Tafakari Jumapili 3 ya Kwaresima: Yesu ni Kisima cha Maji ya Wokovu
Na Padre Alcuin Maurus Nyirenda, O.S.B., - Roma.
Ushauri ni paji la Mungu Roho Mtakatifu linalotuwezesha kuishi vyema upendo wa Mungu.Yesu Kristo alikuwa na paji la Ushauri katika utimilifu wake. Hebu tuone jinsi Bwana wetu Yesu Kristu alivyolitumia paji hili, ili litusaidie nasi kuielewa Injili ya leo: "Ndipo Yesu akawaambia, "Nawauliza ninyi; Je, ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya; kuponya au kuangamiza?" Akawakazia macho wote pande zote, akamwambia yule mtu, "Nyosha mkono wako." Akaunyosha, mkono wake ukawa mzima tena." (Lk 6:6-10). Hapa kuna mambo mawili muhimu. Mosi, kuna amri ya Mungu inayowakilishwa na Waandishi na Mafarisayo. Pili, kuna amri ya upendo inayowakilishwa na Bwana wetu Yesu Kristu. Katika Katekisimu tunafundishwa "Tenda mema acha mabaya." Kumbe kadiri ya paji la Roho mtakatifu la ushauri tunaoneshwa kuwa suala la maadili linahusu kuchagua jambo bora zaidi kati ya mambo mazuri.
Leo, Yesu anakutana na mwanamke msamaria kwenye kisima cha Yakobo. Mazingira ya kituko cha leo yanatatanisha kidogo. Mathlani, kijiografia, kutoka mji wa Sikar hadi kilipo kisima cha Samaria ni umbali wa meta 900. Lakini mjini Sikar kulikuwa pia na visima viwili vya maji kimoja kiliitwa Endafene na kingine Anashkar. Visima hivi vilikuwa na vyanzo nyingi vya maji. Tungeweza kusema "Bomba hii nyumba hii." Lakini mwanamke huyu aliamua kutembea karibu kilometa moja kutoka mjini Sikar hadi kwenye kisima cha Yakobo ili kufuata maji. Hapa hakieleweki. Hata kwa upande wa Yesu kuna utata. Yesu alikuwa safarini akitokea Yudea kuelekea nyumbani Galilea: "Aliacha Uyahudi akaenda zake tena mpaka Galilaya." Wakati huo alikuwa kwenye bonde la mto Yordani. Ilikuwa rahisi tu kwake tena angefupisha sana safari yake kama angelipita barabara inayoambaa bonde la mto Yordani. Lakini Mwinjili anasema: "Naye alikuwa hana budi kupita katikati ya Samaria." Je, kulikuwa na ulazima gani wa Yesu kurefusha safari kama alivyoirefusha yule mwanamke. Hakieleweki! Kwa hiyo hapa tunahitaji paji la Roho Mtakatifu la ushauri ili kufanya uamuzi wa kina. Inawezekana hapa kulikuwa tayari kuna agenda ya siri ya kukutana na yule mwanamke pale kisimani.
Mazingira yanayoweza kutusaidia kuielewa vyema Injili ya leo yako Sura ya tatu ya Injili hii pale Yohane Mbatizaji anaposema: "Mimi siye Kristo, bali nimetumwa mbele yake. Aliye naye bibi arusi ndiye bwana arusi; lakini Rafiki yake bwana arusi yeye anayesimama na kumsikia aifurahia sana sauti yake bwana arusi. Basi hii ni furaha yangu imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua." (Yoh. 3:29-30). Katika sura iliyotangulia kulikuwa na mnuso wa arusi ya Kana ya Galilaya (Yoh 2:1-11). Kisha inafuatiwa na habari ya leo. Katika Injili ya leo unaona upande mmoja kuna Yesu ndiye Bwana arusi mtarajiwa aliyetangazwa na Yohane Mbatizaji. Upande wa pili kuna bi arusi ambaye ni mwanamke msamaria. Katika Biblia bwana arusi ni Mungu anayewapenda Waisraeli kama bi arusi wake. Picha hiyo ya mahusiano ya Mungu na Waisraeli inatokana na ndoa balaa ya Nabii Hosea aliyeanguka kimapenzi na Gomer aliyekuwa kahaba wa kutupwa. Gomer alimzalia Hosea watoto watatu halafu wakakorofishana kisha Gomer akaamua kuingia mitaani na kuendelea kusharatisha. Baada ya muda fulani kupita, Hosea akaingiwa na upendo akaenda kumtafuta Gomer na kumtaka wakae tena pamoja. Nabii Hosea anaitafakari kashehe ya ndoa yake na kuona inavyolingana na kasheshe iliyoko kati ya Mungu na bi arusi wake, yaani kabila la Waisraeli.
