Tafakari Dominika XV ya Mwaka C: Upendo Kwa Mungu na Jirani
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama! Tusi kubwa kabisa ambalo ungeweza kumtusi nalo Myahudi ni kumwita “mbwa” au “mpagani”. Na la pili kwa uzito au ukubwa ni kumuita “Msamaria”, kwani ilikuwa ni sawa na kumuona kama mshenzi, mzushi, aliyekataliwa na kukosa uhalali, au mwanaharamu. (Hekima ya Yoshua Bin Sira 50:25-26 na Yohane 8:48). Wasamaria hawakuwa Wayahudi kwa asilimia mia kwani waliiishi na kuchanganyika na wapagani au watu wa mataifa mengine, na hivyo kujikuta kupoteza baadhi ya mapokeo ya wazee wao na hata ibada zao. Wasamaria hawakukubali na kupokea kama Neno la Mungu vitabu vya Manabii, vitabu vya Hekima na hata Zaburi. (Yohane 4:22 na Luka 9:53) Hivyo Wasamaria walionekana kuwa ni wazushi na watu wasiokuwa na dini sahihi ya mababu wa Taifa la Israeli. Sehemu ya Injili ya leo inajulikana na wengi na hasa ikitambulishwa kama Injili ya Msamaria Mwema. Kwa kweli kivumishi sifa za mwema hakipo katika Maandiko Matakatifu, na hivyo si sahihi sana kuendelea kuitambua kwa jina hilo na badala yake ningewaalika tangu mwanzo tuitambue kama Injili ya Msamaria kwa sababu ambazo nitajaribu kuziweka katika tafakari yetu.
Injili inamtaja Msamaria mmoja aliyekutana na mtu aliyepigwa, kuvuliwa nguo na wanyang’anyi na kuachwa karibu ya kufa. Injili haisemi na wala Yesu hakuthubutu kumwita mwema bali anatumia kuwa fundisho kwetu juu ya jirani yangu ni nani. Yesu anajibu maswali kwa kuuliza maswali, anataka kila mmoja wetu atoe jibu kwa kadiri ya muktadha, hakuna majibu kabla ya muktadha na anatualika nasi kujiuliza maswali katika kila muktadha na kuacha kuwa na majibu tayari kwa kila muktadha. Anayekuja mbele ya Yesu na kumuuliza ili amjaribu sio Msamaria bali ni Myahudi, sio mdhambi bali ni mwenye haki, mtaalamu wa Sheria, yaani Torati: “Nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Mara moja unaona ni swali la mmoja anayejua Teolojia au Taalimungu vizuri, haulizi jinsi ya kuupata uzima wa milele bali kuurithi uzima wa milele. Urithi ni ule tuupatao sio kwa mastahili yetu bali daima kama zawadi, hivyo anatambua tangu mwanzo uzima wa milele ni neema, ni zawadi na upendeleo wa Mungu kwetu sisi wanadamu tulio wadhambi, ni kwa kuutegemea wema na huruma yake nasi tunastahilishwa uzima huo wa Kimungu.
Yesu hatoi jibu kwa swali la huyo Mwana sheria na badala yake anajibu swali kwa kuuliza swali. Mwanasheria anajibu swali la Yesu kwa kunukuu Maandiko Matakatifu. Nukuu ya kwanza inajulikana na kila Myahudi kwani ilikuwa pia ni sala kwa kila asubuhi na jioni walipaswa kukiri na kuisali sala hiyo ya kumpenda Mungu kwa nguvu, kwa akili na kwa kila namna. Ni utambulisho wao kuwa wao ni watu na Taifa lake Mungu na pia kuweka ahadi ya kubaki kuwa waaminifu kama vile Mungu alivyo mwaminifu. (Kumbukumbu 6:5) Na ya pili ya kumpenda jirani kama nafsi yako anainukuu kutoka kitabu cha Mambo ya Walawi 19:18. Hakika ni majibizano ya wataalamu wawili wa Maandiko Matakatifu. Yesu anastaajabishwa na hata anamsifu kwa kujibu vema, kwa kunukuu vema Maandiko. Ila Yesu leo anatukumbusha pia nasi tunaweza kuwa wataalamu wa Maandiko kwa kichwa au kwa akili ila kama alivyosema kwa Mwanasheria anasema pia na kwetu; fanya hivi nawe utaishi. Injili au Neno la Mungu linatualika kuliishi, kuliweka katika maisha yetu ya siku kwa siku, na hapo tunakuwa na hakika ya kuurithi uzima wa milele.
