Rais Volodymyr Zelenskyy Amshukuru Papa Francisko Kwa Kuunga Mkono Juhudi za Amani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine, tarehe 28 Desemba 2023 amezungumza na Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya simu. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kumtakia Rais Volodymyr Zelenskyy pamoja wananchi wote wa Ukraine heri na baraka katika maadhimisho ya Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2023. Amewatakia amani ya kweli watu wote wa Mungu nchini Ukraine. Baba Mtakatifu pamoja na Rais Volodymyr Zelenskyy wamejadiliana kuhusu “Forumla ya Amani Inayopaswa kutekelezwa kwa vitendo.” Huu ni mchakato wa amani unaozihusisha zaidi ya nchi 80 katika ngazi ya uwakilishi na kwamba, mambo mengi zaidi yatajitokeza.
Itakumbukwa kwamba, tarehe 13 Mei 2023 Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine alimtembelea Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican, ikiwa ni mara ya pili kwa viongozi hawa kukutana ana kwa ana, kwani kwa mara ya kwanza walikutana kunako mwaka 2020 kabla Urusi haijaivamia Ukraine. Mara kadhaa, Baba Mtakatifu Francisko amekuwa na mazungumzo kwa njia ya simu na Rais wa Ukraine na daima Baba Mtakatifu ameonesha masikitiko yake kutokana na madhara makubwa ya vita kwa watu wa Mungu nchini Ukraine. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia watu wa Mungu nchini Ukraine uwepo wake wa dhati kwa njia ya sadaka na maisha yake ya kiroho.