Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe: Ibada
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Tume ya Kipapa kwa Amerika ya Kusini inakumbusha kwamba, kwa mara ya kwanza kumbukumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe, Mlinzi na Mwombezi wa Amerika ya Kusini pamoja na Ufilippin, iliadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican tarehe 12 Desemba 2011 na Baba Mtakatifu Benedikto XVI kama kumbukizi endelevu ya Jubilei ya uhuru kwa nchi nyingi za Amerika ya Kusini. Kunako mwaka 2014, Baba Mtakatifu Francisko akaonesha nia njema ya kutaka kuendeleza mapokeo ya Maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kumbukumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe, kama kumbukumbu ya tukio hili miaka zaidi ya 50 iliyopita, wakati Mtakatifu Paulo VI alipoadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ibada hii ilipambwa na kuchukua mwelekeo wa utamadunisho kwa kuongozwa na vionjo vya watu wa Mungu kutoka Amerika ya Kusini, sehemu ya mchakato wa uinjilishaji unaopania kuleta upyaisho katika maisha ya watu na kama njia ya kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili. Baba Mtakatifu Francisko akabahatika kutembelea Mexico kuanzia tarehe 12- 18 Februari 2016 pamoja na kutoa heshima zake kwa Bikira Maria, Mama Yetu wa Guadalupe. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe, Jumanne, tarehe 12 Desemba 2023, Baba Mtakatifu ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro Mjini Vatican. Katika mahubiri yake, amegusia kuhusu: Ibada ya Bikira Maria wa Guadalupe aliyokabidhiwa Mtakatifu Juan Diego Cuauhtlatoatzin, Fadhila zinazoujaza umaskini wa waamini; Utii na Madhabahu ya Bikira Maria wa Gudalupe. Baba Mtakatifu anasema, Mtakatifu Juan Diego Cuauhtlatoatzin alikabidhiwa kazi ya kutangaza na kueneza Ibada ya Bikira Maria wa Guadalupe kama sehemu ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaopaswa kuzaa matunda, kwa kutia manukato katika maisha dhaifu ya binadamu, ili hatimaye, aweze kuzaa matendo mema, kukua katika wema na hivyo kuondokana na chuki pamoja na woga katika maisha.
Bikira Maria akaweka picha yake kwenye kitambaa, matokeo na ishara iliyozaliwa kutokana na utii pamoja na imani. Mwenyezi Mungu akamkirimia Mtakatifu Juan Diego Cuauhtlatoatzin fadhila zinazoujaza umaskini wa binadamu, kwa njia ya matendo madogo madogo yanayosheheni upendo, kwa sura ya Mama Kanisa anayembeba Kristo Yesu tumboni mwake. Mwenyezi Mungu alimjaribu Mtakatifu Juan Diego Cuauhtlatoatzin kutokana na ugonjwa wa mjomba wake aliyetaabika kumtafutia msaada wa maisha ya kiroho na kimwili; akamweka kati kati ya shida, lakini akayaachaa mambo yote haya mikononi mwa Mwenyezi Mungu na kwa hakika Mtakatifu Juan Diego Cuauhtlatoatzin akaushinda mtihani na Bikira Maria akabahatika kumtembelea mgonjwa wake na kujifunua jina lake na hivyo kumwezesha kuwa ni shuhuda na chombo cha upendo wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa waamini anasema Baba Mtakatifu kutojitafuta sana wenyewe, bali wema na huduma kwa jirani zao, jambo ambalo linampendeza Mwenyezi Mungu. Na kwa njia hii, waamini wanashiriki kikamilifu katika ujenzi wa Madhabahu ambayo Bikira Maria alimwomba Mtakatifu Juan Diego Cuauhtlatoatzin kuyajenga. Kumbe, waamini wanawajibika kujenga Kanisa, kukusanya fadhila mbalimbali zitakazo boresha umaskini wa maisha yao na hivyo kumshuhudia Mwenyezi Mungu ambaye amepiga chapa katika akili na nyoyo zao. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 12 Desemba 2022 aliuongoza umati mkubwa wa watu wa Mungu kutoka Amerika ya Kusini katika Ibada ya Misa Takatifu kwa heshima ya Bikira Maria wa Guadalupe.
Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu Francisko aligusia kuhusu: Mwenyezi Mungu katika utekelezaji wa historia ya ukombozi, Bikira Maria wa Guadalupe, matatizo na changamoto zinazoendelea kumsonga mwanadamu na hatimaye, maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya Miaka 500 ya Bikira Maria wa Guadalupe. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwenyezi Mungu anaendelea kutekeleza historia ya ukombozi wa mwanadamu kwa njia ya huruma na upendo wake wa daima; kwa kuwaangalia kwa namna ya pekee watu maskini na wahitaji zaidi; wanaodhulumiwa na kunyanyaswa, wenye hofu na mashaka kuhusu hatima ya maisha yao. “Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana.” Gal 4:4. Kristo Yesu amekuja kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ni Mungu pamoja na waja wake, rafiki na mwandani wa safari katika mambo yote isipokuwa hakutenda dhambi. Baba Mtakatifu alikazia kwa namna ya pekee umuhimu wa kufanya rejea katika tunu msingi za Kiinjili, ili kukutana tena na tena na Bikira Maria wa Guadalupe, ili aweze kuwafariji, kuwasaidia kupata mahitaji yao msingi; kuwalinda na kuwatunza kwa uwepo, upendo na faraja yake ya daima. Bikira Maria wa Guadalupe ni Mama wa wote pasi na ubaguzi kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Juan Diego Cuauhtlatoatzin. Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Guadalupe kwa Mwaka 2022 yaligubikwa na machungu mazito ya hali ngumu ya maisha kutokana na vita, majanga asilia, ongezeko kubwa la ukosefu wa haki, umaskini, njaa na maradhi. Kumbe, Maadhimisho ya Fumbo la Umwilisho yanogeshe imani, matumaini na mapendo ya watu wa Mungu; kwa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani wanaowazunguka. Ni wakati wa kuondokana na tabia ya uchoyo na ubinafsi pamoja na hali ya kudhaniana vibaya, ili kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii.
Bikira Maria wa Guadalupe anapenda kukutana na watoto wake kama ilivyokuwa kwenye Mlima wa Tepeyac alipomtokea kwa mara ya kwanza Mtakatifu Juan Diego Cuauhtlatoatzin. Huu ni muda wa kumruhusu Kristo Yesu kuja na kufanya makao na kuandamana na waja wake kama mwanadani wa safari, ili kukabiliana kwa pamoja na: umaskini, unyonyaji wa kijamii na kiuchumi; ukoloni wa kiitikadi na kitamaduni. Kristo Yesu anaandamana na wale wote wanaotafuta kwa haki uhuru wao; watu ambao utu, heshima na haki zao msingi zimo hatarini na hata katika haya, bado upendo wa Bikira Maria wa Guadalupe anasema yeye yupo pamoja na kati yao. Baba Mtakatifu Francisko alisema kuanzia tarehe 12 Desemba 2022, Watu wa Mungu Amerika ya Kusini walianza maandalizi kwa ajili ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 tangu Bikira Maria wa Guadalupe “La Virgen Morena” alipomtokea Mtakatifu Juan Diego Cuauhtlatoatzin kunako mwaka 1531 na kilele chake ni mwaka 2031. Sanamu ya Bikira Maria wa Guadalupe ni kielelezo cha mapambano ya matumaini. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Bikira Maria wa Guadalupe atawaongoza katika hija ya maisha, ili hatimaye, waweze kufikia umoja na utimilifu wa maisha, huku maskini wakipewa kipaumbele cha kwanza. Kipindi hiki cha maandalizi ya Jubilei ya Miaka 500 ni wakati wa kufanya hija ya kukutana na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Bikira Maria wa Guadalupe; kwa kuendelea kupyaisha umoja na mafungamano ya kijamii. Bikira Maria wa Guadalupe aendelee kuwalinda, kuwatunza na kuwaombea; kuwafariji na kuwasaidia, kutambua kwa mara nyingine tena tunu msingi za Kiinjili Amerika ya Kusini, tayari kutangaza na kushuhudia: huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka, tayari waamini kujikita katika kutunza, kushirikisha na kuendelea kupyaisha mafungamano haya.