Kanisa ni Sakramenti ya wokovu, ni chombo na shuhuda wa upatanisho, umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu dhamana ambayo limepewa na Kristo Yesu. Kanisa ni Sakramenti ya wokovu, ni chombo na shuhuda wa upatanisho, umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu dhamana ambayo limepewa na Kristo Yesu. 

Tafakari Domina 28 ya Mwaka C wa Kanisa: Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu: Imani na Uponyaji

Waamini wanakumbushwa kuwa na moyo wa shukrani kwa Mungu kwa mema yake yote. Pili kwa zawadi ya imani ya kikristo ambayo kwayo kwa njia ya ubatizo tumeondolewa dhambi na kufanywa upya watoto wa Mungu na wa Kanisa na tunaendelea kusamehewa dhambi zetu kila siku katika Sakramenti ya upatanisho na kulishwa kwa chakula cha kiroho yaani Ekaristi Takatifu.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 28 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Huduma makini kwa wazee na wagonjwa ni sehemu ya utekelezaji wa haki msingi za binadamu. Kanisa halina budi kuwa sera pamoja na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya wazee na wagonjwa na kwamba, huduma hii ni sehemu ya Uinjilishaji wa kina unaozingatia mahitaji yam tu mzima: kiroho na kimwili. Masomo ya dominika hii yanatukumbusha kuwa na moyo wa shukrani kwanza kwa Mungu kwa mema yote anayotujalia; kwanza kabisa kwa zawadi ya uhai na maisha ya hapa duniani, pili kwa zawadi ya imani ya kikristo ambayo kwayo kwa njia ya ubatizo tumeondolewa dhambi na kufanywa upya watoto wa Mungu na wa Kanisa na tunaendelea kusamehewa dhambi zetu kila siku katika Sakramenti ya upatanisho na kulishwa kwa chakula cha kiroho yaani Ekaristi Takatifu. Lakini pia tunapaswa kuwa na moyo wa shukrani kwa wenzetu tunaoishi nao ambao mwenyezi Mungu ametupatia kama zawadi katika maisha yetu. Hii ndiyo njia sahihi ya kukua katika mahusiano mema kwa Mungu na jirani.

Somo la kwanza kutoka kitabu cha pili cha Wafalme (2Waf 5:14-17); ni ufupisho wa simulizi la kuponywa ukoma kwa Naamani, jemedari mpagani, mkuu wa Jeshi la Syria na Nabii Elisha Myahudi baada ya msichana Msamaria aliyechukuliwa mateka na Wasyria kumwambia kupitia mke wake kuwa katika Israeli kuna mtu wa Mungu ambaye akimwendea ataweza kumponya. Simulizi zima tunalisoma katika kitabu cha pili Wafalme 5:1-27. Jemedari Naamani baada ya kuponywa ugonjwa wake alitaka kumshukuru Nabii Elisha kwa kumpatia zawadi. Nabii Elisha alikataa ili kuonesha na kukiri ukuu wa Mungu kwamba si yeye aliyemponya bali ni Mungu. Ndipo sasa Naamani naye akakiri ukuu wa Mungu wa Israeli kuwa ana wema na nguvu za kipekee kuliko miungu wa nchi yake. Hivyo akaomba udongo wa nchi ya Israeli ili akamjengee Mungu madhabahu katika nchi yake ili amwabudu yeye peke yake. Ndivyo Bwana alivyoufunua wokovu wake machoni pa mataifa kama tunavyoimba katika wimbo wa katikati (Zab. 98:1-4). Simulizi hili la uponyaji wa Naamani linahitimishwa kwa tukio la adhabu kwa Gehazi mtumishi wa Elisha kwa ulaghai. Gehazi alifikiri kwamba Elisha alikosea kutokupokea zawadi alizopewa na Naamani. Hivyo alimvizia Naamani alipofika mbali na kumlaghai ampatie kiasi cha fedha. Aliporudi nyumbani, Elisha alimuuliza; ulienda wapi? Naye akamdanganya kuwa hakwenda popote. Elisha akamwambia unanidanganya hukujua kuwa roho yangu ilikuwa nawe ulipoomba kupewa fedha na Naamani. Basi akamwambia ugonjwa wake utakuwa wako. Ndipo Gehazi akawa na ukoma.

