Mama Kanisa tarehe 4 Desemba 2023 ameadhimisha kumbukizi ya Miaka 60 tangu Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha “Tamko la Inter Mirifica” Mama Kanisa tarehe 4 Desemba 2023 ameadhimisha kumbukizi ya Miaka 60 tangu Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha “Tamko la Inter Mirifica”   (Vatican Media)

Inter Mirifica Miaka 60: Umuhimu wa Vyombo Vya Mawasiliano ya Jamii Ndani ya Kanisa

Kimsingi Inter Mirifica iligusia mwongozo kwa matumizi manyofu ya vyombo vya upashanaji habari; Wajibu wa Kanisa, Kanuni maadili, Haki ya upashanaji habari, sanaa na maadili; Onesho la ubaya wa kimaadili, maoni ya umma, wajibu wa wapokeaji, vijana na wazazi; watunzi na Serikali. Mababa walipembua kwa kina na mapana kuhusu vyombo vya upashanaji habari na kazi ya kitume, inayotekelezwa na Mama Kanisa, kwa kuangalia kazi ya: Wachungaji, waamini na utendaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa tarehe 4 Desemba 2023 ameadhimisha kumbukizi ya Miaka 60 tangu Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha “Tamko la Inter Mirifica” yaani “Kati ya Mambo ya Ajabu: Kuhusu Vyombo Vya Upashanaji Habari.” Hili tamko ambalo limeleta mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Kanisa Katoliki mintarafu vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Hii ni hati ambayo ilifungua malango kwa tafakari ya kisasa, taratibu, kanuni maadili na utu wema juu ya mawasiliano yanayotekelezwa na Kanisa na kwamba, amana na mchango wake unaendelea kung’ara hata katika ulimwengu mamboleo unaoendelea kushuhudia maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Vatican wanasema, vyombo hivi kama vikitumiwa vyema vyaweza kuleta faida kubwa kwa binadamu. Vinatoa mchango mkubwa katika ukuzaji na ustawishaji wa nafsi za watu na pia katika uenezaji na uimarishaji wa Ufalme wa Mungu. Vyombo hivi vinapotumika kinyume cha maongozi ya Mwenyezi Mungu vinaweza kusababisha madhara na hivyo kusababisha huharibifu kwa Jumuiya ya watu. Kimsingi Inter Mirifica iligusia mwongozo kwa matumizi manyofu ya vyombo vya upashanaji habari; kwa kuangalia wajibu wa Kanisa, Kanuni maadili, Haki ya upashanaji habari, sanaa na maadili; Onesho la ubaya wa kimaadili, maoni ya umma, wajibu wa wapokeaji, wajibu wa vijana na wazazi, wajibu wa watunzi, wajibu wa Serikali. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipembua kwa kina na mapana kuhusu vyombo vya upashanaji habari na kazi ya kitume, inayotekelezwa na Mama Kanisa, kwa kuangalia kazi ya wachungaji na waamini; utendaji wa waamini; mafunzo ya watunzi, malezi na majiundo ya wapokeaji, vifaa na misaada. Mtaguso Mkuu wa Vatican ndio uliopitisha azimio la maadhimisho ya Siku ya Upashanaji Habari Ulimwenguni, ili kuwakumbusha waamini kuhusu wajibu wao katika mchakato mzima wa mawasiliano ya jamii, ili kuchangia katika maboresho na ustawi wa miradi inayoendeshwa na kusimamiwa na Mama Kanisa katika sekta ya mawasiliano ya jamii mintarafu mahitaji ya nyakati hizi.

Kumbukizi ya Miaka 60 ya Inter Mirifica
Kumbukizi ya Miaka 60 ya Inter Mirifica

Ni katika muktadha huu, kuna Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii, Tume za Mabaraza ya Maaskofu pamoja na vyama vya Kimataifa vinavyopaswa kupata ridhaa kutoka Vatican. Mwaliko ni kwa watu wa Mungu kuhakikisha kwamba, wanatumia vyombo vya upashanaji habari kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili jina la Bwana litukuzwe kadiri ya neno la Mitume: “Yesu Kristo ni yeye yule jana, leo na hata milele” Ebr 13:8. Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 23 Septemba 2019 alikutana na kuzungumza na wajumbe pamoja na wafanyakazi wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano. Katika hotuba yake aliyoitoa kwa Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano, ili iwasaidie kwa tafakari, amegusia kuhusu: Changamoto za mawasiliano, mawasiliano kama utume wa Kanisa; umuhimu wa kufanya kazi kwa umoja na mshikamano kama timu na kwamba, mfumo wa mawasiliano ya Kanisa unafumbatwa katika ushiriki na kushirikishana kama ushuhuda wa umoja wa Kanisa la Kiulimwengu na Makanisa mahalia na kwamba, Khalifa wa Mtakatifu Petro ataendelea kuunga mkono miradi mbali mbali ya ushirikiano kati ya Vatican na Makanisa mahalia. Baba Mtakatifu amesema, “cheche za mageuzi” ya vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican imekuwa ni “shughuli pevu” kutokana na ugumu wa mchakato wenyewe pamoja na hali ya kudhaniana vibaya. Baba Mtakatifu anaridhishwa na hatua mbali mbali za mageuzi zilizokwisha kufikiwa, kwa kuwa na mikakati ya utekelezaji kwa muda mfupi na mrefu.

