Kanisa la Kisinodi: Upendo kwa Mungu na Jirani! Mshikamano!
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama! Somo la Injili ya leo, Mk 12: 38-44, linatuonesha Yesu akiwa hekaluni huko Jerusalemu, akiwa na mijadala mizito na ya moto na baadhi ya wakuu wa dini ya Kiyahudi, ndio Mafarisayo, Masadukayo, na Maherodi. Lakini leo Yesu haongei na makundi haya bali na makutano, ndio wale waliomfuata na kumsikiliza mafundisho yake. “Jihadharini na waandishi…” Ndio kusema Yesu anaona hatari ya tabia zile za waandishi inaweza kuwemo hata kati ya wanafunzi wake, ni hatari ya kuwa na dini ya nje, dini ya maumbile, dini ya kutaka kuabudiwa na wengine, ni dini ya maonesho kwani haitoki ndani. Labda yafaa japo kwa ufupi kuwafahamu hawa waandishi ni akina nani haswa. Katika dini ya Kiyahudi, waandishi walikuwa ni watalaamu wa Sheria za Mungu. (Esdra 7:11) Na ni hawa walikuwa na wajibu wa kutafsiri sheria na hata kusimamia sheria na kutoa hukumu katika mahakama.
Kwa kuwa ni watu wenye nafasi katika jamii, hivyo waandishi walipenda pia kuvaa mavazi yaliyoweza kuwatofautisha na watu wengine wa kawaida. “Wapendao kutembea wamevaa mavazi marefu…” Ni kwa njia ya mavazi waliweza kutambulika kirahisi na hivi kupata heshima na sifa maalumu. “…na kusalimiwa masokoni, na kuketi mbele katika masinagogi, na viti vya mbele katika karamu.” Waandishi walisalimiwa sio kwa salamu rahisi tu ya “shalom!”, bali mmoja alipaswa kuinamisha kichwa ili kumsalimu, kubusu mikono na kukaa kimya kumsikiliza kwa heshima kubwa na adabu. Waandishi walipenda kujionesha kuwa ni watu wa daraja na hadhi ya juu tofauti na wengine katika jamii na dini yao. Watu waliamini kuwapa heshima hiyo ilikuwa ni sawa na kumtukuza Mungu, na ndio tunaona Yesu anawaonya na kuwapa tahadhari kubwa wanafunzi wake kujiepusha na dini ya maumbile, ndio ile ya maonesho na kujichukulia nafasi ambayo si yetu bali ni ya Mungu mwenyewe. Yesu daima anatualika sisi sote kuwa ni ndugu, kamwe tusiingie katika kishawishi cha kujiona wa muhimu au wa pekee kuliko wengine.
Na ndio mwaliko wa Kanisa la Kisinodi, ndio Kanisa linalotembea pamoja, kila mmoja ni ndugu katika Kristo Yesu kwa kushiriki Ubatizo ule mmoja. Ni Kanisa ambalo sisi sote tunashikana mikono na kutembea pamoja katika utakatifu. Kanisa la Kisinodi ndilo lile lililoasisiwa na Yesu Kristo tangu mwanzo. Ni Kanisa linalojali na kumsikiliza kila mmoja, ni lile linalokuwa na roho ya kujadiliana kwa upendo, kuthaminiana bila kuweka madaraja na matabaka baina yetu, iwe katika familia zetu, jumuiyani, maparokiani na kadhalika na kadhalika. Kishawishi chochote kile kinachotutoa kuishi kama Kanisa la Kisinodi, basi hatuna budi kukiepuka na kuchukua tahadhari kubwa kama anavyotualika Yesu Kristo katika Injili ya leo. “…ambao hula nyumba za wajane.” Mzaburi anatuonesha wajane, mayatima, wageni ni watu ambao Mungu mwenyewe anawalinda na kuwakinga. (Zaburi 146:9) Hivyo kamwe wasitendewe isiyo haki na sawa. “BWANA huwahifadhi wageni; Huwategemeza yatima na mjane.” Wanakula nyumba za wajane, ndio kusema wanawatumia wajane walio wanyonge na wasio na mtetezi katika kuwadhulumu na kujinufaisha nao.
Na ndio mantiki ya ulimwengu wetu wa leo, kuwatumia na kuwaonea wanaokuwa wanyonge na wasio na sauti kwa ajili ya masilahi binafsi. Yesu anatuonya leo kuwa macho na hivyo kuwa na tahadhari katika namna zetu kwa wajane na walio wanyonge katika jamii. “…na kwa unafiki husali sala ndefu.” Ndio kusema sala zao haziakisi matendo na maisha yao. Sala ya kweli ni ile inayoakisi maisha yetu, ni urafiki wa kweli mbele ya Mungu na hivyo kwa jirani. Kusali daima ni kuingia katika mahusiano ya ndani kabisa na Mungu, ni kukiri na kuuonesha upendo na imani yetu kwa Mungu, hivyo daima ni mwaliko wa kuyafananisha maisha yetu na kile tunachokiamini. Maisha ya Mkristo yanapaswa kuwa taa na chumvi kwa wengine, yalete mwanga panapokuwa na giza na ladha pale penye kukata tamaa na matumaini. Sala ya kweli ni kuingia ndani mwetu na kubaki na Mungu anayetaka kuongea na nafsi ya kila mmoja wetu.
