Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Diominika ya 13 ya Mwaka C wa Kanisa. Wokovu na wongofu ni sehemu ya uumbaji mpya ndani ya mwamini. Tafakari ya Neno la Mungu, Diominika ya 13 ya Mwaka C wa Kanisa. Wokovu na wongofu ni sehemu ya uumbaji mpya ndani ya mwamini. 

Dominika ya 13 Ya Mwaka C: Wokovu na Wongofu wa Ndani

Uwepo wa Mungu katika nafsi na maisha yetu ubadili yote, ufanya yote mapya, tabia zetu, aina za maisha yetu, mitazamo yetu, hulka zetu, mahusiano yetu, na yote yanayokuwa kinyume na utakatifu wa Mungu. Wongofu na wokovu ni uumbaji mpya ndani mwetu, ili Kristo apate kujidhihirisha katika maisha yetu. Neema ya Mungu inakuja ndani mwetu ili kujaza utupu wa awali.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Moja ya ishara zitumikazo katika Torati kuonesha uwepo wa Mungu ni moto. (Kumbukumbu 4:24) Mungu ni moto ulao, na hata pale mlimani Sinai, Mungu anashuka katika umbo la moto, (Kutoka 19:18) na Neno lake kama moto. (Yeremia 5:14) Ishara ya uwepo wa moto ni kuteketeza hali ya kale na zamani ili kufanya yote upya. Uwepo wa Mungu katika nafsi na maisha yetu ubadili yote, ufanya yote mapya, tabia zetu, aina za maisha yetu, mitazamo yetu, hulka zetu, mahusiano yetu, na yote yanayokuwa kinyume na utakatifu wa Mungu. Wongofu na wokovu ni uumbaji mpya ndani mwetu, ni kuteketezwa kwa mtu wa kale ili Kristo apate kujidhihirisha katika maisha yetu. Kama vile uumbaji wa mwanzo ni ex nihilo, basi nasi neema ya Mungu inakuja ndani mwetu ili kujaza utupu wa awali. Haya ndiyo mawazo makuu yanayojitokeza katika Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 13 ya Mwaka C wa Kanisa. Katika Somo la Kwanza Nabii Elisha anapokea vazi kutoka kwa nabii Eliya, na kisha anatoka analitwaa lile jozi la ng’ombe na kuwachinja, anatokosa nyama yao na kuwapa watu wale, anaacha kazi yake ya awali, na hapo anakubali kuanza maisha mapya kama mjumbe wa Mungu. Katika Agano Jipya, Mitume baada ya kukutana na Yesu wa Nazareti na kuwaalika kumfuata wanaacha nyavu zao na kazi zao za awali na kuanza maisha mapya. (Luka 5:27).

Wito wa kumfuasa Kristo Yesu una changamoto nyingi, imani na matumaini ni muhimu
Wito wa kumfuasa Kristo Yesu una changamoto nyingi, imani na matumaini ni muhimu

Kila anayetaka kumfuasa Yesu hana budi kuuza vyote na kuanza maisha mapya ya ufuasi. (Luka 18:22) Maisha ya ufuasi ni kukubali na kuruhusu neema ya Mungu kuingia na kufanyakazi katika maisha yetu. Ni kukubali kufanyika na kuwa kiumbe kipya kadiri ya mantiki ya Mungu na Neno lake. Yesu amekuja ili kuleta na kuwasha moto ulimwenguni na ndio ujio wa Roho wa Mungu katika Kanisa lake. (Luka 12:49) Ni moto unaokuja kuchoma na kuteketeza yale yote yanayokuwa kinyume na wito wetu wa kuwa watakatifu kama Baba yetu wa Mbinguni alivyo Mtakatifu. Moto unaokuja kuangamiza na kutetekeza mtu yule wa kale ili mtu mpya, maisha ya neema yaweze kuchipuka ndani mwetu. Nabii Eliya, mjumbe wa Mungu ambaye maneno yake yalikuwa yanachoma kama moto anaishi katika kipindi kizuri kiuchumi na ustawi lakini pia ni wakati ambapo kumekuwa na kuporomoka kwa maadili na hata katika maisha ya kidini. Mfalme Akab anaoa mwanamke wa mataifa ya kipagani na hivyo analeta kati ya Taifa lile teule ibada za miungu wa Kipagani. Wote wanaomwabudu Mungu wa kweli wanateswa na ni katika mazingira hayo pia Nabii Eliya analazimishwa kutoroka.