Vyombo vya mawasiliano ya jamii katika utume wa Kanisa
Vyombo vya mawasiliano ya jamii katika utume wa Kanisa

Lengo ni kuhakikisha kwamba, rasilimali watu, fedha na vitu vinatumika kikamilifu, ili kupunguza pia gharama za uendeshaji wa sekta ya mawasiliano ndani ya Kanisa. Katika hotuba iliyobubujika kutoka katika sakafu wa moyo wake kuhusu umuhimu wa mawasiliano amekazia mambo makuu matatu: Umuhimu wa watu wote kufanya kazi kama kiu ya Mungu ya kutaka kuwasiliana; mawasiliano yanayofumbatwa katika ushuhuda na ukweli wa Kikristo. Baba Mtakatifu anasema, Mwenyezi Mungu ni chanzo na kilele cha mawasiliano, kwani anataka kuwasiliana na waja wake jinsi alivyo, kutoka katika undani wake. Kumbe, wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii wanapaswa kuwasiliana kwa kutumia akili, moyo na mikono yao; kwa maneno mengine, haya ni mawasiliano yanayomgusa mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, kielelezo cha juu kabisa cha mawasiliano ni upendo wa Mungu ambao umemwilishwa kati ya waja wake. Mawasiliano yanayotekelezwa na Mama Kanisa si matangazo ya biashara wala wongofu wa shuruti. Kanisa linakuwa na kupeta kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Mawasiliano katika maisha na utume wa Kanisa yanafumbatwa katika ushuhuda; ukweli, uzuri na wema. Huu ndio ushuhuda wa wafiadini na waungama imani; watu walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Mawasiliano ndani ya Kanisa ni mchakato unaofumbatwa katika ujasiri pasi ya kukata wala kukatishwa tamaa na hatimaye, kumezwa na malimwengu na hiki ni kishawishi cha Shetani, Ibilisi hata katika karne ya ishirini na moja. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu katika Sala yake ya Kikuhani, aliwaombea wafuasi wake, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwatakasa kwa ile kweli kwani Neno la Mungu ndiyo ile kweli. Wametumwa ulimwenguni lakini wao si wa ulimwengu huu. (Rej. Yoh. 17: 12-19). Wadau wa tasnia ya mawasiliano wasishikwe na kishawishi cha kutaka kujifungia katika upweke wao, kwa kutaka kuendelea kubaki katika udogo wao.

Baba Mtakatifu Francisko akitoa ujumbe wa "Urbi et Orbi"
Baba Mtakatifu Francisko akitoa ujumbe wa "Urbi et Orbi"

Baba Mtakatifu anasisitiza kwamba, wanahabari ni chumvi na chachu ya kuyatakatifuza malimwengu, kwa kuondokana na utamaduni wa watu kukata tamaa na kulalama kila wakati. Hata katika udogo na uchache wao, bado wanaweza kutenda makubwa kwa njia ya ushuhuda. Huu ni ushuhuda unaotangazwa na kushuhudiwa kwa njia ya tunu msingi za maisha ya Kikristo. Kanisa nchini Ukraine limefumbatwa katika ushuhuda unaohifadhi Mafundisho tanzu ya Kanisa. Baba Mtakatifu anasema, waandishi wa habari wanapaswa kutangaza ukweli wa Kikristo unaofumbatwa katika ukweli wa mambo, bila kuweka chumvi au kuwabeza wengine. Ndani ya Kanisa, watu wajisikie kuwa ndugu wamoja na watangaze uzuri. Hii ndiyo lugha ya mashuhuda wa imani na wafiadini, waliotangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Waandishi wa habari wawe mashuhuda wa Kristo kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu, kama inavyoshuhudiwa katika Kitabu cha Matendo ya Mitume. Waandishi wa habari, wawe ni mashuhuda wa furaha ya Injili, changamoto changamani katika ulimwengu mamboleo. Mwishoni, Baba Mtakatifu aliwashukuru na kuwapongeza wafanyakazi wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano! “Tamko la Inter Mirifica” yaani “Kati ya Mambo ya Ajabu: Kuhusu Vyombo Vya Upashanaji Habari” ni mwaliko kwa wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kujifunza kikamilifu juu ya muktadha wa mawasiliano yanayokita mizizi yake katika huruma, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi anasema Kardinali Matteo Maria Zuppi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI. Vyombo vya mawasiliano ni muhimu katika maisha na utume wa Kanisa hasa nyakati hizi ambako kunaendelea kushamiri habari za kughushi, maarufu kama “Fake news.” Haki ya kupata habari haina budi kusimamiwa na kanuni maadili na miongozo inayozingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu wakati wa kufanya tafiti, kuchapa na kusambaza habari yenyewe! Inter Mirifica pamoja na mambo mengine inahimiza juu ya ukweli, uaminifu, utu, heshima ya binadamu pamoja na utimilifu wa habari.

Inter Mirifica 60
03 January 2024, 13:53