Mwinjili anatueleza kuwa: "Yesu akafika hadi mji wa Samaria uitwao Sikari palipokuwa na kisima cha Yakobo. "Kisima hicho kinachotumika bado hadi leo, kilichimbwa miaka elfu moja kabla ya Kristo na kina cha urefu wa meta thelathini na mbili. Kisimani ni pahala walipokutana wachungaji na kunywesha maji mifugo yao. Kisimani walifika na kutulia wafanya biashara kwa vile palikuwa na wateja waliofika kunywa maji. Kadhalika kisimani walifika akina mama kuchota maji. Sana sana kisimani walikutana pia wapendanao. Viko vituko vitatu vya wapendanao kukutana kisimani. Mosi, Abrahamu alimtuma mtumwa wake kwenda Mesopotamia kumtafuta binti wa kumwoza mwanaye Isaak. Mtumwa alipofika huko alisimama kisimani na kusubiri wanawake wafikao kuchota maji. Akafika Rebeka amebeba begani mtungi (Amphora) ya maji. Yule mtumwa akamwomba Rebeka maji ya kunywa na kupiga “stori” kidogo. Kisha akamsindikiza hadi kwa wazazi wake na baadaye mambo yakaja kuwa kama yalivyokuwepo, yaani Rebeka aliolewa na Isaak. Pili, Yakobo alienda pia Mesopotamia. Alipofika kisimani akawaulizia wachungaji waliofika na mifugo yao kunywesha maji endapo wanamfahamu Raban mjomba wake. Wakamjibu ndiyo na kuongeza kusema kuwa hata binti yake Rachel anatazamiwa kufika na mifugo kuchota maji. Yakobo akajiongeza kwa kukifunua kifuniko cha kisima ili mifugo ya Rachel inywe maji na mengine kuchota kupeleka nyumbani. Hatimaye, Yakobo alimwoa Rachele.
Tatu, katika nchi ya ugenini alikoenda Musa alifika kisimani. Hapo walikuwa wachungaji Wengi wakinywesha maji mifugo yao. Zipora binti Raguele akiwa ametanguzana na dada zake nao walikuwa wananywesha mifugo yao hapo. Lakini mara nyingi walicheleweshwa kutokana na vijana wengine waliowazidi nguvu. Musa aliwapiga wachungaji wegine na kuruhusu mifugo ya Zipora kunywa maji. Siku hiyo Zipora na dada zake walirudi nyumbani mapema isivyo kawaida. Baba yao alipoonesha kushagaa, kwa kurudi mapema, walimweleza siri yake kwamba kulikuwa na Mmisri mmoja “aliyewakingia kifua”. Wakaenda kumwita Musa na kumtambulisha kwa mzee wao, na hatimaye Musa alimwoa Zipora. Kadhalika leo Mwinjili Yohane anamkutanisha Bwana arusi (Yesu Kristo) aliyetangazwa na Yohane Mbatizaji pamoja na bi arusi kisimani. Mwinjili anaongeza kusema kuwa:"Yesu alikuwa amechoka sana kwa safari, akaketi vivi hivi kisimani." Ni nafasi pekee katika Injili inayomwonesha Yesu amechoka. Aidha tunasikia kuwa "Wanafunzi wake walikuwa wameenda mjini Sikar kununua chakula." Hapa haieleweki kwa nini Yesu alibaki pale kisimani wakati angeweza kutanguzana na wanafunzi wake kwenda Sikar kulikokuwa na maji mengi ya kumwaga.
Hapa inaonesha tena jinsi Bwana arusi anavyoshidwa kukaa peke yake akisukumwa na busara ya paji la ushauri. Pia inasemwa kwamba ilikuwa saa sita ya mchana pindi mwanamke huyu anaenda mbali peke yake kuchota maji. Hali kadhalika Pilato akipomwonesha Yesu kadamnasi saa sita na kusema "Ecce homo yaani Tazama mtu." Hapa Pilato anamtambulisha Yesu aliye mwanga wa kweli kadamdasi saa sita ya mchana kweupe pe! Mwanamke huyu hatajwi jina bali anatambulishwa kama Mwanamke Msamaria. Yesu anamwendea na kumwambia: "Nipe maji ya ninywe!" Hapa unamwona Mungu ndiye mwenye kiu. Aidha kwa kuomba maji anataka kukaribishwa. Ndivyo ilivyo pia katika mila na desturi za Waafrika kwamba kupewa maji ya kunywa ni alama ya kukaribishwa. Inasemwa pia kwamba maji ni alama ya upendo wa kindoa. Kiu hiyo ndiyo upendo wa Mungu kwa binadamu. Mungu anaomba kupendwa na bi arusi, kama isemavyo zaburi "Nafsi yangu inakuonea kiu" (Zab 63:1). Mungu analihitaji pendo la binadamu.