Ni katika muktadha huo basi na ikiwa tayari Eliya akiwa ni mzee na aliyechoka anahitaji mrithi wake kama nabii kati ya watu wake, na ndio Mungu anamuonesha Elisha mwana wa Shafati wa Abel-Mehola, mtu tajiri aliyemiliki ardhi kubwa. Eliya anamkuta Elisha shambani mwa baba yake na hapo anamvisha joho lake bila kusema neno wala kugeuka kuangalia mwitikio wa Elisha. Nyakati zile joho lilikuwa sio tu vazi bali hasa liliwakilisha nafsi na nguvu na uwezo wa yule aliyelivaa. Elisha kwa mshangao mkubwa hasiti kupokea joho la Eliya na zaidi sana anamkimbilia Eliya na kumuomba ruhusa ya kwenda kuaga wazazi wake na Eliya anamkubalia na kumwambia akimaliza hilo basi arudi. Vazi au joho lilimwakilisha au kumtambulisha mtu. Kukubali vazi lile ni kukubali majukumu mapya. Elisha anafika nyumbani kwake na kutolea sadaka ikiwa ni ishara ya kukubali kuacha yote na kuanza maisha mapya. Wito wa Elisha ni ishara kwa kila aina ya wito tunayokuwa nayo katika Kanisa. Anayeitwa sio mtu asiyekuwa na kazi au uwezo au nafasi fulani muhimu katika jamii au familia yake, bali ni mtu anayekubali kwa hiari kamili kuacha yote ili kumtumikia Mungu. Kila mmoja wetu kwa kuwa mfuasi wa kweli anaalikwa kuacha maisha ya awali na kuanza maisha mapya, maisha ya kufanana na yule anayetuita, yaani Bwana na Mwalimu wetu Yesu Kristo.

Yataka moyo kuacha yote na kujiaminisha kwa Kristo katika maisha na utume
Yataka moyo kuacha yote na kujiaminisha kwa Kristo katika maisha na utume

Wakristo wa Kanisa la Galatia wameipokea Injili kwa hamu na shauku kubwa, lakini wakaanza kuvurugwa na baadhi waliofika kwao na kuanza kuwafanya waanze kushika sio amri ile aliyotuachia Yesu Kristo, yaani ya Upendo kwa Mungu na jirani, bali kwa kufuata mapokeo na sheria. Wao sasa sio watumwa tena bali ni watu huru kwa Kristo Yesu, maana yake sasa lazima kuongozwa na amri ya Agano Jipya nayo ni Upendo. Mahusiano na Mungu sio tena kama yale ya Bwana na mtumwa wake kwa kutii na kufuata kila amri na maagizo, ila sasa mahusiano yamejengeka juu ya upendo kama upendo ule wa bwana na bibi harusi. Imani yetu haina maana nje ya upendo kwa Mungu na kwa jirani. Ukristo ni mahusiano ya upendo kwa Mungu na jirani. Tunaalikwa kuishi kama wana wa Mungu, kuwa huru kwani sasa kuwa wafuasi au kuwa Wakristo sio kwa matakwa ya sheria bali kwa kuongozwa na upendo pekee. Rafiki akikualika umfuate kwa hakika tunamuuliza unaenda wapi? Yesu leo katika Injili anakaza uso wake na kuelekea Yerusalemu kutolea maisha yake.  Somo la Injili ya leo linabeba mawazo makuu matatu labda ni ngumu kuona uhusiano wa bayana kati yao. Wazo la kwanza ni safari yake kuelekea Yerusalemu, la pili ni kukosa kupokelewa kwake na Wasamaria na la tatu ni wito wa wale watu watatu tofauti.

