Tafakari Neno la Mungu Dominika 13: Wito Ni Huduma Kwa Watu!
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Juma hili tunaadhimisha dominika ya 13 ya mwaka C wa Kanisa. Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, karibu katika kipindi hiki tulisikilize Liturujia ya Neno la Mungu tunalolipokea katika masomo ya dominika ya 13 ya mwaka C wa Kanisa. Neno hili linatualika kutambua kuwa ndani yetu, ndani ya wakristo wote Mungu ameweka tunu ya wito ili kwa njia ya wito huo tuweze kumfuasa kwa njia ya kuwahudumia wenzetu. Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza (1Fal 19:16b, 19-21 ) ni kutoka katika kitabu cha kwanza cha Wafalme. Ni somo linaloelezea wito wa Nabii Elisha. Elisha anayeitwa kuwa mfuasi wa Nabii Eliya na hatimaye kuchukua nafasi yake kama nabii wa Mungu. Eliya akiisha kupokea maagizo ya Mungu, alipita karibu na Elisha, aliyekuwa akilima pamoja na ng’ombe wa kulimia, na akatupa vazi lake juu yake. Vazi ni alama ya mamlaka ya kinabii kama ilivyokuwa fimbo kwa Musa. Kulitupa vazi lake juu yake ni alama ya kumvika Elisha mamlaka hayo ya kinabii. Elisha kisha kupokea vazi hilo anafanya tendo la kwenda kuwaaga wazazi wake, baba na mama na kisha anawachinja wale ng’ombe aliokuwa akilimia na nyama yao anawapa watu wale.
Kwa tendo hili Elisha anaonesha kuwa wito wa kinabii anaoupokea ni wito unaomtaka kujibandua na hali na mazingira aliyokwa nayo awali. Anawaaga wazazi kuonesha kuwa japokuwa anabaki kuwa mwanafamilia, anatambua kuwa utume wake wa unabii unamuondoa kwa namna fulani katika familia yake ili aweze kuzishugulia familia zote za wana wa Mungu. Hali kadhalika anawachinja ng’ombe wake wa kulimia kama alama ya kujibandua katika kazi na maslahi yake binafsi ili kushughulikia maslahi ya wote ambao kwao anatumwa kama nabii. Somo la pili (Gal. 5:1, 13:18 ) ni kutoka waraka wa mtume Paulo kwa Wagalatia. Paulo katika somo hili anazungumza juu ya uhuru walioitiwa wana wa Mungu. Anasema Kristo ametukomboa ili tuwe huru. Paulo anazungumza na watu wa mataifa waliouongokea ukristo. Watu ambao hawakuwa wayahudi, na mara kwa mara katika mazingira ya wakati huo walilazimishwa kushika torati na mila za kiyahudi kwanza ili wawe wakristo kamili. Paulo alikuwa kinyume na hayo, alisisitiza kuwa Kristo ametuokoa kutoka utumwa huo wa torati na mila za kiyahudi na kutuingiza katika uhuru wa wana wa Mungu. Mara nyingi sana Paulo ameonesha kuwa Torati ilikuwa ni kwa ajili ya kuwaandaa watu kumpokea Kristo, na tena tunakombolewa kwa njia ya Kristo na si kwa njia ya torati. Hata hivyo, hapo hapo Paulo anasisitiza kuwa uhuru huu ndani ya Kristo sio kisingizio kamwe cha mtu kufanya anachotaka, kuishi anavyotaka bila hata chembe ya maadili. Huu ni uhuru wa kuishi kwa upendo ndani ya Kristo na uhuru unaomwajibisha mkristo kuenenda kwa kufuata matakwa ya Roho Mtakatifu.
Injili (Lk 9:51-62) Injili ya leo, kama ilivyoandikwa na Luka, inaendeleza dhamira ya wito na ufuasi, dhamira ya somo la kwanza. Na katika hili, mwinjli Luka anaweka mbele yetu vijana watatu. Wa kwanza anaomba mwenyewe kumfuata Yesu, anasema “nitakufuata kokote utakakokwenda”. Huyu,Yesu anamjibu kwa kumuonesha ni nini anachokiomba. Ni kumfuata aliye fukara ambaye hana hata mahala pa kujilaza kichwa chake. Ni mfano wa mtu ambaye ana shauku ya kumfuata Yesu bila kutilia maanani undani na madai ya ufuasi huo. Kwa wa pili ni Yesu anayemwita. Naye anaomba ruhusa ya kwenda kwanza kumzika baba yake ndipo arudi. Kuzika wafu ni mojawapo ya matendo ambayo wayahudi waliyapa uzito sana (rej. Tob 1:16-20, 4:3, 6:5). Kumbe katika hali ya kawaida Yesu asingelikataa ombi hili. Mt. Cirilo anasema kijana huyu aliomba kwanza aende kumuhudumia baba yake hadi hapo Mungu atakapomwita ndipo arudi kumfuata Yesu. Ni mtu anayeona kuwa kabla ya kuamua kumfuata Yesu inabidi kupitia yote wanayopitia wengine: ujana, utafutaji wa mali na hata wakati mwingine raha za kidunia na zote zikiisha ndipo amfuate Yesu. Kijana wa mwisho, yeye anaomba kwanza aende kuaga watu wa nyumbani ndipo arudi kumfuata. Huyu ni mfano wa mtu ambaye bado amegawanyika katika ufuasi. Anapenda kuwa mfuasi lakini bado amejishikamanisha na malimwengu. Mtakatifu Augustine anasema ni mfano wa yule ambaye “mashariki inamuita na yeye anageukia magharibi”. Na kwake Yesu anasema “mtu aliyetia mkono wake kulima kisha akaangalia nyuma hafai kwa ufalme wa Mungu”.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Maandiko Matakatifu katika dominika hii ya 13 ya mwaka C wa Kanisa yanatualika tutafakari juu ya mwito wetu. Kwa njia ya ubatizo sote tumeitwa kumvaa Kristo, kumfuata na kumshuhudia katika maisha yetu kwa maneno lakini zaidi kwa njia ya matendo yetu mema na adili. Mwito huu sio kitu cha mara moja na tena sio tendo la siku moja kiasi kwamba ukishaupokea basi hapo hapo umekwishakamilika. Mwito huu ni tendo endelevu. Kila siku na kila hatua ya maisha tunayopiga ni mwaliko wa kuupyaisha: kupata mang’amuzi mapya juu ya ukristo wetu, kuuelewa zaidi, kuyaelewa zaidi matakwa yake katika maisha na kuzidi kuupokea na kusema “ndiyo” - “mimi hapa, nitume Bwana”. Katika mazingira haya, wito wa Nabii Elisha na wa wale vijana watatu katika Injili vinatusaidia kujua madai ya kudumu ya mwito na changamoto zake kulingana na hali na maisha tuliyomo. Mwito unabadilisha maisha kumuelekea Kristo, mwito ni mwaliko wa kujibandua na malimwengu na kujikita kwa Kristo bila kugeuga ugeuka, mwito unazo sadaka zake na magumu yake yanayohitaji uimara na ujasiri wa kuyakabili kwa nguvu zake anayeita, mwito ni mwaliko wa kuupokea bila kuchelewa. Kwa mtakatifu Paulo, mwito huu pia ni mwaliko wa kuwa watu bora zaidi katika jamii: bora katika maadili na na utu wema. Mungu aliyeanzisha kazi hii njema ndani yetu, yeye mwenyewe na aikamilishe hadi kurudi kwake mkombozi wetu Yesu Kristo.