Hivi Mungu anajisikia vibaya kulikosa pendo hilo kwa sababu binadamu ana “vidumu”, michepuko” na nyumba ndogo nyingi yaani miungu wengine anakoweza kwenda kujituliza anapojisikia kuchoka! Taabu kweli kweli! Mwanamke anamwuliza Yesu. "Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni Msamaria?" Hapa Mungu anaomba kupendwa na wakosefu. Kumbe Mungu anawahitaji wadhambi. Yesu anamjibu: "Kama ungelijua karama ya Mungu naye ni nani akuambiaye, 'Nipe maji ninywe,' ungalimwomba yeye, naye anagalikupa maji yaliyo hai." Hapa ndipo tunapoiona zawadi isiyo na uhusiano wowote na maji ya kisima. Yaani tunamwona anayeweza kutoa upendo usio na mipaka yaani mwenye kiu kweli ya Mungu. Mungu peke yake ndiye anayeweza kuizimisha kiu ya mahangaiko ya hapa duniani. Hatua ya kwanza ya kuzimisha kiu hiyo ni kujua kwamba upendo huo ni karama (zawadi) "Kama ungelijua karama ya Mungu." Yaani, jambo muhimu kwetu siyo lile tunaloliwania, bali ni lile tunalozawadiwa kama karama. Mathalani maisha, upendo, ufahamu wa maana ya maisha yetu, haya hatuwezi kuyapata kwa kuyawania kwa nguvu, bali tunakirimiwa na Mungu.
Kumbe, mwanamke huyu haelewi, kwa vile anawawakilisha wale wote wanaowania kuipata amani. Kisha Yesu anaendelea kusema kwamba: "Kila anywaye maji haya ataona kiu tena; walakini yeyote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele, bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele." Hata hivyo mwanamke huyu bado anafikiria kiu ya hapa duniani na anamtaka Mungu amtosheleze kibinadamu tu anaposema: "Nipe basi hayo maji..." Kwa vile mwanamke huyu alikuwa na “washikaji wengi” basi Yesu akaona amlipue, yaani Amtumbue kama jipu” kwa kumwambia: "Nenda kamwite mumewe. Kisha njoo hapa." Mwito huu wa Yesu kwa Mwanamke Msamaria asiye na jina unatuendea pia sisi sote. Kwani inawezekana unatangatanga kufuata dini hii au ile, au huna msimamo na familia au jumuiya yako hapo ujue ni msharatishaji yaani unafuata miungu mingine. Kumbe Yesu anakuambia: "Nenda kamwite mumeo." Yaani kila mmoja binafsi amfute Bwana arusi wake halisi. Yule mwanamke anajibu bila aibu: "Mimi sina Bwana." Yesu akamkubalia: "Umesema kweli. Umeshakuwa na wanaume watano. Na uliye naye sasa siyo bwana wako."
Yesu anakumbuka historia ya Wasamaria kwamba waliwahi kuyakaribisha mataifa matano ya kigeni pamoja na miungu yao ya kipagani. Mapato yake miungu hao wakasababisha malumbano na ushindani na Mungu wa kweli wa Waisraeli (IIWafalme 17). Hali ya kutoridhika na miungu hawa kwa Waisraeli inamithirishwa na ukahaba wa huyu Mwanamke Msamaria. Yesu anadokeza mbinu ya kukata makali ya kiu yao. Kwamba bila ya kukutana na Mungu huwezi kupata maji ambayo Yesu anayatoa. Ndiyo maana sasa mwanamke huyu anachomekea mada ya Hekalu ambapo ni pahala pa kukutana na Mungu. Kwa vyovyote mwanamke huyu alitaka kumaanisha Hekalu lile lililokuwa kwenye mlima Garizim. Yesu akamwambia: "Niamini mimi mwanamke." Kuamini maana yake ni kupenda, kujiaminisha kabisa. Aidha Yesu anamwita yule mama msamaria: "Mwanamke (mama)." Yesu alilitumia jina hili kwa mara ya kwanza alipomwita mama yake mzazi kwenye arusi ya Kana ya Galilaya: "Mwanamke (mama), tuna nini mimi nawe?"
Kwa lugha hii, Yesu anamwalika bi arusi wake yaani Mwisraeli kumwaminia bwana wake. Ndipo yule mwanamke anapotambua na kusema: "Naona wewe ni Nabii..." Yesu anamwitikia: "Mimi ninayesema nawe, ndiye." Kwa tamko hili unashuhudia waziwazi jinsi Bwana arusi anavyojitambulishwa kwa Bi arusi wake. Ndugu zangu, ikumbukwe hadi sasa mwanamke yule hakuwa amechota maji. Yesu anapomaliza tu kujitambulisha kuwa ndiye Bwana arusi wake, hapo yule mwanamke hahitaji tena maji ya kisimani. Anakaubwaga mtungi ule ukiwa mtupu bila maji na kwenda kijijini kwa sababu bi arusi ameshampata mpendwa wake.
Kwaresima njema!