Nifanye nini? Ni swali la msingi na zuri tunalokutana nalo mara kadhaa katika Injili ya Luka na Kitabu cha Matendo ya Mitume. Makutano, watoza ushuru, maaskari wanamuuliza Yohane Mbatizaji tufanye nini?  Nifanye nini? Ni swali la msingi na zuri tunalokutana nalo mara kadhaa katika Injili ya Luka na Kitabu cha Matendo ya Mitume. Makutano, watoza ushuru, maaskari wanamuuliza Yohane Mbatizaji tufanye nini?  

Tafakari Dominika ya 25 ya Mwaka C wa Kanisa: Dumisheni: Uaminifu na Urafiki Kati ya Mungu na Jirani

Tutambue kwamba, kila tulichonacho si mali yetu, bali tumewekwa kuwa mawakili tu, hivyo hatuna budi kutumia kwa ajili ya huduma na kujenga urafiki na wengine. Hatuna budi kuwa mawakili waaminifu na kutumia yote si kwa ubinafsi bali tukikumbuka umuhimu na ulazima wa kujenga urafiki ili tuweze kuja kukaribishwa nao si tu katika ulimwengu huu bali katika maisha ya umilele.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma

Amani na Salama! Mfano wa wakili mjanja na asiyekuwa mwaminifu, unakuwa na ukakasi mwingi, kwani si mfano chanya hasa kwetu tulio rafiki na wafuasi wake Yesu Kristo tunaoalikwa kila mara kuwa waaminifu katika maisha. Hivyo kuupata ujumbe wa Injili ya leo nawaalika tutafakari kwa pamoja na kwa makini, maana kinyume chake tunaweza kuukosa ujumbe kusudiwa wa Bwana wetu Yesu Kristo, juu ya simulizi la wakili asiye mwaminifu. Wataalamu wa Maandiko Matakatifu wapo wanaotueleza kuwa wakili mjanja, alikuwa ameweka mahesabu ya uongo kwa wadeni wake, ili baada ya kupoteza kazi aweze kukaribishwa nao; na wengine wanasema kuwa alifanya mahesabu ya uongo na wizi kabla, na hivyo kupelekea kufukuzwa kazi na mmiliki wa shamba. Yamkini zote mbili bado zinatuonesha kuwa wakili yule hakuwa mwaminifu katika mahesabu na mali au fedha. Ilikuwa ni desturi nyakati zile za Yesu kwa matajiri wakubwa kumiliki ardhi kubwa, na kuiweka chini ya mawakili au waangalizi wa mashamba yao, na wao waliishi sehemu za mijini, hivyo hawa mawakili walipaswa kila mwaka kutoa hesabu na faida kwa wamiliki wa mashamba yale na wao walibaki na ile ziada kama sehemu ya ujira wao.

Kwa ujanja wao mara nyingi hawa mawakili walitoa hesabu za uongo, iwe kwa wamiliki wa mashamba lakini zaidi sana kwa kutoa ujira mdogo kwa maskini waliotumika kama vibarua wa mashamba yale. Hivyo waliweza kufanya ujanja au wizi iwe kwa matajiri wamiliki wa mashamba, lakini pia hata kwa watu maskini waliotumika kuzalisha kwa ujira mdogo sana, kama ambavyo tumesikia katika somo la kwanza la leo kutoka Nabii Amosi, nabii na mtetezi wa haki ya wanyonge. Hivyo yafaa kusoma sehemu ya Injili yetu ya leo kwa kurejea muktadha wa nyakati zile za Yesu, ambazo pia si tofauti sana na hata nyakati zetu za leo. Wakili sio mmiliki, bali kuna mwenye shamba, na hivyo anatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya mali za mmiliki. Na hata wakili tunaona katika tafakari yake anajiuliza maswali mengi kichwani na moyoni mwake. Ni mmoja anayekubali makosa yake na hivyo mara moja kufikiri nini atafanya akiwa hana tena kazi ile ya kuwa mwangalizi au wakili wa shamba.

