Tafuta

Hotuba ya Baba Mtakatifu kwa wajumbe wa Tume ya Taalimungu Kimataifa amekazia umuhimu wa wongofu wa kimisionari tayari kujikita katika mchakato wa uinjilishaji mintarafu Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Hotuba ya Baba Mtakatifu kwa wajumbe wa Tume ya Taalimungu Kimataifa amekazia umuhimu wa wongofu wa kimisionari tayari kujikita katika mchakato wa uinjilishaji mintarafu Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.  (Vatican Media)

Tume ya Taalimungu Kimataifa: Tasaufi, Sinodi na Uekumene

Hotuba ya Baba Mtakatifu kwa wajumbe wa Tume ya Taalimungu Kimataifa amekazia umuhimu wa wongofu wa kimisionari tayari kujikita katika mchakato wa uinjilishaji mintarafu Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Mtaguso wa Nicea wa Mwaka 325 kwa kujielekeza zaidi katika: Tasaufi, Sinodi na Uekumene. Papa amewaomba wajumbe wa Tume ya Taalimungu Kimataifa kulisaidia Kanisa kuondokana na mfumo dume, dhambi ambayo imetawala maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tume ya Taalimungu Kimataifa iliyoanzishwa na Mtakatifu Paulo VI ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican sanjari na Sinodi za Maaskofu. Tume hii kunako mwaka 2019 imeadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake na imechangia sana kuhusu: Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa; Sakramenti za Kanisa, Haki Msingi za Binadamu, Uhuru wa Kuabudu sanjari na Umoja wa Kanisa. Wajumbe wa Tume ya Taalimungu Kimataifa, Alhamisi tarehe 30 Novemba 2023 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko ambaye amewashukuru kwa kazi kubwa ya Kitaalimungu na kuwataka kulisaidia Kanisa kuondokana na mfumo dume. Mkutano ujao wa Makardinali Washauri utajikita zaidi kuhusu “Mwelekeo wa Kike wa Kanisa.” Ikumbukwe kwamba, Kanisa ni Mama na Mwalimu na kwamba, dhambi kubwa ambayo Kanisa limetenda katika maisha na utume wake ni kuendekeza mfumo dume, lakini Kanisa ni Mama na Mchumba wa Yesu. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo na wanawake wengi zaidi katika Tume ya Taalimungu Kimataifa. Katika hotuba aliyoandaa Baba Mtakatifu kwa wajumbe wa Tume ya Taalimungu Kimataifa amekazia umuhimu wa wongofu wa kimisionari tayari kujikita katika mchakato wa uinjilishaji mintarafu Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Mtaguso wa Nicea wa Mwaka 325 kwa kujielekeza zaidi katika: Tasaufi, Sinodi na Uekumene.

Tume ya Kitaalimungu Kimataifa: Tasaufi, Sinodi na Uekumene
Tume ya Kitaalimungu Kimataifa: Tasaufi, Sinodi na Uekumene

Baba Mtakatifu anasema, kuna haja kwa Makanisa mahalia kujitosa bila ya kujibakiza katika wongofu wa kimisionari, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kristo Yesu ndiye mwanga wa Mataifa anayepaswa kuwaangaza watu wote kwa mng’ao wake ung’aao juu ya uso wa Kanisa, kwa njia ya kuitangaza Injili kwa kila kiumbe, dhamana na utume unaowawajibisha watu wote wa Mungu. Hii ni changamoto ya wongofu wa kimisionari unaofahamu jinsi ya kutangaza na kushuhudia uzuri wa imani. Ni dhamana ya kumtangaza Mwenyezi Mungu anayependa na kusamehe; Mungu anayeokoa na kumhimiza mja wake kujisadaka kwa ajili ya huduma ya udugu wa kibinadamu; kumbe, wajumbe wa Tume ya Taalimungu Kimataifa wanapaswa kutoa ushauri kuhusu taalimungu ya uinjilishaji inayofumbatwa katika majadiliano ya kitamaduni na kwamba, taalimungu hii inapaswa kupata chimbuko lake kwa watoto wa Mungu kwa sababu taalimungu inapata chimbuko lake kwa “kupiga magoti” na kumwabudu Mwenyezi Mungu. Tema nyingine zinazopaswa kushughulikiwa ni mwelekeo wa binadamu na ikolojia na imani katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Jubilei ya Miaka 1,700 ya Mtaguso wa NICEA, 2025
Jubilei ya Miaka 1,700 ya Mtaguso wa NICEA, 2025

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo yanajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Nicea ulipoadhimishwa kunako mwaka 325 na kilele cha maadhimisho haya ni mwaka 2025, tukio la pekee na muhimu sana. Mwaka huo Wakristo wote wataadhimisha Pasaka ya Bwana siku moja, matendo makuu ya Mungu kwa waja wake sanjari na maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo. Kanuni ya Imani iliyoandikwa na Mtaguso wa NICEA: “Nasadiki kwa Mungu Baba Mwenyezi Mwumba mbingu na nchi na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Nasadiki kwa Bwana mmoja Yesu Kristo, mwana wa pekee wa Mungu. Aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote. Mungu aliyetoka kwa Mungu, mwanga kwa mwanga, Mungu kweli kwa Mungu kweli. Aliyezaliwa bila kuumbwa, mwenye umungu mmoja na Baba, ambaye vitu vyote vimeumbwa naye. Ameshuka toka mbinguni kwa ajili yetu sisi wanadamu na kwa ajili ya wokovu wetu. Akapata mwili kwa uwezo wa roho mtakatifu kwake yeye Bikira Maria akawa mwanadamu. Akasulibiwa pia kwa ajili yetu sisi. Akateswa kwa mamlaka ya Ponsyo Pilato, akafa akazikwa. Akafufuka siku ya tatu ilivyoandikwa. Akapaa mbiguni, amekaa kuume kwa baba. Atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu wazima na wafu nao ufalme wake hautakuwa na mwisho. Nasadiki kwa Roho Mtakatifu Bwana mleta uzima atokaye kwa Baba na Mwana anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana aliyenena kwa vinywa vya manabii. Nasadiki kwa Kanisa moja, Takatifu Katoliki la mitume. Naungama ubatizo mmoja kwa maondoleo ya dhambi. Nangojea na ufufuko wa wafu. Na uzima wa milele ijayo. Amina.”

Mwaka 2025 Wakristo wote wanaadhimisha Pasaka Siku Moja.
Mwaka 2025 Wakristo wote wanaadhimisha Pasaka Siku Moja.

Huu ni mwanga unaoangaza kwa upendo wa kibaba, mwaliko kwa waamini kuutolea ushuhuda wa furaha ya Injili. Ni dhamana na wajibu wa wanataalimungu kutangaza na kushuhudia mwanga huu ndani ya Kanisa katika giza za ulimwengu. Katika maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa NICEA, Kanisa lilipata nafasi ya kuonesha asili yake, imani na utume na kwamba, Kanisa katika Kristo Yesu ni kama Sakramenti au ishara na chombo cha kuwaunganisha watu kiundani na Mwenyezi Mungu na kuleta umoja kati ya wanadamu wote. Rej. Lumen gentium, 1. Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa ni njia inayotoa fasiri ya ushirika, mchakato wa ushiriki katika Fumbo la Utatu Mtakatifu linalokuja kukutana na watu. Wanataalimungu wamekirimiwa uwezo huu wa kumwilisha dhana hii, kwa kushirikisha amana na utajiri; mateso na mahangaiko ya Makanisa yao yaliyoenea sehemu mbalimbali za dunia. Wajumbe hawa katika urika wao ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya Makanisa mahalia na kitamaduni ambayo kwa mwongozo wa Roho Mtakatifu na yakiwa yamesimikwa katika nguvu za Neno la Mungu sanjari na Mapokeo hai ya Mama Kanisa, analiongoza Kanisa kwa upendo ili kufanya mang’amuzi katika mchakato wa kitamaduni na kwa binadamu wote kama inavyoshuhudiwa kwa wakati huu. Hakuna sababu ya kufurahia hatua iliyokwisha kufikiwa, lakini watambue kwamba, wao kwa Mungu wanadaiwa zaidi. Majadiliano ya kiekumene yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, ili Kanisa liweze kufikia umoja kamili na unaoonekana. Kanuni ya Imani ya NICEA inawaunganisha wafuasi wote wa Kristo Yesu na kwamba, katika Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo wakristo wote wataweza kuadhimisha kwa pamoja Pasaka ya Bwana! Huu unapaswa kuwa ni mwanzo wa maadhimisho ya Pasaka ya Bwana kwa pamoja. Baba Mtakatifu anawaalika wajumbe wa Tume ya Taalimungu Kimataifa kuibeba ndoto hii katika sakafu ya nyoyo zao ili kwa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, mwanga wa Injili na wa Ushirika uweze kung’aa zaidi.

Tume Taalimungu
01 December 2023, 15:25