Ili kuweza kuelewa vema Somo la Injili ya leo ni vema kukumbuka kuwa daima ufuasi kwa Kristo unaelezwa kama safari ya kumfuasa Kristo. Kuamini maana yake ni kukubali kushiriki nasi njia ile ile aliyopitia Bwana wetu Yesu Kristo. Na ndio tunaona waamini wa kwanza katika Kitabu cha Matendo ya Mitume kabla ya kuitwa Wakristo walijulikana kama “WATU WA NJIA”. (Matendo 9:2; 19:9, 23; 24:22) Yesu Kristo anajitambulisha kama njia, na hivyo maisha ya ufuasi ni kukubali kuwa safarini lakini tukizingatia kuwa njia yetu ni Yesu Kristo mwenyewe. (Yohane 14:6) Yote haya kwa Mwinjili Luka ni msaada mkubwa kutoa majibu kwa wale wanaokutwa na vipingamizi au magumu njiani. Na hata wale wanaotaka kujiunga katika njia hiyo. Hivyo katika Somo la leo tunaona muunganiko na mantiki kuwa ile safari ya kwanza ya Yesu kuelekea Yerusalemu ni safari pia ya kila mfuasi wa Yesu Kristo, na kutuweka wazi nyakati za kupingwa na kukataliwa tunapokuwa njiani. Mwinjili Luka ni mmoja anayewazungumzia daima kwa mtazamo chanya Wasamaria, ila katika Injili ya leo tunaona picha hasi kwani wanakataa kumpokea Yesu wanaposikia kuwa safari yake ni kuelekea Yerusalemu, kwa kweli kuna fundisho la katekesi nyuma yake.

Yesu anakaza uso wake, ni msemo kutoka Agano la Kale hasa kutoka Kitabu cha Nabii Isaya, Mtumishi wa Mungu anayeteseka, Anawim wa Mungu anakaza uso wake kama gumegume anapoelekea kutimiza misheni yake. (Isaya 50:7) Hivyo kama mtumishi yule anayeteseka pia Yesu anakaza uso wake kuelekea Yerusalemu mahali ambapo anatolea maisha yake pale juu msalabani kwa ajili ya wokovu wetu na ulimwengu mzima.  Haendi Yerusalemu ili kuyatafuta mateso bali anajua lazima apitie njia ile ya kudharaulika na kukataliwa na kuteswa na kufa pale juu msalabani ili alipe fidia ya dhambi na makosa yetu. Ni sawa kukubali kwa hiari kuzama matopeni na kubeba uchafu wote ili kukitoa kito cha thamani kilichozama matopeni, ni upendo wa ajabu wa Mungu kwetu wanadamu na kwa ulimwengu mzima. Mwenyezi Mungu anampenda kila mmoja wetu kana kwamba ni wewe tu au ni mimi tu nipo duniani! Ni upendo wa ajabu! Wokovu ni upendo wa Mungu kwa ulimwengu mzima! Anatuma wanafunzi wake kumtangulia Samaria na hapo wanakutana na upinzani, katika safari ya kumtangaza Kristo daima Kanisa linakutana na magumu na hata kukataliwa si tu katika nyakati zile bali hata katika nyakati zetu za leo. Injili inaendelea kupata upinzani hata katika familia zetu, mitaa yetu, jumuiya zetu, ndugu zetu na nchi na ulimwengu wetu.

