Utushushie huruma yako, utusamehe makosa yanayotuletea hofu moyoni, utuongezee na hayo tusiyothubutu kuomba. Utushushie huruma yako, utusamehe makosa yanayotuletea hofu moyoni, utuongezee na hayo tusiyothubutu kuomba. 

Tafakari Dominika 27 ya Mwaka C wa Kanisa: Tuongezee Imani Bwana: Imani na Unyenyekevu!

Nguvu ya imani. Nabii Habakkuk, Timotheo na Mitume, walipokabiliwa na matatizo, mateso na mahangaiko, imani yao ikitikiswa wakaona shaka kuendelea kumtegemea Mungu. Nabii Habakuki anaambiwa asiogope Mungu yupo daima na watu wake, Mtume Paulo anamwambia Timotheo awe na uvumilivu asirudi nyuma na Mitume wanamwomba Yesu awaongezee imani thabiti!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 27 ya Mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatuonesha nguvu ya imani. Nabii Habakkuk, Timotheo na Mitume, walipokabiliwa na matatizo, mateso na mahangaiko, imani yao ikitikiswa wakaona shaka kuendelea kumtegemea Mungu. Nabii Habakuki anaambiwa asiogope Mungu yupo daima na watu wake, Mtume Paulo anamwambia Timotheo awe na uvumilivu asirudi nyuma na mitume walipomwomba Yesu awaongezee imani, waliambiwa hata kama imani yao ni ndogo ina nguvu kuliko wanavyofikiria. Basi nasi tukutanapo na mahangaiko na mateso katika maisha yetu imani yetu kamwe isiyumbe bali ikomae zaidi na kujikabidhi mikononi mwa Mungu muweza wa yote kama wimbo wa mwanzo unavyoimba: “Ee Bwana, ulimwengu wote u katika uwezo wako, wala hakuna awezaye kukupinga ukipenda. Wewe umeumba yote, mbingu na nchi, na vitu vyote vya ajabu vilivyomo chini ya mbingu; ndiwe Bwana wa yote” (Esta 13:9, 10-11). Tuamini kuwa upendo wa Mungu kwetu hauna mipaka anatujalia hata tusiyoomba kama anavyosali Padre katika sala ya Mwanzo: “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, unatujalia kwa wema wako mkuu mema mengi kupita yale tunayoomba na kutamani. Utushushie huruma yako, utusamehe makosa yanayotuletea hofu moyoni, utuongezee na hayo tusiyothubutu kuomba.”

Imani inamwilishwa katika matendo ya huruma na mapendo
Imani inamwilishwa katika matendo ya huruma na mapendo

Somo la kwanza ni la kitabu cha Habakuki (Hab 1:2-3; 2:2-4). Kitabu cha Habakuki kimeandikwa kwa mtindo wa mazungumzo kati ya Mungu na Nabii. Habakuki alikuwa nabii katika Yuda wa kabila la Lawi (Hab.1:1;3:1), na mmoja wa waimbaji wa hekaluni wakati wa Nabii Yeremia (Hab 3:19). Jina lake likimaanisha “Kumbatia”. Somo hili ni sehemu ya malalamiko ya Nabii Habakuk kwa Mungu kwa kuwaacha wenye dhambi kunawiri na waadilifu kuteseka akisema: Ee Mungu, kwa nini husikilizi sala za watu wako, kwa nini hutuokoi kutoka maadui wetu? Kwa nini hukumbuki ahadi uliyowaahidia mababu zetu kwamba utatulinda nyakati zote? Ni kweli kwamba tumetenda dhambi, lakini je, maadui zetu ni wema kuliko sisi? Habakuki anamnung’unikia Mungu kwa kutokusikia kilio na maombi yake kwa ajili ya watu wake kwa taabu walizopata kutoka kwa maadui zao. Habakuki anamuuliza Mungu kwa nini anawaruhusu watu waovu kustawi na maskini waadilifu kuteseka. Mungu anamjibu kwamba Wakaldayo – watu walioishi katika nchi ya Babeli ndiyo Iraq ya sasa wangekuja kuwaadhibu. Lakini Habakuki aliumia zaidi na hakuelewa ni kwa jinsi gani Mungu angeweza kuwatumia Wakaldayo/watu wa Babeli ambao walionekana kuwa waovu kuliko Wayahudi waovu, ili kutekeleza hukumu dhidi yao. Jibu la Mungu lilikuwa kwamba wenye haki wangeishi kwa imani kwa Mungu na kwamba walikuwa na uhakika kwamba Mungu alikuwa anafanya lililo sahihi. Mungu alimwambia Habakuki kwamba punde si punde Wakaldayo/watu wa Babeli wangehukumiwa na kwamba hatimaye haki ingeshinda kwa ajili ya watu wa Mungu. Ndiyo maana Habakuki anamalizia kitabu sura ya tatu yote kwa zaburi ya sifa.

