Useja Ni Kiini Cha Utambulisho wa Maisha na Wito wa Kipadre!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Useja au Usafi wa moyo ni hija ya uhuru unaojikita katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu, unaoambata neema na huruma ya Mungu pamoja na kutambua changamoto na magumu wanayoweza kukabiliana nayo Wakleri katika maisha yao ya useja. Daima wakumbuke kwamba, wako kwenye mapambano makali yanayowataka kuwa macho na vishawishi vya dunia hii. Uhuru wao unapaswa kujionesha katika sadaka na majitoleo ya kila siku, yanayopyaishwa kwa njia ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na huduma makini kwa watu wa Mungu, kwa kutambua kwamba, huu ni uamuzi uliofanywa kwa uhuru kamili na udumu maisha yote kwa kumwambata Kristo Yesu aliyekuwa fukara, mseja na mtii! Wakleri wanakumbushwa kwamba, wao ni Kristo mwingine, “Alter Christus” kumbe, wanapaswa kupata utambulisho wao katika maisha na utume wa Kristo, ili kuendelea kufuata nyayo zake, kwani anaitwa, anatakaswa na kutumwa kushiriki kazi ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Ni mtu anayetueliwa kati ya watu kwa ajili ya mambo matakatifu. Kumbe, useja ni wito kwa ajili ya utume na maisha ya Kanisa. Useja kama wito unapaswa kugunduliwa, kupokelewa na kutunzwa kwa imani na uaminifu mkubwa, kama ile changamoto iliyotolewa na Yesu Mwenyewe kwa Mtume Petro alipomwambia kutweka hadi kilindini, “Duc in altum” akitambua uzoefu na mang’amuzi yake katika suala zima la uvuvi, lakini Petro akamjibu Yesu, kwa neno lako, nitashusha nyavu zangu! Wakleri wakuze fadhila na wito wa useja kwa kujenga na kudumisha mahusiano mema na ndugu pamoja na majirani zao; hawa ni wale wanaounda familia na udugu wa kisakramenti. Ni watu wanaoadhimisha kwa pamoja mafumbo ya Kanisa, kusali na kutafakari, huku wakishrikishana hazina ya maisha ya kiroho na shughuli za kichungaji. Udugu huu unapaswa kusimikwa katika huruma na mapendo; umoja na mshikamano ili kujenga Ufalme wa Mungu hapa duniani.
Useja umewekwa mahususi na Kristo Yesu kwa ajili ya utume na maisha ya Kanisa, tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake; kwa kuwapenda wote katika Yesu bila ya kuwa na mahusiano fungamanishi na mtu awaye yote! Hiki ni kielelezo cha upendo unaoonesha uhuru na ukomavu kwa ajili ya huduma. Tasaufi ya useja ina mwelekeo chanya katika maisha ya wakleri na kamwe wasikubali kumezwa na malimwengu. Useja ni zawadi inayopaswa kupokelewa kwa moyo mkuu, kutunzwa kwa uaminifu na kuendelea kudumishwa kwa furaha na matumaini katika hija ya maisha ya wakleri hadi pale watakapoitupa mkono dunia. Pale wanapoanguka na kukengeuka, wapige moyo konde na kusimama, tayari kumkimbilia Kristo Yesu, ili aweze kuwaganga na kuwanyanyua tena katika safari hii yenye changamoto nyingi katika ulimwengu mamboleo. Kwa ufupi kabisa, useja ni kiini na utambulisho wa maisha na utume wa Kipadre. Hii ni sehemu ya ujumbe ulioandikwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko kwenda kwa Majandokasisi na Wakleri 700 kutoka nchini Ufaransa waliokuwa wanakutana kuanzia tarehe Mosi hadi 3 Desemba 2023. Baba Mtakatifu Francisko amewahakikishia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake na kwamba, Daraja takatifu ya Upadre inahitaji ujasiri na ndiyo maana hata katika kipindi hiki chenye changamoto nyingi katika maisha na utume wa Wakleri bado kuna vijana wanaothubutu kujisadaka kwa ukarimu kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza kwa sababu wao kwa hakika ni chemchemi furaha na matumaini kwa watu wa Mungu nchini Ufaransa. Kazi ya Mapadre, maadam imeungana na Daraja ya Maaskofu, inashiriki mamlaka ya Kristo ambayo kwayo mwenyewe hukuza, hutakasa na kuongoza mwili wake na kwa njia ya Roho Mtakatifu hutiliwa mhuri wa pekee unaowafanya kuwa mfano wa Kristo Yesu na katika nafsi yake aliye kiongozi. Rej. Presbyterorum ordinis, n 2.
