Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Matawi. Mwanzo wa Juma Kuu: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Matawi. Mwanzo wa Juma Kuu: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. 

Dominika ya Matawi: Kilele Cha Maisha Na Utume wa Yesu: Ukombozi

Kristo Yesu ni Mfalme wa utukufu anayeingia Yerusalemu; ndiye Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana. Kuingia kwa Kristo Yesu mjini Yerusalemu kunaonesha ujio wa Ufalme wa Mungu: Wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ufalme wa haki, mapendo na amani. Mama Kanisa anakumbusha kwamba, maisha ya kila kiumbe yanaelekea kwenye hatima yake, yaani ufunuo wa Kristo.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

UTANGULIZI: Dominika hii tunaingia katika Juma Kuu la Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo ambapo kilele cha mateso hayo ni kifo chake msalabani, kifo ambacho alikipokea kama sadaka ya ukombozi wetu na wa ulimwengu mzima. Adhimisho linalotuingiza katika Juma hili Kuu ni adhimisho la dominika ya Matawi. Hili ndilo adhimisho tunalokwenda kulitafakari katika kipindi chetu cha leo. Masomo kwa ufupi: Kabla ya kuyapitia masomo ya Misa, ni muhimu tuiangalie kwanza mantiki ya kile tunachokiadhimisha katika dominika hii. Katika dominika ya Matawi tunaadhimisha kuingia kwa Yesu katika mji wa Yerusalemu. Tukio hili linapata umuhimu wa pekee kwa sababu ni katika mji huu wa Yerusalemu ambapo Yesu anakwenda kukamilisha kile kilichomleta duniani. Alikuja ili kumkomboa mwanadamu. Tendo la kumkomboa mwanadamu linakamilika Yerusalemu kwa ishara za kipasaka ambazo ni mateso, kifo na ufufuko wake. Masimulizi ya utume wa Yesu ambayo tunayapata katika Injili, yanatuonesha pia kuwa Yerusalemu ndio kilele cha utume wa Yesu. Tukiangalia kwa mfano Injili ya Marko, tunaona kuwa mafundisho na yote aliyoyafanya Yesu aliyafanya akiwa njiani kuelekea Yerusalemu. Injili ya Luka ambayo ndiyo tunayoitafakari mwaka huu, yenyewe inaonesha wazi zaidi mpangilio huu pale inapoyapanga matukio ya Yesu kama safari ya kutoka Bethlehemu alipozaliwa kwenda Yerusalemu atakapojitoa sadaka msalabani. Maandamano mafupi tunayoyafanya katika adhimisho la Matawi ni maandamano ambayo pia yanaakisi dhamira hii ya Yesu kuingia katika kilele cha utume wake hapa duniani.

Kanisa lina mshangilia Kristo Mfalme wa amani, haki, upendo na mshikamano
Kanisa lina mshangilia Kristo Mfalme wa amani, haki, upendo na mshikamano

Liturujia inaadhimishwa kwa njia ya ishara na alama mbalimbali zinazotoa maana ya fumbo linaloadhimishwa. Kuna ishara ya maandamano, ambayo tumekwisha itaja na alama kama vile mwanapunda, matawi na kiitikizano “hosana, hosana mwana wa Daudi”. Kuingia mahala kwa maandamano ni kitendo kinachoonesha ukuu. Mtu wa kawaida hahitaji kutanguliwa na maandamano. Ukuu wa Yesu unaotambuliwa leo ni ufalme wake, ndiyo maana anaitwa mwana wa mfalme Daudi. Yesu anatambuliwa kama yule anayekuja kuanzisha enzi mpya ya ufalme duniani. Ufalme wake lakini ni ufalme wa amani na kanuni yake ni upendo na sio mabavu. Ndiyo maana anatumia mwanapunda na si farasi mnyama wa vita aliyetumiwa na wafalme wa duniani. Tunamwimbia “hosana, hosana” neno la kiyahudi linalomaanisha “utuokoe”. Kwa utenzi huo tunamsifu, tunamtukuza na kumtambua Yeye kuwa ndiye wokovu wa ulimwengu. Tukirudi sasa katika masomo ya Misa, tunaona kuwa yote kwa pamoja yanatufafanulia fumbo la mateso ya Kristo katika wokovu wa mwanadamu. Somo la kwanza kutoka katika kitabu cha Nabii Isaya (Is 50:4-7) ni kifungu kinachojulikana kama wimbo wa mtumishi wa Bwana. Karibu miaka 600 kabla ya Kristo, Isaya anapaza sauti ya mtumishi ambaye anajitoa kuyakabili mateso kwa hiari yake tu. Isaya anayazungumza haya katika wakati ambapo wale anaowapa ujumbe huu wako utumwani Babeli, wamechoshwa na mateso wanayoyapata na wanakaribia kukata tamaa wakisema Mungu amewaacha na hayuko nao tena. Kinaonekana ni kitu cha ajabu kabisha. Wakati mmoja anaugulia mateso, mwingine anasema hayo mateso mimi ninajitolea kuyapata. Anachokitabiri Isaya ni ujio wa mtumishi atakeyeuonesha ulimwengu kuwa mateso anayoteseka mwanadamu akiwa na Mungu ni njia ya wokovu.

