Ujumbe wa Mshikamano wa Upendo na Amani Sudan Kongwe
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan ya Kusini katika ujumbe wa mshikamano na mwaliko wa amani linasema: “Lakini ninyi, ndugu, msikate tamaa katika kutenda mema.” 2The 3:13. Mgogoro kati ya Jeshi la Sudan Kongwe (SAF) linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, Mkuu wa Baraza la Mpito la Utawala wa Sudan Kongwe na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vikiongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo na hivyo kupelekea zaidi ya watu mia mbili tisini na tisa kupoteza maisha yao katika siku za hizi karibuni. Taarifa zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya 300, 000 wamejeruhiwa kadiri ya tarehe 19 Aprili 2023 na kwamba, hofu imetanda nchini Sudan Kongwe. Ni katika muktadha wa mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu nchini Sudan Kongwe, Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan ya Kusini, limeandika ujumbe mshikamano na wito kwa watu wa Mungu kujikita katika mchakato wa kutafuta na kudumisha amani. Vita inaendelea kufanya wananchi kupoteza maisha yao pamoja na kuendelea kutumbukia kwenye dimbwi la umaskini na magonjwa. Kuna watu wamelazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha yao. Kimsingi, watu wengi wanateseka nchini Sudan Kongwe na wanalilia amani, umoja wa Kitaifa na majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote wa Mungu nchini Sudan Kongwe. Baraza la Maaskofu Katoliki Sudan ya Kusini, linawaalika watu wa Mungu Sudan ya Kusini kusali na kufunga kama kielelezo cha mshikamano na mafungamano yao na watu wa Mungu nchini Sudan Kongwe. Maaskofu wanatambua kwamba, katika mapigano kuna hatari kubwa kwa wananchi wengi kukosa mahitaji yao msingi. Ndiyo maana wanasema kuna umuhimu wa kusali na kuwakumbuka raia wote walioko kwenye uwanja wa mapambano. Maaskofu wa Sudan ya Kusini wanahitimisha ujumbe wa mshikamano na mwaliko wa amani kwa kuwaasa wakisema “Lakini ninyi, ndugu, msikate tamaa katika kutenda mema.” 2The 3:13.
Ufufuko wa Kristo Yesu ni kilele cha ukweli wa imani ya Kikristo, ambayo jamii ya kwanza ya wakristo iliusadiki na kuuishi kama kiini cha ukweli; waliiendeleza kama msingi kwa njia ya Mapokeo; waliithibitisha kwa njia ya Maandiko ya Agano Jipya; na wakaihubiri kama sehemu muhimu sana ya Fumbo la Pasaka yaani: mateso na kifo cha Kristo Msalabani. Kristo amefufuka kwa wafu, kwa kifo chake alishinda dhambi na mauti na amewakirimia wafu uzima wa milele. Huu ndio ujumbe wa Pasaka unaotangazwa na kushuhudiwa na Mama Kanisa katika kipindi hiki cha Pasaka ya Bwana. Lakini kwa bahati mbaya, ujumbe huu wa Pasaka unakumbana na upinzani mkubwa kutokana na vita kuendelea kufumuka sehemu mbalimbali za dunia, kiasi cha kupandikiza hofu na utamaduni wa kifo. Haya ni matukio ya kutisha sana, kumbe, huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Mwenyezi Mungu ili aingilie kati na hivyo kusitisha vitendo hivi vya kikatili vinavyotekelezwa kwa mikono ya binadamu, ili watu waone tena maana ya maisha yanayopyaishwa kwa neema ya Mwenyezi Mungu. Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Huruma ya Mungu sanjari na Pasaka ya Bwana kwa waamini wa Makanisa ya Mashariki, hapo tarehe 16 Aprili 2023 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu, kwa masikitiko makubwa anaendelea kufuatilia kwa karibu zaidi machafuko ya kisiasa nchini Sudan Kongwe ambayo yamepelekea watu kadhaa kupoteza maisha yao. Hii ni nchi ambayo kwa miaka kadhaa inaishi katika hali tete ya kisiasa na mafungamano ya kijamii. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumwomba Mwenyezi Mungu ili wahusika waweke silaha zao chini na kuanza kujizatiti katika mchakato wa haki, amani na maridhiano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Sudan Kongwe.
Wakati huo huo, Baraza la Makanisa Ulimwenguni (WCC) limesikitishwa sana na ongezeko la ghafla la mgogoro kati ya Jeshi la Sudan Kongwe (SAF) linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, mkuu wa Baraza la Mpito la Utawala wa Sudan Kongwe na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vikiongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo na hivyo kupelekea zaidi ya watu mia moja kupoteza maisha yao katika siku za hizi karibuni. Tangu tarehe 15 Aprili 2023 kumekuwepo na machafuko ya kisiasa, mapigano ya silaha na ukosefu wa haki, amani na utulivu; mambo ambayo yamepelekea hata Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP., kusitisha shughuli zake nchini Sudan Kongwe. Shule, vituo vya afya, masoko na huduma msingi zimefungwa au kuathirika vibaya sana. Baraza la Makanisa Ulimwenguni lina wasiwasi mkubwa kuhusu athari kubwa zaidi kwa watu wa Mungu nchini Sudan Kongwe, ambao tayari walikuwa wakipitia mahitaji makubwa ya kibinadamu, changamoto za kisiasa na kiuchumi, kiwango cha juu cha mfumuko wa bei, umaskini ulioenea, na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi. Baraza la Makanisa Ulimwenguni linatoa wito kwa wahusika wakuu kusitisha mapigano, ili amani iweze kurejea na demokrasia kushika mkondo wake. Baraza la Makanisa linatoa wito kwa viongozi wa Serikali kukumbuka wajibu na dhamana yao kwa watu wa Mungu nchini Sudan Kongwe, na kufanya kazi ili kukabiliana na changamoto za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kimazingira zinazoiathiri nchi hiyo. Baraza la Makanisa Ulimwenguni linapenda kuwafariji wale wote waliowapoteza wapendwa wao katika mapigano hayo; wanawaombea majeruhi waweze kupona haraka na hivyo kurejea tena katika shughuli zao za kila siku. Baraza la Makanisa Nchini Sudan Kongwe, litaendelea kutekeleza wajibu wake wa kunogesha mshikamano wa kiekumene kimataifa; kwa kujizatiti zaidi katika mchakato wa haki, amani; utu, heshima na haki msingi za binadamu katika kipindi hiki kigumu cha historia na maisha ya watu wa Mungu nchini Sudan ya Kongwe. Baraza la Makanisa Ulimwenguni linaiombea Sudan Kongwe iweze kurejea katika hali ya amani na utulivu, chachu muhimu sana katika kukuza mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.