Tafakari Dominika 14 ya Mwaka C: Wajumbe Na Mashuhuda wa Amani
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama! “Sina amani!”; Ni kilio katika ulimwengu wetu wa leo, ni kawaida sana kusikia au kukutana na mtu anayelalamika kuwa hana amani na hata mara nyingi sisi wenyewe tunakosa amani ndani mwetu. Kuna sababu nyingi za mmoja kufikia hatua ya kukiri kuwa hana amani. Ni katika muktadha huo Yesu anawatuma wanafunzi wake sio kwa ajili ya kuhukumu ulimwengu, bali kuupatia ulimwengu zawadi ya amani. Kristo Mfufuka daima anawasalimu wanafunzi wake kwa maneno yale ya “shalom”, ni kuwatakia afya na salama maishani mwao, ndio zawadi ya kwanza ya Kristo Mfufuka kwa Kanisa lake, na ndio maneno haya yanatumika kila mara kuhani anapotusalimu tunapoanza maadhimisho ya Ekaristi Takatifu. Ni matashi ya afya na amani kwa kila mfuasi wake Bwana wetu Kristo, ni kumtakia mwingine kuwa na hakika ya amani ya kweli pale tu anapokubali kuongozwa na Bwana na Mwalimu wetu, na ndiye Kristo Yesu. Kwa kuangalia ulimwengu wetu wa leo tunashawishika kuona ni rahisi watu kuamini juu ya uwepo wa Mungu kuliko kuwatangazia habari ya amani. Na amani ndio ujumbe ambao wanafunzi wa Yesu wanatumwa leo kwenda kuupeleka kwa watu wote. Kanisa halina budi kutambua wajibu wake wa kuwa mjumbe wa amani ulimwenguni pote. Uinjilishaji wa kina unatudai kuwa wajumbe wa amani kuanzia katika maisha yetu, familia zetu, jumuiya na parokia zetu na kwa ulimwengu mzima. Ulimwengu hakika una njaa na kiu ya amani!
Yesu Kristo hawatumi tu kupeleka ujumbe wa amani bali hata namna na jinsi ya kuupeleka ujumbe huo wa amani. Nawaalika tutafakari kwa pamoja ujumbe wa amani anaotutuma nao Yesu Kristo aliye Bwana na Mwalimu wetu katika Dominika hii ya 14 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa. Wana wa Israeli wakiwa uhamishoni Babeli, Nabii Isaya anawatangazia habari njema ya afya na amani na mafanikio kwa kurejea tena kwao katika nchi ile yao ya ahadi. “Maana Bwana asema hivi, tazama, nitamwelekezea amani kama mto, na utukufu wa mataifa kama kijito kifurikacho, nanyi mtapata kunyonya; mtabebwa; na juu ya magoti mtabembelezwa.” Lakini hata baada ya kurejea kwao tunaona watu bado wanaishi katika hali ngumu isiyokuwa na amani wala usalama. Watu wanavunjika mioyo na kukata tamaa na hata kupoteza imani kwa manabii wa Mungu. Kwa watu wale waliokata tamaa, kuvunjika na kupondeka mioyo anatumwa tena nabii mwingine na maneno ya faraja kama tulivyosikia katika Somo la kwanza. Anawaalika watu wafurahi maana huzuni yao imefika mwisho. Wasikilizaji wake ni wazi wengi walipuuza na hata kuona ni mmoja aliyechanganyikiwa kwani tayari walishapokea ahadi nyingi bila kuona utimilifu wake. Ni unabii ambao kwa hakika unatimia sio katika nyakati zile bali kwa ujio wake aliye Bwana na Mfalme wa Amani, ndiye Kristo Yesu.
Mtume Paulo katika Somo la pili anatuonesha ishara ya wazi ya mwanafunzi na mfuasi wa Yesu Kristo, haipo katika ishara ya nje ya kutahiliwa bali ni katika kufanana na Bwana na Mwalimu wetu aliyetoa maisha yake sadaka kwa kutupenda sisi sote. Ni kwa kushiriki katika hilo nasi tunakuwa viumbe wapya. Mtume Paulo anaona fahari na kujivunia makovu na mateso aliyoyapata katika mwili kwa kumfuasa Yesu Kristo na si kwa kutahiliwa. Imani yetu haina budi kujikita katika fumbo lile la msalaba, ni hapo tunachota na kuonja upendo na huruma ya Mungu kwetu na kwa ulimwengu mzima. Sehemu ya Injili ya leo inatanguliwa na kutumwa kwa wale tenashara yaani mitume kumi na wawili kuutangaza ufalme wa Mungu na kuponya wagonjwa na huku akiwasisitiza kutokubeba bakora, mfuko, mkate, pesa wala kanzu mbili. (Luka 9:1-6). Sasa tunajiuliza hawa sabini wengine ni akina nani? Ambao mwinjili anatutambulisha hapa na pia hatuwasikiii tena katika Injili ya Luka baada ya tukio la leo? Kwa hakika Mwinjili Luka hakuwa anatupa simulizi la kihistoria bali ni ujumbe wenye katekesi nyuma yake kwa jumuiya yake na hata pia kwa jumuiya zetu leo hii. Tupo katika Asia ndogo katika karne ile ya kwanza, ambapo pamoja na madhulumu na kuteswa kwa Wakristo tunaona Kanisa lile la mwanzo bado lilisonga kwa ujasiri wote kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wote. Ni katika mazingira haya yaliibuka maswali na hata mashaka mengi juu ya misheni hiyo ya kueneza Habari Njema.
Ni katika mazingira haya Mwinjili Luka anaona umuhimu wa kutoa katekesi juu ya utume wao wa kueneza Habari Njema kwa watu wote kwa ujasiri na sadaka kubwa. Msalaba daima unabaki kama msingi wa kila mjumbe wa Habari Njema. Wafuasi sabini ni namba ishara inayobeba ujumbe nyuma yake. Tukirejea kusoma Mwanzo 10 tunaona kuwa nyakati zile iliaminika kuwa idadi ya watu ulimwenguni kote ni 70 au 72. Siku ya sikukuu ya vibanda pale Hekaluni Yerusalemu walichinja wanyama 70 kumaanisha kufanya toba kwa Mungu kwa ajili ya watu wa mataifa mengine ya kipagani. Namba sabini iliwakilisha ulimwengu mzima. Katika jumuiya zile alizokuwa anaziandikia Mwinjili Luka kulikuwa pia na wapagani kwa maana ya watu wa mataifa mengine nje ya Wayahudi. Mwinjili Luka kwa kutaja wafuasi 70 ndio kusema Ujumbe wa Injili au Habari Njema ya wokovu ni kwa ajili ya watu wote wa ulimwengu mzima bila kujali, rangi, kabila au taifa. Kristo ni Bwana wa ulimwengu mzima na si kwa taifa lile teule tu peke yake la Israeli. Na Yesu anawatuma wafuasi 70 ndio kusema utume wake ni kwa mataifa yote ya ulimwengu.
Ni utume kwa kila mbatizwa bila kujali taifa au kabila au rangi au asili fulani. Sisi sote tunatumwa kwenda kuwa wajumbe na wamisionari wa Habari Njema. Na ndio hitaji la Kanisa la Kisinodi, sisi sote kwa Ubatizo wetu ni wajumbe, ni manabii, makuhani na wafalme tunaopelekwa kuwa mashahidi wa upendo na huruma ya Mungu kwa watu wote. Kanisa ni sisi sote yaani jumuiya ya Wabatizwa na asitokee hata mmoja wetu kujiona yupo nje ya misheni ya Kanisa, ya kuwa wajumbe wa Habari Njema ya wokovu. Wanatumwa wawili wawili. Kazi ya kuinjilisha sio kazi ya mtu binafsi au mmoja mmoja bali ni misheni ya jumuiya nzima yaani Kanisa. Anayeinjilisha sio mmoja anayejipeleka bali daima anatumwa na Kanisa na daima kufanya utume huo pamoja na Kanisa na ndio ushirika wa mitume na Kanisa. Tunaona hata wamisionari wale wa kwanza walitumwa wawili wawili, Petro na Yohane (Matendo 8:149), Barnaba na Paulo (Matendo 13:1) na daima wanatumwa. Ndio kusema kazi ya kuhubiri Injili ni utume wa Kanisa na sio wa mtu binafsi, ni kazi ambayo tunaalikwa kuifanya kwa pamoja na kwa kushirikiana kama tunavyohimizwa leo kuishi Kanisa la Kisinodi linalosimikwa katika utamaduni wa umoja, ushiriki na utume.
