Maadhimisho ya Siku ya Maji Duniani 2024: Maji na Amani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 22 Machi inaadhimisha Siku ya Maji Duniani iliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1992. Siku ya Maji Duniani inalenga kuragibisha uelewa miongoni mwa taasisi za dunia na maoni ya umma kuhusu umuhimu wa kupunguza upotevu wa maji pamoja na kujikita katika mchakato wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Maadhimisho ya Siku ya Maji kwa Mwaka 2024 yananogeshwa na kauli mbiu “Maji na Amani.” Umoja wa Mataifa unasema, Maji yanaweza kuwa ni rasilimali yenye uwezo wa kuleta amani duniani na kwamba, maji ni rasilimali muhimu sana kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hadi sasa, ni nchi 24 pekee duniani zilizo na makubaliano ya ushirikiano wa kugawana maji. Zaidi ya hayo, mambo kama vile athari za mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la watu huleta hitaji la dharura la kuwaunganisha watu wote kuelekea ulinzi na uhifadhi wa maji safi na salama. Pia ni vyema kukumbuka kuwa afya ya umma, chakula, mifumo ya nishati, tija ya kiuchumi na uadilifu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni vipengele vinavyotegemea usimamizi sahihi wa mzunguko wa maji. Kwa sababu hizi ni muhimu kuchukua hatua ili kutambua kwamba maji si rasilimali tu ya kutumiwa bali ni haki ya binadamu inayohusishwa kwa karibu na kila nyanja ya maisha. Umoja wa Mataifa unasema lengo la Siku ya Maji Duniani kwa mwaka 2024 ni kuunda athari chanya, kuunganisha idadi ya watu ulimwenguni na kutumia rasilimali maji kama njia ya kuweka misingi wa mustakabali ulio imara na endelevu.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii mintarafu maadhimisho ya Siku ya Maji Duniani kwa mwaka 2024 anasema “Leo hii, rasilimali nyingi za kifedha na teknolojia bunifu, ambazo zingeweza kutumika kufanya maji kuwa chanzo cha uhai na maendeleo kwa wote, zinaelekezwa kwenye utengenezaji na ulimbikizaji wa wa silaha. Badala yake, ni muhimu zaidi kuliko hapo awali kuwekeza katika mazungumzo na amani. Maji ni sehemu muhimu sana kwa maisha, ustawi na maendeleo ya binadamu, changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa ni kusimama kidete ili kujenga utamaduni wa utunzaji bora wa maji, kwani maji ni uhai ikiwa kama ubora na usalama wake utazingatiwa na wote. Maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu na kwamba, kila mtu ana haki ya kupata maji safi, salama na yenye ubora! Binadamu anapaswa kujifunza kutumia rasilimali maji kwa unyenyekevu bila kuyachafua. Haki ya maji safi na salama ni kati ya changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, kuna baadhi ya nchi ambazo bado hazijatambua kwamba, maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu na baadhi ya nchi zinapinga maji kuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Rasilimali maji inapaswa kushughulikiwa kikamilifu kwani hii ni sehemu muhimu sana katika mchakato wa maboresho ya maisha ya binadamu sanjari na mapambano dhidi ya umaskini duniani. Rasilimali maji inapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika sera za kitaifa na Kimataifa kutokana na umuhimu wake kwa maisha ya binadamu.
Sera hizi ziwe na mwelekeo wa kisiasa na kisheria, kama ilivyokubaliwa na Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2010 mintarafu haki ya maji safi na salama pamoja na afya bora. Wadau mbalimbali wanapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu, kwani hii ni sehemu ya mustakabali wa binadamu kwa siku za usoni. Vijana wa kizazi kipya wanapaswa kufundwa barabara kuhusu umuhimu wa rasilimali maji katika maisha ya binadamu. Baba Mtakatifu anatambua kwamba, ujenzi wa dhamiri nyofu ni dhamana pevu inayohitaji utambuzi, majitoleo na sadaka! Vita kuu ya Tatu ya Dunia inayopiganwa sehemu mbalimbali, inaweza kuwa ni njia itakayoitumbukiza pia Jumuiya ya Kimataifa katika vita ya dunia kwa ajili ya maji. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, kuna idadi kubwa ya watoto wanaofariki dunia kutokana na magonjwa yenye uhusiano na maji; kuna mamilioni ya watu wanaotumia maji yasiyo safi wala salama! Kumbe, Jumuiya ya Kimataifa haijachelewa kuchukua hatua madhubuti ili kutambua na kulinda maji kwa ajili ya mafao ya wengi. Utunzaji bora wa maji ni sehemu muhimu sana ya haki msingi za binadamu; ikiwa kama watu wataweza kuheshimu haki hii, itakuwa ni rahisi kwa haki nyingine zote kuweza kulindwa na kudumishwa, hapa mwaliko ni kujenga utamaduni wa kutunza maji unaofumbatwa katika utamaduni wa watu kukutana, ili kuunganisha nguvu kutoka kwa wadau mbalimbali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi mintarafu rasilimali maji.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, umoja ni nguvu, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itaunganisha nguvu kwa ajili ya mafao ya wengi; itafanikiwa kusikiliza na kujibu kilio cha haki msingi ya maji; ardhi inayopaswa kutunzwa na kuendelezwa zaidi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Utamaduni wa watu kukutana utaiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kuwa na maji safi na salama pamoja na uhakika wa ubora wa maji. Mwenyezi Mungu kwa wema na ukarimu wake anapenda watu wote waweze kufaidika na rasilimali maji, lakini hii ni kazi, dhamana na wajibu wa kila mtu anasema Baba Mtakatifu Francisko. Kumbe, watu wanapaswa kutambua kuhusu haki msingi ya maji na kwamba, wanao mchango mkubwa katika mchakato wa kuhakikisha kwamba, kweli maji yanakuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu, ili kuwasaidia watu kupata maji safi na salama! Hapa kuna haja ya kufanya kazi kwa pamoja na kushikamana katika mapambano ya maji kama sehemu ya haki msingi za binadamu! Lengo anasema Baba Mtakatifu, ni kujenga ulimwengu unaosimikwa katika haki, amani, utulivu na mshikamano na wote, bila mtu awaye yote kutengwa! Hii ni dunia ambamo wote wanafaidika na mambo msingi katika maisha ya binadamu, ili kuishi na kukua katika utu. Takwimu za Umoja wa Mataifa kuhusu watu wasiokuwa na huduma ya maji safi na salama; idadi kubwa ya watoto wanaoendelea kupoteza maisha kwa kukosa maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya binadamu ni mambo ambayo wadau mbali mbali wanapaswa kuyazingatia katika kuragibisha mchakato wa maji kuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu!