Dominika hii imepewa jina la “Dominika ya Mchungaji Mwema”, Siku ya Kuombea Miito Duniani. Dominika hii imepewa jina la “Dominika ya Mchungaji Mwema”, Siku ya Kuombea Miito Duniani.   (ANSA)

Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema: Wito: Neema na Utume

Ni siku ya kuombea Miito mitakatifu ndani ya Kanisa kwani Kanisa linawahitaji mapadre na watawa waliokamaa, watulivu, hodari na wakarimu katika kuyaadhimisha na kuyagawa Mafumbo ya Kanisa. Ni siku ya kumwomba Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika shamba lake kama alivyoagiza Yesu mwenyewe. “Mwombeni Bwana wa mavuno apeleke wafanyakazi katika shamba lake” (Mt 9:37): Kauli mbiu ya Siku ya Kuombea Miito: Wito: Neema na Utume!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 4 ya Pasaka mwaka A. Dominika hii imepewa jina la “Dominika ya Mchungaji Mwema”, Siku ya Kuombea Miito Duniani. Imepewa jina hili kutokana na Injili tunayosoma dominika hii Yohane sura ya 10 ambayo inamuelezea Kristo Mchungaji mwema. Ndiyo maana sala na nyimbo zinaashiria uhusiano uliopo kati ya Yesu Mchungaji mwema na sisi waamini kama kondoo wake. Katika kiitikio cha wimbo wa katikati kutoka zaburi 23 tunaimba; “Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu”. Katika sala ya mwanzo Padre anasali; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, utuelekeze kwenye furaha za mbinguni, kusudi sisi kondoo wako wanyonge tufike huko alikotoka mchungaji wetu shujaa.” Na katika sala baada ya komunio anahitimisha akisali; “Ee Mchungaji mwema, ututazame kwa mapendo sisi kundi lako. Upende kutuweka katika malisho ya milele sisi kondoo wako uliotukomboa kwa damu takatifu ya Mwanao.” Ni siku ya kuombea Miito mitakatifu ndani ya Kanisa kwani Kanisa linawahitaji mapadre na watawa waliokamaa, watulivu, hodari na wakarimu katika kuyaadhimisha na kuyagawa Mafumbo ya Kanisa. Ni siku ya kumwomba Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika shamba lake kama alivyoagiza Yesu mwenyewe.  “Mwombeni Bwana wa mavuno apeleke wafanyakazi katika shamba lake” (Mt 9:37, Lk 10: 2). Ni siku ya kumwomba Mungu awaite vijana wengi kuwa wafanyakazi katika shamba lake. Ni siku ya kutafakari na kuona namna tunavyoweza kuwasaidia vijana walioonesha moyo wa kutaka kuwa mapadre na watawa waweze kuendelea kuisikiliza na kuijua vyema sauti ya Kristo Yesu mchunguji mwema, waifuate na kukua katika miito hiyo mitakatifu.

Siku ya 60 ya Kuombea Miito Mtakatifu Ndani ya Kanisa: Ndoa
Siku ya 60 ya Kuombea Miito Mtakatifu Ndani ya Kanisa: Ndoa

Somo la kwanza ni la kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 2: 14a, 36-41). Somo hili ni hotuba ya Mtume Petro siku ya Pentekoste ya kwanza lilipozaliwa Kanisa la kimisionari. Petro aliyeitwa na kuchaguliwa na Kristo kuwa mchungaji mkuu wa Kanisa lake, baada ya kuwasaidia wayahudi kutambua ubaya wa kosa lao la kumtoa Yesu kwa Pilato ili auawe, anawahubiria juu ya ufufuko na anawaongoza waone mpango wa Mungu wa wokovu akiwaambia; “Mungu amemfanya huyu Yesu mliyemsulibisha kuwa Bwana na masiha” (Mdo 2:36). Baada ya kutoa ushahidi juu ya ufufuko wa Yesu, Petro anawaonya Wayahudi wakate shauri la kumsadiki Yeye waliyemsulibisha; watubu na kupokea ubatizo kwa jina lake Yesu ili wapate maondoleo ya dhambi na kumpokea Roho Mtakatifu. Agizo hili lilimhusu kila mtu bila kujali kabila, rangi au taifa lake. Mtume Petro anasisitiza kuwa wanapaswa kumfanya Yesu kuwa Bwana wa maisha yao. Wakristo wa mwanzo walitumia jina “Bwana” kwa Yesu zaidi kuliko majina mengine. Hii ni kwasababu katika Dola ya kirumi jina “Bwana” lilitumiwa kwa mtawala wa Roma tu. Nyakati hizo mtawala wa Roma aliweza kufukuza watu wake, kuchukua mali zao au hata kutoa hukumu ya kifo kwao. Wakristo walichagua jina hili “Bwana” kwa ajili ya Yesu kama njia ya kukiri utawala wake juu ya malaika, watu na viumbe vyote. Kwa kumwita jina hili, wakristo walitaka kusisitiza imani yao katika Kristo mfufuka, kujikabidhi kwake moja kwa moja pamoja na vitu walivyokuwa navyo. Ni katika muktadha huo maneno “wewe peke yako, Bwana Yesu Kristo” kwenye wimbo wa utukufu yanapata uzito wake. Kwa Sakramenti ya Ubatizo tumeondolea dhambi ya asili na adhabu zake zote na kumpokea Roho Mtakatifu na kila mara tunapotubu dhambi zetu na kuziungama. Kwa ubatizo wetu tumefanywa kuwa makuhani, wafalme, na manabii. Kama makuhani inatupasa kumtolea Mungu sadaka na kuwatakatifuza wenzetu kwa sala zetu. Vilevile kama wafalme tumeshirikishwa katika utawala wa Mungu hivyo tunapaswa kuyatalawa maisha yetu kwa kuishi vyema na sio kutawaliwa na dhambi. Na kama manabii inatupasa kumuhubiri Kristo hata kwa njia ya mauti. Tutaweza kuyafanya haya yote kwa sababu tumempokea Mungu Roho Mtakatifu na kujazwa nguvu zake ili kumshuhudia Bwana wetu Yesu Kristo kwa maneno na matendo yetu mema siku zote za maisha yetu.

