Tafuta

Tafakari ya neno la Mungu, Sherehe ya Huruma ya Mungu inakita ujumbe wake kwenye Sakramenti ya Upatanisho na Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu, chemchemi ya Sakramenti za Kanisa. Tafakari ya neno la Mungu, Sherehe ya Huruma ya Mungu inakita ujumbe wake kwenye Sakramenti ya Upatanisho na Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu, chemchemi ya Sakramenti za Kanisa. 

Sherehe Ya Huruma Ya Mungu: Sakramenti na Madonda Matakatifu

Yesu anawavuvia Roho Mtakatifu wafuasi wake, na hivyo kuwapa uwezo wa kuwaondolea watu dhambi zao. Pasaka ni sherehe ya kuonja huruma ya Mungu, Mama Kanisa anatualika katika Dominika hii ya pili ya Pasaka kutafakari Huruma ya Mungu kwetu. Sehemu ya pili ni ile ya Mtume asiyeamini bila kuona na kugusa madonda yake ndiye Tomaso aliyejulikana pia kama Pacha.

Na Padre Gaston George Mkude, Roma.

Kristo amefufuka kweli kweli, Aleluiya! Somo la Injili Takatifu ya leo, Sherehe ya Huruma ya Mungu, Yn 20:19-31 imegawanyika katika sehemu kuu mbili, kwanza ni Yesu anawavuvia Roho Mtakatifu wafuasi wake, na hivyo kuwapa uwezo dhidi ya uovu na yule mwovu, na ndio kuwaondolea watu dhambi zao. Hivyo Pasaka ni sherehe ya kuonja huruma ya Mungu, na ndio leo Mama Kanisa anatualika katika Dominika hii ya pili ya Pasaka kutafakari Huruma ya Mungu kwetu. Sehemu ya pili ni ile ya Mtume asiyeamini bila kuona na kugusa madonda yake Yesu, ndiye Tomaso aliyejulikana pia kama Pacha. Kabla ya mateso, kifo na ufufuko wake, Bwana wetu Yesu Kristo anawafundisha wanafunzi wake kuwa Yeye ndio Uzima na Ufufuo. Hivyo baada ya ufufuko wake anapowatokea wanafunzi wake siku ile ya kwanza ya Juma anawadhihirishia waziwazi mitume wake kuwa kweli ni mzima, na kuwasalimu kwa kuwatakia amani nafsini mwao baada ya kujawa na hofu na mahangaiko mengi baada ya kushuhudia mateso na kifo cha Bwana na Mwalimu wao. Ni kweli yeye mzima, amefufuka na mauti hayana tena nguvu dhidi yake! Ufufuko ni ushindi dhidi ya mauti na dhambi, ni ushindi wa upendo na huruma ya Mungu dhidi ya uovu na muovu. Pasaka ni tangazo la upendo na huruma ya Mungu kwa ulimwengu mzima. Pasaka ni Habari Njema kwetu tunaokimbilia huruma na upendo wa Mungu!

Huruma ya Mungu ni jina jingine na utambulisho wa Mwenyezi Mungu
Huruma ya Mungu ni jina jingine na utambulisho wa Mwenyezi Mungu

Kristo mfufuka anawapa zawadi ya Pasaka Mitume wake kwa kuwavuvia Roho Mtakatifu. Ni kwa uwezo wa Roho Mtakatifu wanapokea uwezo wa kusamehe dhambi, kuwa wagawaji wa huruma ya Mungu kwa watu wake, na ndio kwa msamaha wa dhambi nasi tunapata kushiriki uzima wa kweli, yaani maisha ya urafiki na neema, maisha ya kuunganika na Mungu. Zawadi ya Pasaka sio tu kwa Mitume wale wa mwanzo bali kwa kila Mbatizwa, tunajaliwa huruma na upendo wa Mungu kwetu. Furaha ya Pasaka si kitu kingine chochote bali kujaliwa huruma na upendo wa Mungu, kustahilishwa kuwa wana wa Mungu. Upande wa pili tunakutana na Mtume Tomaso, aliyejulikana pia Pacha kama kielelezo cha wale wote wanaopitia ugumu katika safari ya kuamini ufufuko wa Kristo. Hatujui kwa hakika kwa nini Mwinjili Yohane anamtumia Mtume Tomaso kama kielelezo, kwani kwa hakika ugumu ule haukuwa wa Mtume Tomaso peke yake bali tunasoma na kuona ni kwa wanafunzi wote wa karibu wa Bwana wetu Yesu Kristo.

