Siku Kuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu Siku Kuu ya Moyo Mtakatifu wa Yesu 

Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu:Upendo wa Mungu hutambuliwa na wanyenyekevu

Katika Moyo Mtakatifu wa Yesu yamo mapendo yote ya Mungu anayotupenda nayo sisi wanadamu.Msalabani moyo huu ulifunguliwa kwa kuchomwa mkuki mara ikatoka damu na maji chemichemi za sakramenti za Kanisa na kwa hiyo kwetu sisi moyo huu u-wazi na ni chemichemi ya neema kwa maisha yetu."Ee Mungu Mwenyezi,tunaona fahari juu ya Moyo wa Mwanao mpenzi na kukumbuka jinsi alivyotupenda".

Padre Paschal Ighondo – Vatican.

Tafakari ya neno la Mungu katika Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu mwaka C wa kiliturujia, tarehe 24 Juni 2022. Sherehe hii huadhimishwa Ijumaa baada ya Dominika ya pili baada ya sherehe ya Pentekoste yaani baada ya sherehe ya Utatu Mtakatifu tunayoisherehekea Dominika ya kwanza baada ya sherehe ya Pentekoste na sherehe ya Mwili na Damu ya Kristo/Ekaristi Takatifu ambayo kawaida inapaswa kusherehekewa Alhamisi baada ya sherehe ya Utatu Mtakatifu lakini kwa sababu za kichungaji tunaisherehekea dominika ya pili baada ya Pentekoste. Ni sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Moyo ni alama ya mapendo. Hivyo, tunapoadhimisha sherehe hii ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, tunakumbuka hasa mapendo yake kwetu sisi wanadamu. Yeye alitupenda sisi mpaka upeo, hivi hata akajitoa afe msalabani ili atukomboe kutoka utumwa wa dhambi na mauti kama wimbo wa mwanzo unavyoimba; “Makusudi ya Moyo wake ni ya vizazi na vizazi. Yeye huwaponya nafsi zao na mauti na kuwahuisha wakati wa njaa” (Zab. 33:11,19).

Katika Moyo Mtakatifu wa Yesu yamo mapendo yote ya Mungu anayotupenda nayo sisi wanadamu. Msalabani moyo huu ulifunguliwa kwa kuchomwa mkuki mara ikatoka damu na maji chemichemi za sakramenti za Kanisa; na kwa hiyo kwetu sisi moyo huu u-wazi na ni chemichemi ya neema kwa maisha yetu ndiyo maana katika sala ya mwanzo katika liturujia ya sherehe hii Padre kwa niaba ya jamii ya waamini anasali akisema; “Ee Mungu Mwenyezi, tunaona fahari juu ya Moyo wa Mwanao mpenzi, na kukumbuka jinsi alivyotupenda kwa mapendo yake makuu. Tunakuomba utujalie kupata neema tele katika chemchemi hiyo ya baraka za mbinguni. Kumbe katika sikukuu hii tunamshukuru Kristo kwa mapendo yake. Lakini pia tunakumbuka tunavyokataa mapendo hayo mara nyingi katika maisha yetu. Basi tunapaswa kuomba radhi, kutolea heshima ya ibada yetu na kufanya malipizi yatupasayo.

Somo la kwanza la kitabu cha Nabii Ezekieli (34:11-16); linatueleza jinsi viongozi wa dini na wa siasa wa Israeli walivyowanyanyasa na kuwanyonya watu wao wanyonge. Matokeo ya kukosa uongozi bora, Waisraeli walitawanywa wakati wa uhamisho wa Babeli. Mungu mwenyewe anakusudia kuwarudisha Waisraeli katika nchi takatifu na Yeye mwenyewe atawachunga. Ahadi hii ya Mungu imetimia katika Yesu Mchungaji mwema.

Mchungaji mwema
Mchungaji mwema

Somo la pili la waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (5:5-11); linatukumbusha jinsi Mungu alivyoonyesha mapendo yake ya pekee kwetu sisi wanadamu kwa kumtolea Mwanae afe kwa ajili yetu na kwa kutupelekea Roho Mtakatifu siku ya ubatizo. Maadam alionyesha mapendo hayo makubwa pindi tulipokuwa bado wakosefu; hakika ataonyesha kwetu mapendo hayo zaidi sasa baada ya kukombolewa hata siku ya hukumu. Lakini Mungu ni mwenye haki, upendo wake na huruma yake atatuonyesha kama sisi wenyewe tutapendana, tutahurumiana na kusameheana sisi kwa sisi.

