Tafakari Dominika ya 17 ya Mwaka B wa Kanisa: Upendo na Ukarimu
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 17 ya mwaka B wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatilia mkazo juu ya wajibu wa kila mwanadamu wa kuhudumiana kwa moyo wa upendo. Mungu ametuumba na kutujalia kila mmoja vipawa na karama zake ili kwazo tuzitumie kuwahudumia wengine ili tujipatie neema na baraka zitokazo kwake. Daima tukumbuke kuwa vyote tulivyonavyo ni zawadi kutoka kwa Mungu. Ndiyo maana maneno ya wimbo wa mwanzo yanasisitiza hivi; “Mungu yu katika kao lake takatifu. Mungu huwakalisha wapweke nyumbani. Yeye huwapa watu wake nguvu na uwezo” (Zab. 68:5-6). Mama Kanisa akilitambua hili, katika sala ya koleta anasali hivi akituombea sisi wanawe; “Ee Mungu, wewe ndiwe mlinzi wa wenye kukutumaini; pasipo wewe hakuna lililo thabiti, hakuna lililo takatifu. Utuzidishie huruma yako; utusimamie, utuongoze. Na sasa tutumie vema mambo ya dunia, hali tumeambata na ya milele.” Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya Nne ya Babu, Bibi na Wazee Duniani, tarehe 28 Julai 2024 inayonogeshwa na kauli mbiu inayochota amana na utajiri wake kutoka katika Sala ya mkongwe “Usinitupe wakati wa uzee, nguvu zangu zipungukapo usiniache” Zab 71:9 anasema, inasikitisha kuona kwamba, watu wengi wanagundua wakiwa wamechelewa kwamba, walishindwa kuwatendea vyema wazee. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanawaonea huruma wazee, kwa kuwatembelea mara kwa mara na kuwatia moyo, wale waliovunjika na kupondeka moyo na hivyo kujikatia tamaa ya maisha; tayari kuwarejeshea tena matumaini katika safari ya maisha yao! Wazee ni amana na utajiri wa jamii; wao ni watunzaji wa mapokeo hai na wanayo misingi ya jamii; mambo wanayopaswa kuwarithisha vijana uzoefu na mang’amuzi ya maisha. Katika kipindi hiki ambacho mahusiano na mafungamano ya kifamilia yanalegalega, Siku ya Nne ya Babu, Bibi na Wazee Duniani ambayo kwa Mwaka 2024 inaadhimishwa tarehe 28 Julai, inakuwa ni fursa ya kuboresha mahusiano kati ya kizazi kipya na kile cha zamani kwa kujenga na kudumisha upendo kati ya vijana wa kizazi kipya pamoja na wazee kwani wazee ni urithi unaopaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa ili kujenga na kudumisha maisha ya kidugu!
Somo la kwanza ni la Kitabu cha Pili cha Wafalme (2Fal. 4:42-44). Somo hili linasimulia muujiza wa Elisha wa kuwalisha watu mia kwa kiasi kidogo cha chakula. Itakumbukwa kuwa Nabii Elisha alichukua nafasi ya Nabii Eliya aliyefanya utume wake katika Israeli miaka 850 KK akipambana na Mfalme Ahab kwa dhambi ya kuabudu miungu ya kipagani iliyojulikana kwa jina la Baal, chini ya ushawishi wa mke wake Jezebeli. Mwenyezi Mungu daima alisikiliza sala na maombi ya Nabii Eliya kuthihirisha nguvu na uwezo wake. Elisha alikuwa mkulima maarufu. Baada ya kuchaguliwa kuwa mridhi wa Eliya, alimtolea Mungu sadaka ya ng’ombe, akawapa watu wale, na baada ya sadaka hiyo, alimfuata Eliya tayari kuanza kazi yake mpya ya unabii (1Waf 19:19-21). Eliya alichukuliwa mbinguni, akamuachia Elisha nguvu za kutenda miujiza alizojaliwa na Mungu (2Waf 2:13). Moja ya muujiza ni huu wa kuwalisha watu mia kwa chakula alicholetewa na mtu kutoka Baal-shalisha. Ni chakula cha malimbuko, mikate ishirini ya shayiri, na masuke mabichi ya ngano gunia moja. Elisha alimwamuru mtumishi wake awape watu ili wale. Mtumishi wake alisita kwa kuwa aliona chakula kile ni kidogo tu kwa idadi ya watu waliokuwapo. Ndipo Elisha aliposisitiza na kumwambia; “Uwape watu, ili wale; kwa kuwa Bwana asema hivi; Watakula na kusaza. Basi akawaandikia, nao wakala, wakasaza, sawasawa na neno la Bwana.” Somo hili linatufundisha kuwa tukimtumainia Mungu hatutapungukiwa na chochote. Ndivyo anavyosisitiza mzaburi katika wimbo wa katikati akisema; “Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru, na wacha Mungu wako watakuhimidi. Wataunena utukufu wa ufalme wako, na kuuhadithia uweza wako. Macho ya watu yakuelekea Wewe, nawe huwapa chakula chao wakati wake. Waufumbua mkono wako, wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake. Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote, na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote. Bwana yu karibu na wote wamwitao, wote wamwitao kwa uaminifu” (Zab. 145:10-11, 15-16, 17-18).
