Maadhimisho ya Siku ya 46 ya Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè Barani Ulaya, kuanzia tarehe 28 Desemba 2023 hadi tarehe 1 Januari 2024, huko Ljubljana nchini Slovenia. Maadhimisho ya Siku ya 46 ya Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè Barani Ulaya, kuanzia tarehe 28 Desemba 2023 hadi tarehe 1 Januari 2024, huko Ljubljana nchini Slovenia. 

Maadhimisho ya Siku ya 46 ya Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè 2023-2024

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe kwa washiriki wa maadhimisho ya Siku ya 46 ya Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè Barani Ulaya, anakazia kuhusu: Umuhimu wa vijana katika maisha na utume wa Kanisa, kutembea pamoja kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu, ili kuvuka udhaifu wa vijana, ili kutekeleza ndoto ya upendo, haki, amani na ukweli halisi kutoka katika undani wa kijana mwenyewe. Hii ni hija ya uaminifu duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya 46 ya Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè Barani Ulaya, kuanzia tarehe 28 Desemba 2023 hadi tarehe 1 Januari 2024, huko Ljubljana nchini Slovenia, yananogeshwa na kauli mbiu “Hija ya uaminifu duniani.” Vijana hawa wanaonjeshwa ukarimu na Kanisa mahalia kwa kupewa hifadhi katika familia ziliko kwenye Parokia 50 huko Ljubljana. Huu ni mwaliko wa kufanya hija ya pamoja katika uaminifu duniani. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa washiriki wa maadhimisho ya Siku ya 46 ya Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè Barani Ulaya, anakazia umuhimu wa vijana katika maisha na utume wa Kanisa, kutembea pamoja kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu, ili kuvuka udhaifu wa vijana, ili kutekeleza ndoto ya upendo, haki, amani na ukweli halisi kutoka katika undani wa kijana mwenyewe. Baba Mtakatifu anasema, kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya 46 Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè Barani Ulaya kwa mwaka 2023 inachota utajiri na uzoefu wa Maadhimisho ya Siku ya Thelathini na Saba ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2023 huko Jimbo kuu la Lisbon, Ureno kuanzia tarehe 1- 6 Agosti 2023, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39.

Kauli mbiu: Hija ya uaminifu duniani
Kauli mbiu: Hija ya uaminifu duniani

Hii ilikuwa ni fursa kwa Mama Kanisa kama Jumuiya kuishi uzoefu mzuri wa urafiki na Mungu pamoja jirani, kwa kutambua kwamba, kila kijana ni leo ya Mungu na Kanisa. Kila kijana ni mtu muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa na sehemu muhimu sana ya Fumbo la Pasaka. Leo hii kuna kelele nyingi kiasi kwamba, maadili ya ukimya na kusikilizwa yametoweka, changamoto na mwaliko wa kugundua tena mwelekeo wa utamaduni wa kusikiliza, kwani hili ni tendo la upendo na uaminifu. Kusikiliza ni kutoa nafasi na kutambua uwepo wa mwingine, ili kuondoa hisia kwamba, anayepiga kelele zaidi huyo husikilizwa. Hii ni changamoto kwa vijana kuthubutu kujenga ulimwengu tofauti unaosimikwa katika utamaduni wa kusikilizana katika ukweli na uwazi; kwa kutangaza na kushuhudia uzuri wa ukarimu, huduma, usafi, ujasiri, msamaha, uaminifu kwa wito wao, maisha ya sala, haki, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kujenga upendo na maskini pamoja na kudumisha urafiki wa kijamii. Rej. Christus vivit, 36.

Ndoto ya upendo, haki, amani na ukweli
Ndoto ya upendo, haki, amani na ukweli

Baba Mtakatifu Francisko anasema hija ya uaminifu duniani inapania pamoja na mambo mengine, kuboresha maisha ya kijamii, kwa kuondoa vizuizi ili kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu, tamaduni, dini katika ulimwengu thabiti na wazi. Huu ni mwaliko wa kuachana na tabia ya kuwatenga watu ili kuambata umoja na ushirika unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kristo Yesu hakupenda kuwabagua watu, kwani alitambua uwepo wa sura na mfano wa Mungu kati ya watu wake. Watu wote walipata nafasi katika maisha na utume wa Kristo Yesu. Huu ni mwaliko pia kwa vijana kukabiliana na changamoto pamoja na udhaifu wao, ili kukoleza matukio ya uzuri na ubora zaidi yatakayowasaidia kugundua cheche za kuanza upya kwa ari na uchangamfu mpya. Baba Mtakatifu anawategemea na kuwaamini vijana kama mashuhuda na vyombo vya utekelezaji wa ndoto ya upendo, haki na amani na ukweli halisi kutoka katika undani wa maisha yao kwa kuhakikisha kwamba wanathamini ujana wa maisha yao kuwa ni kito cha thamani. Vijana wasikubali kupokwa matumaini yao na wajanja wachache, bali wajikite katika ujenzi wa jamii inayostahili majina yao.

Jumuiya ya Taize 2023

 

28 December 2023, 15:17