Kutumia Uwezo Kama Wataalamu wa Afya, Vijana katika Kushughulikia Changamoto na Fursa za Sasa ni mada iliyowasilishwa na Jumuiya ya Wakatoliki Hospitali ya Taifa Muhimbili, Jijini Dar es Salaam, tarehe 26 Julai 2024 . Kutumia Uwezo Kama Wataalamu wa Afya, Vijana katika Kushughulikia Changamoto na Fursa za Sasa ni mada iliyowasilishwa na Jumuiya ya Wakatoliki Hospitali ya Taifa Muhimbili, Jijini Dar es Salaam, tarehe 26 Julai 2024 . 

Mama Evaline Malisa Ntenga: Ushauri Kwa Vijana wa Kizazi Kipya!

Kutumia Uwezo Kama Wataalamu wa Afya, Vijana katika Kushughulikia Changamoto na Fursa za Sasa ni mada iliyowasilishwa na Jumuiya ya Wakatoliki Hospitali ya Taifa Muhimbili, Jijini Dar es Salaam, tarehe 26 Julai 2024 na kuchambuliwa kwa kina na mapana na Mama Evaline Malisa Ntenga, Rais wa Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania. Hofu ya Mungu, Uadilifu, Bidii na Muda!

Na Mama Evaline Malisa Ntenga, - Dar es Salaam, Tanzania.

Kutumia Uwezo Kama Wataalamu wa Afya, Vijana katika Kushughulikia Changamoto na Fursa za Sasa ni mada iliyowasilishwa na Jumuiya ya Wakatoliki Hospitali ya Taifa Muhimbili, Jijini Dar es Salaam, tarehe 26 Julai 2024 na kuchambuliwa kwa kina na mapana na Mama Evaline Malisa Ntenga, Rais wa Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania. Kwa taaluma ni: Mkaguzi wa hesabu za nje, Utawala na fedha; Tehama, Rasilimali watu na Operesheni. Anasema, kilichomfikisha hapo alipo ni hofu ya Mungu na kuwaona wengine ni bora zaidi kuliko yeye; Pili ni uadilifu uliomjengea heshima na uaminifu kutoka kwa wengine, bidii katika kazi; matumizi bora zaidi ya rasilimali muda pamoja na kujenga mahusiano na mafungamano mema na wataalamu wengine, jambo ambalo limemwezesha kupata fursa zaidi na mwisho lakini muhimu ni wajibu wa kijamii kama shukrani kwa Mwenyezi Mungu aliyemjalia karama na mapaji haya, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Katika Makala hii Mama Evaline Malisa Ntenga, anapembua kwa kina na mapana: Misingi ya fedha, usimamizi na ujuzi wa uongozi ili kuwasaidia vijana katika maisha. Kila mtu anayo fursa ya kuongoza kwa kuwafanya wengine wafurahie kufanya kazi. Baadhi ya changamoto za kawaida katika maisha ya kazi, sera na mikakati ya kuzishinda kwa ufanisi. Mwishoni anawataka vijana wa kizazi kipya kuthubutu na wala wasisubiri ajira za Serikali. Mama Evaline Malisa Ntenga, Rais wa Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania anasema mambo yaliyomfikisha hapa alipo ni pamoja na: Moja, Kuwa na hofu ya Mungu na kuona wengine ni bora zaidi. Pili, uadilifu - Intergrity. Uadilifu ni msingi wa tabia njema na ni nguzo kuu ya mafanikio. Katika kila jambo tunalofanya, tunapaswa kuwa waaminifu, wanyofu, na wenye kutenda kwa haki. Uadilifu unajenga heshima na uaminifu kutoka kwa wengine. Ni rahisi kufanya mambo kwa njia rahisi au njia ya mkato, lakini ni muhimu kila mara kufanya kile kilicho sawa, hata kama ni kigumu. Watu wenye uadilifu wanaweza kuaminiwa na kupewa nafasi za juu kwa sababu ya tabia yao nzuri.

