Tafakari ya Neno la Mungu Dominika 27 ya Mwaka C wa Kanisa: “Mwenye haki ataishi kwa imani.” “Imani hai” hutenda kazi kwa upendo. Imani bila matendo imrekufa. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika 27 ya Mwaka C wa Kanisa: “Mwenye haki ataishi kwa imani.” “Imani hai” hutenda kazi kwa upendo. Imani bila matendo imrekufa.  

Tafakari Dominika 27 ya Mwaka C wa Kanisa: Imani ni Zawadi ya Mungu: Ishikwe na Kushuhudiwa

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 27 Mwaka C wa Kanisa: “Mwenye haki ataishi kwa imani.” “Imani hai” hutenda kazi kwa upendo. Imani bila matendo imrekufa. Imani inapaswa kusimikwa katika nguzo ya matumaini na mapendo. Mwamini ashike na kuishi imani yake,; Ajitahidi kuishuhudia na kushiriki mkakati wa kutangaza kwa njia ya ushuhuda wa maisha. Rej, KKK1814-1816.

Na Padre Gaston George Mkude, Roma.

Amani na Salama! Imani ni fadhila ya kimungu ambayo kwayo tunasadiki Mungu na kila kitu alichosema na alichotugunulia, ambacho Kanisa Takatifu latutaka tusadiki, kwa sababu Yeye ndiye ukweli wenyewe. Kwa imani mwanadamu hujitoa nafsi yake yote kwa Mungu. Ni kwa sababu hiyo mwamini hutafuta kujua na kufanya mapenzi ya Mungu. “Mwenye haki ataishi kwa imani.” “Imani hai” hutenda kazi kwa upendo. Imani bila matendo imrekufa. Imani inapaswa kusimikwa katika nguzo ya matumaini na mapendo. Mwamini anapaswa kuishika imani, kuishi, kuiungama, kuishuhudia na kushiriki mkakati wa kutangaza kwa njia ya ushuhuda wa maisha. Rej, KKK1814-1816. Sehemu ya Injili ya Dominika ya 27 ya Mwaka C wa Kanisa imegawanyika katika sehemu kuu mbili, ya kwanza ni juu ya imani, na ya pili ni mfano wa mtumwa asiye na faida. Na kwa haraka haraka tunaposoma sehemu zote mbili tunaona lugha inayotumika ni ya mafumbo, na hivyo kutualika tangu mwanzoni kutafakari kwa umakini mkubwa ili kupata ujumbe kusudiwa wa Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe. Marafiki na wafuasi wa karibu wa Yesu, wanaenda kwa Bwana na mwalimu wao na kumwomba awaongezee imani. Yafaa kujiuliza kama imani inaweza kuongezeka au kupungua. Ni rahisi kuona kama mmoja ana imani au hana, na sikuwa nayo zaidi au pungufu. Imani si kama ukweli ambao tungeweza kusema unao kamili au ukweli nusu nusu tu. Imani ni tukio la kukutana na Mungu, ni zawadi ya Mungu mwenyewe kwetu, ni kuingia katika mahusiano naye.

Imani ilindwe, itangazwe na kushuhudiwa
Imani ilindwe, itangazwe na kushuhudiwa

Imani si tu swala linalohusu akili kama ukweli. Ni uamuzi na uchaguzi wa maisha halisia, ni kujikabidhi kikamilifu bila masharti kwa Yesu na kuchagua kufuata njia ile anayotualika Kristo. Ni kuwa mfuasi kwa maisha. Ni safari katika maisha yetu ya kujfunza na kuishi kadiri ya Neno lake Kristo, na hivyo kama safari kila siku hatuna budi kupiga hatua kwa kwenda mbele lakini pia kama safari yeyote yawezekana pia kurudi nyumba badala ya kusonga mbele. Ni katika mantiki hiyo tunaona imani inaweza kukua au kupungua au kuipoteza kabisa. Imani ni safari inayotualika kila siku kupiga hatua. Nasi katika maisha yetu ya imani tu mashahidi kuwa kuna nyakati tunapiga hatua na kukua katika imani, na kuna nyakati tunajikuta tunashindwa kushika na kuishi kadiri ya mashauri ya Injili.  Kuna nyakati tunashindwa kuishi kadiri ya mapenzi na maagizo yake Kristo na Neno lake. Ndio zile nyakati tunazijikuta tunaishi mbali na Mungu mwenyewe, tunakuwa watupu na uchi ndani mwetu, ndio kuishi bila neema za msaada wake Mungu kwetu. Mitume wa Yesu leo wanatuonesha kuwa nao wamefikia hatua ya kutambua kuwa ili kukua kiimani si tu kutokana na juhudi na jitihada zetu binafsi, bali pia tunahitaji neema za msaada wake Mungu ili kupiga hatua mbele. Imani ni zawadi, ni Mungu anayekutana na nafsi ya mwanadamu. Hivyo hatuna budi kila mara kama mitume kukumbuka wajibu wa kwenda mbele ya Yesu Kristo na kumwomba atuongezee imani, ili tuweze nasi kuishi kweli na bila kujibakiza kadiri ya kweli za Injili. Imani ni zawadi kama tulivyotangulia kuona hapo juu.

Ni Mungu anayekuwa zawadi katika nafsi na mioyo yetu, na hasa katika safari ya maisha yetu hapa duniani. Imani ni kuwa tayari kama ambavyo Yesu Kristo anatualika kufanya maamuzi magumu katika maisha yetu ya kila siku. Ni kuwa tayari kuingia kwa mlango ule mwembamba. (Luka 13:24), kuwa tayari kumchukia baba na mama (Luka 14:26), ni kuacha yote (Luka 14:33), ni kuwa tayari kusamehe bila kikomo wala mipaka (Luka 17:5-6). Ni katika muktadha huu mitume wanajikuta hawana jinsi zaidi ya kuomba neema za msaada ili kuweza kuishi Injili. Hata nasi kuna nyakati katika maisha tunaona bila msaada wa Mungu hatuwezi kuishi kadiri ya Neno la Mungu. Ni kukiri na kutambua mipaka na udhaifu wetu, hivyo neema za Mungu hazina budi kutusindikiza katika safari yetu ya imani. Ni katika mazingira ya namna hii hata nasi kama wengi wengine waliomsikiliza Yesu na kuona kushindwa kufanya maamuzi magumu na kuamua kurudi nyuma. Mitume wanaona badala ya kurudi nyuma wanaomba msaada wa Mungu katika safari yao ya imani. (Yohane 6:60) Ni baada ya kumsikiliza Yesu wanaona ni ngumu kulipokea Neno lake na hivyo wakaamua kuachana naye. Ni kwa sababu hiyo mitume wanaona wana kila sababu ya kwenda mbele ya Yesu na kumuomba awaongezee imani. Ni hitaji letu nasi kama kweli tunataka kufanya maamuzi ya kuwa wafuasi wa kweli wa Yesu katika safari ya maisha yetu hapa duniani, hatuna budi kwenda mbele yake na kumuomba daima atuongezee imani, ni kwa imani tu tunaweza kufanya maamuzi magumu hata yanayokinzana na mantiki za ulimwengu huu.

Imani ilindwe, itangazwe na kushuhudiwa na waamini.
Imani ilindwe, itangazwe na kushuhudiwa na waamini.

Yesu leo badala ya kuwasikiliza na kuwajibu ombi lao anatumia nafasi hiyo kuwafundisha kwa mifano. Yesu anatumia mfano wa mti kuweza kuhamishwa na kuoteswa baharini. Ni mfano labda mgumu kueleweka katika mazingira yetu ya leo. Mti wenye mizizi na uliokomaa hatuwezi kuupanda tena kirahisi kama tunavyopandikiza miti midogo kwani utakauka na kunyauka, hivyo ni kwa imani tu hata nasi tunaweza kubadili namna zetu za kufikiri na kuenenda. Hata tabia zetu zilizoota mizizi tunaweza kubadili na kuanza maisha mapya kama mti unaochipua na kutoa matumaini na maisha mapya. Ni imani inaweza kutenda makubwa hata tusiyoweza kuyafikiri kwa akili na mantiki zetu za kibinadamu. Wainjili Mathayo na Marko wao hawazungumzii juu ya mti bali juu ya mlima unaoweza kuhamishwa kwa imani. (Mathayo 17:29 na Marko 11:23) Hata Mtume Paulo pia anatumia mfano huu wa mlima. (1 Wakorintho 13:2) Lakini ujumbe bado unabaki kuwa ule ule kuwa kwa imani tunaweza kufanya mambo makubwa kinyume na uwezo na akili zetu za kibinadamu. Na huo ndio ukombozi wa fikra ambao kila mmoja wetu anaalikwa kubadili kichwa chake, kukivaa kile cha Injili, kile cha Yesu Kristo mwenyewe. Labda wengine tunaposoma sehemu hii ya Injili ya leo tunabaki kushangaa kwa nini hata Yesu, Mama yetu Bikira Maria, Abrahamu au kati ya watakatifu wakubwa na mashuhuri hakuna hata mmoja aliyehamisha milima au kupanda mti baharini? Kwa kweli ndio niliyotangulia kusema tangu mwanzo kuwa lugha inayotumika ni lugha ya picha.

