Tafakari ya neno la Mungu Dominika ya IV ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Wito wa Unabii na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. Tafakari ya neno la Mungu Dominika ya IV ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Wito wa Unabii na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. 

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 4 Mwaka C: Wito wa Kinabii Na Changamoto Zake!

Nabii ni mjumbe wa Mungu kwa watu anayewaeleza mawazo na mapenzi ya Mungu kama anavyotumwa na Mungu. Lakini pia Nabii ni mjumbe wa watu kwa Mungu (Hab.1,3). Mjumbe huyu anateuliwa na Mungu “nimekuweka kuwa nabii kwa mataifa” (Yer.1:5). Kwa ubatizo kila mmoja anashirikishwa unabii, ukuhani na ufalme wa Kristo. Kila mwamini atimize wajibu wa wito wake.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 4 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii ni tafakari ya wito wa kinabii. Itakumbukwa kuwa Nabii ni mjumbe wa Mungu kwa watu anayewaeleza watu mawazo na mapenzi ya Mungu kama anavyotumwa na Mungu. Lakini pia Nabii ni mjumbe wa watu kwa Mungu (Hab.1,3).  Mjumbe huyu anateuliwa na Mungu “nimekuweka kuwa nabii kwa mataifa” (Yer.1:5). Kwa ubatizo kila mmoja anashirikishwa unabii, ukuhani na ufalme wa Kristo. Kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu wake kadiri ya wito aliomjalia Mungu kwa upendo ili kwao yeye mwenyewe aweze kutakatifuzwa kwa kazi anayoifanya. Somo la kwanza kutoka kitabu cha Nabii Yeremia (Yer 1:4-5,17-19), ni kuitwa kwa Yeremia kuwa Nabii. Katika somo hili tunaona jinsi mpango wa Mungu kwa Yeremia ulivyoanza. Ni Mungu ndiye aliyemuumba, akamwita, akamchagua hata kabla hajaumbwa katika tumbo, na kabla ya kuzaliwa alimtakasa, na kumweka wakfu kuwa Nabii wa Mataifa. Kazi ya kinabii kwa Yeremia ni kwa Mataifa yote ya dunia: “Nimekuweka kuwa Nabii wa Mataifa” (Yer 1:5).

Nabii Yeremia anaogopa mpango huu wa Mungu: Ee, Bwana Mungu! Tazama, siwezi kusema, maana mimi ni mtoto!” (Yer 1:6).  Mungu anamwimarisha na kumtia nguvu: Usiogope, nipo pamoja nawe, utanena yale nitakayokuamuru kwani nimetia maneno yangu kinywani mwako. Kumbe tunaona kuwa wito ni zawadi toka kwa Mungu anayemwita na kumchagua mwanadamu hata kabla ya kuzaliwa kwake. Mtume Paulo naye anashuhudia: “Lakini Mungu aliyenitenga tangu tumboni mwa Mama yangu, akaniita kwa Neema yake, alipoona vyema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa Habari zake, mara sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu” (Gal 1:15-16). “Nimekuweka uwe Nuru ya Mataifa, upate kuwa wokovu hata mwisho wa dunia” (Mdo 13:47). Katika kumwita Yeremia, Mungu anamwambia kuwa atapata upinzani na mateso mkali. Ni kweli Yeremia alipata mateso na upinzani mkali kutoka kwa familia yake, viongozi wa dini, viongozi wa serikali na hata kwa watu wengine wakimshutumu kwa uasi, uhaini, na usaliti. Yeremia alitupwa jela na baadae kupelekwa uhamishoni Misri.

Wito wa unabii una changamoto zake
Wito wa unabii una changamoto zake

Kuna nyakati ambazo Yeremia alikataa tamaa na kutaka kuacha kazi aliyopewa na Mungu, kama anavyoshuhudia mwenyewe: “Nami nikasema, sitamtaja, wala sitasema tena kwa Jina lake.” Lakini uaminifu wake kwa Mungu ulikuwa ni kichocheo cha kusonga mbele. “Basi ndipo moyoni mwangu kumekuwamo kama moto uwakao, uliofungwa ndani ya mifupa yangu, nami nimechoka kwa kustahimili, wala siwezi kujizuia” (Yer 20:9). Hapa tunaona kuwa Roho wa Mungu alimwongoza Yeremia kuelezea wito wake na majaribu yake kama ashirio la yale yatakayompata Bwana wetu Yesu Kristo - mateso na kifo chake. Kumbe ujumbe wa Mungu kwa Yeremia, ulimlenga Yesu Kristo kuliko Nabii mwenyewe ndiyo maana katika Injili tunaona anakataliwa na watu wa nyumbani kwake mwenyewe. Kila mkristo kwa Sakramenti ya ubatizo anashiriki unabii, ukuhani na ufalme wa Kristo. Hatupaswi kuwa na mashaka, woga na wasiwasi katika kuusimamia ukweli. Kupambana na mafisadi, kutetea haki kwa wanyonge, kuushuhudia ufalme wa Mungu. Katika kutenda kazi ya Mungu, kushindwa au kufaulu hakupimwi kwa vigezo au viwango vya kibinadamu. Bali ni Mungu mwenyewe anayejua jinsi ya kutathimini kazi zake. Tunapoitwa na Mungu, tusiogope, bali tujikabidhi kwake, tuseme na kufanya kile tu anachotuamuru. Na ujumbe wa Yeremia ni wazi, hakuna kazi yoyote inayotendwa kiaminifu inayoishia kupotea bure.