Mwanasheria hakutaka kuishia hapo kwa vile nia yake ni kumjaribu Yesu alizidi kumuuliza Yesu na jirani yangu ni nani? Kwa haraka haraka tunaweza kuona ni swali la kijinga au swali jepesi na rahisi. Kwa kweli hapana. Ulikuwa ni mjadala mzito kati ya Marabi au Waalimu wa Kiyahudi juu ya mipaka ya jirani, nani hasa napaswa kumchukulia kuwa ni jirani yangu? Wapo walioamini jirani ilikuwa ni kwa wale walio Wayahudi tu, hivyo walipaswa kuwapenda wana wa Abrahamu tu. Na wengine walipanua zaidi uwigo na kuwahusu pia hata wale wasiokuwa Wayahudi ila walioishi pamoja nao na hata kuanza kushika sheria na taratibu zao za kimapokeo. Hivyo karibu makundi yote yaliamini kuwa jirani halikuhusu maadui zao kama taifa teule. Ni katika muktadha huo tunaona Yesu anatumia fursa hiyo kutoa tafsiri sahihi na kamilifu ya Maandiko Matakatifu kwa kumpa mfano wa Msamaria mwema. Yesu anabadili mtazamo wao na hata wetu kuwa cha muhimu sio kile ninachojua au kusema au kukiri bali cha muhimu ni kile ninachokifanya. Mtu mmoja alishuka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko. Umbali wa Yerusalemu na Yeriko ni takribani kilomita 27. Ni mteremko mkali sana na pia njia inakatiza jangwani hata kufika Yeriko. Yeriko ni mji wa mitende, mji uliojulikana kuwa ni wa anasa kwani Herode pia alikuwa na nyumba ya pili hapo na si yeye tu bali hata na Wayahudi matajiri walikuwa na nyumba au makazi ya pili Yeriko. Hivyo si ajabu kukuta baadhi ya Makuhani au Walawi si tu walikuwa na nyumba Yerusalemu bali pia Yeriko. Ni kujaribu kujibu swali kwa nini njiani tunakutana na Kuhani na Mlawi.
Njia hii ya hatari si tu kwa sababu za kimuundo wa kijiografia bali pia ilijulikana na Yesu tangu utoto kwani daima walipanda kwenda Yerusalamu pamoja na wazazi wake kadiri ya Mwinjili Luka. Huyo “mtu mmoja” hatujui lolote juu yake, wala kabila lake, wala dini yake, wala wadhifa wake, wala rangi yake, wala hali yake kama alikuwa mwema au muovu. Tofauti na wengine wote wanapewa utambulisho zaidi ila huyu anatajwa kuwa mtu mmoja. Si kwa nasibu au kwa ajali hapewi utambulisho wa zaidi. Utu wa mtu hautegemei dini au imani, rangi au kabila, au jinsia au utaifa au wema wake bali daima yafaa tukumbuke kwa kila mwanadamu tunakutana na sura ya Mungu (Imago Dei). Mtu mmoja anayeangukia kati ya wanyang’anyi, anavuliwa nguo, anatiwa jereha na kuachwa karibu ya kufa ni nani? Mtu huyo ni karibu kila mmoja wetu katika safari ya maisha amekutana na majeraha na kuumizwa na hata kuachwa karibu ya kufa. Hivyo, njia ile ya hatari ya kutoka Yeriko kwenda Yerusalemu, ndio safari ya maisha ya kila mmoja wetu. Tungali safarini hapa duniani hakika tunakutana na mengi yanayotuumiza na hata kutuacha katika hatari ya kifo. Kila mmoja wetu amekuwa kati ya hawa wanyang’anyi kwa namna mbali mbali katika kuwaumiza na kuwajeruhi wengine, ni vile sawa kuwa kila mmoja wetu pia anakuwa ni kielelezo cha huyu mtu mmoja.