Vijana jengeni hofu ya Mungu, Uadilifu, Bidii na Kujali rasilimali muda
Vijana jengeni hofu ya Mungu, Uadilifu, Bidii na Kujali rasilimali muda

Tatu, Bidii/Zeal katika kila jambo. Unapoamua/kukubali kupokea wajibu, utumikie na ujiridhishe ndani mwako umefanya kile ulichostahili. Nne usimamizi wa muda (Nidhamu). Muda ni rasilimali adimu ambayo haiongezeki. Tunapaswa kujifunza jinsi ya kuutumia vyema muda wetu ili tuweze kufanikisha malengo yetu. Hii inajumuisha kupanga siku yetu – ukiweza kupanga siku yako kabla hujalala, kuweka vipaumbele, na kuepuka kupoteza muda katika shughuli zisizo na maana. Tunapojua jinsi ya kusimamia muda wetu vizuri, tunaweza kuongeza ufanisi wetu na kufanikisha mengi zaidi. Vijana wengi leo tunapoteza muda mwingi katika mitandao ya kijamii. Ni dhahiri kwamba hatuwezi kujitenga na dunia lakini tunafunzwa/tunafunza nini jamii? Tano, mahusiano mazuri na wengine na hasa wataalamu wengine. Kwa kujiunga na vyama vya kitaaluma na mitandao mingine kunajenga mahusiano yatakayowasaidia kupata fursa zaidi. Kuwa na washauri ambao watakupa mwongozo katika safari ya kitaaluma. Sita, wajibu kwa jamii. Toa muda, tumia karama zako kama sehemu ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu aliyekujalia karama na mapaji haya. Ni muhimu kujisadaka kwa kusaidia jamii lakini kwa kuanzia nyumbani. Kama wataalamu wa afya, mnayo nafasi ya kipekee ya kuboresha maisha ya watu. Tumieni maarifa yenu kusaidia jamii, kufanya kazi za kujitolea, na kushiriki katika kampeni za afya. Hii itawasaidia kujenga sifa nzuri na kujenga uaminifu ndani ya jamii. Misingi ya kifedha, usimamizi na ujuzi wa uongozi kusaidia vijana katika Maisha “Basics in finance, management and leadership skills to help youth in life.” Masuala ya fedha: Baada ya masomo, mojawapo ya changamoto kubwa ni usimamizi wa fedha. Ni muhimu kuwa na mipango ya kifedha inayojumuisha kuweka akiba, kuwekeza, na kuepuka madeni yasiyo ya lazima. a) Vijana wafanye maamuzi kuhusu fedha mapema, lengo la kuajiriwa na kujiajiri viende sanjari tangu siku ya kwanza ya kuhitimu masomo (kimsingi ni vyema kuanza ukiwa bado chuoni). Ukiwa unasubiri kuajiriwa wakati unalazimika kuwa na kipato cha kujikimu, kuonesha ni graduate (problem solver) lazima uanze na kutatua matatizo ya kwako binafsi. Mungu anabariki kazi za mikono ya wanadamu. Zaidi tujifunze kuwa radhi kupata mafanikio kutokana na nguvu yako halali ya kuyapata.

Jumuiya ya Wakatoliki Hospitali ya Taifa Muhimbili: Vijana na changamoto zao
Jumuiya ya Wakatoliki Hospitali ya Taifa Muhimbili: Vijana na changamoto zao