Sehemu ya pili ya Injili ya leo, inatuonesha kinyume na dini ile ya maonesho ya waandishi, tunakutana na mmoja anayekuwa ni mfano wa kweli wa mtu anayempenda Mungu na jirani, na huyu ndio mama mjane. Mara kadhaa Mwinjili Marko anatuonesha jinsi Yesu anavyoguswa na imani ya wanawake kadhaa. Mwanamke aliyekuwa na shida ya kutokwa na dam una kugusa vazi la Yesu ili apokee uponyaji wa kweli. (Marko 5:34) “Akamwambia, Binti, imani yako imekuponya, nenda zako kwa amani, uwe mzima, usiwe na msiba wako tena.” Na hata mwanamke wa Kigiriki wa kabila la Msirofoinike anafika na kumwomba binti yake aweze kuponywa na mapepo na Yesu anaguswa na imani ya mama yule. (Marko 7:24-30) “Akamwambia, Kwa sababu ya neno hilo, nenda zako, pepo amemtoka binti yako.”
Mwinjili Marko anatuonesha si tu wanawake wenye imani, bali pia anatuonesha imani ya mjane aliyefika kutoa sadaka yake hekaluni. Mjane anakuwa kielelezo kwa kila mmoja wetu anayekuwa mwanafunzi na mfuasi wa Yesu Kristo. Ni upendo kamili bila kujibakisha, ndio upendo wa kujisahau mwenyewe kwa kuwa tunampenda kweli Mungu. Mwanamke yule mjane hatusikii wala kuambia zaidi habari zake, na hivyo hatuna hakika kama alikuwa mfuasi wa Yesu Kristo, lakini moja kwa hakika Yesu anamchukua na kumweka mbele yetu leo kama kielelezo cha ufuasi wa kweli. Ni kielelezo cha imani na upendo wa kweli. (Mathayo 6:1-4) “Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni. Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu. Amin, nawaambieni, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kulia; sadaka yako iwe kwa siri; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.”
Sifa ya upendo wa kweli ni ile ya kutokujibakisha, ni kujitoa mzima mzima bila kijihurumia, bila kujali kwanza mambo yako mwenyewe. Ndio kama tulivyosikia katika somo la Injili ya Dominika iliyopita, juu ya “Shemah Israeli”, “nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.” Marko 12:30 Ni kupenda bila kujibakiza si tu kwa Mungu bali Yesu anatualika kuwapenda pia na jirani. Na ndio mwaliko wa Kanisa la Kisinodi, linaloongozwa na moto wa upendo kwa Mungu na kwa jirani. Kumuona Mungu kupitia wengine, kwani kila mwanadamu anabeba sura ya Mungu bila ubaguzi wala matabaka ya aina yeyoye ile. Mjane yule tunasikia kuwa alikuwa na senti mbili, ndio kusema angeliweza kutoa moja na yeye kubaki na moja mfukoni kwa ajili yake. Mjane yule hakujijali wala kujibakiza kwa ajili yake, kwani tunasoma alitoa sio ziada kama matajiri na wengine, bali yote aliyokuwa nayo.
Ndio kusema kila mmoja wetu hata kama tunakuwa ni maskini kiasi gani, tunaalikwa kupenda kama mjane wa somo la Injili ya leo. Ndio kuwa na upendo usiogawanyika, upendo kamili usiokuwa na masharti yeyote yale. Mjane ni kielelezo cha upendo wa Mungu kwetu, upendo ambao tunaalikwa kuutafakari katika saa ile ya pale Kalvari, ambapo Mungu anajitoa kamili kuwa sadaka isiyo na doa kwa ajili ya Wokovu wa ulimwengu mzima. Mungu anajitoa mzima mzima, hajibakishi kwa ajili ya mwanadamu na basi tunaalikwa kuomba neema za kuwaka upendo huo wa Kimungu maishani mwetu. Kila mmoja wetu kama Wanakanisa na hasa tunaposafiri katika kutafakari Kanisa la Kisinodi, hatuna budi kujibidisha kuishi kweli za Injili, maisha yetu na hata namna zetu za kufikiri kuakisi na kuongozwa na Neno la Mungu. Kila mmoja anaalikwa kuwa zawadi kwa wengine pasi na kujibakisha, pasi na kufungwa na roho za choyo na ubinafsi na umimi. Dominika na tafakari njema! Mshirikishe pia jirani yako, ili wote tutembee pamoja katika mwanga wa Neno la Mungu!