Hati hii ni muhtasari wa safari nzima ya Maadhimisho haya iliyowahusisha watu wa Mungu katika ujumla wao kwa kutambua kwamba, kiini cha Sinodi kuanzia mwaka 2021-2024 “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume” Hati hii ni muhtasari wa safari nzima ya Maadhimisho haya iliyowahusisha watu wa Mungu katika ujumla wao kwa kutambua kwamba, kiini cha Sinodi kuanzia mwaka 2021-2024 “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume”  (Vatican Media)

Hati ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu: Matunda ya Roho Mtakatifu: Muhtasari wa Sinodi

Hati hii ni muhtasari wa safari nzima ya Maadhimisho haya iliyowahusisha watu wa mungu katika ujumla wao kwa kutambua kwamba, kiini cha Sinodi kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2024 “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume” mwaliko ni kulipyaisha Kanisa katika huduma inayosimikwa katika utume, daima likitafuta njia za kuweza kuwa aminifu na kuendelea kujikita katika Mapokeo ili kumwilisha Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu kuanzia mwaka 2021 hadi tarehe 27 Oktoba 2024, yamenogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Hati ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu imegawanyika katika sura tano, ikiwa na utangulizi pamoja na hitimisho lake. Sura ya kwanza inazungumzia kiini cha hulka ya Kisinodi ni wito kutoka kwa Roho Mtakatifu kuhusu wongofu; Pili, wote wakiwa katika Mtumbwi mmoja wanaitwa kuongoka katika mahusiano; Tatu ni kutupa nyavu katika mchakato wa wongofu; Nne ni Mavuno makubwa yanayosimikwa katika kifungo cha wongofu. Sura ya tano: Ni kutumwa, Majiundo ya watu wa Mungu kama Mitume wamisionari na hatimaye ni kuadhimisha sherehe kwa watu wote. Kama sehemu ya utangulizi, Mababa wa Sinodi wanasema, Roho Mtakatifu anaendele akutenda kazi ndani ya Kanisa, kwa kujenga umoja na ushirika wa watu wa Mungu, hata katika tofauti zao msingi. Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu yanajidhihirisha katika mateso ya watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia; watu wenye kiu ya: haki na amani ambayo ni mchakato wa watu wote wa Mungu, kwani Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, “furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati zetu, hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteswa, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Wala hakuna jambo lililo na hali halisi ya kibinadamu lisiloigusa mioyo yao.” Gaudium et spes, 1.

Wajumbe wa Sinodi ya XVI ya Maaskofu Kutoka Afrika
Wajumbe wa Sinodi ya XVI ya Maaskofu Kutoka Afrika

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yaligawanyika katika awamu kuu mbili na kwamba, hati hii ni muhtasari wa safari nzima ya Maadhimisho haya iliyowahusisha watu wa Mungu katika ujumla wao kwa kutambua kwamba, kiini cha Sinodi kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2024 “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume” mwaliko ni kulipyaisha Kanisa kwa kujisadaka katika huduma inayosimikwa katika utume, daima likitafuta njia za kuweza kuwa aminifu na kuendelea kujikita katika Mapokeo hai ya Kanisa, ili kumwilisha Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kwa kusoma alama za nyakati; kutafuta na kuambata huruma ya Mungu katika maisha. Maadhimisho ya Sinodi Awamu ya Pili yalianza kwa mwaliko wa toba na wongofu wa ndani kwa dhambi dhidi ya haki na amani; Utunzaji wa mazingira nyumba ya wote; dhambi dhidi ya wazawa, wakimbizi na wahamiaji; watoto na wanawake; maskini na kwa kushindwa kusikiliza kwa makini na ujenzi wa ushirika mambo yanayohitaji toba na wongofu wa ndani, kwa kuadhimisha Sakramenti ya huruma ya Mungu, upendo usiokuwa na mipaka sanjari na ushirika. Kanisa linataka kuwa ni kielelezo cha msamaha na upatanisho kutoka kwa Mungu na mashuhuda wa neema ya Mungu.