b) Ukiwa umeanza kuwa na shughuli za kujikimu, anza kuweka Bajeti itakayokusaidia kuweka malengo ya mbeleni. Malengo hayo yatahusisha kuwa na njia mbalimbali za kuweka akiba (savings) na baadae kitega uchumi (investment). Mafanikio ya mtu hayategemei upande wa mapato pekee bali upande wa matumizi zaidi. Jinsi unavyogawa mapato yako vizuri kwenye upande wa matumizi ndivyo utakavyofanikiwa ndiyo maana statistics za TANZANIA zinaonyesha walimu wanaoonekana wana kipato kidogo lakini wengi wana nyumba ukilinganisha na kada zingine zenye kipato kikubwa. Hapa haimaanishi kujenga ndiyo kipaumbele bali inaonesha jinsi ya kufanikiwa kupitia upande wa matumizi. c) Fanya maamuzi sahihi kuhusu uwekezaji kwa kuangalia biashara zenye mtaji unaoweza kupata, eneo la biashara, urahisi wa kutoka kwenye hiyo biashara, uwezekano wa kuongezeka kwa soko la huduma/ bidhaa zako. Kinachosaidia hapo pia ni nidhamu, uaminifu na uchapa kazi. d) Iwapo utakuwa na biashara utambue mtaji ni mkopo lazima urejeshwe. Jifunze kutumia fursa za mikopo inayopatikana katika Taasisi za fedha pia.  Hakikisha unajilipa mshahara kila mwezi, asiyejilipa mshahara ana hatari ya kuua biashaara kwa kuwa shida zake zitatumia fedha za biashara (inaweza kuwa mtaji badala ya faida) badala ya mshahara. e) Ukiajiriwa jitahidi kuwa na kipato mbadala. Unaweza kuanzisha biashara lakini ufahamu kuwa kama huna muda wa kuielewa biashara unaweza kuifilisi pia. Lakini ukivuka hatua za awali za kusimamia biashara ukiwa unafanya kazi utaingia kwenye kundi la wenye nacho huongezewa. Pesa inafuata pesa zingine hasa kwa wenye busara za usimamizi fedha. Hakuna siku mshahara utakupa kila unachotaka “so manage your spending, serve more.” Mtu tajiri zaidi nchini China alisema, "Ukiweka ndizi na pesa mbele ya nyani/tumbili watachagua ndizi kwa sababu hawajui kwamba pesa zinaweza kununua ndizi nyingi. Kadhalika wengi wetu tukipewa kuchaguaa kati ya AJIRA/KAZI na BIASHARA wengi, tutachagua AJIRA/KAZI kwa sababu hatujui/hatuamini kuwa BIASHARA inaweza kutupatia PESA nyingi kuliko mshahara. Moja ya sababu ya inayomfanya maskini kuwa ni maskini ni kwa sababu hatujafundishwa kutambua fursa ya ujasiriamali. Elimu tunayofundishwa darasani tunaelemea zaidi upande wa kufanya kazi za kuajiriwa kuliko kujiajiri wenyewe. Hatutafanikiwa kwa kuishi kutegemea mshahara.

Mama Evaline Ntenga Malisa Ntenga, Rais wa Wanawake Wakatoliki Afrika
Mama Evaline Ntenga Malisa Ntenga, Rais wa Wanawake Wakatoliki Afrika

f) Katika yote, jitahidi sana kuwa na uadilifu, utu, unyenyekevu, upole, upendo na ubunifu katika kila unachofanya. Ndio maana madaktari na wataalamu wa afya ni wengi lakini unakuta mgonjwa yuko tayari kusubiri masaa 5 kumwona daktari fulani wakati wengine wapo na pia wagonjwa wanaambiana yule kimeo, yule mzuri, yule anaringa, yule lazima akutongoze, yule anapenda rushwa, yule mlevi na kadha wa kadha. Sio jina zuri tu unalojijengea mwenyewe na baya pia. Soko la Afrika lina wachache wenye sifa hizo hasa uaminifu. 2. Management (Utawala): Kila mtu ana fursa ya kuongoza kwa kuwafanya wengine wafurahie kufanya kazi) Anayetaka kuongoza wengine lazima awe mfano kwa uhodari wa kazi akiwa na nidhamu na uaminifu. Ukisimamia jambo ulibebe kama jambo lako ndipo utafanikiwa. Ukilifanya kwa ulegevu kisa siyo lako linaambukiza hata kwenye mambo yanayokuhusu. Mtendee mwingine (hata kama ni Kampuni au Serikali) kama unavyotaka kutendewa. b) Uwezo wa mawasiliano (communication skills) ni muhimu kwenye uongozi. Inarahisisha kufikisha ujumbe kwa urahisi kwa walengwa na kwa wakati sahihi. Mawasiliano yanajenga timu na ushirikiano kazini. Upangalo linafikiwa kwa urahisi. c) Kwa kuwa uzingatiaji muda ni jambo muhimu katika mafanikio jitahidi kuwa na uwezo wa kuzingatia muda (time management). Time management ni pana sana linahusisha wakati wa kuanza, kutekeleza na kumaliza. “Bond Univeristy in Queensland Australia” wanasema (Muda sio pesa kwa sababu usimamizi wa fedha na usimamizi wa wakati unahitaji mbinu tofauti) “time is not money because financial management and time management require different techniques.”

