Sikukuu ya Bikira Maria wa Aparecida inaadhimishwa kwa namna ya pekee na watu wa Mungu nchini Brazil kila mwaka ifikapo tarehe 12 Oktoba. Sikukuu ya Bikira Maria wa Aparecida inaadhimishwa kwa namna ya pekee na watu wa Mungu nchini Brazil kila mwaka ifikapo tarehe 12 Oktoba.   (Pe. gerson Schmidt)

Sikukuu ya Bikira Maria wa Aparecida Nchini Brazil: Amani na Utulivu!

Papa Francisko anawasihi wanajitahidi kumwilisha ujumbe wa Bikira Maria katika maisha kwani unafumbatwa katika msingi wa amani na utulivu miongoni mwa Wakristo wote; kwa watu wote pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Papa anamwomba, Bikira Maria wa Aparecida awalinde na kuwapatia tunza yake ya kimama; awasaidie kusonga mbele kwa ari, moyo mkuu na furaha, kwa sababu Bikira Maria wa Aparecida ni chemchemi ya furaha ya kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ibada kwa Bikira Maria miongoni mwa wananchi wa Brazil ina chimbuko lake katika mapambano dhidi ya ukoloni wa Wareno uliowawezesha wamisionari wakati wa mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili kujenga makanisa mengi yaliyowekwa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Kunako mwaka 1717, Sanamu ya Bikira Maria wa Aparecida iliokotwa na wavuvi watatu ambao walikesha usiku kucha wakivua samaki, lakini wakaambulia patupu! Baadaye, wakavua Sanamu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili na huo ukawa ni mwanzo wa mafanikio makubwa katika shughuli zao za uvuvi, kielelezo makini cha uwepo angavu na endelevu wa Bikira Maria kwa watoto wake wanaopambana na hali ngumu ya maisha pamoja na umaskini!

Bikira Maria wa Ararecida
Bikira Maria wa Ararecida

Kunako mwaka 1983 Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil likajenga Kanisa kuu la Bikira Maria wa Aparecida linalopokea idadi kubwa ya mahujaji kutoka ndani na nje ya Brazil, wanaokwenda kutoa heshima zao kwa Bikira Maria Mama wa huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2013 yaliyofanyika nchini Brazil aliitaka familia ya Mungu nchini Brazil, kuendeleza kumbu kumbu hii kama sehemu ya mchakato wa hija ya wananchi wa Brazil kutaka kukutana na Mwenyezi Mungu anayewafunulia waja wake uso wa huruma, hata katika umaskini wao, kwa njia ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, kama alivyofanya wakati wa maadhimisho ya Arusi ya Kana, alipomwambia mwanaye Kristo Yesu, hawana divai! Malkia Isabela D’Orleans-Braganza aliguswa kwa namna ya pekee na Ibada kwa Bikira Maria kiasi kwamba, akawa ni kati ya watu waliosimama kidete kupambana na hatimaye kufutwa kwa biashara ya utumwa, ili kujenga na kudumisha umoja na udugu, kwa kumwachia nafasi Bikira Maria ili aweze kusaidia mchakato wa uponyaji kutokana na madhara ya biashara ya utumwa nchini Brazill.

Sikukuu ya Bikira Maria wa Aparecida 12 Oktoba
Sikukuu ya Bikira Maria wa Aparecida 12 Oktoba

Bikira Maria wa Aparecida ni kielelezo cha Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Bikira Maria wa Aparecida ni changamoto kwa familia ya Mungu nchini Brazil kujikita zaidi na zaidi katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha ya Kikristo wenye mvuto na mashiko! Sikukuu ya Bikira Maria wa Aparecida inaadhimishwa kwa namna ya pekee na watu wa Mungu nchini Brazil kila mwaka ifikapo tarehe 12 Oktoba. Ni katika muktadha wa maadhimisho haya, Baba Mtakatifu Francisko amewatumia salam na matashi mema watu wa Mungu nchini Brazil ili kuwaonesha uwepo wake wa karibu. Amewasihi kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kumwilisha ujumbe wa Bikira Maria katika maisha na vipaumbele vyao kwani huu ni ujumbe unaofumbatwa katika msingi wa amani na utulivu miongoni mwa Wakristo wote; kwa watu wote pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu anamwomba, Bikira Maria wa Aparecida awalinde na kuwapatia tunza yake ya kimama; awasaidie kusonga mbele kwa ari, moyo mkuu na furaha, kwa sababu Bikira Maria wa Aparecida ni chemchemi ya furaha ya kweli!

Bikira Maria wa Aparecida

 

12 October 2024, 14:23