Ni kwa imani daima tunaweza kufanya makubwa na hasa yanayohusiana na maamuzi yetu ya maisha ya kuishi kadiri ya kweli za Injili. Ni kwa imani tunaweza kufanya mabadiliko hata ya zile tabia na hulka mbaya zenye mizizi mikubwa na mirefu katika maisha ya kila mmoja wetu, nasi tu mashahidi ya haya. Milima na miti ya kuhamishwa ndio yale yanayoonekana hayawezekani kwa nguvu na akili na bidii zetu wenyewe bali daima kwa msaada wa neema zake Mwenyezi Mungu. Kwa anayeamini hakika hakuna kitu tunachoalikwa kuishi na Injili kinachoshindikana. Ni wenye imani daima wanabaki kuwa mashahidi wa kweli za Injili. Ni wenye imani ya kweli kwao inawezekana kuhamisha milima na kupanda tena miti mikubwa. Mara baada ya sehemu ya kwanza juu ya imani na matokeo yake, Yesu Kristo anatoa mfano wa mtumwa au mtumishi asiye na faida. Mtumwa ambaye anatumika siku nzima kwa kazi nzito na tena chini ya jua kali hivyo jioni anaporejea baada ya kazi za shuruba kwa siku nzima. Baada ya kufika nyumbani bwana wake badala ya kumpongeza kwa kazi nzuri na nzito ya siku nzima, badala yake anamtaka tena amtumikie kwanza yeye bwana wake ale, anywe na ashibe, na ndipo sasa mtumwa yule naye anaweza kujihudumia.

Imani imwilishwe katika matendo adili na matakatifu
Imani imwilishwe katika matendo adili na matakatifu

Tunajua watumwa na watumishi ni sisi wanadamu na Bwana wetu ni Mungu mwenyewe; Je, nasi baada ya kazi nzito ya hapa duniani tutapokelewa kwake mbinguni kwa namna na mtindo huu? Yafaa pia kukumbuka daima wajibu wetu tukiwa hapa duniani ni kuwa watumishi katika kila eneo, utumishi wa kuhakikisha tunaiishi kweli Injili yake Bwana wetu Yesu Kristo. Mfano huu unatushangaza kwani Dominika kadhaa nyuma tulisikia Yesu akisema kuwa ni heri watumwa wale ambao bwana wao atawakuta wakikesha na wakiwa waaminifu, na Yesu akituhakikishia kuwa Bwana wao atajifunga kiunoni na kuwatumikia. (Luka 12:37) Leo tunaona picha ni tofauti kabisa na ile ya mwanzo. Yesu anatumia lugha ya picha inayoakisi uhalisia wa nyakati zake ambapo mtumwa si tu alikuwa mtumishi wa bwana wake bali zaidi zake ni mali ya bwana wake.  Katika mawaidha ya Yesu katika karamu ya mwisho anawahusia wanafunzi wake kuwa watawala wa ulimwengu huu watawatawala kwa nguvu na mabavu, Lakini kwa wanafunzi wake anawaalika kuongozwa na mantiki ya utumishi na si ukubwa kama wafanyavyo watawala wa dunia hii. Mkubwa ni yule anayetumikia na siyo yule anayetumikiwa. Naye daima anajitanabaisha kama mmoja aliyekuja kutumikia na si kutumikiwa. (Luka 22:24-27) Falsafa ya maisha ya Kikristo ni udogo na utumishi na si kinyume chake. Ni nia na dhumuni la Yesu kutualika kuona jinsi mahusiano yetu na Mungu hayana budi kuwa, sisi daima tunaalikwa kuwa watumishi katika maisha yetu yote hata kufikia kujihesabu ni watumwa tusio na faida, kamwe tusianze kupata kishawishi kuwa mbele ya Mungu tuna mastahili, bali yote ni zawadi na matokeo ya upendo wa Mungu kwetu.

Imani isaidie kupambana na changamoto za maisha.
Imani isaidie kupambana na changamoto za maisha.

Ni mwaliko wa kuepuka daima mtazamo wa mastahili mbele ya Mungu. Hatuna tunachostahili mbele yake hivyo yote ni matokea ya wema na upendo wake kwetu, na ndio mitume wanatambua hilo na kumuomba zawadi ya imani. Imani sio matokeo ya juhudi na jitihada zetu bali ni zawadi inayotoka kwa Mungu mwenyewe bila mastahili yetu, si kwa sababu sisi tumefanya kitu kikubwa hivyo tunaipokea kama mastahili au malipo ya ujira wetu, la hasha, bali ni neema na zawadi bila mastahili. Ni wazi mara nyingi hata nasi tunajikutaka katika kishawishi cha mastahili, kwani tunaona kila jambo jema ninalolifanya basi kuna mastahili yetu au malipo mbele ya Mungu. Leo tunaalikwa kujihesabu kama watumishi tusio na faida, ni msemo mgumu kuupokea na kuulewa kwani inakuaje mtumishi anayejibidiisha na kujituma na kujitesa kwa kufanya kazi kwa bidii halafu mwishoni ahesabike kama asiye na faida? Ni tahadhari kwa wanafunzi wa Yesu kuepuka kila mara na kishawishi cha kujikweza na kujihesabia haki, kujihesabia utakatifu mbele ya wengine. Ni kutualika kuwa macho na kishawishi cha majivuno ya aina yeyote ile, bali daima tujihesabu kuwa wadogo na watumishi kwa jirani na kwa Mungu na tena tusio na faida. Yote tuliyo nayo ni zawadi kutoka kwa Mungu na hivyo hatuna budi kuwa na moyo wa unyenyekevu na shukrani. Tafakari na Dominika njema.

 

01 October 2022, 15:46