Katika kipindi hiki cha wasi wasi na hofu kuu kuhusu vita, mwaliko kwa watu wote wa Mungu ni toba na wongofu wa ndani, ili kujikita katika njia ya haki, amani na maridhiano. Katika kipindi hiki cha wasi wasi na hofu kuu kuhusu vita, mwaliko kwa watu wote wa Mungu ni toba na wongofu wa ndani, ili kujikita katika njia ya haki, amani na maridhiano. 

Tafakari Dominika III Kwaresima Mwaka C: Madhara ya Dhambi

Leo hii dunia imegubikwa na hofu na wasiwasi mkubwa tangu baada ya kusikia vita ya taifa la Urussi kuivamia nchi ya Ukraine huko Ulaya ya Mashariki. Ni vita inayotuweka wengi kwenye wasiwasi mkubwa si tu juu ya hatima ya mataifa hayo mawili, bali hata mustakabali wa dunia nzima mintarafu amani na ustawi wa wote. Toba na wongofu wa ndani ni muhimu sana kwa wote

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Leo dunia imegubikwa na hofu na wasiwasi mkubwa tangu baada ya kusikia vita ya taifa la Urussi kuivamia nchi ya Ukraine huko Ulaya ya Mashariki. Ni vita inayotuweka wengi kwenye wasiwasi mkubwa si tu juu ya hatima ya mataifa hayo mawili, bali hata mustakabali wa dunia nzima mintarafu amani na ustawi wa watu wote. Leo hakuna namna au sababu yeyote ile inayoweza kuhalalisha vita iwe kati ya mataifa, kati ya jamii na jamii, au familia na familia au mtu na mtu na hasa kwetu tunaoongozwa na Neno la Mungu. Neno la Mungu linatualika kusamehe na kupenda kama Mungu anavyotusamehe na kutupenda, na hapo tunaona hakuna kosa hata liwe kubwa kiasi gani linalozidi huruma na msamaha wa Mungu. Dhambi kubwa ni kuamini kuwa kuna dhambi inayoweza kushinda huruma na msamaha wa Mungu. Ni wito wetu wa kuwa wajumbe na mashahidi wa huruma na upendo wa Mungu kwa watu wote ulimwenguni. Pamoja na kukosa sababu za kuhalalisha vita, bado tunajiuliza maswali mengi yatokanayo na vita, na hasa mateso na mahangaiko makubwa yanayowapata watu wasiokuwa na hatia wala kosa lolote. Kwa nini Mungu anaruhusu vita na matukio ya namna hii? Zaidi sana kwa nini mateso na mahangaiko katika maisha ya mwanadamu, iwe yatokanayo na vita, au maradhi, au kupungukiwa kwa kila hali? Kwa nini haya yote mabaya na maovu katika maisha ya mwanadamu?

Hili ni swali ambalo limedumu na kumsumbua mwanadamu sio tu wa kale bali hata katika nyakati zetu leo. Kwa nini Mungu muweza ya yote anaruhusu maovu na mabaya kutokea katika maisha yetu? Je, kwa nini Mungu mwema anaruhusu tupatwe na maovu/mabaya wakati anatupenda upeo na wema wake hauna kipimo? Na zaidi sana kwa nini mateso na mahangaiko yamkute mtu asiye na hatia, mtu mnyofu na hata wale ambao ni wachamungu? Ni maswali tafakarishi na nikiri kuwa ni maswali ambayo si rahisi hata kidogo kupata majibu yake kwa kutegemea tu akili na mantiki za kibinadamu. Ni maswali yanayotualika kuyatafakari kwa neema za msaada wake Mungu mwenyewe, ni kwa msaada wa Mungu tunaweza kulitafakari fumbo la mateso katika maisha ya mwanadamu. Ni kutokana na swali hili, wapo wengine wamefikia hitimisho la haraka na kusema, hakuna Mungu kwa kuwa kuna mateso na mahangaiko ulimwenguni. Na wengine wanakiri uwepo wa Mungu lakini wakijaribu kuutilia mashaka wema na ukuu na uweza wake; Mungu yupo lakini sio mwema kiasi kile tunachofundishwa na kufunuliwa na Neno lake na yawezekana hana uwezo wote, kiasi anashindwa kuzuia tusipatwe na maovu au mabaya maishani. Kwa watu hawa Mungu anapoteza sifa ya ubaba kwani kwao anaonekana kama ni mtawala tu mwenye mipaka na ukomo katika wema na uwezo wake, kwa kushindwa kuondoa fumbo la mateso duniani.