Somo la pili la Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso (Efe. 4:1-6). Katika somo hili Mtume Paulo anawaasa wakristo wa Efeso wawe na umoja ulio kiini cha maisha ya kikristo. Anasema hivi Mtume Paulo; “Nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo, na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani. Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote”. Ekaristi Takatifu, mwili na damu ya Kristo tunayoipokea inatudai kuishi kwa umoja na upendo. Kuishi kwa umoja na upendo kama jamii ya kikristo ndiko kuishi kiekaristi kwani tunashiriki meza moja ambayo inatutaka ushirika katika maisha ya kijamii. Injili ni ilivyoandikwa na Yohane (6:1-15). Itakumbukwa kuwa katika mwaka B wa kiliturujia, dominika Injili ni ya Mwinjili Marko. Lakini kuanzia dominika ya 17 hadi 21 Injili inatoka sura ya sita ya Injili ya Yohane nayo inatoa fundisho kuu juu ya Ekaristi Takatifu Chakula cha kiroho. Sehemu ya Injili ya dominika ya 17B, inahusu muujiza wa Yesu kuwalisha watu elfu tano kwa chakula cha kawaida, mikate mitano na samaki wawili, wakala wakashiba hata kusaza. Hili ni ashirio la Ekaristi Takatifu, chakula chetu cha kiroho kinachotupa nguvu ya kuendelea na safari ya kuelekea Mbinguni. Na chakula hili kamwe hakitakaa kiishe na kila anayekipokea kwa imani na kwa kustahili anashibishwa daima. Kumbe, tunaona kuwa katika miujiza ya kuwalisha watu; muujiza wa Elisha katika somo la kwanza na muujiza wa Yesu katika Injili, wote wawili hawakutumia chakula chao bali ni chakula walichotoa watu wengine kile kidogo walichokuwa nacho kwa moyo wa ukarimu.
Kwa neema za Mungu, hicho kidogo kiliwatosha watu wote kwani neema na baraka za Mungu hazipungua hata kidogo. Ujumbe mahususi hapa ni huu daima, tusiogope kutoa kuwapa wengine wanaohitaji zaidi yetu kwa kuhofia tutabaikiwa na nini? Tumkumbuke mwanamke mjane wa Serapta aliyemsaidia Eliya kwa kumtengenezea mkate kwa unga kidogo aliokuwa nao na mafuta machache tu kwenye chupa kwa neno la Eliya, kopo la unga halikuisha wala chupa ya mafuta haikukauka (1Waf. 17:8-24). Tuwape wenye njaa chakula wale, Mungu atatubariki, wala hatutapungukiwa na chochote, maana mkono utoao ndio upokeao. Katika Injili Andrea alimwambia Yesu; “Yupo mtoto aliye na mikate mitano ya shayiri na samaki wawili; lakini hii ni nini kwa watu wengi kama hawa?” (Yn. 6:8). Na mtumishi alimwambia Elisha; “Je niwaandikie hiki watu mia?” (2Wafalme 4:42). Haya ni malalamiko ya nyakati zote za mwanadamu kuwa raslimali au vitu tulivyonavyo ni vichache, havitutoshi sote. Hivyo wengine lazima wafe, ili wengine waishi. Huu ni moyo wa uchoyo na ubinafsi unaotusukuma kusema tulichonacho hakitutoshi sisi na wao. Tukumbuke kuwa vile alivyotujalia Mwenyezi Mungu sio kwa ajili yetu tu. Kama umejaliwa vingi zaidi ya unachohotaji, fahamu kuwa umepewa jukumu la kuwa mfereji ili vile vya ziada vipitie kwao na kuwafikie wengine. Ndiyo maana tunaambiwa; “wapeni watu ili wale.” Si lazima uchangie mali; changia ulichonacho. Elimu yako; wape watu ili wale, karama ulizojaliwa, wape watu ili wale; nguvu ulizojaliwa, wape watu ili wale; muda ulio nao, wape watu ili wale. Tukumbuke daima kuwa kujilimbikizia mali wakati wengine wanakufa njaa ni kula hukumu yako mwenyewe.
Mbaya zaidi kama ulivyojilimbikizia ni matunda ya uovu kama anavyoonya Mtume Yakobo akisema; “Basi sikilizeni, ninyi matajiri, lieni na kuomboleza kwa ajili ya hali mbaya sana inayowajia. Utajiri wenu umeoza na mavazi yenu yameliwa na nondo. Dhahabu yenu na fedha yenu vimeliwa na kutu. Kutu yake itashuhudia dhidi yenu, nayo itaila miili yenu kama vile moto. Mmejiwekea hazina kwa ajili ya siku za mwisho. Angalieni! Ule ujira wa vibarua waliolima mashamba yenu mliouzuia kwa hila unapiga kelele dhidi yenu na vilio vya wavunaji vimefika masikioni mwa Bwana wa majeshi. Mmeishi duniani kwa anasa na kwa starehe, mmejinenepesha kama vile katika siku ya karamu. Mmewahukumu na kuwauwa watu wenye haki, ambao walikuwa hawapingani nanyi” (Yak. 5:1-6). Basi tuweni watu wa haki, tumtendee na kumpa kila mmoja haki yake. Zaidi sana tuweni watu wa shukrani. Yesu kabla ya kuwapa mitume mikate na samaki ili wawagawie watu, alishukuru kwanza. Tujifunze kushukuru kwa kila jambo. Tudumu katika kusali, tukimwomba Mungu atujalie viongozi bora na wema kuanzia ngazi ya familia, jumuiya, Kanisa, nchi na dunia kwa ujumla wake, wenye moyo wa kushughulikia ustawi na maslahi ya watu wote bila ubaguzi. Atujalie kila mmoja wetu moyo wa ukarimu wa kuchangia alivyotujalia kwa maendeleo ya jamii zetu na kwa kuwasaidia wengine na atuondolee moyo wa ubinafsi, ufisadi, rushwa na wizi wa mali ya umma kwa ajili ya maendeleo ya maisha ya wote hapa duniani, ili mwisho wa yote tukaurithi uzima wa milele mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo!