Fumbo la Pasaka ni kiini na chimbuko la Kanisa. Fumbo la Pasaka ni kiini na chimbuko la Kanisa. 

Dominika ya III ya Pasaka: Fumbo La Pasaka Chimbuko La Kanisa

Liturujia ya Neno la Mungu inaonesha kuwa Fumbo la Pasaka ndio kiini na chimbuko la Kanisa. Kanisa linapata nguvu yake na uhalali wake kutoka katika Fumbo la Pasaka. Masomo yanaonesha nafasi ya Kristo katika maisha ya mwamini. Kwa maana Kristo habaki huko juu juu katika nadharia bali Kristoo Yesu huingia na kuyagusa maisha ya kila siku, tunayoita maisha ya kawaida.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Dominika ya tatu ya Pasaka. Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu dominika ya tatu ya Pasaka. Ni masomo ambayo kwa upande mmoja yanatuonesha kuwa Fumbo la Pasaka ndio kiini na chimbuko la Kanisa. Kanisa linapata nguvu yake  na uhalali wake kutoka katika Fumbo la Pasaka na si kutoka kwa mwanadamu au kutoka mfumo mwingine wowote ule. Na kwa upande mwingine masomo haya yanatuonesha nafasi ya Kristo katika maisha ya kila siku ya mwamini. Kwa maana Kristo habaki huko juu juu katika nadharia au katika mambo ya kufikirika bali Kristo huingia na kuyagusa maisha ya kila siku, tunayoita maisha ya kawaida, ya yule anayemwamini. MASOMO KWA UFUPI: Tunasoma somo la kwanza kutoka katika kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 5:27b-32, 43-52). Hiki ni kitabu ambacho tutakisoma katika dominika zote za Pasaka kwa sababu ndicho kinachotupa picha ya uhalisia wa kanisa la mwanzo na utume wa mitume baada ya ufufuko wa Yesu. Katika somo la leo, mitume wanafikishwa katika baraza kuu la wayahudi. Baraza hili tunaweza kulifanaisha na mahakama kuu ya nchi. Baraza hili lilikuwa chini ya kuhani mkuu kwa sababu kazi yake kubwa ilikuwa ni kusimamia Torati. Mitume wanafikishwa huko kwa sababu awali walikuwa wamekatazwa kuhubiri habari za Kristo lakini wao waliendelea kumhubiri. Wanapohojiwa, Petro na mitume wanajibu bila hofu wala woga “imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.” Uhalali wa mafundisho ya kikristo na uhalali wa utume wa Kanisa, si zao la majadiliano ya nini kifundishwe na nini kisifundishwe kulingana na matakwa ya mwanadamu. Ni zao la utii kwa Kristo mwenyewe kwa maana ni nguvu ya Kristo mfufuka inayofanya kazi ndani ya Kanisa.

Kashfa ya Fumbo la Msalaba iliwakatisha tamaa Mitume wa Kristo Yesu.
Kashfa ya Fumbo la Msalaba iliwakatisha tamaa Mitume wa Kristo Yesu.

Somo la Pili ni kutoka Kitabu cha Ufunuo (Ufu 5:11-14 ). Mwandishi wa Kitabu cha Ufunuo akiwa bado hapa duniani anapata maono, anaona Liturujia ya mbinguni, yaani ibada inayofanyika huko mbinguni. Anachokiona ni kuwa watu wengi maelfu kwa maelfu wanamsujudia Mwanakondoo aliyechinjwa. Ni nani huyu mwanakondoo aliyechinjwa? Katika kitabu hiki cha Ufunuo, mwanakondoo ni alama ya Kristo. Kristo, aliyeteswa na kufa sasa ni mzima na ndiye anayeabudiwa katika liturujia ya mbinguni. Kuielewa vizuri Liturujia hii inabidi turudi nyuma kidogo ambapo tunasikia maneno anayoambiwa “wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu kinachofungwa kwa mihuri ya maisha na kuifungua mihuri yake kwa kuwa ulichinjwa na ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila, lugha, jamaa na taifa.” Kitabu kinachozunguziwa ni kitabu cha maisha. Ni mazingira ambapo watu wanaamini kuwa maisha yao na yote wanayoyapitia tayari yameandikwa na mtu hawezi kufanya chochote kile kujinasua katika yale yaliyokwishapangwa juu yake. Maisha ya mwanadamu yanaonwa kama kitabu kilichofungwa kwa mihuri ambayo mtu hawezi kuivunja. Mwandishi wa Kitabu cha Ufunuo anaonesha kuwa ni kwa njia ya Kristo sote tunawekwa huru. Ni yeye ambaye kwa kifo na ufufuko wake anastahili kukifungua kitabu hicho ili mtu asiishi kama yule ambaye tayari amekwisha hukumiwa bali kama yule ambaye anaitengeneza mwenyewe historia yake kulingana na anavyoishi. Ndio maana baadaye anaeleza kuwa wale watakatifu wanaoishiriki ibada hiyo ya mbinguni ni wale waliokubali kuyaosha mavazi yao katika damu ya mwanakondoo. Kristo mfufuka ni nguvu na tumaini la uhuru wa mwanadamu.

Tukiligeukia sasa somo la Injili, tunasoma tukio ambalo ni mara ya tatu Yesu kuwatokea wafuasi wake baada ya ufufuko (Yn 21:1-19). Katika tukio hilo mitume wamerudi kuvua samaki, hawajapata kitu usiku mzima, Yesu anawatokea anawaambia tupeni nyavu upande wa kulia. Wanafanya hivyo wanapata samaki wengi. Na idadi yao inatolewa kuwa ni 153. Kisha Yesu anamgeukia Petro na kumuuliza mara tatu “Je, wanipenda? Injili hii imepata tafsiri nyingi. Ni hapo tunaona ulivyo utajiri wa Neno la Mungu. Ni Neno linaloangaza nyanja nyingi za maisha ya mwanadamu. Tuziangile tafsiri mbili. Ya kwanza ni ile inayoiangalia Injili hii kama Injili inayolizungumzia Kanisa. Kitendo cha Mitume kwenda kuvua samaki kinachukuliwa kama tendo la uinjilishaji ambalo Kanisa linafanya. Na ni kweli kwa sababu Yesu alimwambia Petro “nitakufanya uwe mvuvi wa watu”. Mitume wanaokwenda kuvua samaki usiku  ni  alama ya Kanisa linalojipambanua kuinjilisha kwa bidii yake binafsi bila mwanga ambaye ni Kristo. Linakesha bure na halipati kitu. Linapomsikiliza Kristo na kutupa nyavu upande wa kulia, yaani kwa kutegemea nguvu ya Mungu, linapata samaki wengi: 153 ni namba inayowakilisha watu wa mataifa yote. Kristo haishii hapo, anawaandalia kifungua kinywa alama ya mlo wa Kiekaristi ili kwa fumbo hilo la Ekaristi Kanisa liendelee kuitambua na kuitegemea nguvu ya Kristo ndani yake. Swali kwa Petro “Je, wanipenda” ambalo Kristo analirudia mara tatu, pamoja na agizo “chunga kondoo wangu” linakuwa ni alama ya ukuu wa Petro katika Kanisa. Yeye anawekwa kama halifa anayeliunganisha kanisa chini ya Kristo na kulinda imani inayojidhihirisha katika mafundisho, maadhimisho ya Liturujia na maisha adili.

Fumbo la Pasaka ni kiini na chanzo cha maisha na utume wa Kanisa
Fumbo la Pasaka ni kiini na chanzo cha maisha na utume wa Kanisa

Tafsiri ya pili ni ile inayosisitiza ufufuko kama nguvu mpya katika maisha ya wafuasi. Hapa tunaona kuwa baada ya kifo cha Kristo, Mitume wa Yesu ni kama wamekata tamaa. Kila mmoja amerudia kazi aliyokuwa anaifanya kabla ya kuitwa na maisha yanaendelea kama kawaida kana kwamba hawakuwahi kuitwa wala kumjua Kristo. Ni kama watu waliomsahau Kristo lakini Kristo hajawasahau. Na hapa anawatokea katika siku mbaya huenda kuliko zote, siku ambayo wamekesha wakifanya kazi lakini hawajapata kitu. Anaambatana nao na kwa neno lake anatenda muujiza katika shughuli yao ya uvuvi. Wanapata samaki aina zote 153 zinazofahamika. Kwa tendo hilo Kristo anawadhihirishia kuwa hajafa, yu mzima. Anawapa nguvu ya kuianza upya safari yao ya utume baada ya kupitia kipndi cha kukata tamaa. Swali kwa Petro “Je, wanipenda” ambalo Kristo analirudia mara tatu linakuwa ni alama ya kukiri upya imani sio tu kwa Petro alimkana Yesu mara tatu bali  ni kiri ya imani kwa matendo ya Mtakatifu Petro na hivyo kuruhusu kipindi cha giza kifute yote ambayo alikuwa amepitia pamoja na Kristo Yesu. Ni hapo anapopokea wito wake “chunga kondoo wangu” ili aianze tena upya safari ya ufuasi. Ni hapa Injili hii inatuonesha kuwa huwezi kujiita mfuasi kamili wa Kristo ikiwa upo naye kipindi cha utukufu peke yake. Mfuasi kamili wa Kristo ni yule anayedumu katika imani hata katika zile nyakati za giza, nyakati ngumu ambazo hamuoni Kristo katika maisha yake.

TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tunachota nini kutoka katika masomo ya dominika hii ya tatu ya Pasaka? Binafsi ninaguswa kutafakari kitendo cha Petro na wanafunzi wengine kutawanyika baada ya kifo cha Yesu. Ni kitendo kinachowakilisha hali inayoweza kumtokea mfuasi yoyote wa Kristo na katika wakati wowote. Hali ambapo mkristo anakosa kuona thamani na mantiki ya imani yake na kujikuta anarudi nyuma na tena wakati mwingine anarudi nyuma zaidi ya hata kule alikokuwa kabla ya kuanza safari ya imani. Inaweza kutokea kwa sababu ya makwazo ya kiimani, inaweza kutokea kwa sababu ya misukosuko ya kimaisha: ugonjwa usiopona, kifo cha mtu wa karibu na hata wakati mwingine kukosa motisha hasa kwa wale walio na nafasi mbalimbali za huduma au uongozi. Sababu zipo nyingi. Masomo ya leo yanakuja kutukumbusha kuwa aliyetuita ni Kristo. Ni Kristo na si mwingine. Na yeye hata kama haonekani kwa macho, haonekani pale tunapomwitaji n.k, yeye yupo daima katika maisha yetu na katika safari yetu ya imani na ya utumishi. Hatuna sababu ya kurudi nyuma kwa sababu ufuasi wetu una thamani kubwa kwake.

Liturujia D3 Pasaka
29 April 2022, 16:59