Vijana: Muda ni rasilimali adimu itumieni vyema
Vijana: Muda ni rasilimali adimu itumieni vyema

3. Leadership (Uongozi): Je, uongozi ni kipaji cha kuzaliwa nacho au waweza kujifunza? Ukweli kuna wenye kipaji hicho tangu kuzaliwa lakini unaweza pi kujifunza kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na mentorship hivyo ni vizuri kuchukua hatua /jitihada za kujindaa. Uongozi ‘Leadership’ inahusisha zaidi uwezo wa kushawishi wengine wafanye unachotaka (followers). Influence others. a) Ili kuwa kiongozi mzuri ni muhimu kuweka malengo au maono na kuyasimamia. Maono ni jambo muhimu kwa vijana na wengi wanashindwa kwa kuwa linahitaji uvumilivu katika kufikia. b) Vijana lazima mjifunze kufanya maamuzi sahihi. Maamuzi sahihi yanatokana na uwezo wa kupata taarifa, kuzichambua na kuziwekea mbadala (options). Kila jambo lina mbadala, maamuzi sahihi ni kuchukua mbadala sahihi na kusimamia kufanikiwa kwake. c) Emotional intelligence (Akili ya kihisia / kujitambua, kujua mazingira yako, kuwafahamu vizuri unaowaongoza) ni muhimu katika Uongozi. Wengi wanapata msongo wa mawazo; yaani ugonjwa wa sonona (stress/depression) kutokana na kukosa jambo hili linalosaidia kujitambua ili kujiandaa kupokea matokeo mazuri na mabaya. d) Vijana ni vyema kuelewa kuwa si binadamu wote wanazaliwa na sifa za kuwa viongozi, kwahiyo wasilazimishe bali wawekeze katika kujifunza. Q3. Baadhi ya changamoto za kawaida katika maisha ya kazi na mikakati ya kuzishinda kwa ufanisi ni pamoja na (Some common challenges in career life and strategies to overcome them effectively include): a) “Work-life balance.” Ni muhimu kutenganisha masuala ya kazini na masuala binafsi ya nyumbani kwa afya yako. Ukishindwa kutenganisha ni rahisi kufanikiwa upande mmoja na ukaharibu upande mwingine na ukaja kujuta baadae. Jitahidi kuzingatia mud awa kusali, muda wa kazi uwe kazini, muda binafsi, muda wa familia, muda wa marafiki na kufanya tathimini. Kujali afya na ustawi binafsi ni muhimu mno. Katika mazingira ya kutoa huduma kuna uwezekano mkubwa wa kuzingatia kazi/huduma kwa wengi na kusahau au kutokuweka mkazo stahiki katika kujijali. Ninyi mnajua vizuri kuwa katika kutoa huduma kwa wenginje, afya yako ni inapaswa kuwekwa kwanza. Najua kuwa kuna nyakati mnalazimika kufanya zaidi ya kazi moja ili kuongeza pato, katika yote hayo - msisahahu afya yako kwanza.

Uongozi ni kipaji lakini unaweza kujifunza na kupeta sana
Uongozi ni kipaji lakini unaweza kujifunza na kupeta sana

