Sikukuu ya Bikira Maria wa Rozari kwa Mwaka 2024 ni Siku maalum ya: Toba, kufunga, kusali na kuabudu Ekaristi Takatifu kwa ajili ya kuombea amani duniani. Sikukuu ya Bikira Maria wa Rozari kwa Mwaka 2024 ni Siku maalum ya: Toba, kufunga, kusali na kuabudu Ekaristi Takatifu kwa ajili ya kuombea amani duniani.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Bikira Maria wa Rozari Takatifu: Siku ya Toba, Kufunga, Kusali na Kuabudu Ekaristi Takatifu

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema: Kutubu na kumwongokea Mungu, kusali na kufunga na kwamba, siku hii inogeshwe kwa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu Jumatatu tarehe 7 Oktoba 2024, Mama Kanisa anapoadhimisha Sikukuu ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu. Hii pia ni siku muhimu sana, Jumuiya ya Kimataifa inapofanya kumbukizi ya mwaka mmoja tangu vita kati ya Israeli na Palestina ilipotimua vumbi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tarehe 7 Oktoba ya kila Mwaka, Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutoa mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema katika Kipindi hiki cha Mwezi wa Oktoba, kujibidiisha kusali Rozari Takatifu, huku wakimwachia nafasi Bikira Maria, ili aweze kuwasindikiza kwenda kwa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu! Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” anamwangalia Bikira Maria aliyemwilisha Heri za Mlimani kuliko mtakatifu yoyote yule. Ni mwanamke wa imani aliyefurahia uwepo wa Mungu katika maisha yake na kuhifadhi yote katika sakafu ya moyo wake! Bikira Maria ni Mtakatifu kuliko watakatifu wote. Bikira Maria ni kimbilio la waamini katika ulinzi na tunza yake ya kimama. Anawafundisha na kuwasindikiza waamini katika utakatifu wa maisha; anawalinda bila kuwahukumu; anawafariji, kuwaombea na kuwatakatifuza kwa uwepo wake mwanana, changamoto na mwaliko kwa waamini kumkimbilia katika sala, lakini zaidi kwa njia ya tafakari ya Rozari Takatifu. Baba Mtakatifu anasema, Rozari Takatifu ni muhtasari wa huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Ni njia muafaka kabisa ya kutafakari maisha na utume wa Kristo Yesu, ili kumfahamu, kumpenda, kumfuasa na kumtumikia kwa njia ya upendo kwa Mungu na kwa jirani wenye shida na mahangaiko mbalimbali wanaokumbukwa katika Sala ya Rozari Takatifu. Waamini wanahamasishwa kuendelea kusali Rozari Takatifu, muhtasari wa historia nzima ya kazi ya ukombozi; maisha na utume wa Kristo Yesu.

Bikira maria wa Rozari: Siku ya Toba, Sala, Kufunga na Kuabudu Ekaristi Takatifu
Bikira maria wa Rozari: Siku ya Toba, Sala, Kufunga na Kuabudu Ekaristi Takatifu

Bikira Maria alipowatokea Watoto watatu wa Fatima yaani: Francisko, Yacinta na Lucia aliwaagiza kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya toba, wongofu wa ndani na amani duniani. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema: Kutubu na kumwongokea Mungu, kusali na kufunga na kwamba, siku hii inogeshwe kwa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu Jumatatu tarehe 7 Oktoba 2024, Mama Kanisa anapoadhimisha Sikukuu ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu. Hii pia ni siku muhimu sana, Jumuiya ya Kimataifa inapofanya kumbukizi ya mwaka mmoja tangu vita kati ya Israeli na Palestina ilipotimua vumbi, yaani tarehe 7 Oktoba 2023. Watu wengi wamepoteza maisha, wamejeruhiwa, wametekwa, kufungwa na wengine wengi wamewekwa kizuizini. Watu wanaendelea kuteseka kwa kukosekana kwa mahitaji msingi kama vile chakula, maji na makazi, kiasi cha kupelekea watu kuyakimbia maeneo yao. Baba Mtakatifu anawataka wahusika wa pande zote mbili kuhakikisha kwamba, wanawaachia huru bila masharti wafungwa na mateka wa vita. Ni wakati wa kusitisha vita kwa sababu waathirika wakuu ni raia wasiokuwa na hatia na ambao wanalazimika kuyakimbia makazi yao. Uhuru na usalama wa nchi husika lazima vipewe kipaumbele na wala kusiwepo mashambulizi dhidi ya taifa jingine au kuvamiwa. Kumbe, huu ni mwaliko wa kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli; haki na amani ili hatimaye kuachana na chuki pamoja na vita.

Vita ina madhara makubwa kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu
Vita ina madhara makubwa kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu

Tarehe 7 Oktoba 2024 ni siku maalum kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumlilia Mwenyezi Mungu kwa njia ya: Toba, Sala na Kufunga, ili aweze kuwakirimia waja wake msamaha na amani ya kudumu anasema Kardinali Pierbattista Pizzaballa, O.F.M. Patriaki wa Yerusalemu na Mlinzi mkuu wa Nchi Takatifu na Mlima wa Sion.  Dominika tarehe 6 Oktoba 2024 waamini na watu wenye mapenzi mema wameshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa Askofu mkuu Peter Rajic, Balozi wa Vatican kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Pompei, Kusini mwa Italia, amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika ushuhuda na wawe wajenzi na waragibishaji wa amani, urafiki wa kijamii miongoni mwa Mataifa mbalimbali, tayari kujiachia na kujiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Rozari Takatifu na matendo ya huruma ni silaha madhubuti katika mapambano dhidi ya vita na ukosefu wa haki, amani na maridhiano. Waamini kamwe wasichoke kusali kwa ajili ya kuombea amani na watu wenyewe wajitahidi kuwa ni vyombo na mashuhuda wa amani na Wasamaria wema, tayari kumwilisha Injili ya upendo katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Vita inasababisha mateso na mahangaiko kwa watu wa Mungu
Vita inasababisha mateso na mahangaiko kwa watu wa Mungu

Kwa upande wake Askofu mkuu Sviatoslav Shevchuk, Mkuu wa Kanisa Katoliki la Kigiriki la Kyiv-Halyč, nchini Ukraine, anamwona Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni mjumbe na chombo cha amani duniani na kwamba, katika kipindi cha miaka mitatu ya vita kati ya Ukraine na Urusi, Baba Mtakatifu ameendelea kusisitiza wito wa kusali na kuombea amani nchini Ukraine. Mababa wa Sinodi wameshiriki kikamilifu katika kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya kuombea toba, wongofu wa ndani, amani na upatanisho sehemu mbalimbali za dunia. Waamini wanaomba ulinzi na tunza Bikira Maria wa Rozari Takatifu ili aweze kuwaombea amani, tayari kushiriki katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu tayari kuambata, kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini. Tume ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya, COMECE inasema, watu wa Mungu Barani Ulaya wajikite katika sala na majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kuondokana na vitisho vya vita na mipasuko ya kijamii inayotishia: haki, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vita inayoendelea sehemu mbalimbali za dunia ina athari kubwa zaidi kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kuondokana pia na chuki dhidi ya Wayahudi. Sheria ya Kimataifa inapaswa kutekelezwa ili kulinda miundombinu ya hospitali, shule na nyumba za Ibada. Majadiliano ya kidiplomasia yanapaswa kuchukua mkondo wake, ili hatimaye, kusitisha vita.

Siku ya Kusali na Kufunga

 

06 October 2024, 16:34