Wokovu wa mwanadamu umetundikwa juu ya Msalaba
Wokovu wa mwanadamu umetundikwa juu ya Msalaba

Katika somo la Pili (Fil 2:6-11), Mtume Paulo anaakisi fundisho la nabii Isaya akimuonesha Kristo kuwa ndiye mtumishi yule wa Bwana ambaye kwa utii wake alikuwa tayari kuyakabili mateso. Yeye aliyekuwa yu namna ya Mungu, hakuona kuwa kule kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kujishikamanisha nacho. Akajishusha, akawa mwanadamu, tena akatii na kwa hiari yake akajitoa afe msalabani ili awe wokovu kwa wote wanaomtumainia. Somo la Injili, ndilo linalokuja kutupatia kile kilichotokea wakati Yesu alipokubali kuyapokea mateso yake. Tunasoma Historia ya Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo kadiri ya mwinjili Luka (Lk 22:14-23:56), historia ambayo inaanza kwa maandalizi ya sherehe ya pasaka ya wayahudi na kujumuisha matukio yote ya Yesu kukamatwa, kuhojiwa, kuteswa, kufa msalabani hadi kuzikwa. Fundisho la pekee la historia ya mateso kadiri ya mwinjili Luka ni kuwa kifo cha Yesu ni kifo cha mtu mwenye haki asiye na hatia. Na anayeshuhudia hilo ni akida, yaani Jemedari wa kijeshi aliyesimamia kusulubishwa kwa Yesu. Ndiye anayekiri “hakika mtu huyu alikuwa mwenye haki” (Lk 23:48). Kifo cha Yesu kama kifo cha mtu asiye na hatia ni fundisho lenye maana sana kwa wafuasi. Linaonesha ubora wa sadaka aliyoitoa kwa hiyari na hapo hapo linawafundisha wafuasi namna ya kupokea fumbo la mateso katika maisha yao wenyewe kama kushiriki mateso ya Kristo kwa wokovu wao na wa ulimwengu.  

TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tukizingatia kuwa dominika hii ya Matawi ni dominika inayotuingiza katika juma la maadhimisho ya mafumbo makuu ya wokovu wetu, ni vizuri katika tafakari ya leo tukaangalia kwa undani nafasi ya mateso na kifo cha Yesu katika fumbo la wokovu wetu. Masomo yenyewe ya leo yametuonesha kuwa Kristo ameingia katika mateso na kifo chake kwa utashi wake kama mtumishi wa Bwana aliyetabiriwa na nabii Isaya. Tena ameyapokea mateso na kifo si kwa sababu alikuwa na hatia, la! Amekubali kuteseka na kufa akiwa hana hatia na akiwa ni mwenye haki. Hiyo yote ni kutuonesha siri kuu ya mpango wa Mungu wa wokovu wetu. Mpango huo wa Mungu usioeleweka wala kuelezeka ipasavyo kwa lugha ya kibinadamu unafafanuliwa na Maandiko Matakatifu kwa lugha inayochukua mifano na taswira mbalimbali ambazo mwanadamu anaweza kuzielewa ili kwa kupitia hizo aweze kulifikia fumbo hili kuu. Tunasoma hasa katika barua za Mtume Paulo ambapo anaelezea kifo cha Kristo kuwa, kwanza ni kwa ajili ya mwanadamu, pili ni ukombozi na tatu ni upatanisho wa mwanadamu na Mungu wake (Rum 3:24-25, 2Kor 5:19, Ef 2:4-10 n.k). Kifo cha Kristo kuwa ni kwa ajili ya wanadamu kinabeba tafsiri kuwa Kristo amekufa kwa niaba ya wanadamu na pia amekufa kwa manufaa au kwa faida ya wanadamu.

Juma kuu Kanisa linatafakari mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu
Juma kuu Kanisa linatafakari mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu

Tukija katika ukombozi, awali ya yote, dhana ya ukombozi kimsingi ni dhana ya kivita inayotoa picha ya mateka wa kivita ambapo wale waliowakamata mateka wanahitaji kutimiziwa masharti fulani ili wawachie huru. Mwanadamu naye kwa dhambi alikuwa ni mateka wa Ibilisi. Sasa haimaanishi kwamba Kristo kwa kifo chake alitimiza masharti ya Ibilisi ili mwanadamu aachiwe huru. Dhana hii ya ukombozi inapotumiwa kwa Kristo inaonesha kuwa mwanadamu katika hali yake ya kuwa mateka wa dhambi hakuwa na uwezo wowote wa kujiokoa mwenyewe. Alihitaji nguvu kutoka juu na nguvu hiyo ilikuja kwa njia ya kifo cha Kristo. Upatanisho wenyewe unamgusa Mungu moja kwa moja kama vile ukombozi ulivyomgusa mwanadamu moja kwa moja. Kwa dhambi, mwanadamu aliipoteza hadhi yake mbele ya Mungu na asingeweza tena kustahili kumkaribia. Mtume Paulo anasema kwa dhambi, mwanadamu “alipungukiwa na utukufu wa Mungu” (Rum 3:23). Kifo cha Kristo kimemrudishia mwanadamu ile hadhi na utukufu aliokuwa ameupoteza na kumstahilisha kusimama mbele ya Mungu. Kumbe, Kifo cha Kristo ni ujio wa neema na nguvu kutoka juu, kifo cha mwanadamu kimefuta hatia ya dhambi ya mwanadamu na kifo cha Kristo kimemstahilisha mwanadamu kusimama mbele ya Mungu kwa kumrudishia hadhi na utukufu alioupoteza kwa dhambi zake. Na huu ndio wokovu aliotuletea Kristo kwa mateso na kifo chake, wokovu tunaouadhimisha katika Juma hili Kuu la Pasaka. Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, ninakutakia maadhimisho mema ya Juma Kuu, Mungu na aamshe ndani yetu neema ya wokovu kwa njia ya maadhimisho haya makuu tunayoyashiriki katika Juma hili.

Liturujia ya Matawi
08 April 2022, 11:58