Kristo Yesu Mchungaji Mwema: Wito wa Daraja Takatifu
Kristo Yesu Mchungaji Mwema: Wito wa Daraja Takatifu

Somo la pili ni la waraka wa kwanza wa Mtume Petro kwa Watu Wote (1Pet. 2:20b-25). Katika somo hili Mtume Petro anawaambia wayahudi waliomwamini Kristo kuwa kutubu na kubatizwa haitoshi wanapaswa kutenda mema na kuvumilia mateso wakiiga mfano wa Yesu katika kutimiza utashi wa Mungu. Ni mwaliko kwetu kuwa katika kutubu na kubatizwa tulichagua kumfuata Kristo ambaye aliteswa kwa ajili yetu. Basi tutende mema na kuvumilia mateso tukiiga mfano wake. Mtume Petro anatuasa kubaki katika imani yetu hata kama katika mateso na taabu za kimaisha. Tunaaswa tuvumilie mateso, tumwamini na kumtegemea Mungu katika shida na raha. Mateso yasiwe chanzo cha kutufanya sisi tutende dhambi. Bwana wetu Yesu Kristo ni kielelezo chetu ambaye pamoja na kwamba hakuwa na dhambi, alivumilia mateso makali ili aweze kutukomboa kutoka katika utumwa wa dhambi. Tukumbuke kuwa hata katika mateso Mungu yupo pamoja nasi akituimarisha katika udhaifu wetu wa kibinadamu tuweze kuyastahimili na kubaki waaminifu kwa imani yetu kwake ili siku moja tuweze kuurithi ufalme wa mbingu. Injili ni ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 10:1-10). Katika sehemu hii ya Injili Yesu anajifananisha na mlango wa zizi la kondoo. Ili kuelewa hili fundisho la Yesu, tunapaswa kukumbuka kuwa waisraeli walikuwa wafugaji wa kondoo. Wachungaji walijenga zizi na kuzungushia ukuta wa mawe. Na zizi hili lilikuwa na mlango mmoja tu kwa ajili ya kondoo kuingia na kutoka. Baada ya malisho ya kutwa, wachungaji walileta mifugo yao katika zizi hili moja wakati wa jioni. Asubuhi kondoo walitolewa nje na kila mchungaji aliwaita walio wake nao walitambua sauti ya mchungaji wao na kumfuata. Lakini pia itakumbukwa kuwa katika agano la kale viongozi wa serikali na wa kidini katika Israeli walichukuliwa kama wachungaji, yaani watu waliopewa mamlaka na Mungu ya kuwaongoza watu wake. Lakini wachungaji hawa walitafuta zaidi maslahi yao binafsi na kusababisha madhara makubwa kwa watu wao. Yesu aliwaita wezi na wanyang’anyi, watu ambao lengo lao ni kuiba, kuua na kuharibu (Yn 10:8,10). Mungu kwa kinywa cha manabii hasa Ezekieli na Yeremia akaahidi kuwanyang’anya mamlaka hayo na yeye mwenyewe kuwa mchungaji wa watu wake (Ezekieli 34). Hivyo kwa kuwa utabiri wa nabii Ezekieli ulifahamika kati ya wayahudi na Yesu alipojitangaza kuwa mchungaji mwema na mlango wa zizi la kondoo wale waliomsikiliza walimuelewa vizuri.

Toba na wongofu wa ndani ni chemchemi ya furaha ya kweli.
Toba na wongofu wa ndani ni chemchemi ya furaha ya kweli.