Kwa nasibu walipita njia hiyo hiyo kuhani na Mlawi. Neno nasibu halitumiki kwa ajali pia hapa kwani mara nyingi tunajiuliza lini na wapi napaswa kufanya tendo la huruma au wema? Sio kwenda na kuwatafuta au kuwasaka wenye shida ili kuwasaidia bali tunakutana nao katika nafasi na hali mbali mbali katika maisha yetu. Nasibu ni kuonesha kuwa wahitaji na wenye shida tunakutana nao katika maisha kama ajali, kwani hatuwezi kujua lini na wapi. Yesu anatolea mfano watu wawili waliokuwa Wayahudi na zaidi sana walikuwa viongozi wa dini yaani kuhani na Mlawi. Kwa hakika ni watu waliojua Maandiko na hata walikuwa pia watu wa sala waliokwenda Hekaluni kusali na kutolea sadaka za wanyama na kulipa zaka. Labda tujiulize kwa nini Yesu anatolea mfano watu hawa viongozi wa dini? Ni fundisho pia kwetu leo kuwa hatupaswi kuwa watu wa kushika dini kwa mazoea na mapokeo na hivyo kukwepa wajibu wetu wa kwanza wa kumpenda Mungu kupitia jirani muhitaji. Mara ngapi sisi tunabaki na dhamiri tulivu kwa kuwa tumeshiriki kwenye ibada na huku tukikosa upendo kwa jirani, tukikosa moyo wa msamaha na huruma kwa wengine?
Mmisionari Madeleine Delbrel huko Paris Ufaransa aliwahi kusema; “Ikiwa kweli Mungu ameingia ndani ya moyo wa mtu, basi hilo litaonekana hata katika ngozi ya mtu yule.” Na hata mahujaji walipomwona Mama Teresa wa Kalkuta walipenda kusema: “Macho yake yaliakisi wema na utulivu kana kwamba ni dirisha la Mungu kwalo akituangalia wanyonge na kutabasamu.” Upendo unaakisi na kuambukizwa kirahisi kwa watu wanaotuzunguka kama kweli tunampenda Mungu na jirani. Upendo unajiimba sifa zake wenyewe! Kuhani na Mlawi walipita njia ile na wakaona na kupita mbali na kwenda zao. Labda walikuwa na hofu ya kukutwa na wanyang’anyi na kuumizwa na kujeruhiwa kama huyo mtu mmoja, labda walijali zaidi usafi wao wa kiibada hivyo kukwepa kumgusa mtu mwenye majeraha wakajikutana wananajisika kwa kushika damu, au waliogopa kuwa amekufa na kwa taratibu zao wasingeruhusiwa tena kushiriki ibada yeyote hekaluni kwao kwa kushika maiti wanakuwa najisi, tunaweza kutaja na kuweka sababu nyingi bila mwisho hapa.
Wanatokea Yerusalemu kwa hakika walitoka kushiriki ibada fulani fulani hekaluni. Makuhani walipangwa kwa zamu kutoa huduma hekulani mfululizo kwa muda wa wiki nzima. Ni kwa kiasi gani ibada zao zimewasaidia kumwangalia huyu mtu mmoja kwa jicho moja na Mungu? Wapendwa kusali na kufanya ibada lengo na nia sio kumshawishi Mungu atende kama tutakavyo sisi bali kumuomba atujalie nasi neema za kupokea mapenzi yake na hivyo kutaka kuona maisha sio kwa jicho letu bali kwa jicho la Mungu. Ni kutaka tufikiri, tuseme, tutende kama Mungu na si kinyume chake. Sala na ibada zetu zinapoteza uhalali na uthamani wake kama bado tunabaki sisi wenyewe na kukosa kuona pamoja na jicho la Mungu, na hasa kwa wanaohitaji huruma na upendo wetu. Wasikilizaji wa mfano huu wa Yesu wanasubiri bila mashaka baada ya kutajwa viongozi wawili wa dini kuwa sasa amtaje mlei lakini Myahudi na si kinyume chake. Labda hata baadhi ya wanakanisa leo hasa wanaokuwa kinyume na makuhani yaani (anti-clericalism) wangetarajia atajwe mlei mmoja, anayeheshimika na kuonekana anafaa zaidi kuliko makuhani. Ila Yesu anamtaja kwa mshangao wao Msamaria mmoja.
