Hija ya Kitume ya Papa Francisko Canada: Misa ya Upatanisho Kitaifa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Wanafunzi wa Emau walibahatika kuandamana na Kristo Yesu katika safari yao ya matumaini ya Kikristo bila kumtambua, kwani macho yao yalikuwa yamefumbwa! Walikuwa wakisafiri kwa huzuni kubwa na hali ya kukata tamaa kwa sababu ya kifo cha ukatili kilichomkuta Kristo Yesu. Walikuwa wakimtumaini kwamba Yeye ndiye Masiha na Mkombozi wao. Wanafunzi wa Emau walikuwa na majonzi makubwa mioyoni mwao kwani Fumbo la Msalaba, yaani mateso na kifo cha Kristo Yesu liliwaachia machungu makubwa kwani liliyeyusha matumaini na maisha yao; wakaonekana kushindwa vita hata kabla ya kuianza. Lakini, wakamtambua Kristo Yesu wakati wa kuumega mkate na hapo hapo akatoweka tena machoni pao! Nao wakaambiana, Je, mioyo yetu haikuwaka ndani yetu pale alipokuwa akizungumza na kufafanua Maandiko Matakatifu? Hija ya 37 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Canada kuanzia tarehe 24-30 Julai 2022. Hija hii inanogeshwa na kauli mbiu “Walking Together” yaani “Kutembea Pamoja.” Lengo ni kukoleza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa unaosimikwa katika msingi wa toba na wongofu wa ndani; ukweli na uwazi kwa ajili ya kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za watu asilia wa Canada. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 28 Julai 2022 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya toba, wongofu na upatanisho wa Kitaifa nchini Canada katika Madhabau ya Kitaifa ya Mtakatifu Anna wa Beaupré: “Sainte Anne de Beaupré.”
Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amejikita kufafanua kuhusu safari ya wanafunzi wa Emau kutoka katika hali ya kushindwa na kuanza kujenga matumaini; ameonya kuhusu kishawishi cha kutaka kukimbia ukweli wa Kiinjili kuhusu mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu; wanafunzi wa Emau wakamtambua Kristo Yesu kwa kuumega mkate, mwaliko kwa waamini kukutana na Kristo Yesu katika, Neno, Sakramenti na Huduma kwa maskini na hivyo kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya Matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo, kiasi cha kukata tamaa! Baba Mtakatifu Francisko anasema, Fumbo la Msalaba, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, ulikuwa ni mtihani mkubwa kwa wafuasi wake, walioliangalia Fumbo hili kama Kashfa, iliyofyekelea mbali matumaini na ndoto zao kuyeyuka kama nta ya mshumaa. Wakabaki wamekata tamaa na kuelemewa na majonzi moyoni. Hali hii ni sawa na safari ya maisha ya kiroho, pale ambapo mwamini anahisi kuelemewa sana dhambi, kiasi hata cha kujikatia tamaa.
Hii ndiyo kashfa ya maovu yaliyoliandama Kanisa nchini Canada, kiasi cha kuacha majonzi makubwa katika maisha ya watu, kama ilivyokuwa kwa wale wanafunzi wa Emau, kuna kishawishi kikubwa cha kutaka kukimbilia uhalisia wa mambo, kwa kudhani kwamba, hakuna jambo lolote linalowezekana kutendeka. Wanafunzi wa Emau walibaki wakiwa wameelemewa na majonzi na hali ya kukata tamaa, lakini Kristo Yesu, alitokea na kuanza kuambatana nao katika safari ya maisha yao ya kiroho, akawafafanulia Fumbo la Pasaka kadiri ya Maandiko Matakatifu, tangu Agano la Kale hadi utimilifu wake kwenye Agano Jipya. Hivi ndiyo inavyotokea hata kwa waamini katika ulimwengu mamboleo, pale wanaposhiriki katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa na hivyo kutiwa tena moyo, ari na ujasiri wa kusonga mbele, ili kujenga Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Hii ni fursa ya kuondokana na chuki, vita, uharibifu na mateso, tayari kujikita katika mchakato wa ujenzi wa mji wa Mungu na nchi katika ujumla wake. Baba Mtakatifu anakaza kusema, wanafunzi wa Emau walimtambua Kristo Yesu kwa kuumega mkate, na hiyo ikawa ni chemchemi ya matumaini mapya, kutoka katika kushindwa kwao, wakapata nguvu na ujasiri uliopyaisha matumaini, moto wa Injili ukawaka tena nyoyoni mwao!
