Tafakari Dominika ya 17 Mwaka C: Nguvu na Umuhimu wa Sala Katika Maisha ya Waamini
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 17 ya Mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanasisitiza juu ya nguvu ya sala ya mwenye haki inayotoka ndani ya mtima wa moyo wake, isiyo na hila wala mawaa ndani yake na umuhimu wa kusali bila kuchoka, kila mara na kila wakati, tukimshukuru Mungu kwa kila jambo (1Thes. 5:17-18). Yeye ni Baba yetu mwema anayetupenda na kutujalia mahitaji yetu ya kila siku. Somo la kwanza kutoka kitabu cha Mwanzo (Mwa 18: 20-32); linatuonesha nguvu ya sala ya mtu mwenye haki. Abrahimu Baba wa imani, mtu mwenye haki anasali na kuomboleza kwa sababu ya dhambi za watu Sodoma ili Mungu asiwaangamize. Dhambi humtenga mtu na Mungu. Dhambi inaua mahusiano kati ya mtu na Mungu. Kwa kutenda dhambi mwanadamu anapoteza urafiki na Mungu muumba wake, anakuwa mbali naye na kupoteza uhusiano mwema naye (Mwanzo 3). Hivyo sala na maombi yake hasikilizwi tena na Mungu. Nabii Isaya anasema; “Dhambi zenu ndizo zinazowatenga na Mungu wenu, dhambi zenu zimemfanya Mungu ajifiche mbali nanyi hata asiweze kuwasikieni” (Isaya 59:2). Dhambi humtenga mtu na wengine na huathiri mahusiano yake na wengine. Aidha, tunapowadhuru wengine kwa mwenendo wetu mbaya tunamgusa pia Mungu mwenyewe kwani kila mtu ameumbwa kwa sura na mfano wake Mungu. Zaidi sana, dhambi humtenga mtu na nafsi yake mwenyewe. Ukitenda dhambi hadhi ya kuwa mtoto wa Mungu anayestahili kupendwa na kuheshimiwa inashuka. Rejea mfano wa mwana mpotevu (Luka 15).
Maisha mazuri, furaha na amani vinapotea na unaanza kusota (Mwanzo 3-4). Taabu, mateso na mahangaiko vinakuandama unazongwa na maumivu ya kimwili kama ni dalili tu za uozo uliomo ndani, mtu anakuwa mkorofi, mgomvi, msingiziaji kwani ili kujipatia faraja lazima mdhambi awapakazie wengine maovu yake, akijihami kwani anadhani anaonewa daima, hapendi upatano na wenzake, kwake amani ni kama mwiba ndani kwake. Mwisho wa yote huingia kifo cha mwili na cha roho maana mshahara wa dhambi ni mauti, ni kifo (Warumi 6:23; Luka 15:32). Kama Abrahamu baba wa imani, mtu mwenye haki alivyosali kuiombea Sodoma isiangamizwe kwa dhambi zake, vivyo hivyo nasi tunapaswa kusali na kujiombea sisi wenyewe kwa dhambi zetu na za wengine ili tusiangamizwe nazo. Lakini ili sala zetu zisikilizwe yatupasa kwanza kujipatanisha na Mungu, kutubu dhambi zetu, kujipatanisha na wenzetu, kutoa msamaha kwa waliotukosea, kufanya malipizi na kujisamehe sisi wenyewe. Tukijiwekea hazina katika utu wema na mahusiano mema na watu pamoja na Mungu na pia tuwe wepesi wa kujirekebisha kasoro zetu.
Somo la pili kutoka Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai (Kol 2: 12-14); linatueleza kuwa mkristo wa kweli ni mtu yule ambaye kwa ubatizo amekuwa sehemu ya mwili wa Krsito yaani Kanisa. Paulo anasema, kama vile tohara, katika Agano la Kale, ilivyokuwa alama ya kuwa mshiriki wa taifa la Mungu, vivi hivi ubatizo hutufanya washiriki wa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ambaye ameifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomelea msalabani, (Kol 2:14). Ukombozi huu ni wa dhamani sana ndiyo maana Mtume Petro anasema; “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani ya mwana-kondoo asiye na hila, asiye na waa, yaani, ya Kristo” (1Pet 1:18-19). Hivyo yatupasa tuwe kielelezo cha Kristo mkombozi wetu, katika maisha yetu ya kila siku kwa maneno na matendo tukiyavumilia mateso na msumbuko yanatupata tukiishuhudia imani yetu.
