Jubilei ya Miaka 1050 na Miaka 1,100 ya Mt. Udalricus, Jimbo Katoliki la Ausgburg, Ujerumani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amemteuwa Kardinali Christopher schönborn, O.P., Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Vienna, nchini Austria kuwa ni mwakilishi wake maalum katika Maadhimisho ya Jubilei ya Jimbo Katoliki la Augsburg, linaloadhimisha Jubilei ya Miaka 1050 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Udalricus, Mlinzi na Mwombezi wa Jimbo Katoliki la Augsburg sanjari na Jubilei ya Miaka 1100 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu. Miaka imeyoyoma, lakini bado anaendelea kung’ara kama taa iliyowekwa juu ya kinara. Rej. Mt 5:15-16 na kilele chake ni tarehe 28 Desemba 2023 kwenye Kanisa kuu la Ausburg, nchini Ujerumani. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa kuzingatia uzito na umuhimu wa maadhimisho ya Jubilei hizi mbili, kwa heshima ya Mtakatifu Udalricus, shujaa na mchungaji aliyejipambanua kwa imani ya Kikatoliki, akaonesha upendo mkubwa kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu aliye mwabudu katika Sala, akamwadhimisha katika upyaisho na upatanisho; haki na amani; akamsikiliza kwa sikio la moyo wake mahitaji msingi ya watu aliokuwa amekabidhiwa kwake. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hiki ni kipindi cha furaha kuadhimisha Jubilei kwa heshima ya Mtakatifu Udalricus.
Baba Mtakatifu anasema, kwa kusikiliza ombi lililowasilishwa kwake na Askofu Bertram Johannes Meier wa Jimbo Katoliki Augsburg, aliyependa maadhimisho haya kupewa uzito unaostahili, ndiyo maana amemteua Kardinali Christopher schönborn, O.P. kumwakilisha kwa sababu ni kiongozi anayestahili na kwamba, Jimbo kuu la Siena lina Ibada pia kwa Mtakatifu huyu, kumbe, ataongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, kama kielelezo cha ushuhuda na ukarimu wake kwa Jimbo la Augusburg pamoja na viunga vyake. Baba Mtakatifu anamwomba Kardinali Christopher schönborn, O.P., Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Vienna, kumfikishia salam na matashi mema kwa watu wa Mungu Jimbo Katoliki Augsburg na maeneo yote ambamo Mtakatifu Udalricus, anaheshimiwa kutokana na utakatifu wake. Anamwombea ili aweze kutimiza dhamana na wajibu huu kwa bidii, ili wachungaji na waamini waweze kutajirishwa kwa neema nyingi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Anamtaka awe ni mpatanishi wa ukweli wa mbinguni wa zawadi na uwezo, tayari kuwapatia watu wa Mungu baraka na neema katika maadhimisho ya Jubilei hii. Kardinali Christopher schönborn, O.P., Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Vienna katika Maadhimisho haya anaambatana na Mheshimiwa Padre Armin Zürn, Paroko wa Kanisa kuu la Ausburg pamoja na Padre Christoph Hänsler, Paroko wa Kanisa kuu la Mtakatifu Udalricus na Afra, Jimboni Ausburg.