Papa:wito wa kusitisha vita,Ukraine,Haiti&Nchi za Mashariki ya kati
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mara baada ya tafakari na Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 13 Oktoba 2024, Mama Kanisa akiwa anakumbuka Ujumbe wa Mwisho Uliotolewa na Bikira Maria wa Fatima kwa watoto watatu mnamo 10 Oktoba 1917, Baba Mtakatifu Francisko ameelezea kwamba: “Ninaendelea kufuatilia kwa wasiwasi kile kinachotokea Mashariki ya Kati, na kwa mara nyingine tena ninatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja kwa pande zote. Tufuate njia za diplomasia na mazungumzo ili kufikia amani. Niko karibu na watu wote wanaohusika, katika Palestina, Israel na Lebanon, ambapo ninaomba kwamba vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa viheshimiwe. Ninawaombea waathiriwa wote, waliohamishwa, mateka ambao ninatumaini wataachiliwa mara moja, na ninatumaini kwamba mateso haya makubwa yasiyo na maana, yanayotokana na chuki na kisasi, yataisha hivi karibuni.”
Papa Francisko akiendelea alisema “vita ni udanganyifu, ni kushindwa, na havileti amani, havileti usalama kamwe, bali ni kushindwa kwa wote hasa kwa wale wanao amini hawawezi kushindwa. Tafadhari acheni! Ninatoa ombi langu ili Waukraine wasiachwe hadi kufa na baridi na kwamba mashambulio ya anga dhidi ya raia, ambayo kila wakati ndio walioathirika zaidi, yakome. Acha kuua watu wasio na hatia!
"Ninafuatilia hali ya kushangaza nchini Haiti, ambapo ghasia dhidi ya idadi ya watu inaendelea, kulazimika kukimbia makazi yao kutafuta usalama mahali pengine, ndani na nje ya nchi. Tusisahau kamwe kaka na dada zetu wa Haiti. Ninaomba kila mtu aombe kwamba aina zote za vurugu zikome na, kwa kujitolea kwa jumuiya ya kimataifa, tuendelee kufanya kazi ya kujenga amani na maridhiano nchini, daima tukitetea utu na haki za watu wote." Baba Mtakatifu Fransisko alisisitiza.
"Nawasalimu, Waroma na mahujaji kutoka Italia na nchi nyingi, hasa, Jumuiya ya ya Kijeshi ya Watakatifu iliyoanzishwa na Mtakatifu Maximilian Kolbe, Parokia za Resuttano (Caltanissetta), wanariadha wa Olimpiki wa walemavu wa Italia wakiwa na viongozi na wasaidizi. Kikundi cha Harakati ya Kimataifa ya Pax Christi, Kwa mara nyingine tena nawasalimia wanafunzi wapya wa Chuo cha Kikuu cha Kipapa cha Urbano niliokutana nao asubuhi ya leo.
"Ijumaa ijayo, Oktoba 18, Shirika la "Msaada kwa Kanisa hitaji litendeleza mpango wa "Watoto milioni moja kusali Rozari kwa ajili ya amani duniani". Asante kwa wavulana na wasichana wote wanaoshiriki! "Tunaungana nao na kujikabidhi kwa maombezi ya Mama - ambaye leo hii ni kumbukumbu ya tukio la mwisho la Fatima na kwa maombezi ya Mama tunawakabidhi Ukraine wanaoteswa, Myanmar, Sudan na watu wengine wanaoteseka kwa vita na kila namna ya jeuri na taabu.”
“Ninawasalimu watoto wote wa Parokia ya Immaculate na ninaona bendera za Kipolishi, Brazil, Argentina, Ecuador, Kifaransa. Ninawasalimu kila mmoja! Nawatakia mlo mwema, Dominika njema na tafadhali msisahau kuniombea.