Tafuta

Wawakilishi wa Kongamano la Kimataifa la Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika kuanzia tarehe 7 hadi 10 Desemba 2023 wanakutana mjini Abijan, Pwani ya Pembe. Wawakilishi wa Kongamano la Kimataifa la Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika kuanzia tarehe 7 hadi 10 Desemba 2023 wanakutana mjini Abijan, Pwani ya Pembe. 

Askofu Kassala: Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika! Binadamu!

Papa anakazia: Umuhimu wa kuendeleza mfumo mpya wa elimu Afrika mintarafu amana, utajiri na rasilimali zilizoko Barani Afrika. Elimu imguse mtu mzima: kiroho na kimwili. Kumbe, Elimu Katoliki ikitajirishwa na Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika itasaidia kupyaisha malezi na makuzi ya vijana wa kizazi kipya katika ukweli na uwazi; kwa kuweka uwiano mzuri kati nadharia na vitendo, bila kutumbukia katika kishawishi cha Bara la Afrika kujitafuta lenyewe,

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ubora wa elimu unapimwa kwa kuangalia thamani yake katika maisha na uwezo wa kuanzisha utamaduni mpya unaowashirikisha watu wengi zaidi. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutoa wito kwa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia, kutoka katika sekta ya utamaduni, sayansi, sanaa na michezo na wafanyakazi katika sekta ya mawasiliano ya jamii kushiriki katika Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” kwa njia ya ushuhuda na kazi zao. Wasaidie kuhamasisha tunu msingi za utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, haki na amani; uzuri, wema, ukarimu na udugu wa kibinadamu. Kila mtu ajitahidi kuwajibika, ili kuendeleza mchakato wa mageuzi; ili kuganga na kuponya ulimwengu huu ambao umejeruhiwa vibaya; kila mmoja, akijitahidi kuwa ni Msamaria mwema, anayeguswa na mahangaiko ya wengine, badala ya kuchochea chuki na uhasama kati ya jamii ya binadamu. Huu ni mfumo wa elimu wenye mwono mpana na wenye uwezo wa kuwashirikisha wote ili kutoa majibu yatakayosaidia kujenga mahusiano na mafungamano ya kijamii kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ulimwengu mamboleo unawahitaji watu watakaojenga na kudumisha amani na utulivu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kila mtu binafsi, anawajibika kutoa kipaumbele cha kwanza katika mchakato wa mfumo mpya wa elimu: utu na heshima ya binadamu, ili hatimaye, kila mtu aweze kuonesha: uzuri na upekee wake; uwezo wa kuhusiana na kufungamana na wengine katika hali na mazingira yanayowazunguka, ili kuondokana na utamaduni wa chuki na uhasama ambao kimsingi umepitwa na wakati. Huu ni muda wa kusikiliza na kujibu kilio cha watoto na vijana wanaorithishwa tunu msingi, uelewa na ufahamu, ili kwa pamoja waweze kujenga leo na kesho inayosimikwa katika haki, amani na maisha bora zaidi.

Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika unakazia mambo makuu saba.
Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika unakazia mambo makuu saba.

Huu ni mwaliko wa kuhakikisha kwamba, watoto na vijana wengi zaidi wanashiriki katika mchakato wa elimu bora. Katika hali na mazingira kama haya, familia zinapaswa kuwa ni sehemu ya wadau wakuu katika sekta ya elimu. Watu wajifunze na kuwafunza wengine: moyo wa ukarimu, kwa kutoa msaada zaidi kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wawakilishi wa Kongamano la Kimataifa la Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika “Africa Compact on Education” kuanzia tarehe 7 hadi 10 Desemba 2023 wanakutana mjini Abijan, Pwani ya Pembe, ili kujadili Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika “Africa Compact on Education.” Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anakazia umuhimu wa kuendeleza mfumo mpya wa elimu Barani Afrika mintarafu amana, utajiri na rasilimali zilizoko Barani Afrika. Elimu imguse mtu mzima: kiroho na kimwili. Kumbe, Elimu Katoliki ikitajirishwa na Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika itasaidia kupyaisha malezi na makuzi ya vijana wa kizazi kipya katika ukweli na uwazi; kwa kuweka uwiano mzuri kati nadharia na vitendo, bila kutumbukia katika kishawishi cha Bara la Afrika kujitafuta lenyewe, bali kujenga uwezo wa kujikita katika majadiliano na dini pamoja na tamaduni mbalimbali; kwa kuwasaidia vijana kutambua utambulisho wao wa Kiafrika na hatimaye kuwasaidia kumtambua Kristo Yesu anayetoa maana halisi ya maisha katika historia na ulimwengu katika ujumla wake; tayari kuleta shauku ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Hii ni elimu inayopania kukuza utu na maisha ya kiroho ya wanafunzi. Baba Mtakatifu anakaza kusema, elimu iwasaidie vijana wa kizazi kipya kupambana na tabia ya uchoyo na ubinafsi, ili kujenga ari na moyo wa jumuiya, mahusiano, mafungamano na mshikamano, ili wawe wajenzi wa jamii inayosimikwa katika udugu wa kibinadamu, huduma kwa wote pamoja na kujali ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Elimu bora Barani Afrika ni msingi wa haki, amani na utulivu.

