Papa ameombea wanaoteseka na vita:ni maisha mangapi ya watu yamepotea?
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika Dominika ya Mwisho wa Mwaka tarehe 31 Desemba 2023, ambapo Mama Kanisa alikuwa anadhimisha Siku Kuu ya Familia Takatifu, Baba Mtakatifu mara baada ya Tafakari ya neno la Mungu na sala ya Malaika wa Bwana, akiwageukia waamini na mahujaji waliofika katika uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican alisema “Kwa bahati mbaya, sherehe ya Noeli nchini Nigeria iliadhimishwa na vurugu kubwa katika Jimbo la Plateau, na waathrika wengi. Ninawaombea wao na familia zao. Mungu ainusuru Nigeria na majanga haya! Na pia ninawaombea wale waliopoteza maisha katika mlipuko wa lori la mafuta huko Liberia.”
Ukraine,Sudan,Israel na Warohingya
Baba Mtakatifu Francisko aidha amesema: “Tunaendelea kuwaombea watu wanaoteseka kwa sababu ya vita: watu wa Ukraine wanaoteswa, Wapalestina na Waisrael, watu wa Sudan na wengine wengi. Mwishoni mwa mwaka, tuwe na ujasiri wa kujiuliza: je ni watu wangapi wamepoteza maisha kutokana na migogoro ya silaha? Vifo vingapi? Na uharibifu kiasi gani, mateso kiasi gani, na ni kiasi gani cha umaskini? Yeyote anayependezwa na migogoro hii anapaswa kusikiliza sauti ya dhamiri. Na tusiwasahau Warohingya walioteswa!”
Kumbukumbu ya kifo cha Papa Benedikto XVI
Baba Mtakatifu aidha alisema: “Mwaka mmoja uliopita Papa Benedikto wa kumi na sita alihitimisha safari yake hapa duniani, baada ya kulitumikia Kanisa kwa upendo na hekima. Tunahisi upendo mwingi kwake, shukrani nyingi, na pongezi nyingi. Kutoka Mbinguni utubariki na utusindikize. Na tumpigie makofu mengi BenediktoXVI!”
Salamu kwa mahujaji na familia:tusisahau familia ni kiini cha jamii
Papa amewasalimu Warumi, mahujaji, vikundi vya parokia, vyama na vijana wote. Amependa kutoa salamu maalum kwa familia zilikuwa hapo uwajani na wale waliounganishwa kupitia televisheni na njia nyinginezo za mawasiliano. Papa ameongeza kusema kuwa: “Tusisahau kwamba familia ndio kiini msingi cha jamii: lazima tuilinde na kuiunga mkono kila wakati!”
Timu ya Mpira wa wavu Italia
Baba Mtakatifu amewasalimia timu ya taifa ya Italia ya mpira wa wavu ya wanaume chini ya miaka 18; na washiriki wa tukio hai la kuzaliwa kwa Bwana la huko Marcellano, mkoa wa Umbria. Amewatakia wote Dominika njema: baraka kwa familia zao, na pia kuwatakia mwisho wa mwaka wa amani. Tafadhali wasisahau kumuombea. Mlo mwema wa mchana na kwaheri ya kuonana!