Yesu si tu anamtaja Msamaria bali anatueleza hata kwa undani kwa kila hatua na tukio analolifanya. Msamaria kinyume na kuhani na Mlawi: anamwona, anamkaribia, anamuhurumia, anamtibu majeraha yake kwa kumpaka mafuta na divai, akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka nyumba ya wageni na kumtunza kwa maana ya kumgharamia pia kwa pesa zake na kutoa maagizo kwa mtunza nyumba juu ya wajibu wa kumwangalia huyu muhitaji. Mbele ya huyu mhitaji tunaona Msamaria hafuati kichwa au akili yake bali moyo wake. Anasahau mambo yake na safari zake na mipango yake, anaweka kando sheria za kidini, uchovu wake, njaa yake, woga, anaweka hayo yote kando na kumsaidia huyu anayekuwa katika uhitaji kwa wakati huo bila kujiuliza au kukwepa wajibu huo kwa sababu kadha wa kadha. Ndugu zangu tunaishi katika ulimwengu wa kutokujali au kila mmoja afanye yake na ashinde mechi zake, kila mmoja na lwake. Ni ulimwengu wa kuona mtu anapata ajali tena mbaya na kubwa, badala ya kuokoa maisha, leo ni kawaida kuona kila mmoja na simu yake na kuwasha video kamera na kuanza kurekodi tukio. Tuna mifano mingi tunaweza kuitoa hapa kujihoji sisi wenyewe katika mazingira yetu ya siku kwa siku. Ni mara ngapi tumebaki bila mioyo kwa maana ya kutoguswa na shida ya mwingine?
Yesu leo kama alivyohitimisha mfano huu wa Msamaria kwa kumuhoji mwanasheria kadiri yake ni nani alikuwa jirani yake hapa, ni swali hilo hilo anaendelea kuniuliza mimi na wewe kila mara tunapokutana na wahitaji wa aina mbali mbali katika maisha. Labda sio tu wahitaji wa mali au vitu bali hasa upendo na huruma, ni mara ngapi tunahukumu na kulaani? Narudia kila mmoja kwa namna mmoja au nyingine anaangukia katika kundi la huyu mtu mmoja na vile vile kila mmoja wetu pia anahusika katika kundi la wanyang’anyi na watesi katika safari ya maisha yetu hapa duniani. Mwanasheria hata sasa Yesu anapomuuliza swali ni nani alikuwa jirani anakwepa kutaja jina Msamaria, labda ni kichekesho kwani ni Myahudi ambaye si tu bado anabaki na mtazamo wake wa awali hata baada ya kusaidiwa na Yesu kupata tafsiri mpya ya nani ni jirani yake, anakwepa hata kutaja jina Msamaria kwani kwake ni sawa na kujitanabaisha na huyo mpagani.
Mwaliko wa Yesu kwa mwanasheria ndio mwaliko kwangu na kwako ndugu yangu yaani kwenda na kufanya nasi kama alivyofanya huyo Msamaria. Naomba tubaki kumtambua kama Msamaria kwani kumuita Msamaria mwema ni sawa na kukwepa wajibu wetu kwa kisingizio alifanya alichofanya kwa kuwa alikuwa mwema, kwa kweli hapana alitenda alichofanya kwa sababu alitii msukumo na mguso wa moyo wake, kutenda wema kwa mwanadamu ni asili yetu kwani daima mioyo yetu inatusukuma kutenda matendo mema na ya huruma kwa wengine wanaohitaji, sio sifa kwa baadhi tu bali ni sifa asili ya kila mwanadamu bila kujali rangi, taifa, dini, itikadi za kisiasa, au tofauti zozote zile za nje. Na jirani yangu daima anabaki kuwa ni mtu mmoja ninayekutana naye katika maisha anayekuwa katika uhitaji, bila kujali namfahamu au la, wa karibu yetu au la, wa dini yetu au la, wa rangi yetu au la, wa itikadi yetu au la, wa kabila letu au la, au Kanisa letu au la, au wa jumuiya yetu au la. Tuzidi kumuomba Mungu neema ya kutufanya tuwake mapendo yake katika safari ya maisha yetu na pia atusaidie kuepuka nafasi za kuwaumiza na kuwajeruhi wengine katika maisha yetu ya siku kwa siku. Tusali ili kwa njia na hasa ushuhuda wa maisha yetu wengine wapate kukutana na upendo na huruma ya Mungu. Nawatakia tafakari na Dominika njema.