Dhambi ni kiini cha mateso na mahangaiko ya watu
Dhambi ni kiini cha mateso na mahangaiko ya watu

Katika somo la kwanza la leo kutoka Kitabu cha Kutoka, Mungu anaona mateso ya watu wake na hivyo kujifunua kwa Musa pale mlima Horebu, ili awatoe watu wale katika utumwa na mateso. Musa ni malaika kwa maana ya mjumbe wa Mungu na kwa historia yake daima ni mtu aliyekuwa anaguswa na kuumizwa na mateso ya watu wake. Sasa Mungu anamwalika na kumuonesha jinsi ya kufanya tofauti na ile ya awali kabla ya Mungu kujifunua kwake Musa. Hivyo sote tunaalikwa kila mmoja kwa nafasi yake kuwa malaika wa Mungu, kuwa mjumbe wa Mungu wa kujenga ulimwengu wa haki duniani kwa njia na jinsi ile anayotuongoza Mwenyezi Mungu katika Neno lake. Kama ambavyo mimi na wewe mara nyingi hujawa na mashaka katika kutimiza maagizo ya Mungu, ndivyo naye Musa leo katika somo la kwanza anasema; “Mimi ni nani hata nimwendee Farao na kuwatoa wa Israeli nchini Misri?”  (Kutoka 3:11) Na si aliona mashaka kwa upande wake bali hata kwa Mungu anayemtuma na hivi kumuuliza Mungu ili ajitambulishe.

Tunaona Mungu hajitambulishi kwa jina au nomino ya kawaida bali kwa nomino kitenzi yaani, “EYEH au HYH/HJH” kwa Kiebrania na kwa Kiswahili likimaanisha “MIMI NDIYE NILIYE – MIMI NI UWEPO WENYEWE”. Nikiri kwa upande wangu ugumu wa kutafsiri jina la Mungu. Mt. Tomaso wa Akwino ndio anajaribu kutuonesha kuwa Mungu sio mmoja kati ya vingi vilivyopo bali ni uwepo wenyewe. Vitu vipo kwa kuwa Mungu yupo! Tupo kwa kuwa Mungu yupo, bila uwepo wa Mungu hakuna chochote ambacho kipo kingepata uwepo wake. “Ipsum divinum esse. It is the divine act-of-being itself which is the essence or nature of God. WHO IS – He, whose essence is to exist, God is sheer existence per se. God is simple, in him there is no distinction between his essence and his existence, between what he is (quidditas) and that he is. God is this simple reality whose very quidditas is to be, and who grounds the to-be of every creature. To be God is to be to-be. God is not, for Thomas Aquinas, ‘a’ being, one thing among many, however ontologically impressive. It is invalid, he says, to refer to God as an ‘individual’. For this reason. Thomas uses the expression ipsum esse subsistens (the subsistent act of to-be itself) to describe God.

Kwa upande mwingine kabla ya Mt. Tomaso wa Akwino tunaona Mt. Agustino pia alijaribu kuelezea jina la Mungu kuwa na maana ya “Yule asiyebadilika”, Mungu ni wa milele, jana, leo na siku zote. Umilele ni kuwa nje ya muda (Kronos), hivyo Mungu habanwi na mipaka ya mahali wala wakati, kwani ni nje ya mahali na nyakati, ni wa milele, kwani kwake hatuwezi kuzungumzia muda, ndio kusema jana au leo au kesho, kwani ni sasa isiyogawanyika na kupimika kwa namna yeyote ile. Nikiri kwa unyenyekevu mkubwa kabisa nia na lengo langu sio kuingia katika kuanza kunyambua kwa undani jina la Mungu, kwani hilo haliwezekani maana ni hanc sublimen veritatem - Ni ukweli ulio juu ya uweza wetu wa kibinadamu. Ila itoshe kuona kuwa Mungu sio mmoja aliyepo kati ya wengi bali ni uwepo wenyewe. Tupo kwa sababu Mungu yupo na hivyo uwepo wetu hauna budi kuongozwa daima na sababu au asili ya uwepo wetu yaani Mungu mwenyewe. Na hivyo kamwe katika maisha yetu hakuna nyanja au aina fulani ya maisha bila kumuhusisha Mungu mwenyewe, iwe katika maisha ya mtu binafsi, kifamilia, au kijamii au kisiasa au kiuchumi na hata kidini.

