Papa Francisko Jengeni Utamaduni wa Kusoma, Kusikiliza, Kutafakari na Kumwilisha Neno la Mungu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Wanafunzi wa Emau walibahatika kuandamana na Kristo Yesu katika safari yao ya matumaini ya Kikristo bila kumtambua, kwani macho yao yalikuwa yamefumbwa! Walikuwa wakisafiri kwa huzuni kubwa na hali ya kukata tamaa kwa sababu ya kifo cha ukatili kilichomkuta Kristo Yesu. Walikuwa wakimtumaini kwamba Yeye ndiye Masiha na Mkombozi wao. Wanafunzi wa Emau walikuwa na majonzi makubwa mioyoni mwao kwani Fumbo la Msalaba, yaani mateso na kifo cha Kristo Yesu liliwaachia machungu makubwa kwani liliyeyusha matumaini na maisha yao; wakaonekana kushindwa vita hata kabla ya kuianza. Lakini, wakamtambua Kristo Yesu wakati wa kuumega mkate na hapo hapo akatoweka tena machoni pao! Nao wakaambiana, Je, mioyo yetu haikuwaka ndani yetu pale alipokuwa akizungumza na kufafanua Maandiko Matakatifu? Hija ya 37 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Canada kuanzia tarehe 24-30 Julai 2022 na kunogeshwa na kauli mbiu “Walking Together” yaani “Kutembea Pamoja.” Lengo ni kukoleza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa unaosimikwa katika msingi wa toba na wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake iliyojikita katika hija yake ya Kitume nchini Canada, Jumatano tarehe 3 Agosti 2022, amewakumbusha waamini kwamba, kama ilivyokuwa kwa wanafunzi wa Emau, hata wao, Kristo Yesu anaendelea kuambatana nao katika hija ya maisha yao hapa duniani, ili aweze kuwakirimia matumaini, huku akiwafungulia njia mpya za kupitia.
Jambo la msingi kwa waamini ni kujipatanisha na Kristo Yesu, ili hatimaye, wajielekeze katika ujenzi wa dunia inayosimikwa katika, udugu sanjari na kuheshimu mazingira nyumba ya wote. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, uwepo wa Kristo Yesu katika maadhimisho ya Liturujia Takatifu yanajionesha kwa namna ya pekee katika Sadaka ya Misa Takatifu, katika nafsi ya Kasisi na kwamba, anajitoa tena kuwa Sadaka Altareni kwa njia ya huduma ya mapadre na Yupo hasa katika Ekaristi Takatifu na katika Sakramenti za Kanisa. Kristo Yesu yupo katika Neno lake, kwa kuwa ni Yeye anayesema wakati Maandiko Matakatifu yanaposomwa katika Ibada ya Misa Takatifu. Yupo Kanisa linaposali na kuimba Zaburi na yupo wakati waamini wanapokusanyika kwa ajili yake! Liturujia ya Neno la Mungu katika Ibada ya Misa Takatifu ni mahojiano kati ya Mwenyezi Mungu na waja wake wanaokusanyika kama Kanisa. Neno la Mungu ni hai linapotangazwa na kusikilizwa kwa imani. Roho Mtakatifu aliyezungumza kwa njia ya Manabii ndiye aliyewawezesha waandishi wa Neno la Mungu kuandika kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu, ili kwamba, Neno la Mungu linapotangazwa liweze kusikika katika nyoyo na masikio ya waamini, ili hatimaye, waweze kumwilisha kile walichosikia katika uhalisia wa maisha yao.
Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kuwa watulivu, wanyenyekevu na wasikivu hodari wa Neno la Mungu wakati Neno la Mungu linapotangazwa, daima wakiwa tayari kufungua akili na nyoyo zao, ili kumsikiliza Mwenyezi Mungu anayezungumza nao, ili hatimaye, Neno la Mungu liwe ni dira na mwongozo wa maisha yao. Baba Mtakatifu anawahimiza waamini pamoja na vyama vya Kitume, kujenga utamaduni wa kusikiliza, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Wajibidiieshe kujielimisha kuhusu usikivu wa Neno la Mungu. Amewapongeza washiriki wa shindano la ujuzi wa Maandiko Matakatifu ambalo hufanyika kila mwaka mjini Nazareti. Mtakatifu Jerome alisema kwamba yeyote anayepuuza Maandiko Matakatifu humpuuza Kristo. Na kinyume chake, ni Kristo Yesu ambaye anafungua akili za waamini wake, ili kuyaelewa Maandiko Matakatifu. Rej. Lk 24:45. Vijana wajitahidi katika kipindi cha likizo ya kiangazi, kujenga uhusiano mwema na mafungamano kati yao na Mwenyezi Mungu kwa: Sala, Neno, Sakramenti na huduma kwa jirani wanaokutana nao katika hija ya maisha yao ya kila siku.