Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Yesu na Kanisa lake kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili na matakatifu Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Yesu na Kanisa lake kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili na matakatifu 

Waamini Jitahidini Kuwa ni Vyombo na Mashuhuda wa Kristo Mfufufuka Kwa Maisha Yenu!

Damu ya wafiadini na waungama imani iwe ni mbegu ya haki, amani na upatanisho kati ya watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kukoleza upendo wao kwa Kristo Yesu kwa njia ya: Sala, Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma, kielelezo makini cha imani tendaji na ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Kipindi cha Pasaka iwe ni fursa ya kuimarisha imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na huduma makini kwa jirani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, njia za utakatifu ni pamoja na ushuhuda wa kifodini “Martyrium” ambacho kwa njia yake mwanafunzi anafananishwa na mwalimu wake aliyekubali kwa hiari kufa kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu, na kulinganishwa naye katika kuimwaga damu, kinathaminiwa na Kanisa kuwa karama bora na uhakikisho mkuu wa upendo. Ushuhuda na kifodini ndiyo kauli mbiu iliyoongoza Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko Jumatano tarehe 19 Aprili 2023. Katika salam na matashi mema kwa waamini, mahujaji na wageni, Baba Mtakatifu amewatakia kheri na baraka katika maadhimisho ya Kipindi cha Pasaka ya Bwana, kiwe ni fursa ya kuimarisha: Imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani  Waamini wajitahidi kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huduma ya upendo, kwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, chemchemi ya furaha ya kweli katika ulimwengu huu ambao umegeuka kuwa kama “tambara bovu.”

Kipindi cha Pasaka kiimarishe imani, matumaini na mapendo
Kipindi cha Pasaka kiimarishe imani, matumaini na mapendo

Daima waamini wajitahidi kuongozwa na upendo wenye huruma inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu kama ulivyotangazwa na kushuhudiwa na Kristo Yesu, Ufunuo wa huruma, msamaha na upendo wa Mungu. Ushuhuda kwa Kristo Yesu na Kanisa lake na unapaswa kuwa angavu na endelevu, hata wakati wa shida, karaha na madhulumu ya aina mbalimbali. Damu ya wafiadini na waungama imani iwe ni mbegu ya haki, amani na upatanisho kati ya watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kukoleza upendo wao kwa Kristo Yesu kwa njia ya: Sala, Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma, kielelezo makini cha imani tendaji na ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Yesu na Kanisa lake, kwa njia ya imani tendaji iliyopyaishwa, ili kusaidia kunogesha mng’ao wa Kristo Yesu mfufuka ulimwenguni kote.

Papa Imani Tendaji
19 April 2023, 14:30