Wito wa Papa wa kusitisha mapigano huko Gaza na karibu na watu wa Ufilipino
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Mwishoni mwa sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 3 Desemba 2023,mawazo ya Papa Francisko yaligeukia Nchi Takatifu, huku akionesha huzuni wake kuhusu ukiukwaji wa makubaliano,moyoni mwake pia kulikuwa na waathiriwa wa shambulio la Kanisa huko Mindanao,nchini Ufilipino. Baadaye alifikiria kuhusu COP28,ambapo Papa Francisko,alilihimiza uongofu wa kiikolojia duniani na hatimaye katika maadhimisho ya Siku ya Walemavu Duniani alitualika kutomtenga mtu yeyote na kuhimiza tofauti.
Kwa njia hiyo mawazo Baba Mtakatiu katika Dominika ya Kwanza ya Majilio, alibainisha kuwa:“Katika Israeli na Palestina hali ni mbaya. Inasikitisha kwamba makubaliano yamevunjwa:hii inamaanisha kifo,uharibifu, taabu. Mateka wengi wameachiliwa,lakini wengi bado wako Gaza. Tunawafikiria, juu ya familia zao ambao walikuwa wameona mwanga, tumaini la kuwakumbatia wapendwa wao tena. Huko Gaza kuna mateso mengi;kuna ukosefu wa mahitaji ya msingi. Ninatumaini kwamba wale wote wanaohusika wanaweza kufikia makubaliano mapya ya kusitisha mapigano haraka iwezekanavyo na kutafuta suluhisho zaidi ya silaha,wakijaribu kufuata njia za ujasiri za amani.”
Shambulio la Ufilipino
Papa Francisko aidha katika tukio la shambuli nchini Ufilipino:“Ningependa kuwahakikishia maombi yangu kwa ajili ya wahanga wa shambulizi lililotokea asubuhi ya leo huko Ufilipino,ambapo bomu lililipuka wakati wa Misa. Niko karibu na familia, kwa watu wa Mindanao ambao tayari wameteseka sana.”
COP28
Mtazamo wa Baba Mtakatifu haukuishia hapo bali anabainisha kuwa: Hata kama kwa mbali, ninafuatilia shughuli za COP 28 huko Dubai kwa umakini mkubwa,niko karibu. Ninasasisha ombi langu la kujibu mabadiliko ya tabianchi kwa mabadiliko halisi ya kisiasa: tuepuke kutoka katika vizuizi vya upendeleo na utaifa,mifumo ya zamani na kukumbatia maono ya pamoja,tukijitolea sasa,bila kuchelewa,kwa ubadilishaji muhimu wa kiikolojia wa ulimwengu.”
Siku ya Walemavu
“Leo ni Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu. Kuwakaribisha na kuwajumuisha wale wanaopatwa na hali hii husaidia jamii nzima kuwa na ubinadamu zaidi. Katika familia,katika parokia,shuleni,kazini,katika michezo:tunajifunza kuthamini kila mtu kwa sifa na uwezo wake na hatuzuii mtu yeyote. “Nawasalimuni nyote, Waroma na mahujaji kutoka Italia na sehemu nyinginezo za dunia,hasa Wapoland ambao wanashiriki katika hafla zilizokuzwa huko Roma kwa heshima ya familia ya shahidi Ulma, ilitangazwa kuwa wenyeheri hivi karibuni. Nawasalimu mahujaji na vikundi vya parokia kutoka Firenze,Siena,Brindisi,Cosenza na Adrano. Ninawatakia wote Dominika njema na safari njema ya Majilio. Tafadhali msisahau kuniombea.”