Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 14 ya Mwaka C wa Kanisa: Uinjilishaji wa kina ni asili na utume wa Mama Kanisa. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 14 ya Mwaka C wa Kanisa: Uinjilishaji wa kina ni asili na utume wa Mama Kanisa. 

Tafakari Neno la Mungu Dominika 14 Mwaka C: Uinjilishaji Ni Asili na Utume wa Mama Kanisa

Leo tunayasoma na kuyatafakari masomo ya dominika ya 14 ya mwaka C wa Kanisa, masomo ambayo yanatualika kuutafakari wito wa kimisionari wa Kanisa, yaani jukumu la Kanisa la kuinjilisha na kutanganza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Hiki ni kiini na asili ya Kanisa kama Sakramenti ya wokovu kwa watu wa Mataifa.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Juma hili tunaadhimisha dominika ya 14 ya mwaka C wa Kanisa. Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican katika kipindi hiki cha tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu. Leo tunayasoma na kuyatafakari masomo ya dominika ya 14 ya mwaka C wa Kanisa, masomo ambayo yanatualika kuutafakari wito wa kimisionari wa Kanisa, yaani jukumu la Kanisa la kuinjilisha na kutanganza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wote wa Mataifa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Hiki ni kiini na asili ya Kanisa kama Sakramenti ya wokovu. UFAFANUZI WA MASOMO: Somo la kwanza (Is 66:10-14c ) ni kutoka katika kitabu nabii Isaya. Nabii anaandika kuwapa moyo wote wanaolia pamoja na Yerusalemu. Yerusalemu, mji wa Mungu unalia kwa sababu umeharibiwa na wavamizi. Kuta zake zimevunjwa na hekalu limebomolewa wakati wa vita na uhamisho wa watu. Watu wanalia kwa sababu baada ya kurudi kutoka uhamishoni hawauoni tena mji wa Yerusalemu katika utukufu uliokuwa nao mwanzo. Hata hivyo, nabii anawaandikia wafurahi, wafurahi kwa sababu Mungu yuleyule aliyewatoa utumwani sasa anawaahidi kuwa mji wa Yerusalemu utajengwa upya: amani yake itarejea, utukufu wake utarudi nao wataufurahia mji wao kama mwana anavyomfurahia mamaye anayemfariji.

Uinjilishaji ni asili na utume wa Mama Kanisa kwa watu wa Mataifa
Uinjilishaji ni asili na utume wa Mama Kanisa kwa watu wa Mataifa

Somo la Pili (Gal. 6:14-18 ) ni kutoka Waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia. Katika waraka huu, Paulo amepambana vikali sana na wahubiri wa kiyahudi walisisitiza uyahudi wao kuliko imani kwa Kristo. Katika barua hii nzima kwa Wagalatia Paulo anaonesha kuwa mtu anakombolewa kwa imani kwa Yesu Kristo na wala si kwa matendo ya sheria au mila za kiyahudi na mapokeo ya wazee yao. Katika somo hili ambalo ni sehemu ya mwisho ya waraka kwa wagalatia, Paulo anahitimisha waraka kwa kusisitiza kwa mara nyingine tena kuwa yeye haoni fahari juu ya kitu chochote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Japokuwa naye ni Myahudi lakini haoni kuwa utu wake wa sasa kama mkristo unajipambanua kwa Uyahudi wake: katika tohara au mila za kiyahudi, bali katika kile ambacho msalaba wa Kristo umempa, yaani ukombozi na neema. Somo hili linatualika tutafute kuweka uwiano sahihi kati ya imani na mila zetu  (pamoja na desturi na tamaduni). Mila zinatupatia utambulisho wetu katika jamii, imani inatupatia lengo letu la maisha.  Vyote viwili hutoka kwa Mungu na hutusaidia kuishi vema kama anavyokusudia Mungu mwenyewe muumba wetu. Kwa sababu hii haviwezi kupingana isipokuwa kama mila zenyewe ni potofu. Mtume Paulo anajiweka leo kama kielelezo cha  kuitanguliza imani kama msingi wa kuzipembua mila njema za kuzifuata na zile zisizo njema za kutokuzipa nafasi.

Mama Kanisa analo jukumu la kuinjilisha na kutamadunisha.
Mama Kanisa analo jukumu la kuinjilisha na kutamadunisha.