Kwa Sakramenti ya ubatizo sisi nasi tumeingizwa kwenye kundi moja ambalo mchungaji wake mkuu ni Bwana wetu Yesu Kristo. Tunapaswa kuisikiliza sauti yake na kumfuata Yeye ambaye ni njia, ukweli na uzima. Yeyote anayeingia na kutoka zizini kupitia yeye atakuwa salama na uhakika wa kupata malisho (Yn 10:9). Upendo wake kwetu unapita ule wa mchungaji wengine. Yeye anatujali na kutupenda kwa upendo usio kifani hata aliyatoa maisha yake kwa ajili yetu sisi. Yesu Mchungaji mwema anamjua kila mmoja wetu kwa Jina, anajua mahitaji yetu, madhaifu yetu, magonjwa yetu, mahangaiko yetu, majeraha ya dhambi zetu na tiba tunayohitaji. Neno lake na Sakramenti hasa Ekaristi Takatifu na Kitubio ndiyo malisho bora yanayotupa nguvu ya kuishi maisha mema na maadilifu ambayo ndiyo mwongozo na kibali cha kuingia katika nchi ya ahadi – Yerusalemu Mpya – Mbinguni, huko tunavishwa taji ya uzima kama wana na warithi wa uzima wa milele pamoja naye mchungaji wetu mwema. Kumbe Kristo kwetu ni kila kitu; ni mlango, ni mchungaji, ni njia, ni malisho, ni mlinzi na ni uzima wetu. Yesu aliwachagua mitume kuwa wachungaji wake wasaidizi na kumweka Petro kuwa mchungaji mkuu hapa duniani. Na anaendelea kuwachagua anaowataka miongoni mwa watu wake kuwa wachungaji ili kulichunga kundi lake kwa jina lake na kwa niaba yake. Kumbe ni Kristo ndiye anayeita na kuchagua, ni yeye anayemnong’onezea mtu moyoni mwake na kumwambia nifuate (Mt 4:19; Yn 21:19). Tukumbuke siyo kwa mastahili binafsi na wala sio kwa ajili ya kupata heshima, wala faida binafsi kuitwa kuwa mtawa au Padre, bali ni upendeleo anajaliwa yeye anayechaguliwa na kuitwa ili awaongoze wengine kwa mambo yamhusuyo Mungu. Kuingia upadre au utwa ukiwa na motisha nyingine zaidi ya kuwa mchungaji au kutumika kwa mambo yamhusuyo Mungu ni kuwa mwivi anayeingia zizini kwa kuruka ukuta ili aharibu. Matokeo yake ni uharibifu wa kondoo na kuangamia kwa wachungaji. Kumbe familia ya kikristo ifahamu kuwa ni upendeleo mkubwa Yesu anapomwita mmoja katika familia hiyo kuwa padre au mtawa.

Kristo Yesu ni Mchungaji mwema
Kristo Yesu ni Mchungaji mwema

Jumuiya ya kikristo nayo ina wajibu na jukumu la kuwasaidia wale walioitwa na Mungu kuwa wachungaji. Kwanza kabisa ni kuwasaidia kwa sala, malezi, kuwapa moyo na kuwasaidia katika mahitaji yao ya kimwili vijana walioitwa na Kristo nao wanaitikia ili wapitie hatua zote za malezi wakiwa na nia moja. Tuwasaidie ili kelele za ulimwengu zisiwazuie kuendelea kuisikia na kuiitikia sauti ya Mungu. Lakini pia kwa wale wazazi wanaowazuia au kuwakatisha tamaa watoto wao kuitikia na kuifuata sauti ya Mungu kuwa mapadre au watawa, nao tuwasaidie ili nao watambue mpango wa Mungu kwa watoto wao aliowajalia. Pili ni kuwasaidia wale ambao wameshakuwa wachungaji yaani mapadre na watawa. Padre na watawa kama binadamu wengine wanaweza kukengeuka na kuvutwa na malimwengu. Tamaa, uchoyo au ubinafsi, unaweza kuwageuza na kuwa wezi na waharibifu wa kondoo waliokabidhiwa na Kristo. Waamini wana wajibu wa kuwasaidia waweze kuwa wachungaji wema. Kama wakiwa waaminifu kwa Kristo, wakifanya kazi yao kwa jina la Kristo siku kwa siku wanaofidika zaidi ni waamini. Na kama wakikengeuka na hivyo kutowajibika kwao, wanaoumia zaidi na kuteseka ni jumuiya ya waamini. Hivyo tunapaswa kuwapa ushirikiano, kuwaombea, kuwasaidia katika mahitaji yao ya kimwili na kiroho ili waweze kutekeleza wajibu wao vyema wa kulichunga kiaminifu kundi walilokabidhiwa. Ni kwa namna hii sote tunaweza kutembea kwa pamoja kuelekea Yerusalemu ya Mbinguni chini ya maongozi ya Kristo Mchungaji wetu mkuu.Tumsifu Yesu Kristo.

D4 Pasaka
27 April 2023, 14:03