Mapadre ni wahudumu wa Neno la Mungu, changamoto ya kutoa ushuhuda wa maisha yaliyo safi; Mapadre ni wahudumu wa Sakramenti na kwa namna ya pekee Sakramenti ya Ekaristi Takatifu; Mapadre ni walezi wa Taifa la Mungu na kwamba, sadaka na majitoleo yao ni kwa ajili ya watu watakatifu wa Mungu. Rej. Presbyterorum ordinis, n. 4, 5, 6. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Majandokasisi na Wakleri kukita maisha na utume wao katika useja, kwa sababu hii ni sehemu muhimu sana ya utambulisho wao kama Kristo Yesu alivyokuwa Mseja. Umuhimu wa useja siyo matakwa ya kitaalimungu bali ni kwa ajili ya Fumbo “Awezaye kulipokea neno hili, na alipokee.” Mt 19:12. Baba Mtakatifu anatoa angalisho kuhusu maisha na wito wa Mapadre kutokana na mabadiliko katika ulimwengu mamboleo pamoja na mgogoro wa upungufu wa miito, lakini asili ya Daraja Takatifu itaendelea kubaki vile vile, hata kama wito na maisha ya Kipadre yataendelea kubezwa, kudharauriwa na hata kupakwa matope, jambo la msingi ni kujikita katika uinjilishaji mpya unaowawezesha watu wa Mungu kukutana na Kristo Yesu ili kupyaisha maisha yao kwa kujikita katika shughuli za kichungaji zinazonesha ule: ukaribu, huruma, unyenyekevu, ukarimu, subira, upole, sadaka na majitoleo kwa wengine pamoja na umaskini. Padre anapaswa kuitambua “harufu ya kondoo wake na hali yao” na kwamba, hivi ndivyo Padre atakavyogusa nyoyo za waamini wake, kwa kuwaimarisha katika imani na kuwasaidia wakutane na Kristo Yesu.
Haya si mambo mapya na kwamba, kumekuwepo na Mapadre watakatifu katika maisha na utume wa Kanisa, haya yanapewa msisitizo wa pekee ili Mapadre waendelee kuaminika na kusikilizwa kwa makini. Ili kupambana kikamilifu na vishawishi pamoja na changamoto za maisha na wito wa Kipadre kuna haja ya kujenga na kudumisha mafungamano na Kristo Yesu, kwa kuonesha upendo, kwa kuwa na kiasi. Hii ni changamoto ya kuwa waaminifu kwa Mungu kwa kujenga mahusiano na mafungamano na Kristo Yesu, chemchemi ya amani na neema na kwamba, Mungu ni mwaminifu ambaye kwa njia yake wanaitwa na Yeye waingie katika ushirika wa Mwanawe, Kristo Yesu. Rej. 1Kor 1:3-9. Wajitahidi kujibu kwa uhakika wito huu na kuendelea kujenga urafiki na Kristo Yesu na kwamba, uaminifu wao kwa Mungu utawakirimia furaha na amani tele. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume: “C'est la Confiance” yaani “Ni Uaminifu” uliotolewa kwa heshima ya Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu na wa Uso Mtakatifu, kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 150 tangu kuzaliwa kwake huko Alençon nchini Ufaransa anasema, Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu anaonesha jambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa: Upendo na imani katika huruma ya Mungu. Huu ni Waraka ambao wanaweza kujichotea utajiri wake kwani umeandikwa kwa lugha ya Kifaransa. Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu anamtambua Kristo Yesu kuwa ni mpenzi wake wa ndani na kwamba, atawaongoza na kuwawezesha kusimama imara katika imani. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko anawaweka Majandokasisi na Wakleri wa Ufaransa nchini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, ambaye ni Mwombezi na Msimamizi wa nchi ya Ufaransa.