Somo la pili la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor 12:13-31,13), linasimulia Wakristo Wakorintho walivyofarakana na kutokuelewana wao kwa wao. Hii ni kwasababu kila mmoja alijiona ni wa maana Zaidi kwa karama alizonazo na kusahau kuwa amejaliwa kwa upendo wa Mungu na anapaswa kuzitumia kwa upendo kwa faida ya wengi. Mtume Paulo anasisitiza kuwa, kunena kwa lugha, kuwa nabii na kujua siri zote na maarifa yote, kuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kutoa mali ili kuwalisha maskini, kuutoa mwili uungue moto, kama huna upendo, haikufaidii kitu. Kila tendo au jambo jema lisipotangulia na upendo halifai machoni pa Mungu. Paulo anatoa sifa za upendo - upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote. Upendo haupungui neno wakati wowote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma, yakiwapo maarifa, yatabatilika. Tuombe basi fadhili ya upendo ili kila neno na tendo tunalofanya liongozwe nao ili kufaa mbele za Mungu kwa ajili ya sifa na utukufu wake ili nasi tutakatifuzwe nao.

Katika Injili kama ilivyoandikwa na Luka (Lk 4:21-30), Yesu anakataliwa na watu wa kijijini kwake kuwa ni Nabii, Kuhani na Mfalme. Sababu kuu ya kumkataa na kutomwamini ni ni kumfahamu yeye, ndugu zake na wazazi wake na kumzoea kumwona kuwa ni mtu wa kawaida asiyestahili kuwa nabii, kuhani na mfalme. Sababu nyingine ni yeye kuwaambia ukweli kuwa Mungu hana upendeleo. Kila mtu mbele ya Mungu ana hadhi ya pekee na anastahili kupokea neema na baraka zake. Hata sisi tunawezakuwa na mzaoea ya kupokea Ekaristi Takatifu na kuona kitu cha kawaida na pengine tunadharau hivyo hatuoni kuwa kutokupokea Ekaristi Takatifu kama ni tatizo. Hali hii ni kumkataa Kristo katika maisha yetu. Hata katika maisha ya kawaida viongozi wa dini, siasa au serikali wanaweza kudharauliwa kwa sababu tu wanafahamika wao mwenyewe na ya familia zao: wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wao. Watu wanajua hali zao za kiuchumi, kiwango cha elimu yao na mengine kama hayo. Kwa sababu tu ya mazoea, labda wamesoma nao au kucheza nao basi inakuwa sababu ya kudharauliwa. Mwingine anawezakuwa anaheshimika sana katika jamii au ofisini anakofanya kazi; akifika wote wanamsalimia kwa heshima na wanampenda; lakini ndani ya nyumba yake hana heshima iwe kwa mke wake, mme wake au watoto. Hii ni kwa sababu wamekaa naye sana wanajua mapungufu yake na wanamdharau kwa sababu hiyo.

Waamini wawe waaminifu kwa wito wao
Waamini wawe waaminifu kwa wito wao

Katika hali hii kiongozi yeyote anapaswa kutambua kuwa yeye ni chombo cha Mungu na amtegemee yeye kwa yote kwa kuwa kazi anayoifanya sio yake ni ya Mungu naye asipoifanya kadiri ya mapenzi yake yeye mwenyewe atakuadhibu. Kumbuka alivyomwambia Ezekieli “Basi, wewe mtu, nimekuweka kuwa mlinzi wa Waisraeli. Utakaposikia neno kutoka kwangu utawapa onyo langu. Nikimwambia mtu mwovu: “Wewe mtu mwovu hakika utakufa”; lakini wewe husemi chochte ili kumwonya yule mtu mwovu aachane na mwenendo wake; mtu huyo hakika atakufa kwa kosa lake; lakini nitakudai wewe kifo chake. Lakini ukimwonya mwovu aachane na mwenendo wake mbaya, naye haachani na mwenendo wake mbaya, yeye atakufa kwa kosa lake; lakini wewe utakuwa umeyaokoa maisha yako” (Eze.33:7-9). Ndivyo Paulo alivyomuasa Timotheo “…hubiri huo ujumbe, sisitiza kuutangaza (iwe ni wakati wa kufaa au wakati suofaa), karipia, onya na himiza watu ukiwafundisha kwa uvumilivu wote (2Tim.4: 2).

Kiongozi yeyote yule daima anapaswa kumtegemea Mungu; usiogope hata ikionekana watu hawapendi kusikiliza ujumbe unaowatangazia. Kumbuka ahadi za Mungu kwa watu wanaofanya kazi yake: “Bwana anazijua siku za wakamilifu, na urithi wao utakuwa wa milele. Hawataaibika wakati wa ubaya, na siku za njaa watashiba (Zab.37:18-19). “Heri yenu ninyi watu wakiwatukana na kuwadhulumu na kuwasingizia kila aina ya uovu kwa ajili yangu. Furahini na kushangilia maana tuzo lenu ni kubwa mbinguni. Hivyo ndivyo walivyowadhulumu manabii waliokuwako kabla yenu” (Mt.5:11). “Nao watapigana nawe lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe…ili nikuokoe (Yer 1:19). Basi tumwombe Mungu atujalie neema zake ili Kristo aliye nasi tusimzoee mno mpaka kupuuza Umungu wake, na kumfukuzia mbali.

Dominika 4 mwaka C
27 January 2022, 07:39