Injili (Lk 10:1-12, 17-20) Katika Injili ya dominika ya leo, Kristo anawatuma wafuasi wake kumtangulia katika kila mji alipokusudia kwenda. Idadi ya wafuasi waliotumwa inatajwa kuwa 70 na wakati mwingine 72. Hii ni namba ya kibiblia inayomaanisha idadi ya mataifa yote. Yesu kutuma idadi hiyo anamaanisha kuwa utume wa wafuasi wake ni wa kwenda katika mataifa yote. Katika kitabu cha Mwanzo 10:1:1-30 yanatajwa mataifa yote ya dunia (yaliyojulikana). Biblia ya kihebrania inayahesabu kuwa 70 na ile ya Kigiriki (Septuaginta, LXX) inayahesabu kuwa 72. Hii ndiyo sababu kuwa katika tafsiri iliyotokana na kiebrania inataja wafuasi 70 na ile iliyotokana na Kigiriki inataja wafuasi 72, ila lengo ni lilelile la kuhusisha idadi ya wafuasi wanaotumwa na idadi ya kibiblia ya mataifa ya ulimwengu. Wanatumwa wawili wawili ili kusaidiana wawapo safarini na utumeni. Lakini pia kadiri ya Kum 19:15 ushahidi unaoaminika si wa mtu mmoja bali wawili. Yesu anawatuma akiwaambia “mavuno ni mengi lakini watendakazi ni wachache”. Katika mazingira karibu yote, kipindi cha mavuno ni kipindi kinachohitaji kazi  ya haraka vinginevyo mazao yataharibikia shambani na kazi ya msimu wote inakuwa imepotea. Manabii katika Agano la Kale walitumia pia lugha ya mavuno kumaanisha hukumu ya siku ya mwisho inayokuja upesi (rej. Yoeli 3:13, Mik 4:11-13). Vivyo hivyo Yesu anajulisha kuwa utume anaowapa ni utume unaohitaji daima kipaumbele: kupewa nafasi ya kwanza. Ndiyo maana anawaambia wasipoteze muda njiani na wla wasijishikamanishe na vitu vinavyoweza kuwaondoa katika lengo lao la msingi ambalo ni utume. Mwisho injili inaonesha kuwa wafuasi wanaojikita katika utume wao na kushika kiaminifu maelekezo ya Bwana wao hujaliwa furaha kama zawadi na tena furaha ya kuwa majina yao yanaandikwa mbinguni.

Injili ya Kristo Inapaswa kuwa ni chemchemi ya furaha
Injili ya Kristo Inapaswa kuwa ni chemchemi ya furaha

TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Kanisa linao utume ulimwenguni. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unafundisha kuwa Kanisa limetumwa na Mungu kwa mataifa yote ili liwe Sakramenti ya Wokovu kwa wote. Nalo kwa asili ya ukatoliki wake na kwa kulitii agizo la Kristo mwanzilishi wake, linafanya bidii ya kuitangaza Injili kwa watu wote ili Neno la Mungu liendelee na kutukuzwa na Ufalme wa Mungu utangazwe na kusimikwa duniani kote (rej. Ad Gentes 1). Hata leo hii utume wa Kanisa unahitajika na utaendelea kuhitajika mpaka Kristo atakaporudi. Habari njema inahitaji kuhubiriwa, Kristo anahitaji kushuhudiwa na sakramenti za wokovu zinahitaji kuadhimishwa kwa ajili ya wokovu wa taifa lote la Mungu. Masomo ya leo yanatualika sote kama wanakanisa kuzidi kujikita kuuendeleza utume wa Kanisa katika changamoto za nyakati. Na kwa namna ya pekee yanatualika kutambua kuwa ujenzi wa haki, amani na uundaji wa jamii bora ni mojawapo ya maeneo ya utume wa moja kwa moja wa Kanisa. Kama kanisa tunaalikwa leo tuzidi kujibidiisha katika kujenga haki na amani: kuweka amani kama mojawapo ya vipaumbele vya utume wetu, kuwa wajumbe wa amani na upatanisho na kuwa mstari wa mbele kulinda amani katika jamii zetu. Tunaona pia kuwa mwendelezo wa utume wa Kanisa haupingani hata kidogo na utambulisho wa watu katika mila na tamaduni zao. Vyote kama tulivyoona katika tafakari ya masomo, vyatoka kwa Mungu na vinamhusu mtu yuleyule hivyo haviwezi kupingana. Imani humsaidia mtu kuziishi vema mila na tamaduni zake kwa kuziendeleza mila njema na kutozipa nafasi zile zinazipingana na utu kama alivoukusudia Mungu muumbaji.

Liturujia D14
01 July 2022, 15:40