Wakamtambua Kristo Yesu aliyekuwa anaambatana nao katika safari ya maisha yao ya kiroho. Wakaamini na kutambua ushuhuda uliotolewa na wale wanawake watakatifu, kama ilivyo kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa na kwa Mtakatifu Anna wa Beaupré: “Sainte Anne de Beaupré” bila kuwasahau wanawake wengi walioandamana na Kristo Yesu katika maisha na utume wake, kiasi cha kumwonesha huruma na upendo wa dhati. Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu Francisko anasema, Dominika, Siku ya kwanza ya Juma, ni njia ya upatanisho, inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo angavu wa Kristo Yesu Mfufuka, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini hata katika mazingira ambamo hakuna tena chembe ya matumaini. Fumbo la Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu yake azizi, kiwe ni chanzo na kilele cha maisha ya waamini. Kristo apewe nafasi ya kushirikiana na waja wake, maisha, udhaifu na matumaini yao, ili aweze kuwanyanyua tena; kuwaganga na kuwaponya, hatimaye, kuwapatanisha na Mungu pamoja na jirani zao. Na wao wakisha kupatanishwa na Mungu wageuke na kuanza kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upatanisho na amani katika jamii inayowazunguka.
Waamini wajitahidi katika maisha yao ya kila siku, kumkaribisha Kristo Yesu ili aweze kushinda pamoja nao kwa njia ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Kristo Yesu akaye pamoja nao katika Neno na Sakramenti zake, wakati ambapo matumaini na hali ya kukata tamaa inapowazonga zonga katika maisha. Kristo Yesu akae pamoja nao wakati giza la maisha linapoanza kuwashukia na kutaka kuwameza. Jambo la msingi, daima waamini wajenge utamaduni wa kumkaribisha Yesu, ili kuweza kuandamana naye katika maisha ya kila siku, ili aweze kuwa kweli ni chemchemi ya matumaini na maisha mapya.
Kwa upande wake, Kardinali Gérald Cyprien Lacroix, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Quèbec, Canada mara baada ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa nia ya kuombea toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa, amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko na kuwakumbusha waamini kwamba, kwa njia ya Fumbo la Pasaka, Kristo Yesu amewakirimia waja wake ujumbe wa imani, matumaini na mapendo, kwa kuwakumbusha kwamba, wao kweli ni watoto wateule wa Mungu. Canada ni nchi ambayo imeinjilishwa na wafuasi wengi wa Kristo Yesu. Licha ya kutangaza na kushuhudia kweli za Kiinjili, lakini pia katika udhaifu na ubinadamu wao wamekuwa ni chanzo cha ubaguzi, utengano na kinzani za kijamii, kiasi hata cha imani kufifia na kupoteza ule mwanga wake angavu, ambao ulipaswa kuwa ni dira na mwongozo wa maisha ya waamini. Baba Mtakatifu Francisko ametangaza tena kwa nguvu zake zote mchakato wa toba, wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa. Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, anaendelea kuwa ni shuhuda wa faraja, hekima na busara inayowajenga na kuwaimarisha watu wa Mungu katika safari ya maisha yao hapa duniani. Watu wengi wanatambua dhamana na utume unaotekelezwa na Baba Mtakatifu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mchakato wa toba, wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa utasaidia kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu nchini Canada. Huu ni mchakato unaohitaji muda na uvumilivu.