Na ndio kwa ukuu wa jina la Mungu wana wa Israeli hawalitamki Jina hilo hata pale wanaposoma Maandiko Matakatifu, na ndio hata nasi tunavyoalikwa leo kutokutaja bure jina la Mungu. Hivyo wakatumia majina mengine kama ADONAI (BWANA – EDONAI). Nasi hatuna budi kutolitamka bila sababu maalumu jina la Mungu wetu, na hata tunapopaswa kulitamka basi tufanye hivyo kwa moyo wa ibada na heshima kuu. Hivyo jina la Mungu, la yule ambaye yupo, ndio kusema daima anabaki na watu wake, anabaki nasi daima katika nyanja zote za maisha kama nilivyotangulia kusema hapo juu. Mungu wetu si yule anayebaki tu mbinguni na kuangalia madhambi yetu, asiyeguswa na shida na mahangahiko yetu. Bali ni Mungu anayesafiri nasi kila siku na hivi kutovumilia uonevu au ukosefu wa haki kati ya watu wake bali anakuja kutukomboa. Na ndio tunaposoma Maandiko Matakatifu hatuoni kwamba wana wa Israeli walimlilia Mungu kwanza, ila ni Mungu aliguswa na mateso na shida zao. Wao walilia kwa mateso na shida zao bila kumwelekea Mungu ila Mungu bado anaguswa na kuingilia kati na kuwatoa katika mateso ya utumwa na uonevu. Na ndio Mungu daima anatutumia kila mmoja wetu kama malaika au mjumbe wake ili kujenga familia, jamii na dunia yenye haki na upendo na amani. Kamwe asitokee mmoja wetu kujitenga na wajibu huo kutoka kwa Mungu mwenyewe ila daima tuongozwe sio kwa mantiki za ulimwengu huu bali kwa njia ya Neno na maongozi yake ya Kimungu.

Katika Somo la Injili sehemu ya kwanza tunaona kuna matukio mawili ya kihistoria yaani Wagalilaya waliouawa na Pilato pale hekaluni, na wale kumi na nane walioangukiwa na mnara wa Siloamu wakafa. Wanahistoria wanajaribu kutuonesha kuwa Pilato hakuwa mtu mwema na Injili ya leo inathibitisha hilo kwa kuwaua hao Wagalilaya.  Yawezekana kabisa Wagalilaya hawa walifika kutoa sadaka zao za wanyama hekaluni wakati wa sherehe za Pasaka ya Kiyahudi wanapokumbuka kukombolewa kwao kutoka utumwa wa Misri. Ni nyakati za sikukuu kama hizi Pilato alihama kutoka mji wa Kaisaria na kuja katika jiji la Yerusalemu hasa kwa ajili ya kulinda amani na utulivu. Yawezekana kabisa Wagalilaya hawa walionesha kuwa wao ni watu huru, na hivyo kupinga utawala wa Kirumi. Hivyo, Wagalilaya wale walihukumiwa kwa kesi ya uasi kwa watawala wa kigeni. Hekaluni ni mahali patakatifu, ni mahali penye uwepo wa Mungu kwa namna ya pekee na hivyo hata makuhani walipaswa kutembea miguu peku ila tunaona Pilato anawaua hapo hekaluni hao Wagalilaya. Hivyo kuua watu hekaluni ilikuwa ni kufuru na kulinajisi hekalu.

Hakuna vita vya haki wala halali, amani inapaswa kutamalaki.
Hakuna vita vya haki wala halali, amani inapaswa kutamalaki.

Swali linabaki kwa nini Yesu hatumsikii akiwakalipia waliofanya kitendo hicho kiovu kutoka upande wa watawala? Mafarisayo walikuwa na mtazamo wao kuwa hakuna adhabu bila kosa. Kama Mungu ameruhusu hawa Wagalilaya kuuawa basi walikuwa wadhambi kwa hakika. Lakini kwetu leo sio rahisi kukubali mtazamo au muono wa aina hii. Ni wazi kosa la wazi ni kwa Pilato na maaskari wake wa Kirumi kwa kitendo kile cha kuwaua Wagalilaya na mbaya zaidi hekaluni. Tunaona baadhi wanafika kwa Yesu kumueleza kilichojiri. Labda walitegemea kutoka kwa kinywa cha Yesu hukumu na kulaani kitendo kile, au kuonesha waziwazi kuwa kinyume na utawala ule dhalimu wa Kirumi. Katika muktadha wa kukufuru na kunajisi kiasi hiki walitegemea Yesu kuwasihi si tu Wagalilaya wenzake bali Wayahudi wote kuwa kinyume na utawala ule wa Kirumi na labda hata kufanya mapinduzi ya kivita ili kuwaondoa katika mji ule mtakatifu na nchi yao ya ahadi. Kinyume chake tunaona Yesu anawashangaza wasikilizaji na wale waliofika kumpa habari hiyo ya kusikitisha na kinyume na dini yao. Na pia anabadili mtazamo ule wa mafarisayo kuwa kama wamekufa basi walikuwa wadhambi. Na badala yake Yesu anatumia nafasi na fursa hiyo kuwaalika katika uongofu, kubadili namna zao za kufikiri na kuishi: “…msipotubu mtaangamia kama wao”.

