Hija ya Kitume ya Papa Francisko Canada: Mahojiano Maalum na Waandishi wa Habari
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Hija ya 37 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko kimataifa nchini Canada kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 30 Julai 2022 imenogeshwa na kauli mbiu “Walking Together” yaani “Kutembea Pamoja.” Lengo ni kukoleza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa unaosimikwa katika msingi wa toba na wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa; ukweli na uwazi kwa ajili ya kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za watu asilia wa Canada. Baba Mtakatifu, kwa niaba ya Mama Kanisa ameomba tena msamaha unaopania kuleta mwanga angavu wa hija ya: toba, wongofu wa ndani, matumaini na upatanisho wa Kitaifa, unaofumbatwa katika misingi ya ukweli na uwazi. Nia ni kuleta utakaso wa kumbukumbu na hatimaye, kuendelea kujikita katika uinjilishaji wa kina unaosimikwa katika mchakato wa kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili ya Kristo Yesu. Msafara wa Baba Mtakatifu nchini Canada ulisheheni waandishi wa habari 80 kutoka katika Mataifa 10, ili kushuhudia na hatimaye, kuwajuza watu wa Mungu, yale yaliyokuwa yanajiri katika hija hii ya toba, wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa. Akiwa njiani kurejea kutoka Canada, Jumamosi, tarehe 30 Julai 2022, Baba Mtakatifu alipata nafasi ya “kuchonga” na wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii, kwa kujibu maswali mazito saba kwa kusema kwamba, dhuluma na nyanyaso dhidi ya watu asilia wa Canada yalikuwa ni mauaji ya kimbari. Bado madhara ya ukoloni mkongwe na ukoloni wa kiitikadi yanaendelea kudhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu anasema, kuna uwezekano kwake yeye kung’atuka kutoka madarakani, lakini kwa sasa hana mpango huo. Amewapongeza na kuwashukuru wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii waliomsindikiza wakati wa hija yake ya kitume nchini Canada na hatimaye, kuwapasha watu wa Mungu yale yaliyokuwa yanajiri.
Baba Mtakatifu anasema madhara ya ukoloni mkongwe, mamboleo pamoja na ukoloni wa kiitikadi yanaendelea kujionesha katika ulimwengu mamboleo. Hii ni tabia ya kudharau, kunyanyasa na kuwatweza watu wengine kwa misingi ya ubaguzi wa rangi inayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kuhusu madhara ya ukoloni na ubaguzi wa rangi, Mtakatifu Yohane Paulo II, aliomba msamaha kwa niaba ya Kanisa kwa madhara makubwa yaliyosababishwa na biashara ya utumwa na hatimaye, ukoloni. Ikumbukwe kwamba, watu wote ni sawa kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baba Mtakatifu anasema, maendeleo ni jambo jema, lakini yanapaswa kulinda na kudumisha utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi na mafao ya wengi. Mikopo na misaada inayotolewa kwa baadhi ya Nchi changa duniani, inahusianishwa na masharti magumu ambayo wakati mwingine yanakwenda kinyume cha haki msingi, utu, heshima na tamaduni za watu husika. Kumbe, kuna haja ya kujitakasa na hatimaye, kuondokana na tabia zinazokumbatia ukoloni mkongwe, ukoloni mamboleo na ukoloni wa kiitikadi. Watu wote mbele za Mwenyezi Mungu wana haki na utu sawa! Kile kinachoitwa “Ugunduzi wa Amerika ya Kusini” na Ukoloni ni kati ya mambo yaliyochangia kufifisha utu, heshima na haki msingi za watu asilia wa Canada, kiasi hata cha kung’olewa kutoka katika ardhi yao asilia. Canada kama taifa lilizaliwa kunako mwaka 1867. Lakini, Mama Kanisa katika maisha na utume wake, amekuwa mstari wa mbele kutetea utu, na heshima ya binadamu kwa kupinga na kukataa mifumo yote ya ukoloni: yaani: Ukoloni mkongwe, ukoloni mamboleo na sasa ukoloni wa kiitikadi kwa sababu mifumo yote hii inakwenda kinyume cha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Watu asilia wa Canada licha ya kutendewa mauaji ya kimbari kitamaduni, lakini kimsingi haya yalikuwa ni mauaji ya kimbari yaliyodhalilisha: tamaduni, lugha, mapokeo na tunu msingi za watu asilia wa Canada, kiasi hata cha kuwapoka watoto kutoka katika familia zao.
Baba Mtakatifu anakiri kwamba, kwa sasa anakabiliana na changamoto za kiafya ambazo haziwezi kumpatia nafasi ya kusafiri kama hapo awali. Lakini, changamoto ya afya si janga ambalo linaweza kulilazimisha Kanisa kufanya uchaguzi, ili kumpata Papa mwingine. Jambo la msingi ni kusoma alama za nyakati na kutumia busara. Madaktari walitumia muda wa saa sita kwa ajili ya dawa za usingizi, wakati wa upasuaji mkubwa waliomfanyia hivi karibuni, hata leo hii, bado anahisi changamoto zake. Baba Mtakatifu anasema, ataendelea kufanya hija za kichungaji, kama njia ya kuwahudumia wa Mungu na kuonesha ukaribu wake kwao. Anakaza kusema, bado ametia nia ya kutembelea Ukraine, Kazakhstan, Sudan ya Kusini na DRC. Hija ya Kitume Sudani ya Kusini, ina mwelekeo wa majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa. Hija hizi, pengine zinaweza kutekelezwa mwaka 2023, kwa sasa bado anasikiliza maumivu ya miguu! Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake Binafsi: “Mortu Prorio” “Imparare a congedarsi” yaani “Kujifunza Kustaafu” anatoa wosia na sala kwa viongozi wa Kanisa kujiandaa vyema kung’atuka kutoka madarakani, kwa kutambua kwamba, hii pia ni sehemu ya huduma inayohitaji mfumo mpya wa uwepo na uwajibikaji. Haya ni maandalizi muhimu sana ya maisha ya ndani, kwani inawezekana kabisa kung’atuka kutoka madarakani kwa kigezo cha umri au pale ambapo Askofu anaombwa kuendelea na utume wake kwa muda mrefu kidogo, hata kama atakuwa ametimiza umri wa miaka 75, ambao kisheria: Maaskofu pamoja na wale walioteuliwa na Papa wanapaswa kuachia madaraka!
Wakati mwingine kiongozi wa Kanisa anaweza kulazimika kung’atuka kutoka madarakani kutokana na sababu za kiafya zinazomzuia kutekeleza vyema dhamana yake ya: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kujiandaa kikamilifu mbele ya Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala, ili kuachana na kishawishi cha uchu wa madaraka kwa kudhani kwamba, wao ni watu muhimu sana na wala hakuna watu mbadala. Mwelekeo huu wa maisha ya ndani unaojikita katika sala utawasaidia viongozi wa Kanisa kuvuka kipindi hiki kigumu kwa: amani, utulivu wa ndani na matumaini, vinginevyo, kinaweza kugeuka na kuwa wakati wa kinzani na machungu katika maisha. Kiongozi wa Kanisa anayetambua ukweli wa kujiandaa, anapaswa kuwa na mang’amuzi yanayofumbatwa katika sala namna ya kufungua ukurasa mpya wa maisha yake baada ya kung’atuka kutoka madarakani, kwa kuanza kuweka mikakati mipya ya maisha inayofumbatwa katika sadaka, unyenyekevu, sala pamoja na kujisomea zaidi! Pale inapowezekana, kiongozi wa Kanisa awe tayari kutoa huduma za kichungaji kadiri ya uwezo na nafasi yake. Baba Mtakatifu katika mahojiano wakati wa kurejea kutoka Canada anasema, kung’atuka kutoka madarakani na kubaki kama Myesuit ni wito kadiri ya mapenzi ya Mungu atakama ni kun’atuka kutoka madarakani, ili kutoa nafasi kwa kiongozi mwingine wa Kanisa bila kusubiri kifo, kwani kama ni kifo, kila mtu atakufa, “changamoto kubwa ni kutangulia tu.”
Kama mtu anasongwa na magonjwa na hali ya kuchoka, kung’atuka kutoka katika shughuli za kichungaji ni jambo la busara. Mafungo ya kiroho na mang’amuzi ya maisha na utume ni mambo muhimu sana yanayomwezesha mtawa au kiongozi wa Kanisa kufanya maamuzi magumu katika maisha. Kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, anajisikia huru zaidi kufikiri na kutenda kama Myesuit katika maisha na utume wake. Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa na Ibada angavu kwa Bikira Maria, kumbe, kila kiongozi wa Kanisa analo “jambo lake” analoweza kuchangia katika maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu. Upapa ni huduma inayomwezesha kiongozi aliyechaguliwa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, akiwa amebeba ndani mwake, karama na mapaji ya Roho Mtakatifu, udhaifu na mapungufu yake ya kibinadamu. Mtakatifu Paulo VI, Muasisi wa maadhimisho ya Sinodi mara baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican anasema, Sinodi ni chombo cha kimisionari na uinjilishaji mpya unaolisaidia Kanisa baada ya kutembea pamoja katika sala, tafakari, mang’amuzi na hatimaye, utekelezaji wake unaofanywa na watu wote wa Mungu kadiri ya wito na nafasi zao katika maisha na utume wa Kanisa. Sinodi ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Juhudi za kichungaji na kitaalimungu zisaidie kuimarisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu majadiliano ya kiekumene, kwa kumpokea Roho Mtakatifu ili kuweza kujifunza mengi kutoka kwa wengine na kuvuna kile ambacho Roho Mtakatifu amepanda ndani yao, ambacho kimekusudiwa kuwa ni zawadi kwa wengine.
Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu nchini Ujerumani na hatimaye, tamko lao, hayakuzingatia ushirika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Kuhusu safari ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, Baba Mtakatifu aliandika Waraka wa Kitume, baada ya sala na tafakari ya kina, ili kujenga na kuimarisha ushirika, umoja na utume wa Kanisa. Aliandika waraka ule kama: Kiongozi wa Kanisa, kama Kaka, Baba na Mwamini, anayepania ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Italia kwa sasa inapitia kipindi kigumu sana cha historia na maisha yake, baada ya madhara makubwa yaliyosababishwa na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuchechemea kwa uchumi Kitaifa na Kimataifa. Hivi karibuni, Waziri Mkuu wa Italia Prof. Mario Draghi, “alibwaga manyanga” na kuachia ngazi. Katika karne hii ya 21 Prof. Mario Draghi anakuwa ni Waziri mkuu wa 20 kuachia ngazi ya madaraka. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa kawaida hapendi kujichanganya na siasa za ndani za Italia. Katika kipindi hiki wanapojiandaa kwa ajili ya kuchagua Waziri mkuu, jambo la msingi kwa wananchi wa Italia ni kuwajibika kikamilifu ili waweze kumpata kiongozi anayefaa.
Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Katiba ya Kitume “Fidei depositum” yaani “Amana ya Imani” iliyoridhia kuchapishwa kwa Katekisimu ya Kanisa Katoliki anasema, Katekisimu ya Kanisa Katoliki inakazia kwamba, hatima na kiini chote cha mafundisho ya imani vinaelekezwa katika upendo ambao hauna kikomo. Iwe inaelekezwa kwa ajili ya ukweli wa imani au, matumaini au wajibu wa utendaji wa maadili, upendo wa Mungu utadumu daima. Kanisa kwa kusoma alama za nyakati, linataka kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na uhai wa binadamu dhidi ya adhabu ya kifo inayokumbatia utamaduni wa kifo. Mwenyezi Mungu anawapatia waja wake nafasi ya kutubu na kumwongokea, ili aweze kuwakirimia msamaha na kuwaonjesha tena huruma na upendo wake usiokuwa na kifani! Baba Mtakatifu Francisko anafafanua kwamba, hapa hakuna kinzani na Mafundisho ya Kanisa yaliyopita, kwani jambo la msingi ni kusimama kidete kulinda uhai wa binadamu tangu pale anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida yanapomfika mtu kadiri ya mpango wa Mungu. Huu ni mwendelezo wa uelewa wa kina wa Mafundisho tanzu ya Kanisa kwani, adhabu ya kifo ina madhara makubwa kwa utu na heshima ya binadamu. Hivyo, Kanisa katika mafundisho, maisha na ibada zake, linaendeleza daima na kuvirithisha vizazi vyote ukweli juu yake, na juu ya yale anayoyaamini. Huu ni muhtasari wa asili na utume wa Kanisa unaofafanuliwa katika mafundisho na maisha yake, kama chachu muhimu inayowaunganisha na kuwawezesha waamini kuwa ni watu wa Mungu. Kimsingi Baba Mtakatifu anakaza kusema, mafundisho tanzu ya Kanisa na kanuni maadili ni mambo yanayoendelea kukua na kukomaa katika maisha na utume wa Kanisa kwa kusoma alama za nyakati. Kuhusu vizuia mimba ni kazi ya Mama Kanisa kufafanua na kutoa mwelekeo unaokazia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Matumizi ya silaha za kinyuklia ni kinyume kabisa cha kanuni maadili na utu wema. Mapokeo hai ya Kanisa ni amana na utajiri katika utume wa Kanisa.
Tarehe 27 Agosti 2022, Baba Mtakatifu Francisko atawasimika Makardinali wapya 21 walioteuliwa hivi karibuni pamoja na kupiga kura kwa ajili ya wenyeheri wanaotarajiwa kutangazwa kuwa watakatifu ndani ya Kanisa na mifano bora ya kuigwa na waamini wengine. Kuhusu sifa na vigezo vya Papa atakayefuata baada yake, si kazi yake kuvibainisha kwani hii ni kazi ya Roho Mtakatifu. Jambo la msingi, awe ni kiongozi mwenye amani na utulivu ndani mwake. “Ipse armonia est.” Baba Mtakatifu Francisko anamshukuru na kumpongeza mwandishi mmoja wa habari aliyebainisha changamoto zilizokuwa zinamkabili Baba Mtakatifu kama kielelezo cha uhakika kwake kung’atuka kutoka madarakani. Hii ni kazi nzuri iliyofanywa kwa umakini mkubwa, lakini haya yalikuwa ni mawazo yake binafsi na si ukweli wa mambo. Jambo la msingi kwa waandishi wa habari wajitahidi kusoma alama za nyakati na kuzipatia tafsiri sahihi, vinginevyo, wanaweza kuwapotosha watu. Hija ya kitume nchini Canada, imekuwa ni fursa ya kujipima jinsi ya kukabiliana na changamoto za kiafya. Hija hii ilikuwa pia ni nafasi ya kuwashukuru na kuwapongeza wanawake watakatifu kwa mchango wao katika ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa. Wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika malezi na makuzi ya watoto wao; kwa kurithisha tamaduni, mila na desturi njema kwa hakika wamekuwa ni Makatekista wa kwanza kwa imani, maadili na utu wema. Waamini watambue kwamba, Kanisa ni Mama na Mwalimu wa: Imani, Maadili na Utu wema. Wanawake wajitahidi kuwa mstari wa mbele katika mchakato wa kuwarithisha watoto wao imani yao.