Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine, tarehe 11 Oktoba 2024 amezungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine, tarehe 11 Oktoba 2024 amezungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Rais Volodymyr Zelenskyy Akutana na Papa Francisko: Mpango Mkakati wa Amani

Mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu na mgeni wake, yamejikita hasa kuhusiana na vita inayoendelea kati ya Ukraine na Urusi; hali tete ya watu wa Mungu nchini Ukraine sanjari na njia zinazoweza kutumika ili hatimaye, kusitisha vita, ili kurejesha tena amani, utulivu, ustawi na maendeleo ya nchi. Wamegusia pia maisha ya kiroho ya watu wa Mungu nchini Ukraine. Hii ni mara ya tatu kwa viongozi hawa kukutana mubashara, ingawa wamekuwa wakiwasiliana kwa simu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa tarehe 11 Oktoba 2024 amekutana na kuzungumza na Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine ambaye baadaye amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa. Mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu na mgeni wake, yamejikita hasa kuhusiana na vita inayoendelea kati ya Ukraine na Urusi; hali tete ya watu wa Mungu nchini Ukraine sanjari na njia zinazoweza kutumika ili hatimaye, kusitisha vita, ili kurejesha tena amani, utulivu, ustawi na maendeleo ya nchi. Wamegusia pia maisha ya kiroho ya watu wa Mungu nchini Ukraine. Hii ni mara ya tatu kwa Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, kwani mara ya kwanza ilikuwa ni tarehe 8 Februari 2020, mazungumzo yaliyodumu dakika arobaini na tano, Baba Mtakatifu alipomhakikishia uwepo wake wa karibu kwa watu wa Mungu katika kipindi hiki kigumu.

Amani, Ustawi na Maendeleo vipaumbele kwa wakati huu.
Amani, Ustawi na Maendeleo vipaumbele kwa wakati huu.

Mara ya pili ilikuwa ni mjini Puglia, Kusini mwa Italia wakati wa mkutano wa Viongozi Wakuu wa Kundi la Nchi Saba zilizoendelea zaidi kiviwanda duniani, G7. Alisema siasa inayohitajika katika kujenga udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii, inapania pamoja na mambo mengine kukuza na kudumisha amani ulimwenguni sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia katika ulimwengu wa kidigitali, yamesaidia maboresho makubwa katika matumizi ya “akili mnemba” katika sekta mbali mbali za maisha ya mwanadamu, iwe kwa mtu binafsi au jamii katika ujumla wake. Mapinduzi haya makubwa ya teknolijia yanawawezesha watu kujifahamu sanjari na kuufahamu ulimwengu unaowazunguka, kiasi hata cha kuathiri maamuzi, uwezo wa kufiki na kutenda katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu.

Mpango mkakati wa kusitisha vita ni muhimu sana
Mpango mkakati wa kusitisha vita ni muhimu sana

Leo hii utashi wa mwanadamu unaathiriwa kwa namna ya pekee na matumizi ya teknolojia ya akili mnemba kutokana na mchango wake mkubwa! Siasa inayojihusisha na matokeo ya haraka ikisaidiwa na sekta ya manunuzi husukumwa na uzalishaji wa muda mfupi na kwa masilahi ya watu wachache ndani ya jamii. Kumbe, ujuzi halisi wa uongozi unajionesha pale ambapo mkazo zaidi ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na ujenzi wa taifa na ujenzi wa familia ya binadamu. Kumbe, kuna haja ya kuweka uhusiano mwema baina ya siasa na uchumi kwa ajili ya mustakabali wa binadamu. Na hii ndiyo hali halisi ya teknolojia ya akili mnemba. Ni wajibu wa binadamu kuweza kuitumia vyema na kwamba, lazima ziwepo sera bora zaidi za matumizi bora ya teknolojia ya akili mnemba.

Rais wa Ukraine
11 October 2024, 15:41