Mitume wa Yesu wanakumbuka nyakati za Nabii Eliya ambapo aliomba moto ushuke na kuangamiza maadui zake (2 Wafalme 1:10-14) na hivyo wanaona hata sasa Yesu hana budi kufanya hivyo hivyo kuwaangamizi wanaompinga na kuipinga Habari Njema ya Wokovu. Hata Yohane Mbatizaji alitishia kuita moto. (Luka 3:9,17) ni kwa mantiki hiyo hiyo mitume nao wanataka moto ushuke uwaangamize Wasamaria Hii si tu mantiki ya wale wana wawili wa Zebedayo, bali wengi hata kati yetu wana Kanisa leo utasikia Mungu aangamize waovu na watenda maovu katika jamii zetu na hasa wale waokwenda kinyume na Injili au kulitesa Kanisa la Kristo kwa namna mbalimbali. Kwa kweli Mungu wetu hayupo hivyo, hatendi kwa mantiki ya ulimwengu huu kwani lazima kukumbuka kuwa Yeye ni Upendo na Huruma kamili hivyo kuchukia na kuangamiza ni kinyume na asili yake.  Najua ni mjadala mkubwa na mpana ila daima yafaa tubaki na sura ya Mungu kama alivyotufunulia Yesu Kristo mwenyewe na kamwe sio ile tunayoitaka na kuiunda sisi wanadamu kwa matashi na matakwa yetu, kinyume chake tunapotosha wengine. Tuepuke mafundisho yanayoenea leo yenye kufanya kufuru kwa Mungu, mafundisho ya laana na mengine yenye kufanana na hayo. Kamwe Mungu wetu halaani mwanadamu hata tukiwa wadhambi kiasi gani na badala yake anatualika kufanya toba na kumgeukia Yeye.

Waamini wamwombe Mungu neema ya kudumu katika wito na huduma.
Waamini wamwombe Mungu neema ya kudumu katika wito na huduma.

Wito wetu Wakristo si kuenenda kwa kulipa kisasi au kuangamiza au kuchukia bali daima kupenda. Moto pekee unaoshuka kutoka mbinguni ni Roho Mtakatifu, Roho ya Upendo wa Mungu anayegusa mioyo na kuifanya upya. Na huo ndio moto aliokuja kuuwasha ulimwenguni, ni Roho wake kubadili mioyo yetu na si kinyume cha hapo. Ni Mungu Roho Mtakatifu anayetufanya kumpenda Mungu na jirani bila masharti yeyote, iwe ni rafiki au ndugu na hata iwe adui na mpingani wa Injili. Huo ndio Upendo wa Kimungu! (Luka 12:49) Moto unaoshuka ni wa kufanya uumbaji mpya kama tulivyotangulia kuona hapo juu kuwa wokovu ni uumbaji mpya ndani mwetu. Ni kukubali kufanyika wapya kwa kuongozwa na Neno la Mungu katika maisha yetu. Ni kukubali kubadili vichwa vyetu kwa kuruhusu neema ya Mungu itawale na kuyaongoza maisha yetu. Ni kutokana na mtazamo wao huo tunaona wana wawili wa Zebedayo wanapata jina lingine kama wana wa radi. (Marko 3:17). Jina hilo pia linabebwa na kila mmoja wetu hata leo pale tunapowaza na kutenda kadiri ya mantiki ile ya wana wa radi. Hivyo hatuna budi kubadili na kukata vichwa vyetu na kuwaza sawa na Bwana wetu Yesu Kristo.

Mwinjili Luka pia anatuingiza katika wito wa watu watatu katika Injili ya leo wanaotaka kumfuasa Yesu. Na kila wito wa kila mmoja wetu unabeba katekesi tosha inayopaswa kuakisi maisha yetu kwani kila muumini Mkristo, ni mfuasi wa Kristo na hivyo tunaalikwa kumfuata/kumfuasa. Wa kwanza anamfuata Yesu akiwa njiani na kumwambia atamfuata popote atakapokwenda. Kwa haraka haraka tunaona utayari na upendo wake wa kumfuasa Yesu hata katika mazingira na nyakati ngeni kwake maana yu tayari popote na hivyo tungelitegemea Yesu kumpokea pia kwa ari na shauku kubwa. Kinyume chake Yesu anamuonya kuwa anayetaka kumfuasa hana budi kujua kuanzia mwanzo kuwa si rahisi, kwani kwake hakuna maisha marahisi, hana hata mahali pakulaza kichwa chake. Kwa maneno mengine Yesu anatualika kila mara kujihoji ufuasi wetu kwake. Je, kwa ajili ya kupata sisi au kujitoa bila kujibakiza kama Yeye alivyokaza uso wake kuelekea Yerusalemu kutolea maisha yake zawadi?