Imani inamwezesha mwamini kujiaminisha mbele ya Mungu
Imani inamwezesha mwamini kujiaminisha mbele ya Mungu

Kumbe, Mungu anaweza kuwatumia waovu kuwaadhibu watu wake wanapotenda uovu ili waache uovu wao. Lakini waovu anaowatumia Mungu kuwaadhibu watu wake, wakiisha kutimiza kusudi lake, adhabu yao ni kubwa zaidi kama nao hawataacha uovu wao. Kama ilivyomshangaza Habakuki kuona waovu wakistawi huku wakiendelea kutenda dhambi nyingi wala Mungu hawaadhibu upesi ndivyo ilivyo hata nyakati zetu katika maisha yetu. Wakati mwingine tunamlalamikia Mungu na kumuuliza kwanini watu wema wanateseka na kuteswa na waovu, kumbe yawezakuwa ni kwasababu hawa watu wema wamemkosea Mungu naye anawaadhibu warudi kwake na mwisho wa waovu ni mbaya zaidi kwani adhabu yao ni ya milele kama nao watabaki katika uovu wao. Habakuki anaamini juu ya mamlaka ya Mungu na anauhakika kwamba Mungu ana haki katika njia zake zote na kwamba bado anaitawala dunia hata kama uovu bado unashamiri na ya kwamba iko siku Mungu atauhukumu na kuadhibu uovu na waovu wote na hatimye kuuangamiza kabisa usiwepo tena ndiyo maana hakukata tamaa kumuuliza Mungu mwisho wa matatizo hayo ni lini? Kumbe hatupaswi kuwa na mashaka juu ya nguvu na uwepo wa Mungu kwa uwepo wa uovu na waovu, cha maana zaidi kwetu ni kujikabidhi na kujiaminisha kwake Mungu muweza wa yote.

Somo la pili ni la Waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Timotheo (2Tim 1:6-9, 13-14). Paulo akiwa gerezani anamhimiza Timotheo ambaye alianza kuogopa kuhubiri Injili sababu ya madhulumu, uwepo wa wahubiri wa uongo na kufungwa kwake Paulo. Hivyo Paulo anamkumbusha nguvu ya Roho Mtakatifu aliyoipokea siku alipomwekea mikono. Hivi asiogope kutangaza Injili. Timotheo alikuwa kijana mwoga na mwenye wasiwasi kama Paulo anavyowaambia wakoritho: “Timotheo akija, angalieni asiwe na hofu yoyote wakati akiwa kati yenu, kwani anafanya kazi ya Bwana kama mimi” (1Kor 16:10). Ndiyo maana katika somo hili anamwambia: “Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu. Shika kielelezo cha maneno yenye uzima uliyoyasikia kwangu, katika imani na upendo ulio katika Kristo Yesu. Ilinde ile amana nzuri kwa Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu”. Paulo kama Habakuki anaamini juu ya nguvu na uweza wa Mungu ambao haushindwi na chochote, licha ya kuwa yuko gerezani na anamtia moyo kijana Timotheo abaki katika imani hiyo na kuendelea kuihubiri Injili mpaka kieleweke, ndivyo tunavyopaswa kuwa sisi tuliyoipokea imani kwa njia ya ubatizo na kuwekewa mikono na wazee wa Kanisa tukampokea na Roho Mtakatifu katika sakramenti ya kipaimara na kila siku kwa neno la Mungu na Ekaristi Takatifu tunaendelea kuimarishwa na kutiwa nguvu ili tuishihudie vyema imani yetu kwa maneno na matendo.

Tuongezee Imani Bwana!
Tuongezee Imani Bwana!

