Papa Franciko ana upongeza Mfuko wa "Casa dello Spirito e delle Arti" kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na upendo kwa wafunga na maskini. Papa Franciko ana upongeza Mfuko wa "Casa dello Spirito e delle Arti" kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na upendo kwa wafunga na maskini.  

Zingatieni Utu, Heshima na Haki Msingi za Wafungwa Magerezani

Ni mfuko unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu, hasa miongoni mwa wafungwa, wakimbizi, wahamiaji, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni mfuko unaowashirikisha wakleri, watawa na walei, mintarafu mwanga wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ili kumtangaza na kumshuhudia Yesu, Mwanga wa Mataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mfuko wa “Casa dello Spirito e delle Arti” ulianzishwa kunako mwaka 2012 na Arnoldo Mosca Mondadori na Marisa Baldoni. Ni mfuko ambao unatoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu, hasa miongoni mwa wafungwa, wakimbizi, wahamiaji, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni mfuko unaowashirikisha wakleri, watawa na waamini walei, mintarafu mwanga wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, Mwanga wa Mataifa. Ni mfuko pia unaowajumuisha wasanii, ili kuwasaidia watu kutumia vyema karama na mapaji yao ili kukuza utu na heshima yao. Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 4 Februari 2022 amekutana na kuzungumza na baadhi ya wanachama wa Mfuko wa “Casa dello Spirito e delle Arti.” Amewapongeza wanachama wa Mfuko huu kwa huduma makini wanayotoa kwa wafungwa kwenye gereza la “San Vittore huko Milano”, Kaskazini mwa Italia kwa kushirikiana na viongozi wa Gereza.

Wajumbe wa mfuko huu ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu
Wajumbe wa mfuko huu ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu

Kwa njia hii, wamewajengea wafungwa uwezo wa kutengeza hostia kwa ajili ya maadhimisho ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu; wanatengeneza ala na vyombo vya muziki. Ni Mfuko unaojihusisha na shughuli mbalimbali za ufundi seramala, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Yosefu na Yesu mwenyewe. Wafungwa hawa ni watengenezaji maarufu wa divai, alama ya furaha na sherehe, kama ilivyokuwa kwenye harusi ya Kana ya Galilaya, Kristo Yesu alipoufunua utukufu wake na kuonesha uaminifu wa Mungu kwa waja wake. Baadhi ya wakimbizi wanajihusisha na ufundi cherehani. Baba Mtakatifu amewasalimia wawakilishi wa makundi yote haya bila kuwasahau watu wa kujitolea na washirika kutoka Hispania, Brazil na Argentina. Baba Mtakatifu anasema, wote hawa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Matumaini, mawe hai katika mchakato wa ujenzi wa urafiki wa kijamii na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Mfuko wa “Casa dello Spirito e delle Arti” pamoja na mafanikio makubwa unaoendelea kuyapata, lakini pia unakabiliwa na matatizo pamoja na changamoto katika maisha na utume wake kutokana na historia ya watu binafsi, makosa na mapungufu yao.

Baba Mtakatifu Francisko anakumbusha kwamba, huruma na upendo wa Mungu unawawezesha kuvuka yote haya, ikiwa kama wako tayari kuwapokea na kuwasaidia watu hawa kama ndugu wamoja. Huruma na msamaha wa Mungu unawawezesha kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza Bwana Arnoldo Mosca Mondadori na Bibi Marisa Baldoni kwa mfano wao mwema kama mashuhuda wa Injili ya huruma na mapendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime, ili waweze kuendelea katika safari hii ya matumaini, huku wakishindikizwa na Bikira Maria, Msaada wa Wakristo pamoja na Mtakatifu Yosefu. Mfuko huu, ujitahidi kujielekeza zaidi katika ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya kijamii, ili kuunda familia moja ya watu wa Mungu wanaowajibikiana na kusaidiana kwa hali na mali, kama ilivyokuwa kwa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.

Injili ya Huruma

 

05 February 2022, 15:18