Lengo la kutumwa kwao ni ili kuandaa ujio wa Masiha katika kila kijiji na mji. Yesu anafika baada ya maandalizi ya wanafunzi wake. Hivyo tunatumwa sisi sote kutangulia kila mara kuwaandaa watu wa kila mji na kijiji au ulimwengu mzima ili waweze kuwa na mioyo tayari ya kumpokea Yesu Kristo. Yesu anawaalika wanafunzi wake kusali ili Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi shambani mwake. Kusali sio kugeuza mawazo au kumshawishi Mungu kufanya tutakavyo sisi bali daima kutusaidia sisi kukubali na kuenenda kadiri ya mipango ya Mungu katika maisha yetu. Ni kwa njia ya Sala tunapata amani na kukubali mioyo yetu kupokea utume na ujumbe wa amani wa Mungu na hivyo kuwa tayari kutoka na kuwashirikisha wengine. Kusali ni kupenda, ni katika sala tunaonesha kwa jinsi gani tunampenda Mungu na tupo tayari kuhusiana naye kwa karibu zaidi. Anawatuma kati ya mbwa mwitu. Mbwa mwitu ni ishara ya hatari na upinzani na uadui. Ni katika mazingira yenye madhulumu na mateso na kukataliwa daima tunatumwa. Lakini Yesu anawatuma wanafunzi wake kuwa kama kondoo. Kondoo ndio ishara ya upole na unyenyekevu na udogo katika utume wetu. Hatutumwi kuwa wajumbe wa mabavu na maguvu na vita na fujo na mengine ya namna hiyo bali daima kuwa wapole katika utume wetu. Tutadhulumiwa ndio lakini sisi tunaalikwa daima kuenenda kama kondoo. Anatutahadhirisha kuwa macho na tabia za mbwa mwitu, hasira, visasi, vita, malumbano, chuki, ubabe na kutaka kutawala kwa gharama yeyote ile na hata kujeruhi na kuumiza walio wanyonge au wengine. Yesu anawaonya wanafunzi wake kutokuwa na tabia na hulka za mbwa mwitu bali za mwanakondoo.
Yesu ameukomboa ulimwengu kama Mwanakondoo wa Mungu na hivyo kutualika nasi kuwa na sifa na tabia kama zake. Ni katika muktadha huo wa kuwa kama mwanakondoo anawaalika wasibebe mfuko, wala mkoba, wala viatu. Kwa ajili ya kufanya propaganda za kisiasa katika ulimwengu lazima kutumia pesa, majeshi, na hata watu wenye ushawishi katika jamii. Hapa tunayo mifano mingi tunayoweza kutoa ila itoshe kuona kwa wanafunzi wa Yesu tunaitwa kuwa wajumbe wa Habari Njema sio kwa mtindo na mantiki ya ulimwengu huu. Kanisa lazima kuwa macho kila mara la sivyo tunapoteza sura ile ya Mwanakondoo wa Mungu yaani Yesu Kristo. Wakiwa njiani wanaambiwa kutosalimu watu, na hapa isieleweke kuwa wanafunzi wa Yesu wanaitwa kuwa watu wasio na utu na kutojali watu wanaokutana nao njiani, bali ni kuonesha jinsi gani hawana budi kutopoteza muda na badala yake kwenda kwa haraka na hima kuwashirikisha watu wote Habari Njema ya Wokovu. Nia na lengo na shauku yao ni kuwashirikisha wengine Habari Njema na hivyo kuwa na agenda moja tu. Wapendwa mara nyingi tunaona wasio waamini au wapagani wanabaki na habari gani kutoka kwetu wanafunzi wa Yesu, labda makatazo fulani fulani ya kimaadili au kuhusu amri kumi za Mungu na za Kanisa, na hata wakati mwingine matisho kuhusu laana za Mungu zitokanazo kwa kukosa kutii amri na maagizo yake. Kwa kweli kama ni hivyo basi hatuna budi kukiri kuwa tumeshindwa kuwa wajumbe wa Habari Njema!