Injili ilivyoandikwa na Luka (15:3-7); inatuonyesha mawazo potovu ya wafarisayo na waandishi kwa mpango wa Mungu wa kumkomboa mwanadamu kwa njia ya mwanao. Wafarisyo na waandishi walidhani Mungu hawezi kuwapokea tena na kuwasamehe wakosefu. Kwa kushirikiana na wakosefu na kwa mfano wa kondoo aliyepotea nyikani, Yesu anawafundisha kuwa Mungu anafurahi sana pale mkosefu mmoja anapojuta na kutubu makossa yake kuliko anapoona Mafarisayo na waandishi 99 waliojikinai na kujiona wenye haki na hawana haja na Mungu. Kwa hiyo Kristo, aliye mchungaji mwema, ilimpasa ashughulike na wakosefu ili awarudishe kwa upendo katika upendo wa Mungu Baba.

Mtoto mpotevu
Mtoto mpotevu

Upendo wa Mungu umeshawekwa bayana kabisa katika nafsi ya Bwana wetu Yesu Kristo. Na kwa kupitia upendo huo ulioonyeshwa na Bwana wetu Yesu Kristo ndio tunaweza kumjua Mungu vile alivyo. “Kama tunataka kumwona Mungu alivyo, kama tunataka kuyaona mawazo ya Mungu, kama tunataka kuuona moyo wa Mungu, kama tunataka kuujua mtazamo wa Mungu kwa binadamu tunapaswa kumtazama Yesu (Yoh.14:9). Ni imani ya Kikristo kwamba ni katika Yesu Kristo peke yake tunamwona Mungu vile alivyo; na pia ni imani ya Kikristo kwamba Yesu anaweza kumpa ujuzi huo yeyote yule ambaye ni mnyenyekevu kutosha na anayemtumainia. Chombo cha pekee cha kuupokea upendo wa Mungu si uwezo wa akili, wala si busara na hekima, wala si elimu na usomi wetu, wala si vyeo vyetu, wala si uwezo wetu wa mali na fedha, bali ni unyenyekevu, na maadui wake ni majivuno na kiburi. Bila kuwaondoa maadui hawa wawili hatuwezi kamwe kuwa wanyenyevu; na hivyo kuupokea upendo wa Mungu na kumjua vile alivyo itakuwa ni ndoto. Upendo chanzo chake ni Mungu. Ni kutoka kwa Mungu ambaye ni upendo wenyewe kwamba mapendo yote yanaanza. Hatuwezi kamwe kuwa karibu na Mungu zaidi ya pale tunapopenda. Anayeishi katika upendo anaishi katika Mungu.

Yesu anasema pendaneni
Yesu anasema pendaneni

Binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu (Mwa.1:26). Mungu ni upendo na kwa hiyo, kuwa kama Mungu na kuwa kama vile Mungu anavyotarajiwa kuwa, binadamu lazima naye apende. Upendo una pande mbili za kuhusiana na Mungu. Ni pale tu tunapomjua Mungu na ndipo tunapojifunza kumfahamu Mungu (1Yoh.4:7-8). Upendo unaotoka kwa Mungu ni upendo unaotupeleka kwa Mungu. Ni kwa njia ya kupenda ndiyo Mungu anajulikana. Hatuwezi kumwona Mungu kwasababu Mungu ni Roho tupu, tunachoweza kukiona ni mapato tu ya uwepo wake. Onyesho pekee la Mungu halitokani na hoja bali linatoka katika maisha ya upendo. Mapendo ya Mungu yanaonyeshwa katika nafsi ya Yesu Kristo (Yoh.4:9). Upendo wa Mungu haujibakizi ndiyo maana alimtoa Mwanae wa pekee na kumfanya sadaka kwa ajili ya wokovu wetu. Ni pendo ambalo hatukulistahili kwa sababu ya dhambi zetu. Kumbe upendo wetu kwa Mungu na kwa jirani usijibakize na tuuelekeze hata kwa wale wasiostahili bila kutarajia kupata chochote kutoka kwao.

Basi tumwombe Mwenyezi Mungu atajalie neema na baraka zake ili tuweze kuuishi upendo daima kati ya ndugu zetu ili yale anavyotuombea Padre katika sala baada ya Komunyo akisema; “Ee Bwana, tunakuomba sakramenti hii ya mapendo ituwashie upendo wako mtakatifu na kutuvutia siku zote kwa Mwanao, kusudi tuweze kumtambua yeye katika ndugu zetu” yaweze kutimia.

TAFAKARI YA SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU

 

23 June 2022, 16:59