Hati hii ni zawadi ya Roho Mtakatifu na muhtasari wa safari ya Kisinodi
Hati hii ni zawadi ya Roho Mtakatifu na muhtasari wa safari ya Kisinodi

Kanisa liliweza kushuhudia matunda ya kwanza ya Maadhimisho ya Sinodi ya Mwaka 2021 katika medani mbalimbali za maisha na hivyo Kanisa linapaswa kuwa ni mahali pa ukarimu, matumaini na furaha. Mama Kanisa kwa sasa anaendelea kufanya tafiti makini katika baadhi ya maeneo: Mahusiano kati ya Makanisa ya Mashariki na Magharibi; Kwa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini; Utume wa Kanisa katika Ulimwengu wa kidigitali; Taalimungu: Sheria na kanuni kuhusu baadhi ya mifumo huduma. Upyaisho wa Sinodi ya kimisionari unaogusia mahusiano kati ya askofu, watawa wanasheria, madaraka ya Askofu mahalia; Asili na muundo wa hija za kitume za Maaskofu mjini Roma; Dhamana na wajibu wa Mabalozi wa Vatican sehemu mblimbali za dunia pamoja na kupokea matunda ya safari ya kiekumene. Vigezo msingi vya kitaalimungu mintarafu mbinu na mkakati wa Kisinodi katika mang’amuzi ya mafundisho ya Kanisa yanayogubikwa na utata, kichungaji na kimaadili. Ndoa za mseto zitashughulikiwa na Shiriko la Mabaraza ya Maaskofu Afrika na Madagascar, SECAM; Malezi ya majiundo katika toba na wongofu wa ndani; ushiriki mkamilifu wa watu wote wa Mungu katika maisha na utume wa Kanisa; Umuhimu wa kutenga rasilimali watu kwa ajili ya mchakato wa Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, daima kwa kuzingatia ubora wa mbinu za Kisinodi za kufanya kazi katika makundi maalum. Hati ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inadai toba na wongofu wa ndani, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Maadhimisho ya Ekaristi Takatifu ni mahali pa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi
Maadhimisho ya Ekaristi Takatifu ni mahali pa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi

Hata siku ya kwanza ya juma Mariamu Magdalene alikwenda kaburini alfajiri, kungali giza bado; akaliona lile jiwe limeondolewa kaburini. Basi akaenda mbio, akafika kwa Simoni Petro na kwa yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, Wamemwondoa Bwana kaburini, wala hatujui walikomweka. Yn 20:1-2. Sura ya Kwanza Sura ya kwanza inazungumzia kiini cha hulka ya Kisinodi ni wito kutoka kwa Roho Mtakatifu kuhusu wongofu; umoja na ushirika wa watu wa Mungu, wanaoitwa kujikita katika msamaha. Kanisa linajitambua kuwa ni sehemu ya watu wa Mungu, Sakramenti ya umoja na kwamba, Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni kiini cha ushirika na umoja unaoendelea kuboresha maisha ya watu wa Mungu. Ushirika wa watu wa Mungu ambao ni Kanisa; huu pia ni ushirika wa waamini na ushirika wa Makanisa na kwamba, Khalifa wa Mtakatifu Petro ni kielelezo cha umoja wa Kanisa. Maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii wanapaswa kupewa upendeleo wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa na kwamba, hata maskini ni sehemu ya mihimili ya uinjilishaji. Kanisa linaitwa na kutumwa kutoa huduma ya kinabii, kwani Kanisa ni sehemu ya Ufalme wa Mungu. Sakramenti ya Ubatizo ni kiini cha maisha na utume wa Kikristo, kumbe waamini wanaalikwa kushiriki kikamilifu katika maisha ya Kanisa, kwa kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene: huu ni uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma.