Magonjwa na udhaifu wa binadamu ni sehemu ya maisha ya mwanadamu
Magonjwa na udhaifu wa binadamu ni sehemu ya maisha ya mwanadamu

Kumbe, somo hili linatufundisha kuwa na moyo wa shukrani kwa wema wa Mungu kama Naamani jemedari mpagani pia kuwa na moyo wa kuwasaidia wenye shida kama msichana Msamaria na tuwe na unyenyekevu kama wa nabii Elisha lakini pia linatuonya tusiwe walaghai kwa neema na baraka za Mungu kama Gehazi tusije patwa na majanga. Naamani ingawa alikuwa mpagani, unyenyekevu ulimpatia uponyaji, lakini zaidi sana zaidi ya imani kwa Mungu wa kweli. Gehazi, kinyume chake, ingawa alikuwa mfuasi wa Nabii Elisha, aliona maajabu mengi ambayo Mungu alitenda kupitia Nabii wake, hakujifunza, ubinafsi ulimponza akajipatia magonjwa ya kiroho na kimwili. Kumbe kwa Elisha tunajifunza Roho ya huduma na uwajibikaji. Yeye ni mchungaji wa kweli wa roho za watu. Yeye anampa Mungu kilicho chake na anatuwezesha kutambua kwamba hatupaswi kumwibia Mungu sifa na heshima anayostahili. Basi nasi tuombe neema na baraka za Mungu tuweze kufanya yale ambayo yeye mwenyewe anatuagiza tuyafanye kwa ajili ya sifa na utukufu wake.

Katika somo la pili la Waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Timotheo (2Tim 2: 8-13); Paulo akiwa gerezani anaendelea kumsihi Timotheo na kumpa maagizo yake kuwa tukiteswa na kutolea uzima wetu kwa ajili ya kazi ya Yesu Kristo tutafufuka pamoja na Kristo na tutashiriki naye furaha ya mbingu. Tusipomwungama Kristo katika mateso, yeye atatukataa siku ya hukumu. Paulo anamwambia Timotheo, amkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuka katika wafu, kama inenavyo injili ambayo kwayo yeye Paulo ameteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi. Kwa ajili ya hilo anastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele. Ni neno la kuaminiwa. Kwa maana, kama tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia; kama tukistahimili, tutamiliki pamoja naye; kama tukimkana, yeye naye atatukana sisi; kama sisi hatuamini, yeye hudumu kuwa mwaminifu, kwa maana hawezi kujikana mwenyewe. Maneno haya ya Paulo yatutie nguvu nasi tusirudi nyuma kamwe na kuiacha imani yetu kwa sababu yoyote ile hata ikitupasa kujitoa sadaka kwani hiyo ndiyo shukrani yetu kwa Kristo aliyetoa maisha yake kwa ajili yetu na ndiyo njia ya kutufikisha katika uzima wa milele.

