Tafakari Dominika 14 Mwaka C: Changamoto za Uinjilishaji wa Watu Ulimwenguni
Na Padre Efrem Msigala, OSA., - Roma.
Karibu mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 14 ya Mwaka C . Somo la kwanza kutoka katika Kitabu cha Nabii Isaya 66:10-14c, tunasikia ahadi ya upendo na huruma ya Mungu ya kuwalinda na kuwaruzuku watu wake. Aliahidi baraka nyingi, akisema: “Nitaeneza ufanisi juu yake kama mto, na utajiri wa mataifa kama kijito kinachofurika.” Aliahidi faraja na amani ya kudumu: “Kama vile mama amfarijio mwanawe, ndivyo nitakavyowafariji ninyi.” Maneno ya faraja ya Mungu kwa watu wake. Somo la pili ni kutoka Waraka Mtakatifu Paulo kwa Wagalatia 6:14-18. Paulo anatoa sifa na utukufu kwa Msalaba wa Kristo: "Nisijisifu kwa neno lo lote, ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo." Ni Msalaba wa Kristo uliofanya upya maisha yake; pia Paulo anahuisha maisha ya ulimwengu akisema: "Kilicho muhimu ni kwamba mtu ameumbwa upya." Kwa hiyo inamaana kwamba watu wanapofuata sheria ya msalaba, basi kunakuwa na amani maishani mwao: kutokana na hilo Paulo anaema: “Amani na rehema kwa wote wanaofuata kanuni hii ya maisha, na kwa Israeli wa Mungu.”
Injili inasimulia kuhusu kutumwa kwa wanafunzi Sabini na wawili ili kumtayarishia njia Kristo Yesu katika vijiji na mahali atakapopita. Yesu anawapa maagizo mahususi ya kiutendaji kabla ya kuanza utume wao wa kutangaza Habari Njema ya wokovu. Maagizo haya yamekusudiwa kuwaongoza katika kazi hii, na pia kuwakumbusha kwamba hatimaye, ni kazi ya Mungu na wao ni vyombo vyake tu. Kwa hiyo wanapaswa daima kubaki wanyenyekevu, watulivu na kumtegemea Mungu kabisa katika shughuli zao za kimisionari. Ni Mtakatifu Luka pekee anayetaja kundi lingine kando au zaidi ya wale Kumi na Wawili yaani wale thenashara. Wale Kumi na Wawili ni kundi maalum lililochaguliwa kibinafsi na Yesu - idadi hiyo ni muhimu kwa kuwa iliwakilisha kiishara makabila kumi na mawili ya "Israeli mpya". Lakini Mtakatifu Luka anataja kundi kubwa zaidi, wanafunzi Sabini na wawili. Katika maandishi ya asili ya Biblia, nambari sabini na sabini na mbili zimetumika kwa kubadilishana.
Namba hii ni ya kiishara na muhimu sana katika historia ya Kiyahudi: Mwanzo sura ya 10 inataja kwa majina wazao 70 wa Yafethi, Shemu na Hamu; Musa aliwaagiza wazee 70/72 katika kitabu cha Hesabu sura ya 11; pia kulikuwa na watafsiri 70/72 waliovuviwa na Mungu wa Agano la Kale katika Kigiriki (Septuaginta). Hivyo basi pamoja na maelezoo hayo tuliyo yasikia, Yesu anapowatuma anasema maneno yafuatayo kama mwongozo kwa utume wao: Anawaambia, ‘Nendeni zenu. Angalieni, mimi ninawatuma ninyi kama wana-kondoo katikati ya mbwa-mwitu.’” ( Luka 10:1, 3 ) Kwa kweli, kuhubiria ulimwengu kuwapo kwa upendo kwa Mungu ni jambo muhimu sana kwa wanafunzi wake na hivyo walifananishwa na wana-kondoo. Ni taswira ya picha, lakini hakika inawatayarisha wale waliotumwa kwa magumu yajayo.
Kwa hiyo maneno: “Nawatuma kama wana-kondoo katikati ya mbwa-mwitu.” Yesu anafahamu upinzani dhidi ya Injili. Ibilisi atajaribu kuzuia kuenea kwa Injili. Wanafunzi hawapaswi kuridhika na kutojua, kwa kuwa ulimwengu umejaa maadui, vishawishi. Yesu mwenyewe aliongozwa hadi msalabani na maadui zake. Onyo la Yesu ni kuwa halisi. Anataka wafuasi wake wawe macho juu ya adui, lakini anawahakikishia kuwapo kwake na ulinzi: “Mimi nitakuwa pamoja nanyi sikuzote hata mwisho wa nyakati.” Lakini pia tumesikia salamu ya Yesu kwa wanafunzi wake. "Amani kwa nyumba hii." Wanafunzi ni wajumbe wa Mungu wa amani. Katika lugha ya Biblia, amani ni “shalom.” Sio tu kutokuwepo kwa migogoro au vita. Bali, ni uwepo wa maelewano na ustawi kamili wa mtu na jamii nzima. Shalom inamaanisha kila kitu kiko sawa kabisa kwa sababu upendeleo wa Mungu uko kwa kila mtu. Ni Mungu pekee ndiye anayeweza kuwa chanzo cha amani hii.
Hivi ndivyo Yesu alisema: “Amani nawaachieni. Amani yangu nawapa.” Siku hizi, watu wanatafuta amani, lakini hawafanikiwi, kwa sababu wanaitafuta mbali na Mungu. Amani ya kweli itakuja tu wakati watu watajifunza kutii amri za Mungu na kuishi kulingana na mapenzi Yake. Yesu aliwatuma wanafunzi wake kama wajumbe wa amani - kuwasaidia kuishi kulingana na mpango na amri za Mungu. Ikiwa wanakataa ujumbe wa wanafunzi, amani haiwezi kubaki nao. Hiki ndicho kinachotokea sasa duniani. Tuko katika misukosuko ya kila mara, kuchanganyikiwa na shida kwa sababu watu hukataa mafundisho ya Mungu na kutotii amri zake. Tuombe Mungu atujalie amani ya kweli katika maisha yetu ya kila siku.