Mwinjili Marko anathibitisha hilo pale anapotuonesha kuwa Kristo Mfufuka anawatokea mitume na kuwaonya juu ya kutokuamini kwao. (Marko 16:14) Mwinjili Luka naye anatuonesha kuwa Kristo Mfufuka anapowatokea mitume wake wanafadhaika na kuwa na uoga. (Luka 24:38) Mwinjili Matayo naye anatuonesha kuwa aliwatokea mitume wake katika Mlima Galilaya na bado baadhi yao walikuwa bado hawajaamini. (Mathayo 28:17) Hivyo kwa kuangalia Injili ndugu tunaona wazi kuwa wote walikuwa na mashaka ya kuamini, na hivyo siyo Tomaso mtume peke yake kama anavyotuonesha Mwinjili Yohane. Na ugumu huo hauishii nyakati zile za mitume wa mwanzo bali hata katika siku zetu leo. Mwinjili Yohane anapoandika Injili yake ni takribani mwaka 95 AD, na hivyo ni kitambo tangu Mtume Tomaso alipofariki kifo dini. Si lengo la Mwinjili Yohane kutuonesha au kutupa picha hasi ya imani ya Mtume Tomaso. Kwa makusudi mazima anapowaandikia kizazi cha tatu cha Wakristo, hivyo wengi wao kama si wote hawakumuona Kristo Mfufuka kwa macho yao, na hata hawakuwafahamu mitume waliokutana na Kristo Mfufuka. Hivyo kwao ilikuwa ngumu kuamini na wengi wao walibaki na mashaka makubwa juu ya ufufuko wake Kristo.

Sakramenti ya Upatanisho ni zawadi ya Kristo Mfufuka, ufunuo wa huruma ya Mungu
Sakramenti ya Upatanisho ni zawadi ya Kristo Mfufuka, ufunuo wa huruma ya Mungu

Mwinjili Yohane anawaandikia kizazi cha Wakristo ambao baadhi walikuwa na mashaka juu ya ukweli huu wa imani juu ya ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo. Injili ndugu zinatuonesha waziwazi kuwa mitume wote walikutwa na ugumu wa kuamini na hata baada ya kutokewa na Kristo mfufuka wengine walibaki na mashaka. Hivyo safari yao ya imani tunaona ni ngumu na ya kukatisha tamaa wakati fulani. Na ndio hapo tunaona Mwinjili Yohane anamtumia Mtume Tomaso kama kielelezo si kwake peke yake bali kwetu sote linapokuja swala la kuamini juu ya Kerygma ya Ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo. Kerygma ya ufufuko sio ukweli wa Kisayansi hivyo kuweza kudhibitishwa kwa njia za ufahamu wa akili zetu za kibinadamu, kuweza kushika na kuona kwa macho yetu ya kibinadamu au kuthibitishwa katika maabara zetu za Kisayansi. Ni lengo la Mwinjili Yohane kutuonesha kuwa Kristo mfufuka yu hai, ila si tena na mwili ule wa nyama bali sasa na mwili wa utukufu, na ndio maana tunaona mara kadhaa anawatokea wale watu wake wa karibu alioambatana nao kila siku na bado hawakuweza kumtambua. Kristo Mfufuka sasa ana mwili wa utukufu usioshikika wala kuonekana kwa macho ya kimwili bali tunaweza kuuona na kuushika kwa jicho la kiimani tu. Ni ukweli tunaoweza kuufikia kwa njia ya imani pekee!

Sisi leo tungeweza kusema heri wao waliomwona kwa macho Kristo Mfufuka, ila Kristo anabadili mantiki yetu ya kibinadamu kuwa heri wanaoamini bila kuona wala kugusa. Mwinjili Yohane anamtumia Mtume Tomaso mara kadhaa katika Injili yake kama mfano wa yule anayekuwa na ugumu katika kuelewa na kuamini katika mafundisho juu ya Kerygma ya Ufufuko. Wakati Yesu anapomjalia tena uzima Lazaro tunaona Mtume Tomaso anawaalika mitume wengine waende pamoja na Yesu ili wafe naye. (Yohane 11:16) Na hata katika karamu ya mwisho tunaona anapata shida kuelewa mafundisho ya Yesu kama Njia. (Yohane 14:5) Mtume Tomaso ni kielelezo anayemwakilisha kila mmoja wetu katika safari yetu ya imani. Mtume Tomaso pia ni kielelezo cha Wayahudi ambao daima walitaka ishara kadiri ya Mtume Paulo. (1 Wakorintho 1:22) Na hata Mwinjili Yohane anaonesha jinsi Yesu alipokuwa anawaonya wasikilizaji wake kuwa wasipoona miujiza na ishara kamwe hawataamini.

Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma ya Mungu
Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma ya Mungu

Baada ya safari ngumu ya imani kwa Mtume Tomaso tunaona mwishoni Mwinjili Yohane anatuonesha jinsi alivyoweza kukiri imani yake mbele ya Kristo Mfufuka. Na kwa kukiri Imani tunaona Mtume Tomaso ni mmoja mwenye Imani thabiti kabisa kwa Kristo mfufuka, na ndiyo anakiri juu ya Uungu wake Kristo. Anamtambua Kristo mfufuka kama Bwana na Mungu. Na ndio daima katika Agano la Kale tunaona Wayahudi wanamtambua Mungu kama Bwana wao. (Zaburi 35:23) Na ndio tunaona katika Kanisa leo sio tu mahali pa maskini na wagonjwa lakini pia kwa ajili ya hata wale wanaokuwa katika ugumu wa kuamini au wasio na imani, wenye mashaka na wasiwasi. Na ndio hao Mtume Paolo anawatambua kama wadhaifu ambao wanakwazika kirahisi hivyo hawana budi kusaidiwa na kuongozwa katika ukweli wote. Na ndio Mwinjili Matayo anawatambua kama watoto wadogo, hivyo hawana budi kulindwa na makwazo. Ni wajibu wetu leo kuwaongoza wale wanaokuwa wadogo na dhaifu ili nao wafikie kuamini katika Kerygma ya ufufuko wake Kristo. Imani ni safari, hivyo hatuna budi kusaidiana katika kuufikia ukweli huu.

Hitimisho la Injili ya Yohane anatuonesha sababu za kuandika Injili hii ya nne. Anatuambia kuwa anaandika baadhi tu ya ishara kwani kuna ishara nyingi alizofanya Yesu ila anatuchagulia baadhi tu kwa nia ya kutusaidia kufikia imani kwa Kristo Mfufuka. Ishara hizi daima zinamfunua Yesu kuwa ni Kristo wa Mungu, ni sura halisi ya Mungu, ni Bwana na Mungu wetu. Na ndio lengo la Injili daima kutusindikiza na kutusaidia kuufikia ukweli huo wa imani kama alivyoweza kufikia kukiri imani Mtume Tomaso au Pacha. Mtume Tomaso ni pacha wa kila mwamini, wa kila Mbatizwa anayekubali kwa unyenyekevu kusafiri katika safari ya imani na matumaini. Ni kwa kuwa katika umoja na jumuiya nzima ya Kanisa nasi daima tunakutana na Kristo Mfufuka na ndio makusanyiko yetu ya kila Dominika. Nje ya jumuiya kama Mtume Tomaso hatuwezi kukutana na Kristo Mfufuka. Ni katika Meza ya Neno lake na Ekaristi Takatifu nasi leo tunakutana na Kristo Mfufuka. Mtume Tomaso alipojitenga na jumuiya ile ya mitume au Kanisa lile la mwanzo hakika alikuwa mbali na imani. Na ndio nasi tunaalikwa kama Kanisa la Kisinodi kudumu katika jumuiya ya Mama Kanisa, kudumu pamoja katika tafakari ya Neno la Mungu na pia kwa kushiriki katika maisha ya Sakramenti ya Kanisa. Ni kwa njia ya kutembea kwa pamoja hapo tunakuwa na hakika ya kukutana na Kristo Mfufuka, ya kuweza kuonja huruma na upendo wa Mungu kwetu. Ni mwaliko wa kujikita katika dhana ya Kanisa la Kisinodi, ili kujenga ushirika, ushiriki na utume wa Kanisa tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Nawatakia tafakari njema na Sherehe njema ya Huruma ya Mungu. Pasaka njema!

 

 

20 April 2022, 16:07