Rambirambi za Papa kwa kifo cha Kard.Renato Martino:Bidii ya Injili
Na Angella rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Jumanne tarehe 29 Oktoba 2024 ametuma salamu za rambirambi kwa Marcello Martino, kufuatia na kifo cha kaka yake, Kardinali Renato Raffaele Martino, kilichotokea tarehe 28 Oktoba 2024 akiwa na umri wa miaka 91. Salamu hizo za rambirambi zinamwendea kaka yake, familia nzima pamoja na Jimbo Kuu la Salerno - Campagna - Acerno mahali ambapo alijulikana kikuhani. Papa anamkumbuka mchungaji huyo kwa bidii alizohudumia Injili na Kanisa, akimfikiria “kwa shukrani Ushirikiano wake wa muda mrefu na watangulizi wake mapapa, ambapo aliwahi kuwa Balozi wa Kitume kwa baadhi ya Nchi za bara la Asia, na hasa katika Mashirika ya Umoja wa Mataifa, mahali ambapo hakuacha nguvu ya kushuhudia ubaba wa Baba Mpole kwa hatima ya ubinadamu.” Baba Mtakatifu ameandika: “Na hatimaye kama Rais wa Baraza la Kipapa la Haki na amani, na katika nafasi mbali mbali zalizokabidhiwa alihamasisha bila kuchoka mazungumzo na maelewano.” Baba Mtakatifu Francisko anamwomba “Bwana ampokee mtumishi wake mwaminifu katika Yerusalemu ya mbingu na kwa Moyo wote anawabariki wanaoombolewa kwa kifo chake na kwa wazo la utambuzi wa wale ambao walimuudumia.
Majukumu aliyoshikilia wakati wa maisha yake
Kardinali Renato alizaliwa huko Salerno tarehe 23 Novemba 1932, alipewa daraja la Upadre tarehe 20 Juni 1957 na kupata shahada ya Sheria ya Kanisa. Aliingia katika diplomasia ya Vatican mwaka 1962 na kufanya kazi katika Ubalozi wa Nicaragua, Ufilipino, Lebanon, Canada na Brazil. Kati ya 1970 na 1975 alikuwa na jukumu la Sehemu ya Mashirika ya Kimataifa ya Sekretarieti ya Vatican. Mnamo 1986 alipokea jukumu la mwakilishi wa kudumu wa Vatican katika Umoja wa Mataifa huko New York, Marekani. Katika nafasi hii alishiriki kikamilifu katika mikutano mikuu ya kimataifa iliyohamasishwa na UN. Baada ya miaka kumi na sita aliyokaa katika Umoja wa Mataifa huko New York, tarehe 1 Oktoba 2002 Mtakatifu Yohane Paulo II alimuita kuliongoza Baraza la Kipapa la Haki na Amani. Alifanikiwa katika nafasi hii iliyoachwa na Kardinali wa Ufaransa, Roger Etchegaray na Kardinali wa Kivietinamu François-Xavier Nguyên Van Thuân. Tayari mwanzoni mwa mamlaka yake, Kardinali Martino alielekeza mawazo yake katika hali ngumu ya Venezuela na mzozo mkubwa wa wenyewe kwa wenyewe nchini Ivory Coast. Zaidi ya yote, hakukosa kuzungumzia hali mbaya ya Mashariki ya Kati.
Aliundwa Kardinali mnamo tarehe 21 Oktoba 2003
Mtakatifu Yohane Paulo II alimuunda kuwa Kardinali katika Baraza la Makardinali la tarehe 21 Oktoba 2003. Tarehe 25 Oktoba 2004, Baraza la Kipapa alililokuwa anaoongoza lilichapisha Mkusanyiko wa Mafundisho ya Kijamii ya Kanisa uliokuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu. Mnamo Machi 2005, Baraza la Kipapa la Haki na Amani kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za vyuo vikuu vya Kikatoliki, waliendeleza Kongamano la Kimataifa mjini Vatican ili kuadhimisha miaka 40 ya Katiba ya maridhiano ya Gaudium et spes. Tangu tarehe 24 Oktoba 2009 amekuwa rais mstaafu wa Baraza la Kipapa la Haki na Amani. Kwa shughuli yake ya mara kwa mara ya kupendelea uhusiano wa amani na faida kati ya watu, uhamasishaji wa watu na tamaduni, Kardinali huyo alitunukiwa digrii na heshima nyingi.
Mazishi tarehe 30 Oktoba 2024 katika Basilika ya Mtakatifu Petro
Mazishi yatafanyika Jumatano tarehe 30 Oktoba 2024, saa 9.00 alasiri, kwenye Madhabahu ya Kiti cha Kanisa kuu la Mtakatifu Petro. Liturujia itaadhimishwa na Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, pamoja na makardinali, maaskofu wakuu na maaskofu wengine. Mwishoni mwa maadhimisho hayo, Papa Francisko ataongoza ibada ya (Ultima Commendatio ed Valedictio), yaani ya mwisho. Kuhusiana na Baraza la Makardinali, kutokana na kifo cha Kardinali Martino, Baraza la makardinali linabaki na makardinali 233, kati yao wapiga kura 121 na 112 wasio wapiga kura.