Mabaya au mateso yanayotupata maishani kamwe sio laana kutoka kwa Mungu, kwani kufikiri namna hiyo ni sawa na kukufuru. Nawaalika kuepuka kabisa namna hiyo ya kufikiri kwani leo Yesu anatuonesha mabaya au mateso au kifo sio laana kutoka kwa Mungu. Na zaidi Yesu pia anatumia wasaa huo kuwapa pia mfano wa kihistoria wa wale watu kumi na wanane waliokufa huko kwa kuangukiwa na mnara wa Siloamu. Kadiri ya Yesu watu wale walikufa kwa ajali na si kwa sababu ya dhambi zao, hivyo wangeliweza kupatwa na maswahiba yale hata watu wengine katika muktadha ule ule bila kujali hali zao za ndani.  Na hivyo hata tukio hilo Yesu analitumia kuwaalika na kutualika nasi leo kutubu yaani kubadili vichwa kwa namna za kufikiri na kuenenda. Yesu anatuonesha kilicho cha hatari sio kifo au mateso au mabaya bali ni kuwa mbali na Mungu na hivyo kutualika kufanya toba, na huu ndio wito na mwaliko wa Kwaresma na maisha yote ya ufuasi. Kwa juu juu tunaweza kusema mbona leo Yesu hatoi majibu kwa mauaji yale ya Kirumi? Wasikilizaji wake walimfahamu kwa hakika kuwa hakuwa mtu muoga na hivyo kwa nini leo hatoi majibu tarajiwa kwa upande wao na hata kwetu pia? Kadiri ya mantiki ya ulimwengu huu, ukatili na mauaji ya namna ile hujibiwa pia kwa njia ya nguvu na mabavu au kifupi kijeshi, yaani ubaya kwa ubaya, uovu kwa uovu. Lakini Yesu leo anatualika kubadili vichwa vyetu, hivyo utumiaji wa mabavu au nguvu au kisasi, kamwe sio suluhisho la ukosefu wa haki na amani na upendo duniani kwani daima zinaongeza chuki na mipasuko na magomvi kati yetu.

Mwaliko na jibu la Yesu ni kutubu, ni kufanya mabadiliko ya ndani ya maisha! Ndio mwaliko kwa kila mmoja wetu wakati huu wa Kwaresima, ni kufanya toba. Ni kuacha njia zile ovu na kumrudia Mwenyezi Mungu. Ni kwa kufanya toba ya kweli na kubadili vichwa vyetu kwa maana ya jinsi ya kufikiri na kuenenda kamwe hatuwezi kuujenga ufalme wa Mungu wa upendo, haki na amani hapa duniani. Hivyo jawabu la matatizo ya mwanadamu leo katika ulimwengu ni kufanya toba ya kweli. Iwe katika familia zetu, katika jamii zetu, katika ulimwengu ule wa kisiasa na kiuchumi, sote tunaalikwa kutubu na kukubali kuongozwa na Neno la Mungu. Hivyo kinyume na Wayahudi walioona njia pekee ni kutumia mabavu, au kisasi au chuki dhidi ya waonevu, tunaona Yesu anatoa suluhisho tofauti, yaani TOBA kwa wote. Hivyo anatualika kung’oa mzizi wa uovu ndani yetu. Ni kubadili maisha yetu na kuongozwa na Neno la Mungu hapo tunaweza kuwa na ulimwengu wenye upendo, haki na amani, yaani ufalme wa Mungu. Na ndio tunaona jibu la Yesu kwa Pilato ni jibu kwa kila mmoja wetu yaani kufanya toba ya kweli na ndio kubadili namna zetu za zamani na kuanza kuongozwa naye. Metanoia ya kweli ni kukubali kubadili vichwa vyetu, namna zetu za kufikiri na kuenenda, ndio kuachana na mantiki ya ulimwengu huu na kuanza kuongozwa na ile ya Mungu mwenyewe.