Wajumbe wa Mkataba wa Mfumo wa Elimu Afrika, Abijan, Desemba
Wajumbe wa Mkataba wa Mfumo wa Elimu Afrika, Abijan, Desemba

Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki la Geita ambaye pia ni Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC,  Mwenyekiti wa Idara ya Elimu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ambaye ni mjumbe wa Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika katika mahojiano maalum na Radio Vatican, amekazia mambo makuu saba yanayopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika mfumo mpya wa elimu: Binadamu anapaswa kuwa ni kitovu cha elimu; Watoto wasikilizwe; Masuala ya jinsia, wanawake na wasichana wapewe upendeleo wa pekee; familia inapaswa kuwa ni mwezeshaji wa kwanza katika masuala ya elimu; umuhimu wa watu kujielimisha wenyewe; elimu na maendeleo endelevu ya binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na kwamba, binadamu anahusika na utunzaji bora wa mazingira, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Ushiriki wa jamii nzima katika maboresho ya elimu Barani Afrika ni muhimu
Ushiriki wa jamii nzima katika maboresho ya elimu Barani Afrika ni muhimu

Itakumbukwa kwamba, wajumbe kuhusu Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika tarehe 1 Juni 2023 walikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko ambaye alikazia kuhusu: Ujenzi wa mtandao wa mfumo wa elimu Barani Afrika; Umuhimu wa elimu bora kwa vijana wa kizazi kipya Barani Afrika na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa ina matumaini makubwa na Bara la Afrika. Mkutano huu ni mwendelezo wa Kongamano la Kimataifa la Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika “Africa Compact on Education” lililofanyika huko Kinshasa, kwa udhamini wa Baraza la Maaskofu Katoliki DRC na kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Kinshasa. Baba Mtakatifu anasema, Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika unapaswa kumwilishwa katika matendo, kwa ushiriki wa watu wengi katika jamii, kwa kujenga mtandao wa mfumo wa elimu Barani Afrika unaojikita katika ushiriki wa jamii nzima. Mchakato huu unakwenda sanjari na ujenzi wa mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu na hapa huu ni msingi wa imani. Baba Mtakatifu amewakumbusha wajumbe wa Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika kwamba, Bara la Afrika bado ni kijana sana na vijana wengi Barani Afrika wana akili sana, kumbe, huu ni mwaliko wa kuwasikiliza vijana wa kizazi kipya kutoka Barani Afrika. Huu ni muda muafaka wa kushirikiana kwa karibu zaidi na serikali mbalimbali kwa ajili ya kuwaandaa waalimu wenye ujuzi na maarifa na pamoja na kuwaundia mazingira bora ya kufundishia, ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao wa kitaaluma vyema zaidi.

Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa
Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa

 

Jumuiya ya Kimataifa inaliangalia Bara la Afrika kwa imani na matumaini makubwa, kutokana na rasilimali, amana na utajiri ulioko Barani Afrika; maendeleo makubwa ya kiuchumi bila kusahau mapokeo ya elimu asilia kutoka Barani Afrika inayojikita katika ukarimu na mshikamano mambo yanayoingia vyema katika Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika na kuboreshwa zaidi na tunu msingi za Kiinjili. Mfumo huu unaweza kuchota amana na utajiri mkubwa kutoka kwa wanafalsafa wa Kiafrika na waalimu na wanasiasa kama Mzee Nelson Mandela katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi, kwa kujikita katika mchakato wa upatanisho na kwamba, elimu ni chombo madhubuti kabisa cha kuleta mabadiliko duniani. Baba Mtakatifu amemtaja Mtumishi wa Mungu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Muasisi wa Taifa la Tanzania aliyetoa kipaumbele cha kwanza katika mapambano dhidi ya adui ujinga kwa kukazia elimu kwa wote. Mtumishi wa Mungu Mwalimu Nyerere aliyarutubisha maisha yake kwa kushiriki kikamilifu katika Ibada ya Misa Takatifu, na kwake Ekaristi Takatifu, kilikuwa ni chakula safi cha maisha ya kiroho, kilichomwezesha kutekeleza vyema dhamana na majukumu yake kwa watu wa Mungu nchini Tanzania. Kwa hakika, Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika ni jambo jipya Barani Afrika linalosimikwa katika mapokeo ya utamaduni wa Kiafrika na Imani ya Kikristo, kumbe, hakuna sababu ya kuogopa. Bikira Maria, Mama wa Afrika awasindikize katika utekelezaji wa Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika.

Papa Francisko: Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa
Papa Francisko: Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa

Wakati huo huo, Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki la Geita ambaye pia ni Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, ambaye ni mjumbe wa Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Barani Afrika katika mahojiano maalum na Radio Vatican amefafanua umuhimu wa elimu kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, wazo kuu linalopewa kipaumbele na Baba Mtakatifu Francisko. Elimu ielekezwe kwa mwanadamu ili iweze kujibu masuala na matamanio yake halali, imwandae mwanadamu kwa ajili ya kutengeneza na kuboresha maisha yake, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Baba Mtakatifu anakaza kusema, elimu itoe kipaumbele cha kwanza kwa binadamu, itoe fursa na mwelekeo mpana zaidi, ili fursa hizi ziweze kufanyiwa kazi; kwa kukazia: usawa na kwamba, watu wote wanapaswa kufaidika na mfumo mpya wa elimu; watu wajisadake kuiendeleza duniani, kuilinda na kuipendezesha na elimu kiwe ni chombo kitakacho tekeleza majukumu yote haya.

Elimu Barani Afrika
09 December 2023, 14:19