Majadiliano ya kiekumene ni sehemu ya matunda ya Sinodi XVI ya Maaskofu
Majadiliano ya kiekumene ni sehemu ya matunda ya Sinodi XVI ya Maaskofu

Uekumene wa damu na ule wa utakatifu wa maisha ni mambo msingi yanayoshuhudiwa na Wakristo sehemu mbalimbali za dunia katika umoja, udugu na upendo kama kikolezo cha ujenzi wa Ufalme wa Mungu na Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Lakini, ikumbukwe kwamba, damu ya mashuhuda hawa wa imani ni chachu ya Ukristo. Uekumene wa maisha ya kiroho na utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu wa kibinadamu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu tunu msingi za Kiinjili, ni kwa kadiri ileile watahamasisha na kutekeleza umoja wa Wakristo na udugu wa kibinadamu kati yao. Uekumene wa huduma unatekelezwa kwa njia ya sera na mikakati ya shughuli za kichungaji sanjari na maisha ya kitume. Mababa wa Sinodi wanakazia pia kuhusu maisha ya Kisakramenti: Sakramenti ya Ubatizo, Sakramenti ya Kipaimara na Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Hati inafafanua kuhusu umuhimu wa hulka ya Kisinodi, Ibada kwa Bikira Maria na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari, daima watu wa Mungu wakitembea kwa umoja na ushirika; katika tofauti zao za kitume na katika ushiriki wao mkamilifu wa matukio ya uinjilishaji na kwamba Roho Mtakatifu ni mhusika mkuu wa mchakato wa Uinjilishaji na kwamba, ndiye anayelihakikishia Kanisa umoja katika tofauti zake msingi. Ikumbukwe kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, kumbe, kuna haja pia ya kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini, ili kukuza na kudumisha ari na mwamko wa Kisinodi unaofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani, ili kutekeleza kazi ya kinabii katika ulimwengu mamboleo, kwa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote.

Utunzaji Bora wa Mazingira ni wajibu wa kimaadili.
Utunzaji Bora wa Mazingira ni wajibu wa kimaadili.

Simoni Petro, na Tomaso aitwaye Pacha, na Nathanaeli wa Kana ya Galilaya, na wana wa Zebedayo, na wengine wawili wa wanafunzi wake, walikuwapo pamoja. Simon Petro aliwaambia, “Naenda kuvua samaki.” Yn 21:2-3. Sura ya Pili, Waamini wote wakiwa katika Mtumbwi mmoja wanaitwa kuongoka katika mahusiano kwa kujenga na kudumisha mahusiano mapya; kwa kusikilizana na kujadiliana kwa pamoja katika ukweli na uwazi; kwa kulinda na kudumisha haki na amani; kwa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa kupinga matumizi mabaya ya madaraka na kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya wokovu. Kumbe, karama, utume na miito mbalimbali ni kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kadiri ya hali na mazingira ya mwamini. Mababa wa Sinodi wamekazia umuhimu wa kuwa makini kwa lugha inayotumika katika mahubiri, mafundisho ya Kanisa, Katekesi na wakati wa kuandaa Nyaraka kutoka katika Makanisa mahalia ambazo kimsingi zinapaswa kutajirishwa na watakatifu wanawake na wanataalimungu. Kipaumbele cha pekee kwa Kanisa kiwe ni watoto, vijana wa kizazi kipya wanaoweza kupyaisha mchakato wa maisha na utume wa Kanisa bila kuwasahau watu wa ndoa na familia. Mchango wa wanawake upewe uzito unaostahili. Wahudumu wa Kanisa wawe ni kwa ajili ya ujenzi wa umoja na utulivu kwa kuhakikisha kwamba, Roho Mtakatifu chemchemi ya umoja na ushirika anapewa kipaumbele katika maisha na utume wa Kanisa. Askofu amewekwa wakfu kwa ajili ya huduma kwa Kanisa ili kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa mungu, ajitahidi kulijenga Kanisa mahalia kama familia ya Mungu inayowajibika pamoja na kushirikiana kwa karibu zaidi na Mabalozi wa Vatican katika nchi husika. Waamini walei wapewe kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa, huku wakishirikiana na mihimili ya Kanisa kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Huu ni mwaliko wa kuhakikisha kwamba, wanaepuka kashfa na nyanyaso zinazoweza kuchafua maisha na utume wa Kanisa. Watu wote wa Mungu wapanie kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Waamini walei wanapaswa kujengewa uwezo wa kimasomo, mahusiano, ushauri wa shughuli za kichungaji na maadhimisho ya Sakramenti mbalimbali za Kanisa. Ushiriki wa waamini walei katika maisha na utume wa Makanisa mahalia ni muhimu sana.