Ekaristi Maana yake ni Shukrani
Ekaristi Maana yake ni Shukrani

Injili Takatifu kama ilivyoandikwa na Luka (Lk 17:11-19), ni simulizi la kuponywa kwa wakoma 10 na kurudi kwa mmoja kumshukuru Mungu naye ni Msamaria. Wakati wa Yesu kulikuwa na makundi manne ya watu ambao walikuwa wanaonekana kama wafu tu: Maskini, Wakoma, Vipofu na Mtu mzima asiye na mtoto. Mwinjili Luka anasema kuwa wenye ukoma walisimama mbali, wakapaza sauti wakesema; “Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu”. Kusimama mbali ni kwasababu sheria iliwakataza kuwakaribia watu wengine ili wasiwaambukize ugonjwa huo hatari. Kitabu cha Walawi kinasema hivi juu ya wakoma: “Mwenye ukoma yeyote, atavaa nguo zilizochanika, nywele zake hatazichana na mdomo wake wa juu ataufunika, na atapaaza sauti akisema, ‘mimi ni najisi, mimi ni najisi.” Ataendelea kuwa najisi kwa muda wote alio na ugonjwa huo. Yeye ni najisi na atakaa nje ya kambi” (Wal 13:45-46). Kumbe Wakoma hawakupaswa kuwakaribia watu wengine hivyo walifungiwa kengele ili wanapotembea watu wasikie wawapishe pia kama wanapita sehemu yenye watu walipaswa kufunika mdogo wa juu, na kupiga kelele, mimi ni najisi, mimi ni najisi ili wampishe. Wenye ukoma kumi walishika vizuizi vya Sheria hii na kubaki mbali na Yesu. Hata hivyo, wao wanapiga kelele kwa sauti kubwa hivi: “Ee Yesu, Bwana mkubwa, Uturehemu!” Yesu alipowaona aliwaambia; “Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani”.

Yesu anawaamuru waende wakajionyeshe kwa makuhani kwa sababu kisheria makuhani walikuwa na mamlaka ya kuwatangaza waliopona ugonjwa huu na kuwapata kibali cha kuishi tena pamoja na watu wenye afya. Hii ni kwasababu ilikuwa ni sheria kwamba kila aliyeponywa katika ukoma aende kwa Kuhani kujionesha na ni kuhani tu aliyekuwa anaweza kumtangaza mkoma kwamba amepona na kwamba amewekwa huru tena (Wal 14:2-7). Kihistoria Wasamaria walikuwa hawachangamani wala kupika chungu kimoja na wayahudi, kwa maana walikuwa maadui. Wasamaria walionekana mbele ya wayahudi kuwa ni najisi na wadhambi kwasababu, wasamaria ni mchanganyiko wa watu wa kabila la Efraimu na Manase walioishi katika Samaria mji mkuu wa ufalme wa kaskazini wa Israeli na makabila mengine walioletwa na mfalme wa Ashuru baada ya wayahudi wengine kuchukuliwa mateka (2Wafalme 17:24; Ezra 4:2-11). Dini yao ilikuwa ni mchanganyiko wa imani na desturi za Kiyahudi na kipagani. Wayahudi hawa walioana na makabila yaliyoletwa wakaiacha dini yao wakaabudu miungu ya kigeni (2 Wafalme 17:26-28). Hivyo wayahudi asili waliporudi utumwani na kukutana na hali hii walichukizwa sana wakawatenga na kuwaona kuwa ni waasi hata wakajenga ukuta ili wasiweze kuingia tena Yerusalemu.

Wagonjwa waonjeshwe mshikamano wa upendo na imani
Wagonjwa waonjeshwe mshikamano wa upendo na imani

Kumbe, kilichowaunganisha Msamaria huyu mmoja na Wayahudi wale kenda ni ugonjwa wa ukoma. Mara nyingi matatizo yanatuunganisha na kutufanya tusahau tofauti zetu. Hawa wakoma katika ugonjwa wao walisahau tofauti zao za Kiyahudi na Kisamaria. Walijiona kuwa wao ni wahitaji. Tatizo la kuungana katika shida tu ni kwamba shida ikiisha tunarudi kule tulikokuwa ndiyo maana msamaria alijitenga na kurudi peke yake. Baba wa Taifa la Tanzania mwalimu Julius Kambarage Nyerere akituonya watanzania kuhusu ukabila alisema kuwa wanajiona kuwa ni Wazanzibari au Watanganyika kwa sababu wako katika muungano, wakishajitoa katika muungano, dhambi ya ubaguzi inabaki pale pale na itaendelea kuwala. Nje ya muungano hawatasema tena sisi Wazanzibari bali watasema; “Sisi Wapemba, ninyi Waunguja.” Hata sisi tukisha wabagua wengine iwe katika jumuiya, katika kazi au serikali hata sisi wenyewe hatutabaki wamoja tutaanza kubaguana sisi wenyewe. Kwa kuwa muungano utokanao na matatizo au mahitaji sio wa kuwadumu bali wa muda tu. Basi tuunganishwe na hitaji lisiloisha kwamba sote tunamhitaji Mungu hata uwe nani utamhitaji Mungu tu.