Waamini wanahimizwa kuwa waaminifu na marafiki wa Mungu na jirani
Waamini wanahimizwa kuwa waaminifu na marafiki wa Mungu na jirani

Nifanye nini? Ni swali la msingi na zuri tunalokutana nalo mara kadhaa katika Injili ya Luka na Kitabu cha Matendo ya Mitume. Makutano, watoza ushuru, maaskari wanamuuliza Yohane Mbatizaji tufanye nini?  Mkulima tajiri tuliyemsikia Dominika kadhaa zilizopita naye baada ya mavuno mengi anajiuliza nifanye nini? (Luka 12:17) Na hata wasikiliza wa Mtume Petro siku ile ya Pentekoste wanajiuliza, ndugu tufanye nini? Ni swali la msingi sana kila mara unapojikuta mbele ya uchaguzi wa maisha. Wakili asiye mwaminifu anajua kuwa hana muda mrefu kabla ya kuachishwa kazi yake. Kama mkulima tajiri aliyetafakari moyoni mwake afanye nini kuhusu mavuno yake mengi, ndivyo hivyo naye anatafakari moyoni mwake la kufanya baada ya kufukuzwa kazi.  Yeye anajua kufanya kazi hiyo, na hivyo anatambua udhaifu wake kuwa hawezi kulima na hata kuombaomba anaona aibu. Mara moja linakuja wazo kichwani mwake, anatambua nini cha kufanya kwani kabla ya kuacha kazi hana budi kufunga na kukabidhi mahesabu kwa mmiliki wa shamba lile, na hivyo anawaita wadeni wake wote.  Wakili huyu mjanja hakuomba ushauri kwa mtu yeyote, au wale waliokuwa wanafanyakazi kama yake na badala yake anang’amua yeye mwenyewe nini cha kufanya katika hali ile, ni matokeo ya tafakari yake na hasa kuzingatia uzoefu wa ile kazi yake.

Anatambua jinsi gani aliweza kukosa uaminifu kwa wadeni wake, kama nilivyotangulia kusema kuwa mara nyingi waliwapa mahesabu ya uongo iwe kwa wadeni, lakini pia hata kwa wamiliki wa mashamba yale. Angeliweza kwa hakika kujipatia tena mali kwa njia ile ile ya uongo na wizi, lakini safari hii hachagui kuwaibia zaidi mali bali kujenga nao urafiki! Ni uchaguzi wa urafiki na si wa mali! Ni uamuzi sahihi ambao Yesu anausifu na ndio uamuzi tunaopaswa kuufanya kila mmoja wetu, kutumikia na kujenga urafiki na wale wote tunaokutana nao katika maisha ili kujiwekea akiba ya kudumu na si mali za ulimwengu huu ambazo zote ni za kupita na za muda tu. Urafiki wa upendo ni thamani na mali ya milele. Urafiki ni matunda ya upendo, urafiki ni tunu tena yenye thamani, urafiki ni katika kuwatendea wengine yanayokuwa mema. Hivyo wadeni hawa kwa hakika hawatamsahau kamwe wakili yule mjanja kwa jinsi alivyowafanyia wema na ukarimu na urafiki. Yesu anausifu uamuzi wake wa kuunda urafiki na watu na si na mali. Ni vema kujiuliza sisi mara nyingi tunajali watu au mali/vitu/ pesa na hata kuna wakati tunafikia kuvipa nafasi ya kwanza bila kujali wengine. Labda sisi tulitegemea hitimisho tofauti la Yesu kumkaripia na kumuonya vikali wakili yule mjanja, kwa kukosa kuwa mwaminifu kwa bwana wake na wadeni wake.

Ukweli na uaminifu ni tunu msingi za maisha ya kiroho
Ukweli na uaminifu ni tunu msingi za maisha ya kiroho

Tulitarajia kumsikia Yesu pia akituonya nasi kutokufuata mfano wa wakili yule. Yafaa pia tukumbuke kuwa hasifu kwa kukosa kuwa mwaminifu bali anasifu ujanja wake, kwa jinsi anavyofanya uchaguzi ulio sahihi wa kujenga urafiki na watu na si na mali kama nilivyosema angeweza kufanya ujanja wa kujilimbikiza mali kwa njia ya wizi na uongo, bali kinyume chake anaamua kufanya ujanja wa kujenga urafiki. Na si tu Yesu anayemsifu wakili yule mjanja bali hata mmiliki wa shamba, na ndio kusema hakuwa ameibiwa chochote, kwani kama nilivyotangulia kusema daima walionufaika kwa njia zisizo za haki hawakuwa tu mawakili au waangalizi wa mashamba yale bali zaidi sana matajiri wamiliki wa ardhi zile waliokuwa wanaishi mijini na kusubiri tu kuvuna kile ambacho hawakukitolea jasho. Ilikuwa ni dhuluma na wizi na uonevu iwe kwa waangalizi na hata pia wamiliki wa mashamba.