Sinodi ni mwaliko kwa waamini kujikita katika toba na wongofu wa ndani
Sinodi ni mwaliko kwa waamini kujikita katika toba na wongofu wa ndani

Basi Yesu akawaambia, Wanangu, mna kitoweo? Wakamjibu, La. Akawaambia, Litupeni jarife upande wa kuume wa chombo, nanyi mtapata. Basi wakatupa; wala sasa hawakuweza kulivuta tena kwa sababu ya wingi wa samaki. Sura ya Tatu ni kutupa nyavu katika mchakato wa wongofu; kwa kujikita katika mangamuzi ya maisha na utume wa Kanisa, ili kushiriki katika utume wa kinabii wa watu wa Mungu. Mang’amuzi ya Kikanisa yasimikwe katika uhuru wa ndani, unyenyekevu, sala, hali ya kuaminiana; ukweli na uwazi pamoja na kujiaminisha kwenye mapenzi ya Mungu. Watu wa Mungu wajenge utamaduni wa kusoma, kusikiliza na kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha na utume wao na kwamba, wahusishwe kikamilifu katika miundo ya utoaji wa maamuzi ya maisha na utume wa Kanisa. Yote yaisimikwe katika ukweli na uwazi; uwajibikaji pamoja na kuhakikisha kwamba, kuna kuwepo na tathmini, ili kuliwezesha Kanisa kujifunza kutoka katika uzoefu, mang’amuzi sera na mikakati mintarafu maisha na utume wa Kanisa, daima kwa kuendelea kuwa wasikivu kwa maongozi ya Roho Mtakatifu. Hati hii inawataja washiriki katika mchakato wa Sinodi mintarafu Sheria za Kanisa.

Wongofu wa ndani na mahujaji wa matumaini
Wongofu wa ndani na mahujaji wa matumaini

“Na hao wanafunzi wengine wakaja katika mashua; maana hawakuwa mbali na nchi kavu; ila yapata dhiraa mia mbili; huku wakilikokota lile jarife lenye samaki. Na ijapokuwa ni wengi namna hiyo, jarife halikupasuka.” Yn 21: 8, 11. Sura ya Nne ni Mavuno makubwa yanayosimikwa katika kifungo cha wongofu unaosimikwa katika mahujaji wa matumaini wanaotoka kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Huu ni mwaliko kwa Kanisa kujikita katika utamaduni wa kidigitali maarufu sana kwa vijana wa kizazi kipya, kwa kuhakikisha kwamba, Kanisa pia linajihusisha kutoa malezi na makuzi ya matumizi bora zaidi ya mitandao ya kijamii. Kila mwamini anahamasishwa kuwa ni hujaji wa matumaini. Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yapewe mkazo wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa, kwani hap ani mahali pa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari. Watawa wanayo nafasi ya pekee katika maisha na utume wa Kanisa; katika huduma hasa katika sekta ya elimu, afya na maendeleo ya jamii. Watawa wanahamasishwa kushiriki katika maisha na utume wa Makanisa mahalia, ili kukuza na kudumisha ukatoliki wa Kanisa. Majadiliano ya kiekumene ni mchakato wa kubadilishana zawadi katika kukuza na kudumisha: utakatifu wa maisha, upendo, tasaufi, taalimungu, mshikamano na utamaduni. Huu ni mwaliko kwa Makanisa mahalia kukuza na kudumisha mshikamano wa umoja na upendo miongoni mwa Mabaraza ya Maaskofu pamoja na ushiriki wa maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kukuza umoja na utofauti wa Kanisa. Sekretarieti kuu ya Vatican ni kwa ajili ya huduma kwa Kanisa la Kiulimwengu. Ari na mwamko wa majadiliano ya kiekumene ni kati ya matunda ya Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu, kwa ushiriki mkubwa wa wajumbe kutoka katika Makanisa na Jumuiya za Kikristo, kama sehemu muhimu sana ya ujenzi wa umoja wa Kanisa. Mwaka 2025 ni Jubilei ya Miaka 1700 tangu kuadhimishwa kwa Mtaguso wa Nicea iwe ni fursa ya kuungama tena imani kwa pamoja na kwamba, Mwaka 2025 Makanisa yote yataadhimisha Pasaka ya Bwana kwa wakati mmoja. Hii ni fursa ya kuimarisha nguvu za kimisionari za kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia kweli za Kiinjili
Waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia kweli za Kiinjili