Katika Biblia namba 10 ni namba kamili inayodhihirisha ukamilifu wa jambo. Kwa hiyo wakoma 10 wanawakilisha idadi kamili ya watu wote wenye ukoma. Ukoma unawakilisha hali ya dhambi, ni ishara ya mwanadamu kujitenga na Mungu na jirani yake, ni hali ya msiba. Kila mwandamu anaalikwa kukutana na Kristo, kwani kila mwanadamu ni mkoma – mdhambi. Kila mwanadamu anahitaji kuhuishwa na kurudishwa kundini. Anahitaji wokovu. Nasi tumkimbilie Yesu na kumwambia; “Yesu Bwana mkubwa uturehemu”. Lakini tunaona kuwa ni Msamaria tu aliyerudi kumsifu na kumshukuru Mungu! Nasi tuwe na moyo wa shukrani kwa Mungu kwa mema yote anayotujalia kila siku hasa kwa uponyaji wa kiroho kwa kutusamehe dhambi zetu kila tunamkosea na kuomba msamaha naye anatuambia nenda kwa amani imani yako imekuponya. Daima tunapaswa kuwa watu wa shukrani kwa upendo, ukarimu na uponyaji huu wa ndani. Daima tumshukuru Mungu kwa mahitaji ya kimwili anayotupatia kila siku. Tukumbuke kuwa kila tulicho nacho ni zawadi kutoka kwa Mungu: afya, maisha, uhai, makazi, chakula, familia, marafiki na uhulushi wote: Jua, mwezi, nyota, mvua inayoinyeshea ardhi tukapata mavuno, misitu, wanyama, maporini. Mambo mengi tunayaona lakini hayatufikirishi, mpaka tunapopoteza ndiyo tunatambua umuhimu wake. Wahenga wanasema; Ng’ombe hatambui thamani ya mkia wake mpaka umekatwa.

Mshikamano na wagonjwa katika sala
Mshikamano na wagonjwa katika sala

Daima tumshukuru Mungu kwa zawadi za kiroho anazotujalia: Imani yetu kwa Kristo, maisha katika Roho Mtakatifu, kwa Neno lake tulipatalo kupitia Maandiko Matakatifu, kwa Ekaristi Takatifu, kwa familia ya Kikristo, kwa shauku ya sala na majitoleo, kwa kutuongoza kwa njia ya wokovu. Uponyaji wa Naamani Jemadari, uliibua hisia za uchaji na utambuzi wa ajabu juu ya Mungu na kusema; “Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani mwote, ila katika Israeli,” 2Fal 5:15. Tuyakumbuke kila mara matendo makuu anayotutendea Mungu nayo yatufanye tuwe na imani thabiti katika maisha yetu kwani mzaburi anasema; “Msifu Bwana, moyo wangu; wala usizisahau fadhili zake” (Zab.103). Naamani aliahidi akisema; “kwa maana mtumwa wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa na dhabihu kwa miungu mingine, ila kwa Bwana”. Nasi tuweke ahadi za kudumu imara katika imani ya Mungu mmoja iliyosimikwa na Yesu Kristo katika Kanisa Moja Takatifu Katoliki na la Mitume ili nasi siku moja tupate kuurithi uzima wa milele.

08 October 2022, 10:01