Injili ilivyoandikwa na Luka (Lk 11:1-13); inatufundisha umuhimu wa sala na namna tunavyopaswa kusali. Yesu ni kielelezo chetu cha maisha ya sala. Yeye katika kila jambo alilolifanya alianza kwa sala. Katika nafasi mbalimbali, Yesu alienda mahali pa faragha hasa milimani nyakati za usiku il kusali. Wakati akingoja kubatizwa na Yohani huko mtoni Yordani, Yesu alisali (Lk 3:21), kabla ya kuwachagua mitume wake 12, Yesu alikesha usiku mzima akisali (Lk 6:12). Yesu alimwombea Petro, ili akiisha kukomaa katika Imani awaimarishe na wenzake (Lk 22:32). Yesu alisali kabla ya kugeuka sura: “Aliwatwaa Petro, Yohani na Yakobo, akapanda milimani ili kuomba” (Lk 9:27-28). Alisali Wagiriki walipotaka kumwona: “Sasa roho yangu inafadhaika; nami nisemeje? Baba uniokoe katika saa hii? Lakini ni kwa ajili ya hayo nilivyoifikia saa hii. Baba ulitukuze Jina lako. Basi ikaja sauti kutoka mbinguni ikasema: “Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena” (Yn 12:27-28). Mda mfupi kabla ya kuteswa alikwea Mlima wa mizeituni na huko akasali: “Akaenda mbele kidogo akaanguka kifudifudi, akaomba akisema; Baba yangu ikiwezekana kikombe hiki nikiepuke, walakini si kama nitakavyo mimi, ila mapenzi yako yatimizwe. …hamkuweza kukesha nami walau kwa saa moja? Kesheni msije mkaingia majaribuni, roho i radhi lakini mwili ni dhaifu” (Mt 26:39-42). Pale juu msalabani Yesu alisali: “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha” (Mt 27:46).
Yesu alisali kabla ya kumfufua Lazaro: “Baba nakushukuru kwa kuwa umenisikia, nami nalijua ya kuwa wewe wanisikiliza siku zote, lakini kwa ajili ya mkutano huu wanaoshiriki nalisema haya, ili wapate kusadiki kwamba wewe ndiwe uliyenituma” (Yn 11:41-42). Na wakati wa karamu ya mwisho, tunayo ile sala pekee ndefu ya kikuhani kwa ajili ya wateule wake (Yn 17). Mitume wake walivyoona jinsi alivyokuwa mtu wa sala walimwomba awafundishe kusali naye akawafundisha sala ya Baba Yetu. Luka katika injili ya dominika hii ya 17 mwaka C ameiandika tofauti na Mathayo (Mt 6:9-13). Katika sala hii, Yesu anatufunulia kuwa Mungu ni Baba mwenye huruma anayetutunza, siyo hakimu. Hivi tumwombe kwa imani na matumaini atujalie ridhiki kwa maisha yetu. Yesu anasisitiza; “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa. Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa”. Lakini sharti ni kuwa lazima nasi tuwapatie wanaoomba, tuone mahitaji ya wanaotafuta, tuwafungulie wanaopiga hodi, tuwasaidie wahitaji, tuwasamehe wanaotukosea na kuomba msamaha kwa kuwa nasi tu wakosefu tunahitaji kusamehe kama anavyosema Mtakatifu Agustino; “Basi ni hivyo hivyo masharti ya kusamehewa ni kusamehe bila masharti”. Tujitahidi kuwa watu wa haki na kweli siku zote katika maisha yetu ili tuwe kweli wana wa Mungu walio huru kwani ukweli unatuweka huru.
Tukumbuke kuwa sala ni tendo la imani la kuongea na Mungu. Katika mazungumzo haya kuna pande mbili. Binadamu anapoongea, Mungu anamsikiliza, na Mungu anapoongea, mwanadamu anapaswa kusikiliza. Kumbe sala yetu inapaswa kuwa na pande mbili: kuongea na kusikiliza. Tukisali tu bila kusikiliza anachotuambia Mungu matokeo yake ni kutokupata tunachoomba, kwa sababu tunampangia Mungu atupatie kile tunachotaka. Mtume Yakobo anasema; “Mnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya na mnaomba ili mpate kutosheleza tamaa zenu” (Yk. 4:3). Kitabu cha kutoka kinasimulia tukio ambalo litatusaidia kuelewa jambo hili: “Kila asubuhi, Mwenyezi Mungu aliwapatia Waisraeli Manna huko jangwani”. Wakati manna hiyo ilipoanguka kwa mara ya kwanza baadhi ya watu walijilimbikia kuliko kile walichohitaji kwa siku, na kule kujilimbikizia kwao kulifanya kile cha ziada kioze (Kut 16:19-21). Hali hii iliwafanya Waisraeli watambue kwamba wanapaswa kuweka matumaini yao kwa Mungu kwamba atawajalia kila wanapohitaji na wasiwe na ubinafsi wa kujilimbikizia na wawe wasikivu Mungu anapoongea nao na kuwapa maelekezo. Mwisho, tunaposali tusali kwa unyenyekevu, tumruhusu Mungu atimize mpango wake katika maisha yetu, tusimpangie Mungu. Basi tujibidishe kusali, tuwapo nyumbani na sehemu zetu za kazi, asubuhi, jioni, kabla na baada ya kulala. Tushiriki pia katika sala za Jumuiya Ndogondogo za Kikristo tukikumbuka kuwa Yesu alisema; “wakusanyikapo wawili au watatu kwa jina langu nami nipo kati kati yao”. Tumsifu Yesu Kristo.