“Basi Yesu akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu.” Yn 20:21-22. Sura ya tano: Ni kutumwa, Majiundo ya watu wa Mungu kama Mitume wamisionari. Hapa kuna haja ya kujikita katika malezi na majiundo makini ya watu wa Mungu kama sehemu ya mchakato wa kuwaunda ili waweze kuwa kweli ni wamisionari, tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, mchakato unaopata chimbuko lake katika Sakramenti za Kanisa, lakini zaidi katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Kumbe, Kanisa linapaswa kuwekeza katika majiundo ya walezi ili liweze kuwafunda waamini walei barabara katika: Katekesi, Sera na mipango ya shuhguli za kichungaji, Maisha ya Jumuiya Ndogondogo za Kikristo na kwamba, mahali muafaka pa malezi na majiundo ya waamini walei ni shuleni na kwenye taasisi za elimu. Waamini walei washiriki pia katika malezi na makuzi ya Majandokasisi. Waelimishwe zaidi katika matumizi ya utamaduni wa kidigitali, kama sehemu ya maboresho ya maisha na wito wao, lakini pia watambue athari za matumizi ya mitandao ya kijamii kama vile unyanyasaji wa kijinsia, habari potofu na utegemezi wa mitandao hii, hali inayogeuka na kuwa ni ugonjwa. Kanisa lijikite katika kufundisha matumizi bora ya mitandao ya kijamii. Mafundisho Jamii ya Kanisa yapewe kipaumbele cha pekee kati ya waamini pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. “Basi waliposhuka pwani, wakaona huko moto wa makaa, na juu yake pametiwa samaki, na mkate. Wala hakuna mtu katika wale wanafunzi aliyethubutu kumwuuliza, “U nani wewe?” wakijua ya kuwa ni Bwana. Yesu akaenda akautwaa mkate, akawapa, na samaki vivyo hivyo.” Yn 219.12.13. Hati hii inatihimishwa kwa mwaliko wa sherehe kwa watu wote wa Mungu kujikita katika ushuhuda wa kinabii katika kupyaisha shughuli za kisiasa na kiuchumi, pamoja na kuendelea kutafuta haki na amani na watu wote wa Mungu, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Waamini waendelee kujikita katika malezi na majiundo ya Kisinodi na Kimisionari na kwamba, Kanisa linapaswa kujikita katika malezi na majiundo makini ya mihimili ya uinjilishaji. Waamini watambue mchango wa ulimwengu wa kidigitali, wajenga mahusiano na mafungamano pamoja na kutambua madhara ya matumizi ya mitandao ya kijamii. 

Hati Sinodi 2021-2024
28 October 2024, 11:57