Muungano wa Wafanyabiashara wa Kifamilia Nchini Italia AIDAF, Italian Family Business, ulianzishwa kunako mwaka 1997 na Bwana Alberto Falck pamoja na kundi la wajasiriamali. Muungano wa Wafanyabiashara wa Kifamilia Nchini Italia AIDAF, Italian Family Business, ulianzishwa kunako mwaka 1997 na Bwana Alberto Falck pamoja na kundi la wajasiriamali.  (Vatican Media)

Kanisa ni Familia ya Mungu: Ushuhuda Katika Ujenzi wa Ufalme wa Mungu na Haki

Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia kuhusu Kanisa kuwa ni familia ya Mungu; Maisha na utume wa Kanisa unaofumbatwa katika ushuhuda na kwamba, wanapaswa kujisikia kuwa ni sehemu ya familia kubwa tayari kutoa huduma kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Familia ni Kanisa dogo la nyumbani; ni shule ya tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kimaadili na kijamii. AIDAF iweke uhusiano mzuri kati ya familia na kazi, kielelezo cha ujasiri na uwajibikaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Muungano wa Wafanyabiashara wa Kifamilia Nchini Italia AIDAF, “Italian Family Business” ulianzishwa kunako mwaka 1997 na Bwana Alberto Falck pamoja na kundi la wajasiriamali walioongozwa na kanuni maadili na maono haya ya kifamilia. AIDAF inajionesha kama sehemu ya kumbukumbu hai nchini Italia kwa biashara za kifamilia; leo hii Muungano huu unaunganisha pamoja zaidi ya makampuni 290, ambayo yanawakilisha takriban asilimia 16% ya Pato la Taifa la Italia, GNP. Lengo kuu la AIDAF ni kukuza, kusambaza na kuunga mkono mtindo wa kimaadili wa "kufanya biashara" msingi kwa ukuaji endelevu wa biashara. Biashara ya kisasa ya familia, iliyoanzishwa kwenye ulimwengu wa maadili dhabiti ambayo hutolewa kizazi baada ya kizazi, inawaweka wadau wake katikati, na kutoa mchango chanya na katika jamii ambayo inafanya kazi kwa umoja na ushirikiano; shukrani, ufanisi kwa kujisadaka na kwa kustahili.

Kanisa ni familia ya Mungu inayowajibika
Kanisa ni familia ya Mungu inayowajibika

Ni katika muktadha huu, Wajumbe wa Muungano wa Wafanyabiashara wa Kifamilia Nchini Italia, AIDAF, Jumamosi tarehe 5 Oktoba 2024 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia kuhusu Kanisa kuwa ni familia ya Mungu; Maisha na utume wa Kanisa unaofumbatwa katika ushuhuda na kwamba, wanapaswa kujisikia kuwa ni sehemu ya familia kubwa tayari kutoa huduma kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Familia ni Kanisa dogo la nyumbani; ni shule ya tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kimaadili na kijamii. Familia ni tabernakulo ya Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; ni mahali pa kufundana umuhimu wa kumwilisha: huduma, upendo, ukarimu, msamaha, kuvumiliana na ujenzi wa udugu wa kibinadamu.

Waamini wanaitwa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za kifamilia
Waamini wanaitwa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za kifamilia

Hapa ni madhabahu ya sala, ibada, na tafakari ya Neno la Mungu; mambo msingi yanayowawezesha wanafamilia kujivika upendo, busara, rehema, utu wema, upole na unyenyekevu. Tunu hizi msingi za maisha ya ndoa na familia kwa sasa ziko hatarini kutokana na taasisi ya familia kupigwa vita kana kwamba ni “Mbwa koko!! Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Baba Mtakatifu amewataka wajumbe wa Muungano wa Wafanyabiashara wa Kifamilia Nchini Italia, AIDAF kuweka uhusiano mzuri kati ya familia na kazi, kielelezo makini cha ujasiri wa wafanyabiashara unaosimikwa katika uwajibikaji; mambo ambayo ni sawa na chanda na pete. Maono ya mbali na uwajibikaji ndiyo siri ya ukuaji wa uchumi. Neno uchumi linatokana na neno la Kigiriki “Oïkos”, yaani nyumba, na “Nomos,” yaani sheria. Hapo awali haimaanishi chochote zaidi ya serikali yenye busara na halali ya kaya kwa ustawi wa kawaida wa familia yote.

Waamini walei wawe ni mashuhuda na wajenzi wa tunu msingi za familia
Waamini walei wawe ni mashuhuda na wajenzi wa tunu msingi za familia

Maana ya neno "Economy" yaani "Uchumi" baadaye ilipanuliwa kwa Serikali ya familia kubwa ambayo ni serikali. Kumbe, hii ni changamoto kwa AIDAF kutunza familia, biashara yao, mazingira nyumba ya wote pamoja na kuwatunza vijana wa kizazi kipya. Kama yalivyo maisha na utume wa Kanisa yanasimikwa katika eneo, hata wao wanaitwa na kutumwa kutangaza tunu msingi za Kiinjili zinazobubujika kutoka katika familia zao, na kuendelea kuwa makini kwa taaluma zao. Wawe ni mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo, tayari kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu. Katika utekelezaji wa majukumu yao sehemu mbalimbali za dunia watangaze na kushuhudia tunu msingi za maisha ya familia. Wajisikie kuwa ni sehemu muhimu sana ya Kanisa, tayari kushiriki katika familia kubwa ya binadamu, kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu na haki yake. Kumbe, huu ni mwaliko wa kupanua akili na nyoyo zao kwa kuwa na mtazamo mpana zaidi katika ujenzi wa familia; wajenge na kudumisha utamaduni wa kusikilizana; kushirikiana na kushikamana, tayari kukuza na kuendeleza talanta walizokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi, mafao na matumizi ya wote.

Wafanyabiashara
05 October 2024, 14:20