Injili ilivyoandikwa na Luka (Lk. 17: 5-10), imegawanyika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza ni ombi la mitume kuongezewa imani baada ya kuona ugumu wa mafundisho ya Yesu akiwa njiani kuelekea Yerusalemu kujitoa sadaka kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu jambo alilowaambia mara mbili (Lk 9:22, 9:44; 18:31-34). Mtazamo huu wa mitume haujatuacha salama. Mara nyingi tunaona mafundisho ya Kanisa aliyotuachia Yesu kuwa ni magumu na pengine ya ukandamizaji hatuwezi kuyaishi. Mitume waliomba kuongezewa imani naye Yesu akawambia imani hata iwe ndogo ina nguvu ya ajabu hata ikiwa ndogo kiasi cha chembe ya haradali, inaweza kung’oka miti (Lk 17:6)   au kuhamisha milima (Mt 17:20). Hii yamaanisha kuwa nguvu ya imani ipo katika kuweka tumaini lote kwa Mungu, na sio kutegemea nguvu zetu, mali zetu, akili zetu, mamlaka yetu bali ni katika kuweka tumaini letu kwa Mungu mazima mazima bila kujibakiza na bila mashaka wala wasiwasi wowote. Sehemu ya pili ya Injili ya dominika hii ya 27 Mwaka C inahusu mfano wa mtumwa unatufundisha, ukweli wa kuwa mtumwa hawezi kujiinua na kujipongeza kwa kazi yake, zaidi ya kufanya na kutimiza wajibu wake kadiri ya mapenzi na matakwa ya Bwana wake. Na hivi ndivyo Mtume Paulo asemavyo, “Maana, ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri Injili” (1Kor 9:16).

Hakuna la kujisifia, zaidi ya kutimiza kwa uaminifu lile tupaswalo kutimiza. Sisi tumeumbwa na Mungu, kwa ajili ya sifa na utukufu wake. Hivyo hatupaswi kujisifia kazi na mafanikio yetu bali yote yawe na kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu, ili kwazo Mungu atukuzwe nasi tutakatifuzwe. Fundisho hili ni kinyume kabisa na mwono wa mafarisayo waliojiwekea mapambio kwa kazi zao na kusahau ukweli kwamba siyo kazi ndizo zinazotuhesabia haki, bali ni neema za Mungu ambayo ni zawadi ya Kimungu kwetu. Kamwe hatuwezi jifananisha na vitu au idadi ya yale tuyatendayo, bali roho na upendo ule utusukumao kufanya mambo hayo hata kama ni madogo na macheche sana. Hivyo roho hiyo na upendo huo katika kutenda, na kwa kibali chake Mungu na kwa kadiri ilivyompendeza twahesabiwa haki. Ndiyo maana Yesu, anasema; “Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya” (Lk 17:10). Kuna furaha ya kweli tunapojibandua kutoka vitu na mali, na kutovifanya ndio mwisho wa kila kitu ingawa twavihitaji hapa na pale.

Imani inatangazwa, inaenezwa na kushuhudiwa.
Imani inatangazwa, inaenezwa na kushuhudiwa.

Tumruhusu Roho Mtakatifu atawale maisha yetu, atufundishe na kutuongoza vyema ili tuweze kutambua mipango na makusudi ya Mungu katika maisha yetu kwani Yesu anatuambia; “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, bali yote atakayoyasikia kutoka kwangu na kutoka kwa Baba atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake” (Yoh 16:13). Na ndiyo maana Padre katika sala baada ya komunyo kwa niaba ya waamini anasali: “Ee Mungu Mwenyezi, utujalie sakramenti hizi tulizopokea zizidi kutuburudisha na kutusitawisha tupate kuwa na uzima wake yeye tuliyempokea”. Nasi tuifungue mioyo yetu ili neema za sakramenti tunazozipokea ziingie na kufanya kazi ndani mwetu kwa sifa na utukufu wa Mungu ili sisi tuweze kutakatifuzwa na mwisho tuufikie uzima wa milele mbinguni ndipo Bwana wetu Yesu Kristo atakapotupokea na kutuhudumia milele yote kama anavyofanya kwa kutulisha kwa mwili na damu yake katika kila adhimisho la Ekaristi Takatifu. Na wanaofaidika ni wale wanaoamini kuwa katika mafumbo ya Mkate na Divai yumo Yesu mzima kabisa anayetulisha na kutunyweshwa kwa mwili na damu yake kwa ajili ya uzima wa milele.

01 October 2022, 17:30