Jisadakeni kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu bila kukata tamaa.
Jisadakeni kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu bila kukata tamaa.

Anakutana na wa pili njiani na Yesu ndio anamwalika amfuate. Lakini huyu wa pili anaomba kwanza kwenda kuzika wazazi wake kabla ya kumfuata. Yesu anamwambia aache wafu wazike wafu wao. Kwa Wayahudi jibu hilo la Yesu ni makwazo makubwa kwani kama walivyoamriwa na Mungu kuwatii wazazi ili kujaliwa miaka mingi na heri duniani, amri hiyo iligusa pia wajibu mtakatifu wa wana kuzika wazazi wao. Kuzika wazazi kadiri ya marabi wa Kiyahudi ililegeza hata amri ile ya sabato na hivyo hata Kuhani Mkuu aliyekuwa amekatazwa kufika makaburini au kusogelea maiti lakini aliruhusiwa kuzika wazazi wake. Hivyo hatuna budi hapa kusoma na kuelewa kwa mtindo anaoutumia mwinjili Luka. Mwinjili Luka kwa kutaja wazazi, kwa Wayahudi ndio kusema mapokeo ya mababa. Hivyo kwa Mkristo anayekuwa tayari kumfuata Yesu kama tulivyosikia somo la pili la leo ni lazima kuanza maisha mapya kwani sasa amri kuu ni mapendo kwa Mungu na kwa jirani na si tena kuwa watumwa wa sheria na mapokeo ya kale.

Na wa tatu tofauti na pili aliyealikwa na Yesu amfuate tunaona yeye anamwambia Yesu nitakufuata lakini kwanza aende akaage wazazi wake, ni kama alivyofanya Elisha katika Somo la kwanza la leo. Hapa Yesu anaweka wazi kuwa kwa yeyote anayemfuata basi hana budi kumpa Yesu nafasi ya kwanza kabla ya kitu kingine chochote kile. Si kwamba Yesu anapinga mahusiano yetu na wazazi na ndugu na familia zetu ila daima lazima kukumbuka kuwa nafasi ya kwanza lazima kumpa kwanza Yeye kabla ya mengine yote. Na ndio amri ya kumpenda Mungu kwanza na hapo tunaweza kumpenda jirani.  Ni kwa kuunganika kwanza naye hapo mahusiano yetu mengine yote yanakuwa na afya. Chimbuko la mahusiano ya kweli yanapata uhalali na kibali kwa kuanza kujihusianisha na Mungu kwa nafasi ya kwanza. Ni kwake tunajifunza kuwapenda wengine na kuwatumikia, kuweza kuiona sura yake katika uumbaji (Imago Dei). Ni kwake tunachota neema ya upendo na moyo wa kuwatumikia wengine, kwake ni chimbuko na kilele cha maisha ya neema. Wapendwa katika safari yetu ya kumfuasa Yesu, inayotudai upendo usio na masharti hakika haikosi vikwazo ila daima hatuna budi kukumbuka msaada wetu daima watoka kwake na si kwa kutegemea mantiki na namna zetu za kibinadamu. Tumwombe basi Mungu neema za kuwa wafuasi wa kweli wa Yesu si tu kwa maneno bali kwa maisha yetu ya kila siku. Nawatakia tafakari na Dominika njema.

22 June 2022, 08:36