Injili ni Habari Njema! Na ndio Yesu leo anawatuma wanafunzi wake ujumbe wao wa kwanza kwa kila nyumba na mtu wanayemfikia ni AMANI. Ni wajumbe wa amani kwa mtu mmoja mmoja, familia, nyumba, kijiji, mji na ulimwengu mzima. Huo ni ujumbe unaoleta faraja na matumaini tena kwa wale waliokata tamaa na kupoteza matumaini. Na anayepokea ujumbe huo na kumpokea mjumbe wa Habari Njema anaalikwa kukaa na kubaki katika nyumba hiyo bila kuhamahama, na kula na kunywa viwekwavyo mbele yenu. Mwanafunzi wa Yesu nyakati za Luka hasa waliokuwa na asili ya Kiyahudi walikuwa na masharti mengi kuhusu vyakula, ila kwa ujumbe huo Yesu anaondoa vikwazo vyote kuhusu vyakula na vinywaji mintarafu imani yetu. (Wagalatia 2:11-14; Matendo 11:2-3; 1Wakorintho 10:27). Habari Njema inaendana na matendo ya huruma na ndio mwaliko kuponya wagonjwa na kuwasaidia wanaokuwa maskini. Injili inaweza kupokelewa na hata kukataliwa. Tunajua Mungu kwa asili hajui kuchukia wala kukasirika maana Yeye ni wema na upendo kamili. Ila Yesu anatumia lugha hiyo kali kuonesha ni kwa jinsi gani anayeikataa Injili anachagua njia iliyo ya upotevu na yenye hasara kubwa. Kumwona shetani akianguka.
Kwa kweli lugha hii haimaanishi kuwa Yesu aliona kiumbe wa ajabu akidondoka bali akiona nguvu za yule mwovu zikishindwa kwa kila anayeipokea Habari Njema ya Wokovu. Na ndio chuki, mafarakano, magomvi, masengenyo, majungu, fitina, wivu, kisasi, ukosefu wa haki, ubinafsi, majivuno, ulafi wa fedha, na tamaa mbaya za kila aina na uovu wote. Kudondoka kwa shetani ndio kutangazwa kwa ushindi utokanao na Habari Njema. Na ndio anawaambia wanafunzi wake anawapa uwezo wa kukanyaga nyoka na nge. Nyoka na nge ni ishara za nguvu za yule mwovu na maovu yote tunayoweza kufikiria katika maisha yetu. (Mwanzo 3 :15; Zaburi 91:13) Wanyama wakali na wa hatari ndio hatari zote watakazokutana nazo katika safari ya utume wa kueneza Habari Njema ila ikiwa kweli wanambeba Kristo basi wasiwe na wasiwasi wala mashaka yeyote kwani Kristo Mfufuka alishamshinda yule mwovu. Wapendwa niwatakie tafakari njema na kuzidi kualikana kusonga mbele katika utume wetu wa kueneza Habari Njema kwa kila kiumbe ulimwenguni kote na daima tuwe na hakika ya kushinda kwani KristoMfufufuka daima yupo pamoja nasi. Kila anayemwamini Yesu Kristo na Neno lake basi afurahi kwa kuwa jina lake limeandikwa mbinguni. Dominika na tafakari njema.