Amani ya kweli inasimikwa katika toba na wongofu wa ndani.
Amani ya kweli inasimikwa katika toba na wongofu wa ndani.

Ndio kusema Yesu anatuonesha leo kilicho kibaya katika maisha ya mwanadamu sio mateso au ugonjwa au kifo au kupungukiwa na badala yake ni kuendelea kuishi katika uovu, katika maisha ya dhambi. Mateso na mahangaiko katika maisha ya mwanadamu sio matokeo ya laana, au adhabu kwa kuwa tumetenda dhambi, kwani kuwaza namna hiyo ni sawa na kumkufuru Mungu aliye upendo na huruma yenyewe kwetu. Moja ambalo tunapaswa kulifanyia kazi na kuhangaiko nalo ni kuwa mbali na Mungu, ni kuendelea kuishi maisha ya dhambi na sio mateso au mahangaiko mengine ya maisha. Mateso, kifo au maradhi sio adhabu, na ndio tunaona Yesu anajaribu kutuonesha nini tunapaswa kufanya, ndio toba ya kweli, mabadiliko ya ndani ya maisha yetu, ya mahusiano yetu kwa Mungu na kwa jirani. Kinachoangamiza maisha ya mwanadamu sio kifo au maradhi au kupungukiwa bali ni maisha ya dhambi na ndio Yesu anatualika leo kufanya toba, toba maana yake ni metanoia, ndio kuuvua utu wa kale na kuuvaa utu mpya. Ni kuvua akili na kichwa cha kale na kuvaa kichwa kipya, yaani, kuenenda kadiri ya Neno la Mungu kwa maongozi ya Mungu Roho Mtakatifu.

Dunia leo inapitia kipindi kigumu, ni matokeo ya mwanadamu anayeshindwa kufanya mabadiliko ya ndani na ya kweli, ndio metanoia ya kukubali kuongozwa na mantiki ya Mungu kwa kuivua ile ya ulimwengu huu. Mantiki ya ulimwengu huu ndio ile inayotutaka kutawala wengine, kuwamiliki wengine, kulipa ubaya kwa ubaya, uovu kwa uovu. Labda swali linakuja ni kwa muda gani tunaweza kuongoka au kubadili vichwa vyetu ? Jibu la swali hilo linajibiwa katika sehemu ya mwisho ya Injili ya leo kwa mfano wa mtini au fiki. Katika Biblia tunaona mara nyingi mtini ukizungumziwa kama mti ambao ulitoa matunda yake matamu na mazuri mara mbili kwa mwaka.  Hivyo mtini ulijulikana kama ishara ya mafanikio na amani. (1Wafalme 4:25; Isaya 36:16). Wakiwa jangwani wana wa Israeli walikuwa na njozi ya kuwa na nchi yenye chemichemi ya maji, hivyo nchi yenye kustawi ngano na mitini. (Kumb 8 : 8 ; Hesabu 20 :5) Hivyo ujumbe wa Injili upo wazi kuwa kila anayesikiliza Neno lake na kulishika basi huyo hakika atazaa matunda mengi na mema. Na ndio matendo ya upendo na huruma.

Tofauti na Wainjili wengine wanaozungumzia juu ya mtini usiozaa ambao Yesu aliamuru unyauke na kusinyaa mara moja (Marko 11:12-24 na Matayo 21:18-22). Mwinjili Luka anayejulikana sana kwa mada ya Huruma ya Mungu, anazungumzia juu ya kuupa mwaka mwingine wa kulimwa na kupaliliwa kabla ya kuukata.  Hivyo anatuonesha sura ya Mungu mwenye huruma kwa watu wake anayejua ugumu wa mioyo na akili zetu, hivyo daima anatupa muda wa kufanya toba ili kubadili namna zetu na hivyo kuanza kuzaa matunda. Hivyo mfano huu ni mahususi kwa kipindi hiki cha Kwaresma, kwani ni kipindi cha neema (Kairos) kwetu ili kuweza kufanya toba ya kweli na ndio kubadili vichwa na maisha yetu ya kufikiri na kutenda. Daima Mwenyezi Mungu anasafiri nasi katika nyanja zote za maisha, hivyo turuhusu kuongozwa naye ili tuweze kuzaa matunda. Nawatakia tafakuri njema na Dominika njema!

17 March 2022, 14:30