Mwenyeheri Kardinali Eduardo Pironio: Shuhuda wa Matumaini Na Mtetezi wa Wanyonge!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mwenyeheri Kardinali Eduardo Francisco Pironio alikuwa ni mchungaji mnyenyekevu na mwenye bidii sana; shuhuda wa matumaini; mtetezi wa maskini na wanyonge ndani ya jamii. Alishirikiana kwa karibu sana na Mtakatifu Yohane Paulo II katika mchakato wa kuwafunda waamini walei na katika Maadhimisho ya Siku za Vijana Ulimwenguni. Mfano na ushuhuda wa maisha yake, uwasaidie waamini kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni Kanisa linalotoka nje, tayari kusafiri na kuwaendea watu wote na husan kwa watu maskini na dhaifu zaidi ndani ya jamii. Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 17 Desemba 2023 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, baada ya Kardinali Eduardo Pironio kutangazwa kuwa ni Mwenyeheri, Jumamosi tarehe 16 Desemba 2023 kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Lujàn, nchini Argentina Ibada hii imeongozwa na Kardinali Fernando Vérgez Alzaga L.C. Rais wa Tume ya Kipapa ya Jimbo la Vatican na Gavana wa Jimbo la Vatican ambaye aliwahi kuwa Katibu muhtasi wa Mwenyeheri Kardinali Eduardo Francisco Pironio. Katika mahubiri yake amemtaja Mwenyeheri Kardinali Eduardo Francisco Pironio kuwa ni chombo na shuhuda mwaminifu wa tunu msingi za Kiinjili, aliyejitahidi kurutubisha maisha yake kwa maadhimisho ya Ekaristi Takatifu na kwa hakika alikuwa na Ibada maalum ya Kuabudu Ekaristi Takatifu; Ibada kwa Bikira Maria na kiongozi mintarafu matakwa ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.
Ni shuhuda wa matumaini na uvumilivu wa Kiinjili, msimamizi na mtetezi wa wanyonge na maskini. Mwenyeheri Eduardo Francisco Pironio alikuwa na upendo mkamilifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Alijibidiisha katika malezi na makuzi ya waamini walei kwa kukazia: Majiundo, Umoja na Ushiriki wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa. Alikuwa na unyenyekevu wa kitume uliomwezesha kuwahudumia watu wa Mungu kwa ari na moyo mkuu na kwamba, unyenyekevu huu ulikuwa unafumbatwa katika huduma ya upendo. Alifurahia sana wito, maisha na utume wake wa Kipadre. Alikuwa na upendo wa dhati kwa Bikira Maria na kwa Fumbo la Msalaba. Alipenda sana kusali Rozari muhtasari wa historia nzima ya kazi ya ukombozi.
Kwa upande wake Kardinali Kevin Joseph Farrell, KGCHS, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema, Mwenyeheri Kardinali Eduardo Francisco Pironio aliyasimika maisha yake katika Fumbo la Msalaba na Pasaka ya Bwana chemchemi ya maisha mapya na utume kwa Wakristo. Kwa hakika alikuwa ni Kardinali wa vijana wa kizazi kipya, aliyependa kuwashirikisha ule uzuri na furaha ya Injili kama kielelezo cha upendo kwa Mungu. Aliwapenda, kuwaheshimu na kuwathamini vijana. Alijisadaka bila ya kujibakiza katika maandalizi ya Maadhimisho ya Siku za Vijana Ulimwenguni. Alikuwa ni mtu wa imani iliyomwilishwa katika matendo ya huruma kwa Mungu na jirani. Alikita maisha yake katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene.
Itakumbukwa kwamba, Mwenyeheri Kardinali Eduardo Francisco Pironio alizaliwa tarehe 3 Desemba 1920 huko Mercedes-Luján, nchini Argentina. Tarehe 5 Desemba 1943 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 31 Mei 1972 akawekwa wakfu kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo Katoliki la Plata, Argentina. Tarehe 20 Septemba 1975 akateuliwa kuwa ni Askofu mkuu na Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume. Tarehe 24 Mei 1976 akateuliwa kuwa ni Kardinali. Alikuwa ni Padre Muungamishi wa Mtakatifu Paulo VI. Tarehe 8 April 1984 akateuliwa kuwa ni Rais wa Baraza la Kipapa la Walei na akafariki dunia 5 Februari 1988. Kimsingi Mwenyeheri Kardinali Eduardo Francisco Pironio amelitumikia Kanisa kama Padre kwa muda wa miaka 54.1, Kama Askofu miaka 33.6 na kama Kardinali miaka 21.6. Ni kiongozi aliyechangia sana mafanikio ya Mkutano wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caraibi, CELAM uliofanyika mjini Puebla, mwaka 1979 na ukachangia kwa kiasi kikubwa Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican hususan kuhusu uinjilishaji wa awali, “Ad Gentes” pamoja na mchango wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa. Alisimamia maisha na utume wa vyama na mashirika ya Kitume sehemu mbalimbali za dunia, akaratibu maadhimisho ya Siku za Vijana Ulimwenguni.