Sehemu ya Injili ya Dominika ya 25 ya Mwaka C wa Kanisa inahitimishwa na misemo maarufu ya Yesu yote ikiwa na lengo la kutusaidia kupata ujumbe wa Yesu katika Dominika ya leo. Sisi sote hatuna budi kutambua kuwa kila tulichonacho si mali yetu, bali tumewekwa kuwa waangalizi au mawakili tu, hivyo hatuna budi kutumia daima kwa kuwatumikia na kujenga urafiki na wengine. Hatuna budi kuwa mawakili waaminifu na kutumia yote si kwa ubinafsi bali tukikumbuka umuhimu na ulazima wa kujenga urafiki ili tuweze kuja kukaribishwa nao si tu katika ulimwengu huu bali katika maisha ya umilele. Uhakika wa maisha yetu haupo katika mali bali katika upendo kwa wengine, ni upendo unaodumu na kubaki milele. Mali, vitu, pesa na vyote tunavyokuwa navyo hatuna budi kuvitumia kwa upendo ili tubaki na mali ya milele yaani upendo. Vyote tulivyo navyo ni mali ya Mungu nasi ni waangalizi tu na hivyo hatuna budi kutumia vyote tulivyonavyo kwa kujenga urafiki na si kinyume chake.

Waamini wawe ni mawakili waaminifu na wa kweli mbele ya Mungu na jirani
Waamini wawe ni mawakili waaminifu na wa kweli mbele ya Mungu na jirani

Urafiki ni tunu njema, ni mwaliko wa kuishi upendo wa kweli kwa wengine. Na ndio wito wetu wa msingi kama Wakristo kuwatendea wengine yanayokuwa mema, kwa njia hiyo tunajenga urafiki na wengine. Yafaa kutambua urafiki wa kweli ni katika kuwatendea wengine yanayokuwa mema, ni katika kuwapenda wengine na kuepuka kuwatendea yanayokuwa maovu na mabaya. Yafaa kila mmoja wetu ajiulize ni kwa kiasi gani tunajenga urafiki na wengine? Ni kwa kiasi gani tunawatendea kwa mapendo watu wanaotuzunguka katika maisha yetu? Utajiri wa kweli na wenye kudumu milele sio mali au vitu au pesa au mashamba, magari, majumba na kadhalika kama anavyotukumbusha Mzaburi kuwa tikifa vyote tunaviacha hapa duniani. (Zaburi 49) Utajiri wa kweli ni kuwekeza katika upendo kwa Mungu na kwa wengine. Ni kuuona sura ya Mungu (Imago Dei) katika nafsi za wengine na hasa wanaokuwa wahitaji zaidi yetu. Ni katika kuujenga urafiki wa upendo nao, hapo tuna hakika ya kubaki na tunu ya milele. Watakatifu ni marafiki wa Mungu na wanadamu, na ndio maana tunasali kuwaomba watuombee kwani tunayo hakika watakatifu ni marafiki wetu wa hakika.

Mwandishi mmoja wa habari nchini Italia Augusto Guerriero, alibahatika kukutana na Mtakatifu Mama Theresa wa Calcutta katika moja ya Parokia jijini Roma, na zaidi sana akaibusu mikono yake. Mwandishi yule anaandika anasema; “Niliibusu mikono ya mwanamke yule maskini na mwenye furaha. Nikafikiri moyoni mwangu, mikono ile imetenda mema mengi, imefuta machozi mengi, imefariji watu wengi! Na kisha nikatazama mikono yangu na kutambua kuwa imejaa tamaa za kila aina…ni hapo nikajutia kuona maisha yangu nimetumia sio katika vitu vya maana na thamani”. Na ndio hali inayoweza kuwa ya kila mmoja wetu katika maisha yetu, Je, nayatumia maisha yangu kwa ajili ya wengine, kuwaletea furaha na amani wengine au kwa ajili ya mimi, mimi na mimi basi!? Nawatakia tafakari na Dominika njema.

15 September 2022, 16:30