Papa awaombea wahanga wa shambulizi wakati wa Misa nchini Ufilipino
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko kama kawaida yake, mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana, akiwa katika Nyumba ya Mtakatifu Marta mjini Vatican, Dominika tarehe 3 Desemba 2023 aliwaombea wahanga wa shambulio la bomu kwenye Misa ya Wakatoliki nchini Ufilipino. Inasadikika kuwa Watu wanne walifariki na arobaini na wawili walijeruhiwa katika shambulio kwenye jumba la mazoezi ya michezo katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Mindanao ambapo Misa ilikuwa ikiadhimishwa.
Katika ukaribu huo Papa kwa kusaidiwa kusoma ujumbe wake na Monsinyo Paolo Braida, wa Sekretarieti ya Vatican alisema,"Ningependa kuwahakikishia maombi yangu kwa ajili ya wahanga wa shambulizi nchini Ufilipino asubuhi ya leo,ambapo bomu lililipuka wakati wa Misa. Aliongeza kuwa"Niko karibu na familia na watu wa Mindanao ambao tayari wameteseka sana."Papa Francisko alithibitisha.
Katika telegramu aliyomwandikia Askofu Edwin de la Peña Y Angot, Papa Francisko aliongeza kuwa amehuzunishwa sana kufahamishwa kuhusu majeraha na kupoteza maisha kulikosababishwa na mlipuko huo. Ujumbe huo uliotiwa saini na Katibu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin,unaendelea kubainisha kwamba,“Baba Mtakatifu Francisko anaomba uwasilishe ukaribu wake wa kiroho kwa wote walioguswa na janga hili. Anaungana nanyi katika kuziombea roho za wale waliokufa kwa huruma ya upendo ya Mwenyezi Mungu na anasihi zawadi za Mungu kwa ajili ya uponyaji na faraja kwa waliojeruhiwa na waliofiwa.” Katika telegramu hiyo Papa Francisko alihitimisha ujumbe wake na “maombi kwamba Kristo Mfalme wa Amani awape nguvu zote za kugeuka kutoka katika vurugu na kushinda kila uovu kwa wema na kutoa baraka zake kama dhamana ya nguvu na faraja katika Bwana.”
Kitendo kisicho na maana na cha kuchukiza, Shambulio hilo lilitokea Marawi. Mji mkubwa zaidi wa Kiislamu nchini Ufilipino,ulizingirwa kwa miezi mitano mwaka 2017 na wapiganaji wanaounga mkono Serikali ya Kiisilamu. Kamanda wa polisi katika eneo hilo alisema kuwa shambulio la Dominika linaweza kuwa kisasi kwa operesheni ya hivi majuzi ya serikali ambayo iliua wanachama 11 wa kundi la kigaidi la Kiislamu nchini Ufilipino. Rais wa Ufilipino Bwana Ferdinand Marcos Mdogo alisema kuwa:“Ninashutumu kwa nguvu iwezekanavyo vitendo vya kipumbavu na vya kikatili zaidi vinavyofanywa na magaidi wa kigeni.” Picha zilizotolewa na mashirika ya habari zinaonesha Waislamu wa Ufilipino wakikusanyika kwa ajili ya mshikamano na wahanga wa shambulio hilo, huku wakiwaombea dua na kulaani mlipuko huo katika umati wa watu waliokuwa wakisali.