Kard.Pizzaballa:Ninaogopa vita virefu sana,tufanye kazi juu ya makubaliano
Vatican News
Kulaani unyanyasaji, kwa namna zote, hitaji la kufanyia kazi la usitishaji vita na zaidi ya yote, kuhakikisha kuwa silaha zimenyamazishwa ili kuruhusu "sauti nyingine kusikilizwa", ndiyo maoni ya Kardinali Pierbattista Pizzaballa, Patriaki wa Kilatini wa Yerusalemu, alivyobainisha huku akihuzunishwa, lakini hata hivyo bila kushangazwa kabisa na hali hii ya kutisha inayofanyika huko Israeli na Gaza, kwa sababu kwa muda yeye mwenyewe alikuwa ameona kuongezeka kwa mvutano, ingawa si kwa hatua hiyo inavyojionesha sasa. Kadinali huyo mpya alirejea Yerusalemu tarehe 9 Oktoba 2023, akiwa anatokea Italia, mahali ambapo alikuwa mmoja wa Makardinali 21 waliowekwa wakfu tarehe 30 Septemba 2023 na kushiriki Misa ya shukrani na Ufunguzi wa Sinodi ya Kawaida ya XVI Maaskofu, tarehe 4 Oktoba. Kwa njia hiyo Patriaki Pizzaballa katika maelezo yake anahofia sana kwamba vita hivyo vitakuwa vya muda mrefu hadi suala la Wapalestina litatuliwe!
Na kuhusiana na Jumuiya ya Wakristo huko Gaza alisema kila mtu yuko sawa. Baadhi ya familia zimeharibiwa nyumba zao, lakini ziko salama. Wote wamekusanyika katika eneo la parokia na shule yao, wakidhani kwamba hawa hawatalengwa. Hiyo ni kawadia kwa wako chini ya mvutano mkubwa. Wana akiba ya chakula kwa muda, lakini ikiwa hali ya kuzingirwa itaendelea itakuwa shida. Kwa sasa Kardinali Pizzaballa alisema wanafurahi kujua kwamba wote wako salama na wamekusanyika katika eneo la parokia.
Akihojiwa na mwandishi wa Vatican News, Roberto Cetera alisema: Niliweza tu kurudi jana usiku na kwa ujasiri kabisa, kwa msaada wa mamlaka ya kiraia na kijeshi, Israeli na Jordan, kwa sababu niliingia kupitia Jordan. Nilikuta nchi ambayo ilikuwa na hofu na kushangazwa na kile kinachotokea. Kuongezeka kwa vurugu kwa hakika kulitarajiwa, japokuwa kwa hakika si kwa aina hizi, na kwa kiasi hiki na kwa ukatili huu. Pia nilipata hasira nyingi na kusubiri sana kusikia neno la mwelekeo, la faraja, na pia la uwazi juu ya kile kinachoendelea kutokea. Kwa kifupi, nilikuta nchi ambayo ilikuwa imebadilika sana na mara moja.
Akijibu swali la mwandishi wa habari wa Vatican kuhusu kile anachohisi kueleza kwa Jumuiya ya Kimataifa alisema kwamba ni lazima ianze kulitazama suala la Mashariki ya Kati na Israeli na Palestina kwa umakini zaidi, kuliko ilivyooneshwa hadi sasa. Na lazima ifanye kazi kwa bidii sana ili kutuliza hali, ili kufikisha pande zote kwenye busara kwa njia ya upatanisho ambao sio lazima uwe wa umma, kwa sababu kwa umma hazitafanya kazi kamwe. Wanahitaji kuungwa mkono, kukemea aina zote za vurugu, kuwatenga wahalifu na kufanya kazi bila kuchoka ili kuelekea usitishaji mapigano. Kwa sababu maadamu silaha zinazungumza haitawezekana kusikiliza sauti nyingine.