamu yakageuka kuwa udhaifu na uadui kati yao. Somo hili linaletwa katika dominika ya kwanza ya kwaresima ili kutualika kutafakari upya juu ya mahusiano yetu na Mungu. Na hasa ni kujiuliza, ni nini hasa maana ya mahusiano kati ya mtu na Mungu?

Somo la pili (Rum. 5:12-19) ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi. Katika somo hili mtume Paulo analinganisha hali mbili zinazotawala mahusiano kati ya mwanadamu na Mungu. Hali ya kwanza ni ile ya Adamu na ya pili ni ya Kristo. Hali ya kwanza, yaani ile ya Adamu, ilikuwa ni ya dhambi kwa sababu kwa njia yake dhambi iliingia ulimwenguni na wote waliozaliwa kwake wanairithi. Hali ya pili, yaani ile ya Kristo ni ya karama au neema. Na kama jinsi ile wale wanaozaliwa kwa Adamu wanairithi dhambi basi vivyo hivyo wale wanaozaliwa kwa Kristo wanairithi neema. Katika mazingira yake haya, mtume Paulo alikuwa anawaalika warumi kumuongokea Kristo, wazaliwe katika neema ili waokolewe na mauti yaliyoletwa na dhambi ya Adamu. Mwaliko huu wa mtume Paulo, mwaliko wa wongofu ni mwaliko wetu pia. Ni mwaliko ulio hasa kiini cha kipindi hiki cha kwaresima: kumgeukia Kristo.

Injili (Mt. 4:1-11 somo la Injili ni kutoka kwa Mwinjili Mathayo na linaeleza tukio la kujaribiwa kwa Yesu. Ibilisi, ambaye ndiye anayemtia katika majaribu anamwendea wakati akiwa na njaa ya kimwili baada ya kuwa amefunga kwa siku arobaini mchana na usiku. Anamjaribu ageuze mawe yawe mkate, anamjaribu ajitupe chini kutoka mnarani ili aone kama Mungu atamuokoa na anamjaribu amjusudie ili apewe heshima na fahari zote za ulimwenguni. Yesu anayashinda majaribu yote hayo na anamfukuza ibilisi. Majaribu haya ya Yesu ni majaribu yaleyale waliyoyapata Adamu na Eva katika bustani ya Eden lakini hapa yakiwa yamekuja kwa sura nyingine. Ni yaleyale kwa sababu yote yana msingi wake katika kuharibu mahusiano na Mungu.

Katika mfululizo wa matuko katika Injili ya Mathayo, tukio la Yesu kujaribiwa linafuata lile la ubatizo wake katika mto Yordani. Pale mtoni baada ya kuwa amebatizwa, sauti ilisikika ikisema “huyu ni mwanangu, mpendwa wangu ninayependezwa naye” (Mt. 3:17). Ni mara tu baada ya tukio hilo, Ibilisi anamfuata Yesu na kumwambia “ikiwa wewe ni mwana wa Mungu...fanya hivi, fanya hivi na fanya hivi”. Mwana wa Mungu ni jina, lakini pia ni cheo na ni heshima ambayo kimsingi inaonesha mahusiano aliyonayo Yesu na Mungu. Shetani, kwa majaribu haya na tena kwa kuanza kumwambia “ikiwa wewe ni mwana wa Mungu” ni kumshawishi auishi uhusiano wake huo na Mungu sio kama Mungu anavyotaka bali kama yeye anavyotaka. Yesu anamshinda kwa kuonesha utii mkubwa alionao kwa mpango wa Mungu. Na hilo analifanya kwa kunukuu Maandiko Matakatifu ambayo ni ufunuo wa mapenzi ya Mungu kwa wanawe. Kwa majaribu haya, Yesu analirekebisha kosa la Adamu. Pale ambapo Adamu alianguka kwa kutokutii, Yesu anainuka na kuuonesha ubinadamu mzima kuwa kiini cha kudumisha mahusiano na Mungu ni kutunza utii kwake na kwa mpango wake wa uumbaji. Kwa jinsi hii Yesu anakuwa ni mwanzo wa kujenga upya mahusiano yaliyokuwa yameharibika kati ya Mungu na mwanadamu.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, baada ya kuyasikiliza masomo ya dominika hii pamoja na ufafanuzi wake, ninawaalika sasa tuingie katika tafakari fupi. Tafakari ya leo itaongozwa na ujumbe wa Kwaresima alioutoa Baba Mtakatifu Francisko unaoongozwa na maneno “Tunawasihi kwa ajili ya Kristo: mpatanishwe na Mungu” (2Kor 5:20).  Katika ujumbe wake huu, Baba Mtakatifu anatualika tuipokee Kwaresima ya mwaka huu kama kipindi mahsusi cha wongofu; kipindi cha kumrudia Mungu. Kwaresima kwa makusudi yake ni kipindi cha kujiandaa kwa maadhimisho ya Pasaka. Lakini hapo hapo Baba Mtakatifu anaonesha kuwa Pasaka hiyo inayoandaliwa na Kwaresima ndiyo chemichemi yenyewe ya wongofu. Fumbo la Pasaka ambalo ni Habari Njema ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ndilo linalopyaisha mahusiano na Mungu na kuyafanya yashamiri.

Wongofu huu, anaongeza Baba Mtakatifu Francisko tuupokee kama mwaliko unaotoka kwa Mungu. Hivyo ni kitu kinachohitaji jibu la haraka bila kungojangoja. Anatukumbusha kuwa tusijidanganye au kujisubirisha kuuitikia kana kwamba sisi ndio waamuzi juu ya lini ni wakati mzuri wa kumrudia Mungu na ni kwa namna gani nimrudie Mungu. Tusiuchukulie kama kitu ambacho kipo tu au  kitu ambacho ni sisi tulio na maamuzi ya mwisho juu yake. Mwisho anatualika tuuishi utajiri wa neema ya Mungu si kwa kujilimbikizia bali kwa kuwashirikisha wengine. Na hili Baba Mtakatifu anatualika tuliweke si tu katika mahitaji ya kiroho bali hasa yale ya kimwili yanayogusa mahangaiko halisi ya mwanadamu. Kwa namna ya pekee anagusia uchumi fungamani ambao unamgusa mtu mmoja mmoja na bila kukuza matabaka na kuwaacha wengine nje. Mungu atujalie ili kipindi hiki cha kwaresima kitusaidie kumrudia kwa wongofu wa kweli.

Liturujia J1 Kwaresima
29 February 2020, 10:01