b) Kuweka malengo yanayofikika. Ni muhimu sana kuweka malengo yanayofikika na kusherehekea unapoyafikia. Hili linasaidia kutofanya kazi zinazoharibu afya na mwili wako. Malengo ya aina hiyo yanakusaidia kupata likizo na kugawa kazi kwa wengine inapobidi badala ya overworking. Wakati mwingine unaweza kuangukia mtego wa kufikiri mimi nikiondoka ama nisipokuwepo kazi zitasimama na wengine huenda wakalazimisha mazingira hayo. Madhara yake ni makubwa. Ni vizuri kila mara kuhakikisha kuna mtu anafahamu/ anaweza kufanya unachofanya wewe. c) Migogoro kazini ni jambo la kawaida sana. Kinachotakiwa mgogoro ukitokea kati yako na kiongozi au mwenzako kazini ni kuelewa chanzo na kuwa msikivu unaweza kupata jambo la kujifunza. Baadhi ya migogoro inatatuliwa kwa kukubali tatizo ili kumsaidia msababisha mgogoro kwa sababu lazima ukweli utajulikana wakati wa utulivu. Pia hakikisha unakuwa msuluhishi wa migogoro ya wengine na siyo muanzisha migogoro. Migogoro mingi inakuzwa kwa mitazamo na siyo katika uhalisia wa tatizo. d) Kujiendeleza katika taaluma ni changamoto kwa vijana. Wengi wakianza kazi au binafsi wanakwama kujiendeleza. Hilo linarudisha vijana nyuma kwa kuwa mahitaji ya dunia yanabadilika hivyo bila kujiendeleza unabaki nyuma. Unaweza kujiendeleza kwa kwenda masomoni, networking (mtandao), kujitolea kutatua changamoto mpya (innovation) na njia zingenezo. Teknolojia na mbinu za kisasa zinabadilika kwa kasi – AI / Akili Mnemba inateka dunia kwa kasi ya ajabu. Yapo mengi na mazuri tunaweza kunufaika nayo mfano UBUNIFU, UFANISI, KUBORESHA MAAMUZI YAKO KWA TAFITI ZILIZOCHAMBULIWA NK – Muhimu kuwa na uadfilifu/uaminifu na matumizi yanayokubalika. Ni muhimu sana kuwa na tabia ya kujifunza kila mara. Jiungeni na vikundi vya kitaaluma, hudhurieni semina na warsha, na fuatilieni masomo ya juu ili kuboresha ujuzi wenu. Mkiwa na maarifa mapya, mtaweza kukabiliana na changamoto zinazojitokeza na kutumia fursa mpya kwa ufanisi.

Vijana msisubiri Serikali kutangaza ajira!
Vijana msisubiri Serikali kutangaza ajira!

e) Changamoto ya mahusiano kwa vijana ni tatizo kwasasa kutokana na malezi. Wengi kukataliwa au kusalitiwa kimapenzi wanalichukua personal hadi kufikia hatua ya kuumizana, kuuana au kujiua. Ukweli ni kwamba “Emotional intelligence” inaweza kusaidia kujitambua na kuona mapenzi ni jambo la furaha na raha. Abraham alimkabidhi mkewe kwa mfalme ili asiuawe kwanini vijana wanakufa kwa sababu ya mapenzi. Ukimshindwa tumia usemi wa tenda wema uende zako. f) Vijana wengi wanadhani maisha ni rahisi, la hasha! Lazima mkubali maisha ni mapambano, ukiyachekea yatakupiga kipigo kikali. Tumia hekima ya Mungu kukabiliana na maisha. Adam aliambiwa atakula kwa jasho na aliishi miaka ya kutosha huku akipambana bila kuchoka. Vijana watumie Changamoto kukua zaidi kimawazo na kuweka misingi ya baraka kwa kuwa changamoto hazitaisha bali hekima ya jinsi unavyoziona na kuzitatua ndiyo itabadilika. Mwisho: Fursa ni nyingi kama hatuchagui kwa maana ya kubeza kazi nyingine. Kwa kuanzia waweza kuanza na kazi ndogo ya kuweza kukupa mkate. Usisubiri serikali itangaze ajira. Sio wote watapata. “What you need is open mind, open heart and open hands. Be aggressive, be proactive,” usijidogoshe wewe mwenyewe, “standout in the crowd,” ongeza thamani (add value) kwenye kila unachowaza au kufanya kwa sababu mko wengi hivyo lazima watu waone tofauti yako na wengine. Muwe tayari kuungana, kusaidiana kufanya mambo makubwa. Kuna vijana wataalam wameungana, wamejenga kliniki, hospitali, maduka ya dawa etc au wamekodisha mahali wana run clinic etc. Jichanganyeni na wataalam wenzenu kujua fursa za maisha na biashara ziko wapi, namna ya kufanya uwekezaji kwenye maeneo ambayo hayachukui muda wao mwingi ili kuweka mizani kati ya biashara na huduma kwa wagonjwa.  Msimamo kuhusu mambo ya staha: kuna ukweli kuwa mafanikio yanapatikana kwa namna nyingi. Katika yote hakikisha kuwa unajiwekea falsafa ya maisha inayokupa kufanikiwa bila kuathiri masuala ya utu na staha yako. Hivi vitu ni rahisi kuvipoteza lakini kwa huduma yenu, ni vya muhimu sana maana vina mchango katika wewe kuwa wa kuaminika na kutegemewa.

Ushauri kwa Vijana
30 July 2024, 14:29